Uhakiki wa riwaya ya Dunia Uwanja wa Fujo
Wasiliana na Mwalimu ili Kujiunga Darasa la Uhakiki wa Vitabu vyote vya Fasihi Mtaala Mpya kwa Kugusa Hapa
Mwandishi: Euphrase Kezilahabi
Mwaka: 1975
Mhakiki: Mwalimu Makoba
Nilipofika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa ajili ya masomo yangu, mtu wa kwanza kutamani kumuona alikuwa ni Profesa Euphrase Kezilahabi. Nilimsoma katika kazi zake mbalimbali ikiwamo hii ya Dunia Uwanja wa Fujo. Nilianza msako mara moja wa kumtafuta Profesa Kezilahabi bila mafanikio. Baadaye niligundua kupitia kwa mwalimu wangu M.M. Mulokozi, ambaye aliwahi kuwa mwanafunzi wa Kezilahabi kwamba, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kilimfuta kazi Kezilahabi miaka mingi iliyopita!
Mwishoni mwa miaka ya 1990 Kezilahabi aliomba likizo ya miaka miwili kwenda kufundisha Botswana. Alikubaliwa na akaenda Botwana mwaka 1995. miaka miwili ilipokwisha Botswana walimwongezea muda, akakiomba Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimwongezee muda lakini akakataliwa na kuambiwa arejee mara moja. Aliposhindwa kurejea alifutwa kazi na kujikuta hana ajira tena nchini Tanzania, hivyo akalazimika kubakia Botswana.
Kezilahabi alistaafu akiwa katika ngazi ya Profesa Mshiriki. Chuo Kikuu cha Botswana hakikukubali kumpandisha cheo kuwa Profesa kamili kwa sababu maandiko yake mengi yalikuwa katika lugha ya Kiswahili na hawakuweza kuyasoma ili kuyatathmini. Alimuomba Mulokozi amsaidie kutafuta orodha ya makala, vitabu na tasnifu zinazojadili kazi zake kwa lugha mbalimbali ili aweze kuitumia kukishawishi Chuo Kikuu cha Botswana kuwa alistahili kupandishwa cheo kutokana na hadhi na mchango wake katika fasihi ya Kiswahili na ulimwengu. Bahati mbaya, Kezilahabi alifariki kabla kazi hiyo haijakamilishwa. Kezilahabi alifariki mwaka 2020 na kuzikwa nchini Tanzania.
Kuhusu Dunia Uwanja wa Fujo
Dunia uwanja wa fujo ni riwaya inayohusu mgongano wa kimfumo na kitabaka kati ya ujamaa na ubepari kwenye miaka ya 1960 na 1970 nchini Tanzania. Riwaya hii inaonesha jitihada za serikali ambayo inataka kujenga jamii ya kijamaa, kudhibiti tabaka la makabaila wenye kumiliki ardhi, ambalo lilionekana kama mojawapo ya vikwazo vya kufikia ujamaa kamili.
Dunia uwanja wa fujo ni riwaya ambayo inaonesha kuwa kila mtu huja Duniani kufanya fujo zake kisha hujiondokea.
Simulizi kwa ufupi
Tumaini alikuwa mtoto ambaye alipewa malezi ya kudekezwa sana na wazazi wake kwa sababu alikuwa mtoto wao wa pekee. Wazazi wanapofariki wanamuachia kiasi kingi cha pesa Tumaini.
Tumaini anaanza fujo zake, ana mahusiano na wasichana wengi kijijini na anampachika mimba Leonila. Katika harakati zake, Tumaini anatoroka na msichana Anastasia ambaye alikuwa ameposwa tayari, anatoroka naye wakaishi Mwanza, lakini wanakaa hapo kwa muda mfupi na kutofurahishwa na eneo hilo hasa kwa sababu palikuwa ni karibu sana na nyumbani kwao. Wanaamua kwenda Dar es Salaam, hata hivyo wanaishia mjini Shinyanga na kuendelea na maisha yao hapo.
Baada ya starehe nyingi, pesa zinaanza kumuishia Tumaini, anaomba msaada wa kazi kwa rafiki yake aitwaye Dennis, Tumaini anafanikiwa kupata kaziy ya upelelezi, yaani upeleleza watu wanasema nini kuhusu serikali kwenye mabaa.
Tumaini anaifanya kazi yake kwa weredi, lakini anajikuta akichukiwa na watu, mwenye baa hampendi Tumaini kwa sababu akiingia humo wateja wanaondoka kwa sabau walikwisha ifahamu kazi yake. Zengwe linaundwa, Tumaini anatekwa na kushambuliwa vibaya.
Tumaini anafanikiwa kupona, anapopona, Tumaini si yule tena wa zamani. Mtazamo wake kuhusu maisha sasa umebadilika, anaacha kazi hii ya upelelezi, anajikita katika kilimo cha pamba na mazao mengine.
