Uhakiki wa Tamthiliya ya Ngoswe Penzi Kitovu cha Uzembe

Uhakiki wa Tamthiliya ya Ngoswe Penzi Kitovu cha Uzembe

JINA LA KITABU: NGOSWE PENZI KITOVU CHA UZEMBE

MWANDISHI: EDWIN SEMZABA

Mhakiki: Mwalimu Makoba

Utangulizi

Afisa aliyetumwa kuhesabu watu-Ngoswe, anashindwa kuifanya kazi yake na kuanzisha ajenda nyingine ya mapenzi. Anapanga kutoroka na binti Mazoea aliyekwisha kuposwa tayari, Mazoea naye kusikia atakwenda kuishi mjini anakubaliana na mpango huo.
Wanapotoroka, Ngoswe anasahau mkoba wenye takwimu za watu waliokwisha kuhesabiwa, Mzee Ngengemkeni Mitomingi ambaye ndiye baba yake na Mazoea, anazichoma moto takwimu hizo na kumsababishia hasara kubwa Ngoswe.

Jina la Kitabu

Jina la kitabu “Ngoswe penzi kitovu cha uzembe” ni jina ambalo limesawiri vyema yaliyomo ndani ya kitabu hicho, kwani Ngoswe ndio jina la mhusika mkuu anayebeba dhamira kuu ya tamthiliya. Pia penzi limeonekana kuwa ni kitovu cha uzembe kwani ndio yaliyopelekea kuteketezwa kwa karatasi za takwimu za sensa. Hivyo jina la kitabu si tu kwamba limesawiri yaliyomo katika kitabu bali pia katika jamii.

Maudhui

Dhamira

1. Mapenzi

Mapenzi yametajwa kuharibu kazi katika tamthiliya hii. Ngoswe anampenda msichana Mazoea na kuamua kutoroka naye, baba yake Mazoea kwa hasira anachoma moto makaratasi ya sensa na kusababisha hasara kubwa.

2. Ulevi

Ulevi nao umeonekana kuwa chanzo cha uharibifu wa kazi. Wanakijiji wengo wanapofuatwa ili wahesabiwe, hawapo majumbani mwao, wapo katika pombe na hii inasabisha zoezi la kuhesabu watu liwe gumu.
Pia, Ngoswe na mwenyeji wake Ngengemkeni Mitomingi walikunywa pombe ya mnazi na kuharibu baadhi ya makaratasi ya sensa.

3. Suala la elimu

Jamii ya Mzee Mitomingi haikuzingatia elimu kwa watu wake. Watoto wengi hawakwenda shule kwa madai kuwa, shule zilijengwa mbali na makazi ya watu. Suala hili linadumaza na kukwamisha maendeleo ya muhimu kwa wanajamii.

4. Ndoa za mitara

Ngengemkeni ana wake wawili: Mama Mainda na Mama Mazoea. Kuoa kwake wake wawili, kunamfanya awe na familia kubwa ambayo huenda ndiyo sababu ya yeye kushindwa kutoa huduma stahiki hata kusababisha binti yake alaghaiwe kwa urahisi.
Pia, inatia shaka kama kweli Mitomingi aliwapenda wake zake wote kwa upendo wa kipimo sawa.

5. Imani za kishirikina

Wanakijiji wanaamini katika ushirikina na mambo yasiyofaa. Mama anakataa kuhesabiwa kwa madai kuwa, anayefanya hivyo ni mchawi na lengo lake ni kuwahesabu watu ili baadaye awaroge. Upuuzi huu unaonesha kazi ngumu ya kutoa elimu vijijini na wakati mwingine hata mjini ili kuleta ujenzi wa jamii mpya.

6. Nafasi ya mwanamke katika jamii

Tamthiliya ya Ngoswe inamchora mwanamke katika vipengele mbalimbali. Vipengele hivyo ni:

- Chombo cha Starehe:

Kijiji cha Ngengemkeni inaonekana kuwatumia wanawake katika starehe. Dhana hii inathibitishwa na tabia ya kuoa mitara kila mara; ili wanawake watumike kukidhi haja ya wanaume.

- Mama Mzazi na mlezi wa familia:

Wanaonekana wanajishughulisha na kazi za malezi baada ya kuzaa.

