Uhakiki wa Wimbo Baba wa Stamina Akimshirikisha Profesa Jay

Baba na mtoto wanazungumza

Swali

Kwa kutumia wimbo wa BABA ulioimbwa na Stamina akimshirikisha Profesa J, fanya uhakiki wa muziki huo ukizingatia vipengele vya Fani na Maudhui huku ukionyesha mifano ya maneno yaliyotumika katika wimbo kumdhalilisha mwanaume.

Jibu

Wimbo Baba ulioimbwa na mwanamuziki Stamina akimshirikisha Profesa Jay na One Six, ulitoka mwaka 2021 mwezi Januari. Mwezi uliofuata, mwezi Februari, marehemu na aliyekuwa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Joseph Magufuli, alitinga katika studio za TBC na kuomba apigiwe wimbo huo. Kitendo hicho kiliufanya wimbo huo uzidi kupata umaarufu zaidi ya ulivyokuwa na pengine kuwafikia watu wengi zaidi.

Baba ni wimbo wenye majibizano ya pande mbili: mtoto na baba yake. Mtoto anamlaumu baba kuwa, yeye ndiye sababu ya maisha ya mtoto kuwa mabaya. Baba naye anazikataa lawama hizo kwa kusema kuwa maisha magumu anayopitia mtoto huyo kayasababisha mtoto mwenyewe. Katika wimbo huu, tutachambua vipengele vya fani na maudhui halafu tutaeleza mifano ya maneno yaliyotumika katika wimbo huu ambayo yanamdharirisha mwanaume.

Wamitila (2003) anaeleza fani kama dhana inayotumika kuelezea muundo. Maana hii inaweza kukamilishwa kwa kusema kuwa, fani ni umbo la nje la kazi ya fasihi au mbinu anazotumia mwandishi au msanii kufikisha maudhui.

Kwa ujumla, fani ni mbinu anayoitumia mwandishi au msanii ili kufikisha ujumbe kwa watu aliowakusudia/hadhira. Fani inabebwa na vipengele vingi kama: muundo, mtindo, mandhari, wahusika na matumizi ya lugha.

Tunaanza na uhakiki wa vipengele vya fani katika wimbo huu:

Wahusika ni kipengele cha fani ambacho kimejitokeza katika wimbo. Wahusika waliojitokeza katika wimbo huu ni:

-      Mtoto ni mhusika ambaye anaanza kuzungumza katika wimbo. Anasikika akisema,

“Hivi unajua nimekuvumilia Sana

Angekuwa mtoto mwingine tayari ungeshampa laana…”

Maneno hayo yanamdhalilisha baba, mtoto kumwambia baba yake kuwa nimekuvumilia sana ni ukosefu wa nidhamu na adabu. Pia, kauli hiyo inalenga kueleza kwamba, Baba amekuwa akifanya makosa mengi ambayo yanavumiliwa na mwanaye.

-      Mhusika mwingine ni Mama. Mhusika huyu tunamfahamu pale anapodokezwa na mtoto,

“Mama anasema mwanzo mimba ulikataa…”

Maneno hapo juu yanamdhalilisha Baba kwa mara nyingine. Kumbe Baba alikataa mimba na hili si jambo zuri.

-      Baba ni mhusika anayeonekana katika wimbo huu. Baada ya kushambuliwa kwa maneno makali ya mtoto wake, baba anasikika akijibu,

“Mwanangu nimekusikia nakuombea kua uyaone,

Nilijua umekuja kwangu kuniombea ili nipone,

Kumbe umekuja kwa shari, kunilaumu na kunihukumu

Inaonyesha ningesinzia ungeninywesha hata sumu…”

Maneno haya yanamdhalili mwanaume. Mtoto anadhalilishwa kwa kuambiwa kwamba angemnywesha sumu baba yake. Hii inaonyesha kuwa mtoto ni muuaji tena hafai. Inaonyesha waziwazi kuwa, Baba hamwamini mtoto wake.

Kipengele kingine cha fani kilichojitokeza ni mtindo. Wimbo huu upo katika mtindo wa kisasa. Japo kuna vina, hakuna mizani inayoonekana na hii inapelekea kazi hii ikae upande wa kazi zenye mtindo wa kisasa.

Kipengele kingine cha fani ni mandhari. Yanaonekana mandhari ya nyumbani. Hapa ndipo majibizano ya baba na mtoto yanafanyika. Mandhari haya ni nyumbani kwao mtoto. Baba anasikika akilalamika,

“Mwanangu nimekusikia nakuombea kua uyaone,

Nilijua umekuja kwangu kuniombea ili nipone,

Kumbe umekuja kwa shari, kunilaumu na kunihukumu…”

Haya ni mandhari halisi yanayoeleweka kwa urahisi na kuifanya kazi hii iwe na uhalisia kwa kuendana na jamii.

Kipengele kingine cha fani ni matumizi ya lugha. Wimbo huu umetumia lugha rahisi inayoeleweka vizuri. Baadhi ya vipengele vya matumizi ya lugha vinavyoonekana ni pamoja na:

-      Matumizi ya tafsida, msanii ametumia tafsida ‘kinga’ badala ya kondomu ili kupunguza ukali wa maneno.

Mtoto anamdhalilisha Baba yake kwa kiwango cha juu. Si tabia njema kwa mtoto kumuuliza baba swali baya kama hili, “Halafu, hivi hauzijui kinga, au hukujua peku peku kama italeta mimba…” mtoto amekosa adabu kwa kiwango kikubwa na hii inamdhalilisha Baba.

