Uhakiki wa Riwaya ya Watoto wa Maman’tilie
MWANDISHI: EMMANUEL MBOGO
WACHAPISHAJI: HEKO PUBLISHERS
MWAKA: 2002
MHAKIKI: MWALIMU MAKOBA
Wasifu wa Mwandishi
Emmanuel Mbogo ni Profesa wa
drama na fasihi na amehudumu katika vyuo vikuu mbalimbali ikiwemo, Chuo Kikuu
cha Kenyatta Kenya na Chuo Kikuu Huria. Mbogo ni mwanafasihi mahiri sana katika
Afrika ya Mashariki.
Muhtasari wa Riwaya
Maman’tilie, mama mwenye watoto
wawili lakini wote wamefukuzwa shule kwa kukosa ada na sare. Anajitahidi hapa
na pale ili apate, lakini wapi? Pesa imegeuka nyoka inateleza kwenye nyasi.
Mumewe Mzee Lomolomo hana muda, yeye kila kukuchapo huelekea bunge la walevi
kunywa pombe tani yake. Akiwa huko hunywa na kurudi nyumbani akiwa mbwii!
Mwisho mwandishi anauliza swali gumu, ‘Nani anajali?’
Uchambuzi wa Fani na Maudhui
Maudhui Katika Riwaya ya Watoto wa Maman’tilie
Maudhui hujumuisha mawazo na
pengine mafunzo mbalimbali yaliyomsukuma mtunzi ama mwandishi wa kazi ya fasihi
akaandika kazi yake.
Dhamira
Dhamira ni lile wazo linalomfanya
mwandishi wa kazi ya fasihi aandike kazi yake. Katika riwaya hii, dhamira
nyingi zimejadiliwa kama:
Umasikini
Dhamira hii imetawala katika
riwaya. Asilimia kubwa ya wahusika ni watu wenye maisha ya dhiki na kazi za
kijungujiko. Umasikini wao unadhihirishwa na mitaa wanayoishi kama: Manzese,
Msufini, Tabata, Kisutu na Temeke. Maeneo haya ndiyo yaitwayo uswahilini leo
hii.
Zita na Pita wanafukuzwa shule
kwa sababu ya kukosa ada na sare (uk 1). Mamant’ilie naye anatumia maji ya
mwarobaini kutibu homa yake kwa sababu hana pesa ya kununulia dawa za
hospitali.
Ulevi
Unywaji wa pombe kupitiliza
huweza kusababisha madhara makubwa kwa mtumiaji. Mzee Lomolomo ni mlevi mzoefu,
kutokana na ulevi wake, anashindwa hata kuwalipia ada wanae ili waendelee na
shule. Ni ulevi huohuo unamfanya aishi maisha ya dhiki huku akishindwa kutoa
mchango kwa familia yake na taifa linalomtegemea. Mwisho Lomolomo anakufa kwa
sababu ya pombe.
Mwandishi anasema, “… Lomolomo
alikuwa lofa, mtu wa kazi za kijungujiko na vipesa vyake viliishia kwenye
pombe…” (uk 7).
Malezi ya watoto
Watoto wasipopata malezi
yanayostahili kutoka kwa wazazi wote wawili huwa ni rahisi kwao kujiingiza
katika mambo yasiyofaa.
Mwandishi anaonyesha aina tatu za
watoto. Kwanza kuna Zita na Pita. Hawa wana wazazi wote wawili lakini baba
hajishughulishi na malezi yao. Pia mama naye ametingwa na shughuli nyingi
katika genge lake la uuzaji wa chakula. Zita na Pita hawana malezi ya
kueleweka. Hali hii inamfanya Pita ajiingize katika biashara ya madawa ya
kulevya.
Pili, kuna Dan na Musa hawa
hawana baba, wanaishi na mama zao tu. Mama zao hawawajali wala kuwakemea kwa
chochote kibaya wanachofanya. Dan anajiingiza katika ujambazi na kupoteza
maisha. Musa anajiingiza katika biashara ya madawa ya kulevya na kuishia jela.