- Duni na asiye na mchango katika maisha:

Mwanamke anadharauliwa na wanaume na kumfananisha akili zake na mtoto. Mwanamke haelekei kuthaminiwa na kufikiriwa kuwa anaweza kuchangia jambo lolote la maana. Wakati Mazoea anatoroshwa na Ngoswe. Mitomingi anauliza:

MITOMINGI:

(...) Hivyo na nyie hamkuona dalili zozote juu ya watu hawa wawili.
MAMAMAZOEA: Zilikuwepo.
MITOMINGI: Kumbe mliziona na mkanyamaza tu!
MAMAINDA: Sasa Baba mazoea tungefanya nini?
MITOMINGl: Mngefanya nini? Nyie wanawake akili zenu wote sawa. Si Mazoea, si mama yake. (...) (uk. 26)
Kauli hii inaonyesha kuwa Mitomingi hawezi kumthamini mke wake kwa sababu hana akili za kikubwa - ni kama za mtoto wake Mazoea! Tabia ya Mitomingi ni ya wanaume wengi - jambo ambalo lazima lipigwe vita.

- Mwenye tamaa na maisha mazuri

Mazoea anatamani kuishi maisha mazuri ya mjini ndiyo sababu ya yeye kukubali kutoroshwa na Ngoswe.

Ujumbe

1. Tusiendekeze mapenzi kiasi cha kuharibu kazi

Ngoswe anaharibu kazi kwa sababu ya kuendekeza mapenzi.

2. Ulevi ni chanzo cha uharibifu wa kazi

Ngoswe na Mzee Mitomingi ni walevi, kazi zao zinasuasua. Pia, wanakijiji nao hawapatikani majumbani mwao kwa sababu muda mwingi wanautumia kuwa katika vilabu vya pombe.

3. Elimu itolewe maeneo yote, mjini na vijijini ili kufuta ujinga

Kijiji cha Mzee Mitomingi watu wake hawana elimu ya kutosha. Watoto wengi hawaendi shule kwa sababu shule ziko mbali na makazi yao.

4. Imani za kishirikina zinarudisha nyuma maendeleo ya jamii

Kuamini katika ushirikina kunasababisha zoezi la sensa liwe gumu hasa pale Mama anapokataa kuhesabiwa kwa madai kuwa, anayefanya hivyo ana mpango wa kuwaroga watu.

Migogoro

Migogoro ya wahusika

Ngoswe na Mitomingi

Mgogoro huu unasababishwa na Ngoswe kutoroka na Mazoea. Mitomingi anaamua kuyachana makaratasi ya sensa.

Mitomingi na wake zake

Mgogoro huu unasababishwa na kitendo cha kutoroshwa kwa Mazoea na Ngoswe. Ana hoji kwa nini wake zake hawakutoa taarifa mapema ikiwa dalili waliziona.

Mama na Ngoswe

Mgogoro huu unasababishwa na Ngoswe kutaka kumhesabu Mama. Anakata kwa madai kuwa, anayefanya hivyo ni mchawi.

Kifaruhende na Mitomingi

Mitomingi anamlaumu Kifaruhende kwa kitendo chake cha kutokuwa nyumbani wakati alipewa taarifa kuwa, zoezi la uhesabuji watu linaendelea.

Migogoro ya nafsi

Mgogoro huu unampata Mazoea pale anapotongozwa na Ngoswe. Anawaza akubali au akatae hasa ukizingatia tayari alikuwa amechumbiwa na mwanamume mwingine. Mazoea, anaamua kukubali kuwa na Ngoswe na kuongozana naye mpaka mjini.
Pia, mgogoro wa nafsi unampata Ngoswe baada ya makaratasi ya sensa kuchomwa moto. Anawaza ataieleza nini serikali iliyomtuma. Vipi hatma ya ya kazi yake ukweli ukijulikana?

Falsafa

Mwandishi anaamini kuwa, mapenzi yakizidi huleta hasara.

Msimamo

Mwandishi ana msimamo wa kimapinduzi kwa sababu anaamini kuwa, mapenzi yakizidi sana ni hasara. Katika matatizo makubwa yasababishwa na mikasa ya mapenzi, mwandishi ana shauri watu wapende kwa kiasi na kamwe wasichanganye mapenzi na kazi.

Fani

Mtindo

Dayolojia

Mtindo huu wa majibizano umetumiwa kwa kiasi kikubwa. Wahusika wengi wanajibizana.

