Uhakiki wa Riwaya ya Ua la Faraja

Ganda la Kitabu cha Ua la Faraja
Wasiliana na Mwalimu ili Kujiunga Darasa la Uhakiki wa Vitabu vyote vya Fasihi Mtaala Mpya kwa Kugusa Hapa

Mwandishi: W.E. Mkufya

Mwaka: 2004

Mhakiki: Mwalimu Makoba

Utangulizi

Profesa Madumla akiizungumzia riwaya ya Ua la Faraja alisikika akisema, “Mkufya anajua kuitumia lugha ya Kiswahili vilivyo… ni fundi wa ujenzi wa taharuki.”

Huwa sipendi kubishana na Profesa Madumla, lakini katika hili alidanganya. Haifahamiki kwa nini Madumla alidanganya, ila moja kati ya hoja hizi huenda ikawa kweli: pengine hakukisoma kitabu, na kama alikisoma, huenda kuna manufaa fulani aliyapata, kama hakuna kabisa manufaa yoyote, basi Madumla uzee umeanza kumwingia!

Mkufya ni Mwanasayansi aliyeivamia sanaa, sanaa ikamgaragaza vilivyo, Ua la Faraja ni Riwaya ndefu kama andiko la tafiti za Kisayansi, ina kurasa 423! Ni kama riwaya yake mwenyewe ilikuwa ikimdhihaki na kumweleza, “Sanaa ina wenyewe!”

Riwaya hii imekosa ujenzi wa taharuki, kila tukio linalofuata linatabirika na matukio mengine wala hayakupaswa kusimuliwa, japo riwaya hii ina kurasa 423, jibu la kisa halisi linapatikana katika ukurasa wa 20!

Hata hivyo tuweke akiba ya maneno, mbali na Mkufya kuandika riwaya isiyovutia sana kusoma hasa kwa kukosa ufundi na taharuki, Mkufya amekuwa bora sana katika ujenzi wa dhamira. Dhamira ya UKIMWI ameizungumzia kiundani sana, ni uwezo huu ulimuibua Saifu Kiango ambaye kwa sauti ya kujiamini alisikika akisema, “Katika riwaya zote zenye maudhui ya UKIMWI, hii ni ya aina yake…

Mkufya katika Ua la Faraja analo jambo ambalo ameliweza sana. Jambo hilo ni namna alivyoijadili falsafa ya maisha. Ameyajadili maisha katika namna ya pekee akiwafanya watu waendeleze mjadala huu ambao jibu lake bado halijapatikana.

Naye Privatus Karugendo akiwa ameishikilia riwaya hii ya  Ua la Faraja kauli ilimtoka anayetikisa miguu yake, “Nina imani watu watakaosoma Ua la Faraja Wataguswa na jambo moja ama jingine na watafarijika na hili ama lile.”

Mkufya ni mwandishi wa muda mrefu na ameandika vitabu vingi, amewahi kufanya kazi kama Mwanabiokemia, pia amefanya kazi kama Mhariri Mkuu katika shirika la uchapishaji la Mangrove Publishers jijini Dar es Salaam.

Simulizi kwa ufupi

Ngoma anaendekeza maisha ya anasa. Anafanya starehe za kila namna kama ulevi wa pombe na kujiburudisha na wanawake wa kila aina. Japo bwana huyu ni tajiri, nyumbani hatoi fedha hali inayomfanya mkewe Tabu afungue genge ili kukidhi mahitaji ya familia.

Ngoma kama lilivyo jina lake anaipata Ngoma. Inasemekana UKIMWI huo anaambukizwa na Queen, mwanamke msomi lakini malaya wa kutupwa.

Japo Tabu ni mwanamke mwema, anayemheshimu mume wake, asiyeendekeza starehe na ambaye unaweza kumuweka katika kundi la wanawake wenye tabia njema, analetewa UKIMWI na mumewe, Ngoma.

Baada ya kuambukizwa UKIMWI, ngoma anabadilika japo kwa kuchelewa. Anakuwa Mswalihina asiyekosa ibada msikitini. Siku ya kwanza Mashehe wanapomuona wanapiga ukelele wa furaha, “Allah kamleta Mja wake!”

