Uhakiki wa Kazi za Fasihi Simulizi | Kidato cha Pili

Kitabu kikiwa kimefunuliwa kurasa.
Uhakiki wa kazi za fasihi simulizi huzingatia fani na maudhui ili kuchambua yale yaliyokusudiwa.

Uhakiki wa ushairi

Mashairi kama kazi nyingine za kifasihi huhakikiwa kwa kutumia vigezo sawa na vinavyotumika katika kazi nyingine za kifasihi. Vigezo hivyo ni kwa kuzingatia vipengele vyake viwili yaani fani na maudhui.

Vipengele vya Fani na Maudhui katika Kuhakiki Ushairi

Vipengele vya fani
Uhakiki wa fani za ushairi ni uchambuzi wa kina na kuziweka wazi mbinu za kisanaa alizotumia mshairi katika kutunga kazi yake. Vipengele muhimu vya kuhakiki katika fani ya ushairi ni kama vifuatavyo:

1. Mtindo

Jambo la kuonyesha hapa ni kwamba iwapo shairi ni la kimapokeo ama ni la kisasa.

2. Muundo

Katika kuhakiki muundo wa shairi mhakiki inatakiwa aweke wazi mambo yafutayo:
Idadi ya beti
Idadi ya mistari na aina ya vibwagizo
Idadi ya vipande
Idadi ya mizani
Aina na mpangilio wa vina

3. Wahusika

Ikiwa shairi limehusisha wahusika ni vema pia mhakiki awabainishe

4. Matumizi ya lugha

Katika kipengele hiki mhakiki huchunguza:
Mpangilio wa maneno. Mfano Wengi wari badala ya wari wengi
Matumizi ya : Mazida – kurefusha neno mfano, kibirika badala ya birika;
Ikisari – kufupisha neno mfano siombe badala ya usiombe;
Tabdila – kubadilisha mwendelezo wa neno mfano kujitanuwa badala ya kujitanua.
Matumizi ya methali, misemo na nahau
Matumizi ya lugha ya picha
Matumizi ya tamathali za semi kama vile takriri, sitiari n.k
Mbinu nyingine za kisanaa
Mhakiki anapochunguza vipengele vya fani, jambo muhimu la kuzingatia ni jinsi vipengele hivyo vinavyosaidia kuwasilisha maudhui.

Vipengele vya maudhui
Ili kuhakiki na kupata maudhui ya shairi inatakiwa kulisoma shairi kwa kulielewa zaidi. Baada ya kupata picha fulani kuhusu shairi na kutafakari maana za maneno muhimu, itatubidi tuelewe vipengele vya maudhui, ambavyo ni dhamira, mtazamo, msimamo, falsafa ya mwandishi, ujumbe na maadili, migogoro na muktadha.

Uhakiki wa maigizo

Igizo huhakikiwa kwa namna lilivyo katika maumbo yake yote mawili yaani fani na maudhui.

Vipengele vya Fani na Maudhui katika Kuhakiki Maigizo

Fani
Uhakiki wa fani katika maigizo unajihusisha na ufundi uliotumiwa. Ufundi huu unajumuisha mambo kadhaa kama ifuatavyo:

Mtindo

Mtindo ni sura ya maigizo inayojitokeza kupitia mpangilio wa maneno na vitendo. Inabidi mhakiki achunguze kama kazi ni:
Mchezo wa jukwaani – wenye mpangilio wa mazungumzo baina ya watu na matendo yao.

Majigambo

Vichekesho – mpangilio wa maneno yanayowasilisha ujumbe kwa kuchekesha.
Mazungumzo – maongezi ya kujibizana baina ya watu.
Ngonjera – mpangilio wa tungo za kishairi ambapo watu wawili au makundi mawili hukinzana.
Miviga – sherehe za kitamaduni kama vile matambiko
Pamoja na haya, mtindo hutegemea lengo la maigizo ambalo laweza kuwa kuelimisha, kukejeli, kuburudisha, kuonya, kukosoa na kadhalika.

Mandhari

Mazingira ya kutendea ni kipengele muhimu cha fani. Mhakiki hana budi kujiuliza iwapo utendaji unadhihirisha wakati au mahali halisi. Jambo hili huweza kutekelezwa kupitia vifaa, maleba, maneno n.k.

Wahusika

Maswali ya mhakiki kuuliza ni:
Wamejitokeza kikamilifu?
Wanaaminika?
Matumizi ya lugha
Vigezo anavyotumia mhakiki kuchunguza lugha ni:
Kama usemaji ni wa kisanaa, yaani unatumia picha, tamathali za semi, methali, nahau n.k.
Kama lugha imetumika vile inavyotumiwa katika jamii. Mfano: kiimbo, mkazo, miguno, vihisishi n.k.
Matumizi ya maneno ya ajabu kama yale yanayotumiwa na waganga.

Maleba na vifaa

Hivi huakisi mandhari na husaidia kuzua muktadha. Kwa hiyo ni muhimu kuchunguza kama vimetumiwa ipasavyo.
Matumizi ya ala
Matumizi ya ala kama ngoma, baragumu, au sauti zingine ili kuamsha hisia za hadhira ni jambo muhimu kuchunguza.
Mbinu nyingine
Mhakiki anapaswa pia kuchunguza matumizi ya nyimbo, uchezaji ngoma, usimulizi na mbinu nyingine katika kuibua hisia za watazamaji.
Maudhui
Kwa upande wa maudhui, mhakiki wa maudhui hutakiwa kuchunguza vipengele vyote vya kimaudhui ambavyo ni dhamira, migogoro, maadili, mtazamo na msimamo wa fanani pamoja na ujumbe bila kusahau kipengele cha falsafa. Yote hayo kwa pamoja ndiyo humsaidia mhakiki kubaini ukinzani wa igizo na maisha halisi ya jamii ambayo huwa ndiyo hadhira ya igizo hilo.

Maswali

1. Soma shairi hili kisha hakiki fani na maudhui:

Mabingwa nawauliza, hali vipi duniani?
Utadhani miujiza, au ni kama utani,
Kweli ninaona giza, hayapiti akilini,
Maisha yanishangaza, yanavyokosa kanuni.

Maisha ya kidunia, kweli hayana kanuni,
Mengi tunashuhudia, hapahapa duniani,
Kila siku twasikia, au kuona machoni,
Makubwa kupindukia, na madogo yalo duni.

Kwa sifa twagawanyika, kaskazi na kusini,
Kwa jinsia nazo rika, toka juu hadi chini,
Yapo mengi matabaka, kimwili na akilini,
Maisha kama kichaka, tofauti ziko ndani.

(HRT Muzale)

2. Hakiki kazi hii ya maigizo:
Bodaboda: Habari yako dada. (Akisimamisha pikipiki yake.)
Msichana: Nzuri, shikamo!
Bodaboda: Aaaah, usinizeeshe binti, vipi, panda nikupeleke, mtoto mzuri kama malaika, haifai kutembea kwa mguu.
Msichana: Sitaki, niache nisome, ukiendelea kunifuata nakupigia kelele za mwizi.
Bodaboda: tobaa! Yamekuwa hayo tena. (Anawasha pikipiki yake na kuondoka.)

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024

Jinsi ya Kuandika Risala | Kiswahili Kidato Cha Nne