Tatu kuna Kurwa na Doto. Hawa
hawana wazazi kabisa. mwandishi anasema, “… walikuwa chokoraa namba moja,
kupigana kulala na njaa, kukamatwa na polisi… yalikuwa sehemu ya maisha yao…”
Doto anajiingiza katika ujambazi,
huko anauawa na mlinzi Simango.
Rushwa
Rushwa imeota mizizi katika
jamii. Kila uendako, kila upitako na kila utokako utaambiwa toa rushwa ili
upate kitu fulani.
Mamant’ilie alishindwa kuyamudu
maisha ya mjini kwa sababu ya rushwa aliyokuwa akiwapa askari wa jiji. Kwa
kalamu yake isiyoisha wino, Mbogo anaandika, “Kodi na hongo kwa askari wa jiji,
ziliikamua faida yake.” (uk 32).
Mmomonyoko wa Maadili na Kukosekana kwa Utu
Maadili ya siku hizi si yale ya
zamani. Miaka inabadilika na vizazi navyo vinabadilika. Watu ni watu tu lakini
hawana utu. Watoto wadogo sasa wanavuta sigara na kutafuna mirungi kama
tumuonavyo Dan na Musa. Watu hawana moyo wa kusaidiana tena, wao wanaamini kuwa
kila mwenye janga atalila peke yake. Zita anazidiwa na maradhi yaliyosababishwa
na kuumwa na mbwa mwenye kichaa. Watu hawakumsaidia, badala yake
walivishangilia vioja alivyovifanya. Mwandishi anatuonesha Zenabu akiwaomba
msaada na kuwakalipia, “Nisaidieni, mnacheka nini? Wendawazimu wakubwa.” (uk
82).
Nafasi ya Mwanamke Katika Jamii
Nafasi ya mwanamke ni jumla ya
matendo yote yafanywayo na mwanamke katika jamii yake. Mara nyingi huwa mabaya
na yenye mtazamo hasi, lakini mara chache huwa mazuri yenye mtazamo chanya.
Mwandishi wa riwaya hii, amemchora na kumjadili mwanamke kwa mawanda mapana
kama inavyoelezwa:
-
Mama
mlezi na mwangalizi mkuu wa familia. Maman’tilie ndiye aliyejua familia yake
ile nini, ifanye nini na iishi vipi. Mumewe mzee Lomolomo hakuwa na mchango
wowote. Yeye kila kukuchapo alikwenda kilingeni kufakamia mataputapu na pombe
haramu.
-
Mwenye
huruma na moyo wa kutoa msaada. Zenabu
anawakilisha tabia hii. Alimsaidia Pita alipokuwa na njaa. Ni yeye
akishirikiana na Mama sara walimpeleka Zita hospitali.
-
Mwenye
mapenzi na kazi. Kurwa anapenda kazi, alifuatana na Maman’tilie kwenda gengeni,
huko alimsaidia kuuza chakula. Hata siku moja kurwa hakuchoka kufanya kazi.
-
Aliyenyimwa
elimu. Zita ni mwanamke aliyenyimwa elimu. Anafukuzwa shule kwa kukosa ada na
sare.
-
Mzembe
na asiyejali malezi ya watoto. Mama Musa ni mzembe na hajali malezi ya mwanae.
Yeye ameshika themanini zake na Musa kashika hamsini zake.
Dhamira nyingine zilizojitokeza
ni:
Hatari ya ugonjwa wa Malaria
Elimu
Athari ya sayansi na teknolojia
Adha ya usafiri
Wizi na ujambazi
Ujumbe
Ujumbe ni funzo litolewalo na
kazi ya fasihi. Mafunzo mengi yametolewa katika riwaya hii:
i.
Watoto
wasifukuzwe shule kwa sababu ya kukosa ada, kwani kufanya hivyo kunawanyima
haki yao ya kupata elimu.
ii.