Ngoma aliyekuwa ameitelekeza familia, anaanza kuijali kwa kutoa mahitaji ambayo hapo zamani hakuwahi kutoa. Anamhamashisha mtoto wake aitwaye Juma asikose ibada, hata hivyo Juma anamchukia Ngoma kwa sababu kamwambukiza Mama UKIMWI. Katika mzozo mkubwa Juma anaondoka nyumbani na kwenda kuishi kwa babu yake.

Baada ya Ushauri wa watu akiwemo mdogo wake, Grace, Tabu anakwenda kupima UKIMWI, Dkt Hans anampima na kumwambia ni kweli virusi vimeonekana!

Anarudi nyumbani akilalamika. Ngoma anamgeuzia kibao, “Kama umepimwa ukakutwa navyo, basi wewe ndiye uliyevileta!” Ngoma anaandika talaka na kumfukuza mke na watoto.

Ngoma anabaki akiugua peke yake ndani ya nyumba. Jirani yake, Omolo, anafika mara kwa mara kumsaidia hili na lile. Mwisho afya yake inadhorota. Anapelekwa hospitali, mke anapokuja kumuona, anamuomba msamaha na kufuta ile talaka aliyomuandikia. Ngoma anakufa kwa UKIMWI.

Mbali na mkasa huo, riwaya ya ua la faraja imejadili kwa kina falsafa na maana ya maisha. Mwishoni mwa kitabu, Mkufya anatuacha na swali gumu, “Ni kipi kisa cha walimwengu kuitwa waja?”

Maudhui

Maudhui yanayopatikana katika riwaya hii yanajadiliwa kupitia vipengele mbalimbali:

Dhamira

Dhamira mbalimbali tena zenye uhalisia na yale yanayoendelea katika jamii yetu zinajadiliwa:

Ugonjwa wa UKIMWI

Ugonjwa wa UKIMWI umejadiliwa kwa kina. Sababu mbalimbali zimetajwa kusababisha ugonjwa huu ikiwemo ulevi na kufanya ngono bila kutumia mpira. Kubwa kuliko yote ni kuendekeza ngono, ngono yenyewe ngono zembe.

Ngoma anaambukizwa UKIMWI kwa sababu alijihusisha na wanawake wengi. Alizoa mbegu kila mahali.

Asha Mmanyema naye anaambukizwa UKIMWI, yeye anaamini ameambukizwa na Ngoma. Anamlalamikia Ngoma lakini maji yakimwagika hayazoleki.

UKIMWI unatajwa kuwa wa ajabu, kwani hata wema waliotulia nyumbani wanaletewa gonjwa hili. Tabu anaambukizwa UKIMWI bila kujali kwamba yeye alikuwa mwenye maadili. Hapa ndipo tunaposhauriwa kwamba, kuwa na mpenzi mmoja siyo kinga, ila mpenzi mmoja aliyetulia.

Queen ndiye anayetajwa kumwambukiza UKIMWI Ngoma. Naye Ngoma akamwamwambukiza Mkewe, kisha Ngoma huyuhuyu akamwambukiza Asha na wengine wengi wakaambukizwa baada ya hapo.

Ulevi

Ngoma anaishi maisha ya ulevi. Haipiti siku bila kunywa pombe. Ni katika ulevi huu ndipo anapojiokotea wanawake wa kila aina. Lakini ni katika ulevi huu pesa nyingi zinatumika na kumfanya ashindwe kuhudumia familia yake japokuwa alikuwa na biashara ya magari ya abilia yaliyokuwa yakimwingizia pesa nyingi kila siku.

“Lete Safari kumi!” Ngoma aliagiza bia kwa kupaza sauti.

Ulevi huu unaleta maafa makubwa kwa Ngoma. Kwanza ni kushindwa kuhudumia familia yake, na pili ni tamaa ya kuwa na wanawake wa kila aina ambao mwisho wanampatia UKIMWI. Ugonjwa huu anaubeba na kuupeleka kwa mkewe.

Umalaya

Ngoma ni malaya. Japo alikuwa na mkewe, Tabu, bado aliendelea kuwa na wanawake wengine aliokutana nao katika sehemu za starehe.