Tumaini anafanikiwa kupata utajiri, akiwa katika kilele cha utajiri wake, serikali inakuja na sera ya ujamaa!
Mali yote ya Tumaini aliyoitafuta kwa jasho inachukuliwa na serikali, mashamba, trekta, kila kitu kinakwenda. Tumaini hakubali, anavamia mkutano na kumpiga risasi mkuu wa wilaya.
Tumainia anakamatwa, anahukumiwa kunyongwa, kwa ujasiri anasema, “Waambie nitakufa. Lakini nitakufa kiume. Sitatoa hata chozi moja. Wambie sina masikitiko kwa jambo nililotenda. Nitakufa na heshima yangu. Kama nilifanya kosa vizazi vijavyo vitamua.”
Riwaya hii iliandikwa mwaka 1975 wakati Tanzania ikiwa katika ujamaa. Tumaini anasema vizazi vijavyo vitaamua endapo alifanya kosa.
Miaka 10 baadae yaani mwaka 1985, sera ya ujamaa ilikufa, na Mwalimu Nyerere aliachia urais akimpisha Mwinyi. Vizazi vijavyo vilivyosemwa na Tumaini kuwa vitaamua endapo alikosea ni sisi, na jibu liko wazi!
Maudhui
Dhamira
Sera ya ujamaa
Serikali ya Tanzania inaanzisha sera ya ujamaa. Kutokana na sera hii, matajiri wanachukiwa. Hata hivyo, wanakijiji hawafurahishwi na sera hii, serikali inafanya juhudi kubwa kuwaelimisha. Katika mkutano mwananchi mmoja anapinga,
“Kukaa pamoja, kutembea pamoja kama wafungwa. Sisi si wafungwa? Vijiji kama hivyo vinawafaa wafungwa!” uk 210.
Wananchi hawafurahishwi na hoja ya kuishi katika vijiji vya ujamaa, wanatamani waendelee na maisha yao ya kawaida.
Pia viongozi wameshindwa kuwa mfano wa maisha ya ujamaa, wanahubiri kuishi katika vijiji vya ujamaa ilhali wao wanaishi mjini. Mwananchi mmoja anamuuliza kiongozi anayehubiri ujamaa. Kiongozi huyu anahubiri watu waishi katika vijiji vya ujamaa ilhali yeye anaishi mjini.
“Tumesikia, unatoka Dar es Salaam; sijui nacho ni kijiji cha ujamaa?” uk 210.
Kutokana na sera ya ujamaa, Tumaini ananyang’anywa mali zake zote, naye analipa kisasi kwa kumuua mkuu wa wilaya. Hata hivyo anaishia kukamatwa na kuhukumiwa kunyongwa.
Matabaka
Jamii imejaa matabaka mengi. Wasomi na wasiosoma, masikini na matajiri. Katika harusi ya Dennis, watu wa maana waliovalia suti walipelekewa vyakula vizuri ndani, wanakijiji walitengwa nje. Mwanangwa hakuweza kuvumilia, alimuita Kasala na kumweleza,
“Waliokaa ndani ni nani? Wao hawakuzaliwa kama sisi? Walianguka kutoka juu angani labda!” uk 123.
Vilevile tunaliona tabaka tawala likiwaonea wananchi kwa kisingizio cha ujamaa. Tumaini ananyang’anywa mali yake yote aliyoitafuta kwa jasho.
Imani za kishirikina
Mugala anafukuzwa kijijini kwa madai ya imani za kishirikina. Inasemekana Mugala anaroga watu na kuwageuza vizuu ili wamlimie mashamba yake.
Anaaminika kuwafanya vizuu wanakijiji wengi akiwemo baba na mama yake Tumaini. Anafukuzwa kijijini na kupelekwa kisiwa cha wachawi.
Vera naye amejaa ushirikina, yeye anamfanyia madawa ya kiarabu mumewe, analo baibui ambalo hulivalia pindi anapokwenda kupewa madawa hayo.
Upande mwingine tunamuona Leonila akimwekea dawa Tumaini katika kinywaji ili ampende na hatimaye aweze kumuoa. Hata hivyo, jambo hili halifanikiwi kwani Tumaini anahamishia mapenzi yake kwa Anastasia.
katika mkutano wa hadhara, mwananchi anaonesha hofu kubwa juu ya kwenda kuishi kijiji cha ujamaa, hofu yake ni juu ya kurogana, anauliza, vipi kama huko watu watarongwa. Mzungumzajia anayehubiri habari za ujamaa, anamweleza waziwazi kuwa, uchawi hakuna.