Monolojia

Kwa kiasi kidogo mtindo huu wa masimulizi umetumika ili kufafanua zaidi vitendo vinavyofanywa na wahusika.

Matumizi ya nafsi

Nafsi zote tatu zimetumika. Hata hivyo, matumizi ya nafsi ya kwanza yametawala.

Muundo

Tamthiliya hii imetumia muundo wa moja kwa moja. Inaanza kwa kumuonesha Ngoswe akiwa katika kijiji cha Mzee Mitomingi, akianza kazi zake, akitoroka na Mazoea na mwisho karatasi za sensa zikichomwa moto.
Pia, matukio haya yamepangwa katika maonyesho matano.

Wahusika

Ngoswe

- Kijana anayeaminiwa na serikali kwenda kuhesabu watu
- Ni mlevi
- Anaendekeza mapenzi na kujikuta akiharibu kazi

Mazoea

- Mtoto wa kike wa Mzee Mitomingi
- Hana elimu
- Ana tamaa. Pamoja na kuwa alikuwa tayari kaposwa, alimua kuwa na Ngoswe.

Ngengemkeni Mitomingi

- Ni balozi katika kijiji chake
- Ana wake wawili
- Baba yake Mazoea
- Ana hasira sana. Hili linathibitika pale anapochoma moto makaratasi ya sensa.

Mzee Jimbi

- Hana elimu
- Ni mlevi
- Hajui umri wake
Mama Inda na Mama Mazoea
- Wake zake Mitomingi
- Hawana nafasi ya kufanya maamuzi

Mandhari

Mandhari ya tamthiliya hii imechorwa katika mazingira ya kijijini. Maeneo mbalimbali yanaonekana kama: shambani, katika vilabu vya pombe, chumbani, kisimani, nyumbani n.k.

Matumizi ya lugha

Matumizi ya semi (Nahau, misemo na methali)

Methali

Uk.22 “Penye nia pana njia”.
Uk.27 “Waona vyaelea vyaundwa.”

Misemo

Uk.14 “Akuwaniae uovu haji kweupe”

Nahau

Uk.11 “hebu keti tutupe mawe pangoni” – tule chakula
Uk.7 “mbongo zimelala”- ana maarifa
Uk.14 “pombe na yeye ni pete na chanda”- anapenda pombe sana.

Matumizi ya tamathali za semi

Tafsida

Uk.21 “Wala hajarudi, kama ingekuwa ni kujisaidia si angekuwa amekwishamaliza?”
Tashibiha
Uk.1 “vumbi jekundu kama ugoro wa subiana”
Uk.8 “sarawili yake miguuni kama kengele ya bomani”

Mubaalagha

Mama mazoea : “Kujibu swali ndio ukachukua mwaka mzima!”

Mbinu nyingine za kisanaa

Mdokezo

Uk.22 Mazoea : “sijui… siwezi… namuogopa baba”
Uk.16 Ngoswe : “huyo mtoto wenu wa kwanza anaishi hapa au…..”

Takriri

Uk.9 “Mama Masikio! We Mama Masikio!”
Uk.13. “Hodi! Hodi!”
Uk.2 “karibu karibu”
Tashtiti
Uk.5 Ngoswe: “hivyo waitwa nani?”
Mazoea: “mie?”
Hapa wahusika waliuliza maswali ambayo majibu yake waliyaelewa ila kutokana na kutaka kudhihirisha hasira, msisitizo nk. Ndio maana wametumia tashtiti.      

Ujenzi wa taswira

Mwandishi anaeleza matukio na kuwafanya watu wawe kama wanaona kitu katika luninga, usomapo kazi hii, utakuwa kama unaona vitu fulani ubongoni. Tazama mfano huu,
Mazoea aingia ndani huku macho ya Ngoswe yakiwa mgongoni kwake. Atikisa kichwa, na mara hiyohiyo Mitomingi na wazee wawili wanaingia.

Kufaulu kwa Mwandishi

Mwandishi amefaulu kuonyesha athari za mapenzi endapo yataendekezwa kupita kiasi.

Kutofaulu kwa Mwandishi

Mwandishi hajaonyesha faida za mapenzi. Yeye kaegemea katika hasara pekee, jambo hili si kweli kwani kwa kiasi fulani mapenzi yana faida zake ambazo hazijatajwa na mwandishi.

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Uhakiki wa Tamthiliya ya Kilio Chetu