Ngoma ana mahusiano na Asha, lakini ana mahusiano na Queen, zaidi ya hapo ana mahusiano na wanawake kutoka katika kila pembe ya jiji la Dar es Salaam, anatajwa kwamba, anaokoteza mbegu kutoka kila sehemu.

Ujinga

Japo watu wanaelimishwa kila siku kuhusu njia za kujikinga na ugonjwa wa UKIMWI, waliendelea kuwa wajinga wasiochukua tahadhari yoyote hali inayosababisha maambukizi yaongezeke kila siku.

Jose, muuza Kondomu anawaelimisha watu wasifanye ngono bila kinga. Lakini wanaishia kumfukuza huku wakimtukana matusi ya kila aina.

Pendo na Chiku ni vichwa ngumu kwelikweli, hawakujali faida za matumizi ya kondomu, kwa hasira, wanamsindikiza Jose kwa matusi:

“Kafie mbali mjinga mkubwa! Mtu na akili zako unawauzia wanaume wenzio mipira wakafanye zinaa! Ngoja siku moja wakubake na hizo kondomu zako!” uk 18.

Mwandishi anataja kondomu kuwa na uwezo wa kuzuia maambukizi ya virusi vya UKIMWI endapo itatumiwa kwa usahihi. Omolo anapofanya mapenzi na Queen, anatumia mpira. Japo Queen anakufa kwa UKIMWI, Omolo anasalimika.

Tunamuona Msafiri akiwa mtu mjinga. Anapoambukizwa UKIMWI, anadanganywa kwamba ugonjwa huo una dawa, anauza gari lake la mizigo ili aweze kununua dawa hizo.

Ndani ya jamii yetu tunao akina msafiri wengi. Yametokea matukio mengi ya watu kujitangaza kuwa wanatibu UKIMWI. Aliwahi kutokea mzee mmoja aliyejipatia umaarufu kwa jina la Babu wa Loliondo, watu wengi walikwenda kwake wakitafuta tiba ya UKIMWI.

Hata hivi sasa, wapo manabii ambao wanasambaza shuhuda za waumini wao walioponywa UKIMWI kwa maombi hayo.

Ukweli ni kwamba, mpaka hii leo, UKIMWI hauna tiba.

Uhuru wa vyombo vya habari

Mwandishi anatueleza kwamba, vyombo vya habari havikuwa huru kusema ukweli wote. Vilikuwa huru kusema yale tu yasiyowakwaza wakubwa.

Jose anafungwa baada ya kuandika habari iliyofichua rushwa katika jeshi la polisi. Anapoteza ajira yake na anapotoka jela, anafanya kazi ya kuuza Kondomu. Wenye akili wananunua ili kulinda afya zao. Wajinga wakiwakilishwa na akina Pendo na Chiku wanamtukana.

Ndoa

Suala la ndoa limejadiliwa kwa undani wa kutosha. Wapo wanaoshabikia ndoa, lakini wapo wanaopinga masuala ya ndoa.

Omolo hakubaliani na ndoa. Haoni faida ya kuwa na mke, haoni ulazima wa jambo hilo na hataki litokee. Hata hivyo, kwa ushauri wa Dkt Hans, Omolo anabadili msimamo wake na kuamua kumuoa Grace.

Tabu aliyeolewa na Ngoma, haipendi ndoa yake kwa sababu imejaa misukosuko mingi. Hata hivyo, hachukui uamuzi wa kuachana nayo kwa sababu anahofia wazazi, jamii na kile kiapo alichokula siku anakubali kuolewa.

Asha aliyeolewa, ana mahusiano na Ngoma aliyeoa. Ndoa imeonekana kushindwa kuwatosheleza wawili hawa hata wakaamua kwenda nje.

Dkt Hans anaitetea ndoa,

“Kuoa pia ni wajibu, na kuolewa pia. Ndoa ndiyo asasi ya kukuzia mbegu tutakazowajibika kuzizaa,” uk 347.