Imani za kishirikina zinapewa nafasi kubwa mno katika jamii za Kiafrika. Katika jamii yetu, wengi wanaamini katika ushirikina. Mfanyabiashara hafanyi biashara mpaka apate mganga, wasanii nao hawaimbi ila mpaka waaguliwe na waganga. Suala la kuamini katika ushirikina linayarudisha nyuma maendeleo ya jamii yetu. Ni ukweli ulio wazi kuwa, dunia inaongozwa na kanuni zinazoweza kuthibitishwa kisayansi. Kuamini katika ushirikina, ni kujirudisha nyuma katika maendeleo yetu wenyewe.
Tamaduni za kigeni
Dennis amezama katika tamaduni za kigeni. Yeye si baba kama baba wa Kiafrika anavyopaswa kuwa. Amepangiana zamu ya kupika na mkewe na anamshirikisha kwa kila jambo. Wageni wanapokuwa, Vera anamwambia mumewe awafungulie mlango.
““Baba Resi kuna wageni nje. Kawafungulie mlango.” Dennis aliamka. Alikwenda kuwafungulia akiwa amevaa gauni lake la usiku,” uk 183.
Hata hivyo mwisho wa maisha hayo unafika, Dennis anagundua mkewe anamsaliti kwa kuwa na mahusiano na John, anamrejesha kwao, mwandishi anasema,
“Na ndani ya nyumba ya Dennis huo ndio ulikuwa mwisho wa jaribio la utamaduni wa ‘kizungu’ katika jamii ya Kiafrika,” uk 196.
Upande mwingine tunaziona dini za kigeni zikiingia kwa kasi, Waafrika walikuwa na dini zao kabla ya kuja dini hizi, maarufu zaidi zikiwa ukiristo na uislamu.
Katika riwaya hii, mwandishi anaonesha wanakijiji wakishangaa ujio wa dini hizi mpya, ambazo inasemekana ziko mjini. Wanakijiji wa kijiji cha Bugolola wao walikuwa bado wakiendelea na dini zao za jadi, dini zilizohusisha kuabudu mizimu. Wanashangazwa na dini hizi mpya, namna zinavyoendeshwa na Mungu wanayemuabudu.
Kuhusu dini ya Kikristo, wanakijiji wanashangazwa nayo:
“Lakini mimi jambo moja linanishangaza. Siku moja niliingia kanisani nikaona watu wanapewa vijidudu fulani mdomoni. Hivi ni nini?”
“Mimi zamani nilifikiri ni shilingi. Lakini nasikia wanavitafuna,” uk 66.
Pia wanakijiji hawa wanashangazwa na dini ya uislamu:
“Jambo jingine ni kwamba kwa nini waislamu hawali nyamafu?” Kasala aliuliza.
“Ni wagonjwa,” Tembo alijibu. “Nyamafu wana magonjwa.”
“Mbona sisi tunakula na tuna nguvu kuwazidi?” uk 67.
Naye Tumaini ameshikilia tamaduni za kigeni. Tamaduni zinazohamasisha uzinzi, ulevi na kukaa bila kazi yoyote.
Baadae tunamuona Tumaini akibadili msimamo wake, anaanza kupata mashaka juu ya tamaduni hizi mpya, anaandika makala gazetini akilalamikia kuanzishwa kwa vyama vya kizungu vinavyohamasisha watu kutembea uchi na kutumia miili yao ili kujiletea starehe.
Yote yaliyoandikwa na mwandishi kitabuni yametokea kwa kasi katika jamii zetu. Dini za ukiristo na uislamu tayari zimejibebea umaarufu mkubwa huku waafrika wakisahau dini zao za jadi. Upande wa ajira unasikitisha, zipo nafasi za kazi zinatangazwa leo hii, lakini kigezo ni lazima uwe muumini wa dini fulani. Ni aibu, ni simanzi kuona Wana wa Afrika wanatengana kwa sababu ya tofauti ya dini za kuletewa!
Katika familia, tunaona vyama vingi vya wanawake vimeanzishwa wakidai haki zao, wakidai usawa nje na tamaduni zilivyo. Suala hili limepelekea kuvunjia kwa ndoa nyingi hususani ndoa za wanawake wasomi.
Upande aliouhofia Tumaini Kapinga sasa ni jambo la kawaida katika jamii yetu. Ni hali ya kawaida kukutana na wanawake wakitembea nusu uchi, wengine wakijiuza na mikanda ya ngono ya watu maarufu iliyovuja ikionyeshwa katika mitandao ya kijamii, video hizi hujulikana na vijana kwa jina maarufu la ‘connection’.
Umasikini
Mwandishi anatueleza kuwa familia ya Kasala ilikuwa masikini. Kasala na familia yake waliishi maisha ya tabu na masumbuko, hata hivyo waliyazoea maisha hayo. Si familia ya Kasala tu, bali wanakijiji wengi Bugolola walikumbwa na umasikini.