Majalala
ya kuchoma takataka yajengwe mbali na makazi ya watu. Mwandishi anasema,
“Mapafu ya wakazi yaliendelea kuteketea kwa moshi siku hadi siku… watu wale
walikuwa wanakufa taratibu.” (uk 27).
iii.
Pombe
si suluhisho la matatizo.
iv.
Mzaha
mzaha hutumbua usaha. Zita alikwaruzwa na mbwa mwenye kichaa, lakini
wakapuuzia, mwishi ni kifo cha Zita.
Migogoro
Migogoro ni kukosekana kwa
maelewano baina ya watu binafsi, jamii, taifa au mataifa. Migogoro
iliyojitokeza ni:
Migogoro ya wahusika
-
Mwalimu
Chikoya na wanafunzi wasiokuwa na ada wala sare za shule. Huu unasababishwa na
wanafunzi wasiokuwa na ada wala sare. Suluhisho lake ni wanafunzi hao kufukuzwa
shule.
-
Maman’tilie
na mzee Lomolomo. Huu unasababishwa na ulevi wa Lomolomo. Suluhisho ni kifo cha
mzee Lomolomo.
-
Peter
na Doto. Huu unasababishwa na Doto kumfukuza Pita jaani. Suluhisho la mgogoro
huu ni Kurwa kumsaidia Peter.
Mgogoro wa nafsi
-
Huu
unampata Peter, yeye anamawazo ya kurudi shule lakini hajui ni kipi afanye ili
apate pesa za kumrudisha.
Migogoro mingine ni: migogoro ya
kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni na kijamii.
Falsafa
Falsafa ni imani ya mwandishi.
Emmanuel Mbogo anaamini kuwasaidia watoto kupata elimu yao kutaondoa matatizo
yanayozuia ujenzi wa jamii mpya.
Mtazamo/Msimamo
Mwandishi anamsimamo wa
kimapinduzi. Anaamini kuwapatia watoto elimu na kusimamia malezi yao kutaliokoa
taifa.
Uchambuzi wa fani na vipengele vyake
Fani ni ule ufundi wa kisanaa
anaoutumia msanii katika kazi yake. Fani ndiyo hutupatia kile kiitwacho
maudhui. Katia riwaya hii, fani imechambuliwa kama ifuatavyo:
Wahusika
Wahusika ni watu au viumbe
waliokusudiwa uwakilisha tabia za watu katika kazi ya fasihi. Wahusika waliopo
katika riwaya hii ni:
-
Maman’tilie.
Ni mke wa mzee Lomolomo. Ni mchapakazi. Ni mama yao Zita na Peter na anafaa
kuigwa na jamii.
-
Lomolomo.
Ni mume wa Maman’tilie. Ni mlevi wa pombe haramu. Hawajibiki katika malezi ya
watoto wake na hafai kuigwa na jamii.
-
Zita.
Mtoto wa Maman’tilie na mzee Lomolomo. Alifukuzwa shule kwa kukosa ada na sare
akiwa darasa la sita. Pia, alikwaruzwa na mbwa mwenye kichaa. Mwisho anakufa
kwa kupuuzia ule mkwaruzo wa mbwa.
-
Peter.
Mtoto wa Mzee Lomolomo na Maman’tilie. Anafukuzwa shule akiwa darasa la tano.
Anatafuta ridhiki dampo. Baadaye anajiingiza katika biashara ya madawa ya
kulevya.
-
Chikoya.
Ni mwalimu mkuu wa shule ya msingi Makurumla. Anawafukuza wanafunzi wasiokuwa
na sare wala ada.
-
Musa.
Anafukuzwa shule kwa kukosa ada na sare. Hamheshimu mama yake. Anajiingiza
katika biashara ya madawa ya kulevya.
-
Sara.
Mwanafunzi wa Makurumla na ni jirani yao Zita.
-
Mama
Sara. Mama yake Sara. Alimsaidia Zita alipopatwa na kichaa.
-
Zenabu.
Anafanya kazi Kikale Bar. Ana huruma. Anafaa kuigwa.