Utamaduni wa mwafrika

Suala la utamaduni wa mwafrika limejadiliwa kwa undani. Umuhimu wa jando na unyango unatajwa kuwa ukitiliwa mkazo utasaidia sana katika mapambano dhidi ya UKIMWI.

Inatajwa kwamba, UKIMWI unaenea sana kwa sababu Mwafrika ameacha tamaduni zake.

Dini mpya za kisasa hazifundishi lolote kuhusu ngono, zinafanya iogopwe.

Mwandishi anafichua kwamba, vijana wa kimasai ambao huelimishwa katika jando na unyago, hawakuonekana kuambukizwa UKIMWI kwa kasi.

Tunaona Mwafrika anakataa utamaduni wake kiasi cha kuichukia rangi yake nyeusi. Grace aliichukia ngozi yake, akajichubua, akapata madhara, hali iliyomfanya aache na akubaliane na ngozi yake nyeusi.

Suala la malezi

Mwanamke ameachiwa suala la malezi ashughulike nalo peke yake. Japo Ngoma ni tajiri, hakujihusisha na malezi ya watoto wake. Hakuwa na msaada wowote hali iliyofanya Tabu afungue biashara ya genge ili aweze kuendesha familia.

Rushwa

Rushwa imetawala ndani ya jamii. Ngoma anapolazwa hospitalini, inabidi manesi wapewe rushwa ili wamruhusu aendelee kuuguzwa hospitalini hapo.

“Lakini Ngoma alimwambia Juma awape bahashishi ili waweze kumruhusu augulie palepale hospitalini,” uk 302.

Biashara ya ukahaba

Wanawake wamekosa cha kuuza, sasa wanajiuza wao wenyewe. Biashara hii ya ukahaba ni kongwe na imekuwepo kwa miaka mingi.

Asha anao wanawake warembo wanaofanya kazi katika hotel yake. Ili uweze kumpata mhudumu yeyote, sharti uongee na Asha, umpe fedha kisha akuachie uwe naye kwa muda mtakaokubaliana.

Zito anampa fedha Asha na kumchukua Helena. Anamfanya kimada wake. Hata hivyo, Helena mambo yanamshinda kwani Zito anataka kila siku apewe kinyume na maumbile, mchezo ambao Helena hakuwahi kuuzoea. Helena anarudi kwa bosi wake, Asha kuendelea na kazi.

Ukoloni mamboleo

Mwandishi anaeleza suala la ukoloni mamboleo kwa marefu na mapana.

Katika suala hili anasema mbali na UKIMWI huu unaotesa watu, nchi yetu ya Tanzania nayo inaumwa UKIMWI. Jamii yetu haina uwezo wa kuzuia mambo yatokayo nje.

Kila jambo linalotoka nje tunalipokea bila kuhoji. Watanzania wengi sasa hawajui lolote kuhusu dini zao za jadi, wengi wamegawanywa katika makundi mawili: waislamu na wakristo.

“Mwafrika amezoea kutofanya jambo lolote sharti kwanza ajipime kwa Mzungu au Mwarabu,” uk 357.

Nafasi ya mwanamke katika jamii

Mwanamke amejadiliwa katika namna mbalimbali:

- Msomi

Queen ni mwanamke msomi. Hata hivyo usomi huu haumsaidia katika tabia yake, kwani anafanya umalaya na kuambulia kuambukizwa UKIMWI

- Chombo cha starehe

Wanaume wanamtumia mwanamke kujistarehesha. Ni sharti umpe fedha Asha ili akuruhusu ukalale na mfanyakazi wake.

- Mama mlezi wa familia

Tabu analea familia yake peke yake. Mume, yupo katika pombe huko anazoa mbegu za kila aina na usiku anarejea nazo kumgawia mkewe. Nyingine zina UKIMWI!

- Mwathirika wa UKIMWI

Wanawake mbalimbali wanatajwa kuugua UKIMWI, Tabu, Queen, Asha na wengine wengi.

- Hana maadili

Queen hana maadili hata kidogo, ana mlaghai Omolo kwa kumchganganyia mkuyati katika pombe, hali iliyomfanya Omolo alale na mwanamke huyu.