“Wakati wa kiangazi taabu ya maji; upepo mwingi na magonjwa ya kila aina. Wakati wa masika ni nzi mchana, mbu usiku.
lakini miili yao iliweza kujirekebisha na majira yote ya mwaka. Hayo ndiyo yaliyokuwa maisha yao, maisha ya taabu na masumbuko,” uk 6.
Umasikini unaonekana katika familia ya Mulele, Tembo anaisaidia familia hii hivyo Mulele anapanga kumuozesha Anastasia kwa Tembo kama shukrani na kuendeleza ujamaa.
Gamba la nyuma la kitabu hiki cha Dunia Uwanja wa Fujo, kilichochapwa na Ape Network toleo la mwaka 2022, limepotosha kuwa Tumaini alitokea familia ya kitajiri. Si kweli, Tumaini hakutokea familia ya kitajiri kama inavyoeleza na gamba la nyuma la kitabu chenyewe. Familia aliyotokea Tumaini ni familia ya kawaida, baba yake Tumaini alikuwa mwalimu ambaye alijinyima ili kumuwekea akiba mtoto wake. Wazazi wake Tumaini waliamini akiba hii itamsaidia mtoto huyu pindi watakapoondoka.
Familia ya Tumaini iliishi maisha ya kawaida, kama wanakijiji wengine, kuna wakati walikula mboga za majani mpaka wanakijiji wakaanza kuwasema. Muyango, mama yake Tumaini, alizunguka katika mashamba ya watu akichuma majani ya mihogo ambayo yangepikwa kama mboga. Majirani waliwatania,
“Nafikiri ukiwapasua kina Muyango utakuta matumbo yao yana rangi ya kijani!” uk 21.
Mapenzi
Kasala na mke wake walipendana.
Dennis alimpenda sana mke wake Vera. Alimpenda kiasi cha kukubali kuwa na zamu ya kupika pamoja.
Mwishoni tunamuona Tumaini akiamua kuwa na mwanamke mmoja. Anastasia. Baada ya pilikapilika za maisha, anagundua hana mwanamke zaidi ya Anastasia. Anasikika akisema, mke wangu kuanzia sasa ni Anastasia.
Tunawaona wanakijiji wakipendana, wanapokwenda nyumbani kwa Mulele kunywa pombe, wanataniana na kucheka kwa furaha.
Mmomonyoko wa maadili
Leonila anapewa mimba akiwa bado anaishi nyumbani kwa wazazi wake.
Tumaini anasoma kitabu cha ngono, ‘sex and you’ na bila shaka anayafanyia kazi aliyoyasoma humo.
Vera anamsaliti mume wake Dennis na kutembea na John, tena haya yanafanyika Tumaini akiyasikia.
Vera anambembeleza John azini naye, “Usifunge Mlango. Heshima yangu nimekwishaipoteza! John! Ukiniacha hivihivi tu nitaona aibu sana!”
Wakati huohuo Tumaini alisikia ufunguo ukilia kacha! Aliskia kitu kizito kinakalia kitanda. Aliposikia kitanda kinalia tena alifahamu kwamba watu wawili walikuwa sasa kitandani. Tumaini aliweza kusikia pumzi ya yule mnene.”
Ndoa
Tumaini anazifahamu changamoto zilizopo katika ndoa, hata hivyo yeye anaamini ndoa ni jambo jema na mtu ambaye hana ndoa basi ameshindwa maishani. Ndoa inayosemwa na tumaini hapa ni hali ya mke na mume kuishi pamoja.
Katika ndoa ya kwanza ya Dennis, tunamuona Vera akiwa na mahusiano na watu wengi, kwanza mtoto aliyenaye wala si wa Dennis, lakini Vera anakuwa na mahusiano na John na analala naye hapohapo nyumbani.
Ndoa ya pili ya Dennis imejaa makelele mengi, wanagombana mara kadhaa kiasi cha mke kufikia hatua ya kufungasha mabegi yake ili arejee nyumbani, hata hivyo, haondoki.
Ucheshi
Wanakijiji wa Bugolola walitaniana kila walipokutana katika pombe. Kasala anataniwa kuhusu mkasa wake wa kupigwa na watoto wadogo alipokwenda mjini.
“kama ungekuwa na nguvu namna hiyo ilikuwaje hata ukapigwa mjini na vitoto vidogo ukalia - “batoto bananisondogora!” watu walicheka” uk 66.
Kasala anamtania bwana mmoja ambaye ilisemekana alimpa mimba binti yake. Bwana huyo anaondoka baada ya watu kuanza kucheka.
Kasala anamtania Makaranga kuwa mke wake alikojoa ndani ya motokaa. Hata hivyo Makaranga utani hauwezi, anamfokea Kasala kuwa mama yake ni mchawi, wanataka kupigana, lakini Mulele anakataa kuwa hawawezi kupigana nyumbani kwake, anawaruhusu wapigane mweleka. Kasala anashinda.