-
Kurwa.
Ni yatima. Anaishi vichochoroni. Anategemea chakula cha dampo. Anasingiziwa
kujihusisha na biashara ya madawa ya kulevya.
-
Doto.
Ni yatima. Anauawa kwa kujihusisha na ujambazi.
-
Rhemtulah.
Ni mfanyabiashara wa kihindi.
-
Simango.
Ni mlinzi wa Rhemtulah. Anawaua Doto na Dan.
-
Dan.
Ni mtoto ambaye hamjui baba yake. Anauawa kwa kujihusisha na ujambazi.
-
Jane.
Aliwalea Doto na Kurwa baada ya kufiwa na mama yao. Naye pia anakufa.
-
Master
Baroni. Anawatumia watoto katika biashara yake ya madawa ya kulevya. Si mfano
wa kuigwa na jamii.
Matumizi ya Lugha
Fasihi ni sanaa itoayo maudhui
kwa kutumia lugha ya maneno ambayo hutamkwa au kuandiwa. Kipengele cha lugha ni
muhimu kwani ndicho kinachotofautisha fasihi na sanaa zingine.
Lugha iliyotumika katika riwaya
hii ni nyepesi na yenye kueleweka. Mwandishi ametumia vipengele vingi
vipatikanavyo katika matumizi ya lugha kama: ucheshi na lugha ya picha, misemo
na tamathali za semi.
Tamathali za Semi
Tamathali za semi ni maneno au
sentensi ambazo hutumiwa na wasanii wa fasihi ili kutia nguvu katika maana,
mtindo na hata sauti katika maandishi ama kusema. Wakati mwingine hutumiwa ili
kupamba na kuongeza utamu wa kazi za fasihi. Mwandishi ametumia tamathali
nyingi za semi kama:
-
Tanakali
sauti (onomatopoeia). Tanakali sauti ni maneno au nomino ziundwazo katika
sentensi kutokana na sauti zinazofanana.
“Bwee!”
“Paah!” (uk. 5)
-
Tashibiha.
Katika tamathali hii, watu ama vitu viwili au zaidi hulinganishwa na watu au
vitu vingine kwa kutumia maneno, ‘kama’, ‘mithili’…
“Masikio yamesimama wima kama anasisitiza kitu.” (uk.
2)
“Mdomo wake uliokaa kama bakuli la pombe.” (uk. 10)
-
Tafsida.
Hii hutumika kupunguza ukali wa maneno.
“Akaenda haja ndogo.” (uk. 2)
“Akakitibu kidonda chake kwa maji ya chumvichumvi.”
(uk 55)
-
Takriri.
Katika tamathali hii, maneno hurudiwarudiwa ili kuonyesha msisitizo.
“Yalaa! Yalaa!” (uk 2)
“Mjomba! Mjomba!”
-
Mdokezo.
Hapa msemaji husema kitu bila kukimalizia kukitaja.
“Shikamoo mama…” (uk 6)
“Una… una…” (uk 11)
-
Tashihisi.
Hapa vitu hupewa sifa alizonazo binadamu.
“Maman’tilie alimtupia jicho bintie.”
“Mabega yameangalia juu.” (uk 10).
-
Mjalizo.
Katika tamathali hii maneno hufuatana pasipo kiunganishi.
“Walikaa, wakala, wakanywa maji, wakamshukuru Mungu.”
-
Kejeli.
Hii ni tamathali ya semi ambayo maneno yake huwa kinyume na maana yanayotoa.
“Naye pita aliitikia salamu hizo za ukarimu kwa kupiga
chafya mbili au tatu.” (uk 19).
“Lomolomo uso wake uliopendeza kwa chang’aa…” (uk 70).
-
Sitiari.
Tamathali hii hulinganisha vitu bila kutumia viunganishi.
“Wakatembea mwendo wa farasi.” (uk 86).
-
Ritifaa.
Katika tamathali hii, mtu huongea na kitu ambacho husikika kwa fikra tu.