Ujumbe

Mafunzo mbalimbali yanapatikana katika riwaya hii:

Majuto ni mjukuu

Ngoma anajuta kuendekeza starehe ambazo ziliigharimu afya yake.

Ngono za holela ni jambo la kipuuzi

Watu wanaambukizwa UKIMWI kwa sababu ya kuendekeza ngono kupita kiasi. Queen akiwa kitandani anataabika, anamwachia ujumbe Omolo,

“Ngono za holela ni jambo la kipuuzi. Nimegundua ngono haina starehe yoyote zaidi ya majuto baada ya kuifanya,” uk 200.

Matumizi ya kinga kwa usahihi yanazuia maambukizi ya UKIMWI

Omolo alitumia kinga alipokutana na Queen, hali hii inamfanya aokoke kuambukizwa UKIMWI.

Ulevi ni chanzo cha maambukizi ya UKIMWI

Katika riwaya hii tunaona wengi wanaopata UKIMWI ni wale ambao walijihusisha na ulevi. Ngoma ni miongoni mwa walevi waliopata UKIMWI kwa ulevi wao. Mara nyingi ulevi huambatana na umalaya, mtu anapolewa uwezo wa kufikiria hupungua, hivyo hujikuta akifanya ngono zembe na kuwa katika hatari ya maambukizi ya virusi.

Migogoro

Migogoro mbalimbali imejitokeza: miongoni mwa migogoro hiyo ni:

Migogoro ya wahusika

Mgogoro wa Juma na Baba yake

Juma ana hasira na Ngoma kwa sababu amesababisha mama yake apate UKIMWI. Pia Ngoma analazimisha Juma ahudhuria swala zote, Juma anaona jambo hili ni jipya kwa baba ambaye hapo mwanzo hakuwa na msaada wowote. Anaamua kutoroka kwenda kuishi kwa babu yake. Mwisho, kwa ushauri wa Omolo, Juma anamuomba msamaha baba. Ngoma anapofariki, anamuandika Juma kama mrithi wa mali zake.

Tabu na Ngoma

Tabu anamlaumu Ngoma kwa kumuambukiza UKIMWI. Mgogoro huu unafikia hatua ya Ngoma kumpa talaka mkewe. Siku za mwisho za uhai wa Ngoma, anamuomba msamaha mke wake na kuifuta ile talaka.

Jose dhidi ya Pendo na Chiku

Wanawake hawa hawataki kusikia lolote kuhusu kondomu, wanamtukana Jose kijana anayeuza kinga. Jose anaondoka bila kuwajali.

Queen na Omolo

Chanzo cha mgogoro huu ni Queen kumfanyia hila Omolo kwa kumuwekea dawa kwenye pombe na hatimaye kufanikiwa kulala naye.

Mgogoro huu unakuwa mkubwa zaidi pale Omolo anapomtembelea Queen halafu ndani ya chumba akatoka Ngoma akiwa amevalia taulo. Omolo anaondoka kwa hudhuni na kuamua kuachana na Queen.

Migogoro ya nafsi

Omolo

Mgogoro wa Omolo unahusu hali yake ya kiafya. Alifanya mapenzi na Queen, mwanamke anayetajwa kufa kwa UKIMWI. Hata hivyo, Omolo alitumia mpira. Changamoto ni kwamba, mpira ulichanika, akawahi bafuni kujisafisha kwa sabuni.

Omolo anapima ili ajue afya yake. Bahati imekaa upande wake, hakuwa na virusi vya UKIMWI.

Queen

Msichana huyu anawaza mambo mengi. Anawaza nini maana ya maisha ikiwa uhai wenyewe haudumu kwa muda mrefu. Anapata maumivu makala anapoanza kushambuliwa na UKIMWI, kwa kutokutaka kuendelea kuumia zaidi, anakatisha maisha yake.

Falsafa

Katika riwaya hii maana ya maisha imejadiliwa kwa mawanda mapana.

Omolo anajiuliza nini maana ya maisha. Kila siku anafanya kazi, kisha anapita baa kunywa pombe halafu anakwenda nyumbani. Anaendeleza mzunguko huo kila siku, haelewi jambo hilo maana yake ni nini?