Nafasi ya mwanamke katika jamii
Mwanamke amechorwa katika nafasi mbalimbali kama inavyoelezwa
Malaya
Vera ni malaya, kila anapopita anapewa jina linaloendana na sifa zake. Akiwa shule aliitwa ‘Rahisi’, akiwa chuo cha ukarani aliitwa ‘Toa’, akiwa jeshi la kujenga taifa aliitwa ‘Pijo’. Vera huyu kwa sababu ya umalaya wake, anapewa mimba, lakini anambambika Dennis kuwa baba wa mtoto huyo.
Mvumilivu
Anastasia ni mvumilivu, anamvumilia mumewe tangu akiwa mlevi na malaya, mpaka alipobadilika na kuwa mchapakazi hodari.
Jambazi na muuaji
Hadija ni jambazi lililokubuhu, likiwa nyumbani kwa Tumaini linajeruhi kwa bastola kisha linapora fedha na kukimbilia Tabora.
“Hadija sasa alikuwa Hadija kweli. Alilenga bastola kwenye kichwa cha Tumaini,” uk 150.
Mchawi
Mgala anafukuzwa kijijini kwa tuhuma za kujihusisha na uchawi.
Mwenye wivu na chuki
Vera hataki Tumaini awe juu ya mumewe. Anafanya kila namna ili kuhakikisha Tumaini hafanikiwi. Anashiriki jaribio la kutaka kumuua Tumaini.
Ujumbe
Mtoto umleavyo ndiyo akuavyo
Tumaini alipewa malezi mabaya, alidekezwa na wazazi wake. Wazazi wanapofariki, kwa sababu ya malezi mabaya aliyopewa, anaibukia kuwa mwenye tabia mbaya akijihusisha na umalaya na ulevi.
Sera ya ujamaa haikukubaliwa na wote
Sera ya ujamaa haikukubaliwa na watu wote. Wananchi wengi waliipinga. Kwa mfano, kasala hakubalina na ujamaa, naye Tumaini hakubaliani na sera hii.
Ushirikina unabeba nafasi kubwa katika jamii za kiafrika
Tunaona Mugala akifukuzwa kijijini kwa sababu anageuza watu vizuu.
Naye Vera anamwendea mumewe kwa waganga ili apewe dawa za kumfanya ampende.
Upande mwingine, Anastasia anamuwekea dawa Tumaini ili aweze kuolewa naye.
Katika jamii yetu tunauona ushirikina ukipewa nafasi kubwa. Ukisikiliza katika maredio, yamejaa matangazo ya waganga wanaotatua shida mbalimbali.
Tabia ya kuamini miujiza imevuka kasi kiasi kwamba hata katika majumba ya ibada watu wanauziwa maji, mafuta, udongo na keki ambazo zinaaminika kuponya magonjwa, kuleta utajiri na mafanikio chungu nzima. Tabia hii ya kuamini katika miujiza, inachelewesha kwa kiasi kikubwa kupatikana kwa maendeleo, kwani badala ya kuamini katika sayansi, watu sasa wanaamini katika miujiza. Uhalisia wa maisha ni kwamba, hakuna mafanikio yanayomfuata mtu akiwa amekaa, hakuna uchawi, matatizo yote yanayowapata watu ni kanuni za kila siku za ulimwengu. Mathalani mtu akiumwa, ni bora akila lishe bora na kwenda hospitali pale inapobidi kufanya hivyo.
Ulevi ni chanzo cha umasikini
Ulevi umewasababishia wengi umasikini. Fedha alizoachiwa Tumaini na wazazi wake zinapukutika kwa sababu ya ulevi. Bahati inamtokea kwa kupewa kazi ya kupeleleza watu katika mabaa, hata hivyo huko nako anashambuliwa na kupigwa vibaya hali iliyomfanya aache kazi hiyo.
Kazi ni kipimo cha utu
Heshima ya mtu hutokana na kazi anayofanya. Mtu anayefanya kazi huweza kujipatia mafanikio hata kama ni kidogo. Tumaini tangu aachiwe fedha za urithi hakuwahi kufanya kazi yoyote. Kijiji kizima kilimdharau na kumchukia.
Hata hivyo Tumaini anaamua kubadilika, anafanya kazi kwa bidii na anafanikiwa kuwa tajiri mkubwa.
Upande mwingine tunamuona John, yeye hataki kufanya kazi. Anaishi na kulishwa nyumbani kwa Tumaini. Tumaini anapoenda shambani, John anabaki nyumbani akichezea shanga za shemeji yake. Tumaini anachoshwa na jambo hili, anamfukuza John.
Migogoro
Migogoro ya wahusika
Mungere na Tumaini
Mgogoro huu unasababishwa na Tumaini kumpa mimba Leonila.
Tumaini na John
John hataki kufanya kazi, tumaini naye hataki kuishi na mtu ambaye hafanyi kazi.