“Kumbe wewe na mwanao mna hila kiasi hiki? Mmepatana
kuondoka na kusafiri katika dau moja.” (uk 94).
-
Misemo.
“Ukienda Tabata utapata.”
“Waswahili hawana dogo.”
-
Matumizi
ya lugha za kigeni.
“Nikukonekti.” (uk 78).
-
Methali.
“Kamba hukatikia pembamba.”
-
Ucheshi
na lugha ya picha.
“Alikunywa funda moja, akajisikilizia kabla ya
kulimeza. Alisikia pombe ikisafiri kufuata barabara ya lami hadi tumboni.” (uk
87).
Mtindo
Mtindo ni ule upekee wa mtunzi
wakazi ya fasihi na mtunzi mwingine. Mfano, mwandishi anaweza kutumia, nyimbo,
mashairi, nafsi zote, dayolojia, monolojia n.k. mwandishi amefanikisha mtindo
wake kwa kutumia,
-
Matumizi
ya nyimbo. Mfano katika ukurasa wa 10 Lomolomo aliimba,
“Kuleni nae,
Hata bangi vuteni nae,
Lakini ni bure,
Mwenzenu nimezaa naye…”
-
Mwandishi
katumia monolojia (masimulizi) na dayolojia (majibishano).
-
Mwandishi
katumia nafsi zote tatu.
Muundo
Muundo ni mpango na mtiririko wa
kazi hiyo kwa upande wa visa na matukio.
Riwaya hii imetumia muundo wa
kurukia. Mwandishi amemuonyesha Lomolomo akiwa katika hali ya ulevi, baadaye
anatukumbusha alipokuwa anafanya kazi bandarini. Vilevile anawaonyesha Kurwa na
Doto wakiishi peke yao. Lakini baadaye anatukumbusha kipindi walipokuwa
wanalelewa na mama yao ambaye hata hivyo alifariki kisha wakalelewa na Jane
ambaye naye anafariki.
Mandhari
Mandhari ni sehemu ambayo kazi ya
fasihi hutendeka. Riwaya hii imetumia mandhari ya jiji la Dar es Salaam na
mitaa yake kama, Manzese, Msufini, Tabata, Kisutu, Urafiki na mtaa wa Ajentina.
Jina la Kitabu
Jina la kitabu, Watoto wa
Maman’tilie, linasadifu yaliyomo, kwani ndani ya riwaya hii kuna mhusika mkuu
ambaye ndiye Maman’tilie.
Riwaya hii inamwonesha mama huyu
akijaribu kujinasua yeye na watoto wake katika wimbi la umasikini, lakini wapi?
Jitihada zote anazofanya zinagonga mwamba na matatizo yake yanazidi kuongezeka.
Kufaulu na Kutofaulu kwa Mwandishi
Kufalulu Kimaudhui
-
Mwandishi
amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuonyesha shida wazipatazo watoto wa mitaani.
-
Mwandishi
amefanikiwa kuonyesha madhara ya umasikini.
-
Mwandishi
ameonyesha madhara ya unywaji wa pombe kupita kiasi na ulevi.
Kufaulu Kifani
-
Amekitendea
haki kipengele cha mtindo, kwani humo ametumia vipengele vingi kama nyimbo n.k.
-
Kazi
yake imeshibishwa kwa tamathali nyingi za semi.
-
Ametumia
lugha ya picha inayomwelewesha zaidi msomaji.
Kutofaulu kwa Mwandishi
-
Kimaudhui.
Mtazamo wa mwandishi katika suala la umasikini hauko sawa. Yeye anaamini hata
ukifanya kazi kwa bidii kama ni masikini utaendelea kuwa masikini kama
tumuonavyo Maman’tilie.
-
Kifani
wahusika wa mwandishi hawana uwiano. Wengi wao ni watu masikini.
-
Pia,
mandhari yote yaliyotumiwa na mwandishi ni ya mjini. Mwandishi ameutenga upande
wa kijijini ambao nao kama ungetazamwa, jamii ingejifunza mengi.