Queen naye haelewi hasa maana ya maisha. Anayaona maisha kama upuuzi.

“Kweli hata mimi nilikuwa sina tabia ya kuulizauliza. Niliyaishi maisha jinsi yenyewe yalivyojileta. Lakini sasa nimeshalikaribia kaburi, ndipo ninapofumbukiwa kwamba: kumbe ulikuwa upuuzi mtupu!”

Omolo anashangazwa na tabia ya masikini wanaoishi maisha ya mateso, wanapougua, hutumia gharama kujitafutia matibabu ili wapone waendelee kuteseka.

Dkt Hans ana maoni magumu kuhusu uwepo wa Mungu,

“Muweza na mjuzi wa yote hawezi kuwa na sababu ya kuumba kiumbe chenye dosari, kisha akipe mitihani; ndipo akipokee tena kwenye raha yake ya milele. Muweza wa yote ataumba kilicho kamili. Mjuzi wa yote hana sababu ya kukipa kitu chochote mtihani kwa sababu amekwishajua kufeli au kufaulu kwake kitu hicho. Siyo kweli, mtu haumbwi au hawi, kwa makusudi hayo ya kumtumikia muumba na kupewa mitihani ya maisha.”

Pia, tunawaona wahusika ambao wanamrudia Mungu hasa baada ya kupatwa na matatizo. Ngoma anageuka Mswalihina baada ya kuambukizwa UKIMWI.

Mjadala huu ni mpana, wataalamu wa imani, bila shaka wana mengi ya kumjibu.

Kwa ujumla hasa tukiitazama dhamira kuu katika riwaya hii, basi mwandishi anaelekea kuamini kwamba, watu warejee katika tamaduni zao. Mtu asiyejua tamaduni zake ni ndondocha.

Anaeleza kuwa, hata katika mapambano dhidi ya UKIMWI, jando na unyango ni silaha nzuri zaidi kukabiliana na maambukizi. Anatoa mfano wa vijana wa kimasai kutokuambukizwa kwa wingi ukilinganisha na vijana wa makundi mengine.

Msimamo/mtazamo

Mwandishi ana msimamo wa kimapinduzi. Anaitazama dunia kisayansi. Anahoji uwepo wa Mungu mmoja muweza wa yote. Anakataa kushikilia imani bila ushahidi wa kuonekana.

Katika kuleta suluhisho dhidi ya ugonjwa wa UKIMWI, mwandishi anatueleza kwamba, ni vyema kama tutarejea katika tamaduni zetu za Mwafrika. Jando na unyago anaona kuwa suluhisho.

Katika kurejea katika tamaduni za Mwafrika, mwandishi yupo sahihi kwani, mafundisho mengi ya Mwafrika, yamekataza ufanyaji ngono holela suala ambalo endapo litafuatwa, maambukizi yatapungua kwa kasi.

Fani

Vipengelel mbalimbali vya fani vimejadiliwa:

Wahusika

Katika kipengele cha wahusika, mwandishi amefaulu sana kutumia wahusika ambao wanabeba vizuri dhamira zake. Hata hivyo, katumia wahusika wengi sana ambao hawana mchango wowote katika simulizi: baadhi ya wahusika wanaoonekana ni:

- Ngoma Abdallah

Mlevi

Malaya

Anaambukizwa UKIMWI

Mwishoni anabadili tabia na kuwa mswalihina

- Tabu

Mke wa ngoma

Ni mwanamke mwaminifu katika ndoa yake

Ni mchapakazi

Anakufa kwa UKIMWI

- James Omolo

Anajulikana kwa jina jingine la Jaluo

Mhasibu kiwanda cha kusindika samaki

Anamsaidia Ngoma pale anapougua na kubaki peke yake katika nyumba

Anajiuliza maswali mengi ikiwemo maana ya maisha

Haamini katika ndoa, hata hivyo kwa ushauri wa Dkt Hans, anabadili msimamo wake.