Tumaini na Vera
Vera hataki Tumaini awe juu kumshinda mumewe. Anamfanyia visa vya kila namna ikiwemo kusuka mpango wa kumuua Tumaini.
Tumaini na Anastasia
Baada ya kumpa ujauzito, Tumaini hamtaki Leonila. Tumaini anatoa maneno makali kuwa mtoto atakayezaliwa si wake hivyo wanaweza kumtupia hata mbwa!
Anastasia na Leonila
Hawa walikuwa marafiki wa muda mrefu, ni Anastasia ndiye aliyemchokoza Leonila kwa kumchukulia mpenzi wake, Tumaini.
Tumaini na Makoroboi
Makoroboi ni jambazi sugu, bado linamkumbuka Tumaini hasa kwa sababu alimpiga na fimbo iliyomwachia alama usoni kipindi ambacho aliiba nguo kijijini. Makoroboi anapata nafasi ya kulipa kisasi kwa kutumwa kwenda kumshikisha adabu Tumaini, Tumaini anapigwa na kujeruhiwa vibaya.
Migogoro ya nafsi
Anastasia anapatwa na mgogoro wa nafsi pale anapoposwa na mtu mzee umri sawa na baba yake. Anaamu kutoroka na Tumaini kama suluhisho.
Tumanini anapatwa na mgogoro wa nafsi juu ya hatma ya maisha yake hasa pale fedha zilipoanza kumuishia. Anaamua kuchagua njia mpya, njia ya kufanya kazi kwa bidii.
Migogoro ya kisiasa
Serikali inatangaza kuufuta mfumo wa ubepari na kuhamia mfumo mpya wa ujamaa. Wananchi wengi hawakubaliani na mfumo huu mpya, naya Tumaini ambaye amepambana kwa bidii kutafuta mali yake, hakubaliani na mfumo huu. Mgogoro unafika juu zaidi pale tunapomuona Tumaini akinyang’anywa mashamba na mali zake, Tumaini anachukua maamuzi ya kumuua mkuu wa wilaya.
Migogoro ya kitamaduni
Tamaduni za Kiafrika zinahitaji mwanaume awe kiongozi katika familia yake na kamwe hakuna usawa kati ya mume na mke. Kwa Dennis hali ni tofauti, katika familia hii, Dennis na mkewe wamepangiana zamu ya kupika. Mwisho wa mgogoro huu unafika pale Dennis anapogundua mkewe alimsaliti kwa kutembea na John, anamfukuza na huo ndiyo unakuwa mwisho wa jaribio la tamaduni za kizungu katika mji wa Dennis.
Migogoro ya kiuchumi
Matajiri wanachukiwa kwa kudhaniwa kuwa ni wanyonyaji. Katika mkutano, Tajiri Tumaini anasimamishwa mbele ya watu na kuzomewa kwa sababu yeye ni tajiri. Nchi inafanya bidii kuingia katika ujamaa, mfumo ambao iliaminika ungekuwa na usawa kwa watu wote.
Falsafa
Mwandishi anaamini kwamba, Dunia ni uwanja wa fujo. Yeye anaamini kuwa, kila mtu huja duniani kufanya fujo zake kisha hujiondokea.
“Zamani niliamini kwamba kila mwanadamu ameumbwa kuja hapa duniani ili apate kufurahia ulimwengu kiasi awezavyo kabla hajafa. Lakini sasa ninaamini kwamba Dunia uwanja wa fujo” uk 111.
Msimamo/mtazamo
Mwandishi ana msimamo wa kidhanifu. Anaamini kwamba dunia ni uwanja wa fujo. Fujo ni sehemu ya dunia, lakini haiwezi kuwa lengo hasa la dunia kuwa uwanja wa fujo. Mtu yeyote anaweza akaamua atakavyo yeye aifanye dunia kuwa uwanja wa kitu gani. Mwingine anaweza kuamua dunia iwe uwanja wa mema, uwanja wa kujifunza ama uwanja wa kuwasaidia wengine.
Fani
Upande wa fani unajadiliwa kama ifuatavyo:
Wahusika
Tumaini
Amepewa malezi mabaya na wazazi wake.
Ni mlevi tena malaya.
Anaamua kubadilika na kufanya bidii katika kazi.
Kasala
Baba yake Anastasia.
Mume wa Mungere.
Ana upendo wa watu wote. Hutoa pombe ya bure nyumbani kwake.
Mungere
Mke wa Kasala.
Mama yake Anastasia.
Ana ishi vyema na wanakijiji.
Mugala
Mama yake Kasala
Anafukuzwa kijijini kwa tuhuma za kujihusisha na ushirikina
Dennis
Mtoto wa kasala.
Anaishi mjini.
Katika familia yake, anaishi maisha ya kizungu ikiwemo kupangiana zamu ya kupika na mkewe.