-      Matumizi ya nidaa, msanii anashangazwa na jambo pale anaposema, “Elimu siku hizi ni bure, ila cha ajabu umeshindwa hata kunipeleka shule.”

Kauli hiyo inamdhalilisha Baba. Inaonyesha kwamba, Baba hajielewi, pamoja na elimu kuwa bure, lakini bado kashindwa kumpeleka mtoto wake shule.

-      Matumizi ya msemo, “kua uyaone”, baba anamwambia mwanae msemo huo ili kujitetea kuwa, pengine mtoto asidhani maisha ni kitu rahisi tu kama anavyofikiria.

Sambamba na hayo, sasa tuangazie vipengele vya maudhui:

Dhamira zimeonekana katika wimbo huu. Baadhi ya dhamira hizo ni:

-      Umuhimu wa elimu. Kwa vyovyote vile matatizo haya yanasababishwa kwa sababu ya kukosa elimu. Mzazi alijitahidi kumsomesha mtoto kama anavyolalamika, lakini mtoto alikaidi shule.

Mzazi anasema, “Niliuza mali zangu ilimradi wewe usome…”

-       hata hivyo mtoto analalamika kwa nini hakupelekwa shule. jambo ambalo linaleta mkanganyiko juu ya ni upi hasa ukweli.

Mtoto anasema, “Elimu siku hizi ni bure ila Cha ajabu umeshindwa hata kunipeleka shule…”

Baba alimpeleka mtoto shule kama anavyosema, au mtoto hakupelekwa shule kama anavyolalamika? Hata hivyo, wote tunakubaliana kwa pamoja kuwa, mtoto hana elimu.

Dhamira nyingine ni malezi ya watoto. Mtoto anaonekana amelelewa vibaya na wazazi wake ndiyo sababu anamtukana na kumdhalilisha baba yake bila aibu wala uonga. Hivyo basi, wazazi wajitahidi katika malezi ya watoto wao kwani, samaki mkunje angali mbichi na mtoto umleavyo ndivyo akuavyo.

Ujumbe unaopatikana katika wimbo huu ni, jamii ipewe elimu ya malezi ya watoto ili kujenga taifa bora. Malezi ya watoto ndiyo kila kitu na endapo wana jamii watayumba katika hili, basi matatizo makubwa yatatokea. Kwa mfano, katika jamii yetu kipo kikundi cha watoto wadogo wafanyao vitendo vya uharifu maarufu kama ‘Panya road” watoto hawa ni matokeo ya malezi mabaya.

Migogoro nayo imejitokeza katika wimbo huu. Tunaona mgogoro wa baba na mtoto. Mtoto anamlalamikia baba yake kwa nini hakumpeleka shule, na baba anamkumbusha mtoto kwamba aliuza vitu vyake ili amsomeshe. Mgogoro wao unasababishwa na ukosefu wa elimu pamoja na umasikini uliokithiri ambao ndilo limekuwa tatizo kubwa kwa watanzania wengi.

Tumeona vipengele vya fani na maudhui, na ndani yake tumegusia baadhi ya maneno yanayomdhalilisha mwanaume. Sasa tumalize kwa kuangalia maneno yaliyosalia ambayo nayo yanamdhalilisha mwanaume:

“Usingemrubuni mama labda angemuoa bakhresa…” ni maneno ambayo yanamdhalilisha mwanaume. Baba anadhalilishwa kuwa pengine hakuwa na hadhi ya kuwa na mama yake mtoto.

“Au ma-nurse walichanganya babangu haukuwa ni wewe…” maneno haya yanamdhalilisha Baba kwa kuonyesha labda hakuwa na uwezo wa kuwa na mtoto kama yule na hapo tu, amesingiziwa.

Mbona mzee mushi namwona anahela

“Mzee mwakalinga mwenzio anahela, Mzee luta sho ndio kabisa anamihela, Wewe ulikuwa wapi mpaka unakufa kabwela…” Baba anadhalilishwa kwa umasikini wake, mbaya zaidi anafananaishwa na wazee wenzake waliofanikiwa. Jambo hili linamuumiza Baba ambaye hata hivyo ni mgonjwa.

Kwa kuhitimisha, nyimbo nyingi za kizazi kipya zina mwelekeo wa mapenzi na burudani. Baba ni miongoni mwa nyimbo chache ambazo hazina muelekeo wa mapenzi na umejikita katika uhalisia wa mambo ya msingi yanayotokea katika jamii. Haina maana kwamba mapenzi si kitu cha msingi, lakini hayapaswi kupewa kipaumbele kikubwa kupita mambo mengine. Baba utaendelea kuwa wimbo mzuri wenye mafunzo lukuki.

Marejeleo

Mwamanda, J. (2008) Nadharia ya Fasihi Uchambuzi na Uhakiki. JPD           Company & General   Supplies Ltd: Da es Salaam.

Stamina na Professor Jay na One Six. (2021) Baba. Inapatikana katika         https://www.youtube.com/watch?v=_cim7dsia6Q. Ilisikilizwa tarehe    21 Julai 2022.

Unahitaji Kufanyiwa Swali Lako? Wasiliana na Mwalimu kwa Kugusa Hapa

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Uhakiki wa Tamthiliya ya Kilio Chetu