- Dkt Hans

Ni daktari anayehusika na wagonjwa wa UKIMWI

Ana upendo

Ni mcheshi

- Pendo na Chiku

Wahudumu Malaika Bar

Wanapendwa sana na wateja wao

Wote wawili, wanafukuzwa kwa kusababisha shoti

Chiku anaumwa UKIMWI na anarudishwa kwao Tabora

- Dadii

Mtoto wa marehemu kaka yake Queen.

Queen anamtaja kama mrithi wa nyumba yake.

- Grace

Msaidizi wa Omolo

Ni dada yake Tabu

Anaolewa na Omolo

Aisha, Nuru, Rahma, Abu na Juma

Watoto wa Ngoma

- Profesa Raleigh

Mkurugenzi taasisi ya UKIMWI

Hakubaliani na mawazo ya Dkt Hans katika kuendeleza mapambano dhidi ya UKIMWI

- Abdallah Kungwe

Dereva wa magari ya Ngoma

Ni mwaminifu

Anamjulia hali Ngoma mara kwa mara alipoanza kuugua.

- Queen

Mwanamke msomi

Ni malaya

Ana UKIMWI

- Asha

Amewahi kuolewa na mzee Mzungu aliyeitwa Hastings

Kwa sasa ni mke wa msafiri

Ni malaya

Ana UKIMWI

- Jose

Kijana muuza Kondom

Aliwahi kuwa mwandishi wa habari akafungwa kwa sababu aliandika habari iliyofichua rushwa ndani ya jeshi la polisi

- Msafiri

Mume wa Asha

Anatapeliwa ipo dawa ya UKIMWI, anauza gari lake ili apate tiba hiyo

Anarudi kwao baada ya kuzidiwa na maradhi

- Hastings

Mzee mzungu kutoka Australia

Anamuoa Asha na kumjengea hotel

Anapofariki, Asha anarudi Tanzania kuendelea na biashara yake ya hotel

- Mzee Loti

Baba yao Grace na Tabu

-Bibi Upendo

Mama yao Grace na Tabu

- Daudi

Kaka yake Grace na Tabu

- Popo na Oza

Wanafanya kazi sokoni

Wanamsaidia kufanya manunuzi Juma pamoja na kubeba mizigo ya biashara ya genge.

Wahusika wengine ni: Yakobo, Mamudi, Hiza, Bibi Kimono, Kassim, Pengo, Mangori, Zuberi, Mashaka, Zubeda, Rukia, Shehe Rajabu, Dkt Chale, Dkt Grace, Roda, Kristina, Zito na Mpemba

Mandhari

Riwaya hii imetumia mandhari halisi ikitaja maeneo mbalimbali kama:

- Malaika Bar

Ni baa anayopenda kunywa Omolo na Ngoma, katika baa hii wahudumu Chiku na Pendo wanapatikana.

- Tandika

Sehemu anakoishi Omolo

- Kanga Moja Club

- Mwangaza Bar

- Hotel Victoria

Inamilikiwa na Asha Mmanyema, hotel hii alijengewa na Hastings

- Australia

- Buguruni

- Morogoro

- Arusha

- Alwatan Bar

Muundo

Riwaya hii imetumia muundo changamano. Tunaona urejeshi wa matukio na kurukiana kwa visa.

Mwandishi ameigawa riwaya yake katika sura nne: sura ya kwanza ikiwa na jina la Hofu, ya pili ikiitwa Majuto ya Tatu ikijulikana kama Faraja na sura ya nne inahitimisha kwa jina la Hitimisho.

Mtindo

Kwa kuwa hii ni riwaya, mtindo wa monolojia umetawala, nao mtindo wa dayolojia unaonekana hususani katika maeneo yenye majibishano ya wahusika.

Nafsi ya tatu imetawala katika usimuliaji wa matukio.

Mwandishi ameutajirisha mtindo wake kwa kutumia nyimbo. Afro Band ilitumbuiza wimbo huu,

“Afrika tushangilie ngoma!

Tushangilie!

Ngoma tushangilie Afrika!

Tushangilie!

Shangwe, tushangilie ngoma!

Tushangilie!”