Leonila
Mtoto wa Kasala
Anapewa mimba na Tumaini
Vera
Mke wa Dennis.
Ni malaya.
Mvivu.
John
Rafiki yake Tumaini.
Ni mlevi na malaya.
Hafanyi kazi yoyote.
Mkuu wa wilaya
Anahubiri habari za ujamaa.
Anakufa kwa kupigwa risasi na Tumaini.
Makoroboi
Jambazi sugu.
Anahusika katika tukio la kumteka Tumaini na kumjeruhi.
Hadija
Jambazi.
Malaya.
Kimada wa Tumaini.
Fatuma
Mwanamke anayefanya kazi baa.
Ni mwanamke wa John.
Baada ya fedha kuishi, Fatma anaiba nguo zote za John na kuondoka nazo, majirani wanapomuona na furushi kubwa, anadai anazipeleka kwa dobi!
Mandhari
- Mandhari ya kijijini mfano, Kijiji cha Bugolola
- Mandhari ya mjini mfano: Mwanza, Shinyanga
- Baa
- Nyumbani
- Chumbani
- Stendi ya mabasi
Muundo
Riwaya hii imetumia muundo wa urejeshi: tunaona maisha ya Dennis akiwapokea Tumaini na wenzake, lakini tunakuja kukumbushwa maisha ya Tumaini yalivyokuwa hapo kabla na namna alivyompata mkewe, Vera.
Pia, mwandishi ametumia muundo wa rukia au changamano ambapo visa vinakuwa vinarukiana. Kwa mfano, mwanzoni mwa riwaya, tunaelezwa kisa cha Kasala na mji wake kabla hakijaisha kinakuja kisa cha Tumaini.
Mwandishi pia ameigawa kazi yake katika sehemu kuu tatu ambazo zinafanya kitabu kiwe na jumla ya sura kumi na nne.
Katika sehemu ya kwanza amewachora wahusika kwa kuonyesha adha na matatizo mbalimbali yanayoikabili jamii ya Bugolola.
Sehemu ya pili Tumaini anaamua kuhama kijijini na kwenda mjini. Anaondoka akiwa na Anastasia na John.
Sehemu ya tatu Tumaini anakata shauri kufanya kazi kwa bidii, tena anaamua kufanya kazi ya kilimo. Anapata mafanikio makubwa, lakini serikali inakuja na sera ya ujamaa inayomfanya apoteze vyote.
Mtindo
Mtindo wa monolojia
Mtindo huu umetawala katika riwaya hii, mwandishi anasimulia riwaya yake mwanzo mpaka mwisho.
“Hadija alienea damu. Alijaribu kusimama ili apambane na Anastasia” uk 150.
Mtindo wa dayolojia
Majibishano baina ya wahusika yanaonekana:
“Nilifikiri kwamba watu wa huku wameendelea lakini kumbe bado washenzi.”
“Kwa nini?” uk 90.
Matumizi ya nyimbo
Mwandishi ametumia nyimbo nyingi, mojawapo huu:
“Wanaume wa Bogolola
Mchana hawajambo
Usiku hawana tendo
Vifaranga vya kuku
Baridi kujikunyata.”
Naye Tumaini aliimba akiwa amelewa.
Ushairi
Tumainia aliandika shairi zuri darasani lililokuwa likisifia mwanamke atakayemuoa.
Hadithi ndani ya hadithi
Tembo anamsimulia Anastasia hadithi ya msichana ambaye alikataa kuolewa na mtu aliyemfahamu akaenda kuolewa na mtu asiyemfahamu, huko anapatwa na matatizo makubwa ikiwemo kuambukizwa magonjwa ya kila aina.
Barua
Tumaini anamwandikia barua John aliyekuwa akiishi kijiji cha Lutare.
Vera anamwandikia barua Dennis, katika barua ya mwisho anamtaka asimtajetaje kwani sasa ana mahusiano na mtu mkubwa.
Matumizi ya lugha
Tamathali za semi
- Onomatopea au Mwigo wa sauti
“Ksuu! Ksuu!”
Vifua vyao vililia ‘ngi’
- Tashibiha
Sasa alifanana na kitumbili.
“Akitupa watu chini kama mzigo wa kuni.”
“Baba yako atakuwa mkali kama simba.”
“Mimi ninauma kama panya” uk 30.
Akitembeatembea kati ya migomba yake kama padri kaburini.
- Tashihisi
“Miaka ni kama kunguni, inamnyonya mtu polepole, halafu huacha gofu kuanguka kaburini.
Mbwa hunywa maji akisema, “sitaki kunywa maji”
“Kesi hiyo ya bia ikiwa imesimama ilionekana kujidai kwamba mwanadamu alikuwa kiiumbe duni mbele yake.”
- Takriri
Kukurukakara kukurukakara
Nihurumie! Nihurumie!