Matumizi ya lugha

Mwandishi ametumia lugha rasmi inayoeleweka kwa wasomaji. Vipengele mbalimbali vinaonekana kama inavyojadiliwa:

Tamathali za semi

Riwaya hii imepambwa kwa tamathali mbalimbali za semi. Baadhi ya tamathali hizo ni:

- Tafsida

Siku moja tutakuwashia sigara kubwa

Au mzee kalala usingizi wa kudumu

- Tashibiha

Wanaume wote walimtazama kwa shauku kama simba anavyomkodolea pofu nyikani.

Macho yalikuwa mekundu yamelegea kama yanataka kutoka kwenye mashimo yake

Ngoma akaanza kubembeleza kwa mikono kama anayeimbisha kwaya

Mtu mwenyewe ananguruma kama mbwa mwenye fupa

- Takriri

Hii ni mbinu nyingine ya kisanaa iliyotumika, mifano mbalimbali inaonekana:

Ngoma! Ngoma!

Matumizi ya lugha za kigeni

- Ash tray

- Sitiari

Kumbe urembo ni sanaa

Mtu na kizuka wakiafikiana

- Mubaalagha

Taa zote za mtaa ule zilikuwa zimeungua

- Ritifaa

Hii ni mbinu ya kuzungumza na mtu aliyekufa au kitu kisichoonekana. Mfano huu umechukuliwa kutoka ndani ya riwaya,

“Usilie mwanangu, usilie mpenzi, yote tumeshamkabidhi Mungu…”

Misemo

Mfuko wako tu

Twende na wakati

Methali

Mshahara wa dhambi ni mauti

Kupanda mchongoma kushuka ndiyo ngoma

Mwanamke jikoni hafi njaa

Siri ya kitanda ajuaye kunguni

Majuto ni mjukuu

Msahau kwao ni mtumwa

Ponda mali kufa kwaja

Mali ya bahiri huliwa na wadudu

Simba mwenda pole ndiye mla nyama

Nahau

Hatuivi chungu kimoja

Lugha ya picha

Mwandishi anatuchorea picha pale anaposimulia:

“Mafuta ya nyama iliyokuwa ikichomwa yalidondokea kwenye makaa na kuhanikiza eneo lote kwa harufu tamu ya mishikaki.”

Taswira

Watu wanatumia neno ‘mkanda wa jeshi’ kumaanisha ugonjwa wa UKIMWI.

Maoni ya mhakiki

Ua la faraja ni riwaya bora inayojadili kwa undani suala la UKIMWI, njia zinazosababisha gonjwa hilo na suluhisho lake.

UKIMWI unatajwa kusababishwa na ngono zembe, ulevi na ujinga. Suluhisho linalotolewa hapa ni kubadili mienendo na kuhamasisha matumizi ya mpira.

Mwandishi amefaulu sana katika kuijadili falsafa ya maisha. Anatuweka katika mjadala ambao haujawahi kupata jibu. Nini maana ya maisha. Aliyeanzisha mradi wa maisha alilenga nini hasa? Kwanza mradi huu una mwenyewe? Ama tuliibuka tu kama uyoga? Japo haji na jibu kamili, ile hali ya kuwa katika mjadala inatosha.

Hata hivyo, mwandishi ameshindwa kuimudu sanaa. Kazi yake haivutii kusoma, inachosha kwa sababu haina taharuki. Matukio yajayo yanatabirika na hakuna kiu hasa ya kuendelea kusoma. Kama tafiti zitafanywa, huenda wasomaji wengi hawakumudu kukisoma kitabu hiki mpaka mwisho.

Kila unapoisoma riwaya hii, unatamani kuishusha ufanye mambo mengine, Mwandishi anazungukazunguka ili kujaza kurasa. Siyo kosa riwaya kuwa na zaidi ya kurasa 400, hata hivyo, kurasa 400 zisizovutia ni kuwachosha wasomaji!

Wasiliana na Mwalimu ili Kujiunga Darasa la Uhakiki wa Vitabu vyote vya Fasihi Mtaala Mpya kwa Kugusa Hapa

Popular posts from this blog

SMS 20 za Vichekesho Zinazochekesha Sana

SMS 20 za Mahaba Makali Kumtumia Mpenzi Wako

Uhakiki wa Tamthiliya ya Ngoswe Penzi Kitovu cha Uzembe