- Mdokezo
Kumbuka huu ni mji wa…
- Sitiari
Anastasia anasema Simba akimaanisha mwanamume anayetaka kumuoa aliyeitwa Tembo. “Basi yule simba amefika tena leo.”
Pia, sitiari inaonekana pale boti inapofananishwa na kiboko, “Kiboko alikuwa akiyumbayumba kidogo.”
- Tafsida
Tumaini alikuwa akishika mahali pabaya
Mjalizo
“Wenye mashoka! wenye mikuki na miundu! Wenye pinde na wenye mapanga walianza kulifyeka lile chaka”
Misemo
Dunia uwanja wa fujo
Ponda mali kifo chaja
“Wajinga waliwao” uk 34
Dunia mviringo
Methali
Maziwa yaliyomwagika hayazoleki
“Mtoto akililia wembe mpe” uk 33.
Afichaye ugonjwa ndiye hufa
Paka akitoka panya hutawala
Waswahili hujuana kwa viremba
Milima haikutani lakini binadamu hukutana
Ulimwengu hauna mwema
Ukishikwa shikamana
Nahau
Mdomo wa simba
“Unamvika kilemba cha ukoka” uk 126.
Matumizi ya lugha za kigeni
“You are too optimistic about life.”
Lugha ya matusi
Katika baadhi ya maeneo mwandishi amekosa tafsida. Tunayaona matumizi ya lugha kali kama inavyonukuliwa,
“Vijitako hivi vikavu ndivyo vyakuletea nyege!”
Matumizi ya lugha ya picha
Mji wa Dennis ukaonekana kwa taa ya kijani.
Matumizi ya taswira
Tumaini anawakilisha ubepari. Anafanya kazi kwa bidii, anaajiri watu wengi anaowalipa na anaonekana kuwa mnyonyaji kama ulivyo mfumo wa ubepari.
Mkuu wa wilaya anawakilisha ujamaa. Mfumo ambao unatenda haki kwa wote, mfumo ambao hauna unyonyaji ndani yake.
Maoni ya mhakiki kuhusu kufaulu na kutofaulu kwa mwandishi
Kufaulu
Kezilahabi amefaulu kueleza upande wa pili wa sera ya ujamaa. Katika wakati wake, vitabu vingi viliandikwa vikisifu ujamaa, yeye alikuja na mtazamo wa kweli uliobeba hisia za upande wa pili kuhusu ujamaa.
Amefaulu kuwaeleza watu namna ujamaa ulivyohusika kwa namna moja ama nyingine kupora haki za wanyonge.
Lakini anafaulu zaidi kwani miaka kumi baada ya kuandikwa kitabu hiki, ujamaa ulikufa, hii inathibitisha kuwa, Kezilahabi aliona kwa usahihi zaidi.
Katika matumizi ya fani, mwandishi ameitendea haki lugha. Ndani ya riwaya utakutana na utajiri wa kutosha wa tamathali za semi, misemo, nahau, ujenzi wa picha na taswira na mengine mengi.
Amefanikiwa vyema kujenga mandhari yake, mandhari haya, yameionyesha kama ilivyo jamii yake, ni kitabu chenye uhalisia wa kutosha.
Kutokufaulu
Mwandishi ameegemea upande mmoja tu. Yeye anaonesha mabaya ya ujamaa, haelezi jema walao moja la vijiji vya ujamaa.
Falsafa ya mwandishi kuhusu dunia nayo imepotoka. Anaamini kwamba Dunia ni uwanja wa fujo, suala hili si kweli. Wakosoaji wakubwa wa Kezilahabi husema kuwa, Kezilahabi amekata tamaa ya maisha. Hata hivyo, Kezilahabi mwenyewe hupinga jambo hilo kwa kusema kuwa, maana ya maisha imo katika kuutafuta ukweli.
Mwandishi anaonesha ushirikina kuwa kitu halisi, hili ni kosa kubwa. Katika riwaya yake, anaaminisha wasomaji kuwa, Mugala aliwabadili mama yake Tumaini na baba yake kuwa vizuu. Habari hizi zinapotosha watu. Ukweli ni kwamba, hakuna mtu mwenye uwezo wa kumfanya mwingine kizuu.
Habari za kuzika mgomba huku mtu halisi akichukuliwa si za kweli na ni jambo la hatari mno kuzungumzwa katika fasihi. Wasomaji wa riwaya hii huenda wakachotwa na uongo huu na kujikuta wakiamini habari hizi za vizuu. Hakuna vizuu, hakuna misukule, ukifa umekufa!
Hata hivyo, nje ya changamoto hizo, Dunia uwanja wa fujo, kinasalia kuwa miongoni wa vitabu bora sana vya fasihi.
Wasiliana na Mwalimu ili Kujiunga Darasa la Uhakiki wa Vitabu vyote vya Fasihi Mtaala Mpya kwa Kugusa Hapa
