Uhakiki wa Riwaya ya Mirathi ya Hatari
Mwaka: 1977
Mhakiki: Mwalimu Makoba
Utangulizi
Mirathi ya hatari kisomwe kwa tahadhari. Yale yanayojadiliwa humo, ni mambo ya kufikirika ambayo katika dunia hii iliyojaa uhalisia hayana nafasi.
Kitabu hiki kisiposomwa kwa tahadhari, kinaweza kusababisha changamoto tatu:
Kwanza, wanafunzi wataamini habari za uchawi kuwa ni za kweli. Wataanza kuiona dunia kama sehemu ya miujiza na si uhalisia wa bidii ya kufanya mambo.
Pili, wanafunzi watapatwa na hofu, watakapougua, watahisi pengine wamechezewa ilhali kuugua ni hali ya kawaida katika maisha na vipo visababishi mbalimbali wakiwamo mbu waenezao malaria.
Changamoto ya tatu bado haijajulikana na inaninyima usingizi!
Kwa hivyo unaposoma kitabu hiki, na unapohakiki riwaya hii, tambua jambo moja, yanayosemwa humu hayawezi kutokea katika ulimwengu wa kawaida. Dunia yetu inaongozwa na kanuni nayo sayansi imethibitisha uchawi haupo.
Jamii za kiafrika bado zinaamini katika ushirikina, mwandishi, anaonyesha imani hiyo, lakini anatia chumvi kupitiliza pale anaposhuhudia kuona matukio ambayo kusema kweli ni uongo!
Simulizi kwa ufupi
Gusto anarithishwa mikoba ya sihiri, mikoba ya uchawi ya hayati baba yake, Mzee Kazembe.
Ili kutimiza masharti ya uchawi na kupokelewa kama mshirika kamili, anamtoa kafara mjomba yake, Kapedzile.
Rafiki yake Kapedzile, Mzee Malipula hakubaliani na jambo hili, anaapa kulipa kisasi.
Gusto anatoroka katika kijiji chake cha Kitelevadzi, lakini anatoroka akiwa na mpenzi wake Dina, mtoto wa Mchawi Malipula.
Gusto na Dina wakiwa katika gari wakielekea Dar es Salaam, gari inapigwa na radi, Dina anafia hospitali, Gusto ananusururika.
Inaaminika kwamba, ajali hiyo ilisababishwa na Malipula, ambaye anamuua binti yake mwenyewe hasa kwa sababu ya usaliti alipomfanyia.
Wakati Gusto akitafakari kuhusu tukio hilo na aliyejawa na upendo wa kuondokewa na mtu aliiyempenda kuliko kitu chochote, anasikia habari zingine ambazo hazikumfurahisha, Mama na dada yake, wamekufa kwa kuungua kwa moto ndani ya nyumba! Inasemekana aliyefanya haya ni mchawi Malipula.
Gusto anaapa kulipa kisasi, anapaa kwa ungo akiwa na Mzee Mavengi, wanavamia nyumba ya Malipula wanamwanga madawa makali yanayomzidi nguvu Malipula kisha wanaichoma moto nyumba na Malipula anafia humo.
Mwisho mwandishi anatuambia Mzee Mavengi anayachoma moto mapango ya wachawi wote, na huo ndiyo unakuwa mwisho wa uchawi katika jamii ya Kitelevadzi.
Maudhui
Vipengele mbalimbali vya maudhui vinajadiliwa:
Dhamira
Mwandishi ameibua dhamira nyingi, miongoni mwa dhamira hizo zinajadiliwa.
Uchawi
Uchawi umeonekana katika maeneo mengi ya riwaya hii. Watoto wa jamii ya Kitelevadzi walivaa hirizi kama kinga ya uchawi.
Pia, tunamuona Mzee Kazembe akimrithisha Gusto mikoba yake ya sihiri.
“Mwanangu nakuachia kazi kubwa. Ni urithi mkubwa ukiutumia vema; bali pia ni mirathi ya hatari usipojihadhari nayo. Nakuachia dawa zote na milki yangu katika mizungu ya sihiri!” uk 12.
Pia, tunaona tukio la kuuawa kwa Kapedzile kichawi. Tunaona namna ambavyo wachawi wanaingia ndani ya nyumba aliyolala na milango ilifunguka yenyewe.
Yapo mauaji ya kutisha ambayo yanatajwa kufanywa na wachawi. Inasemekana Mzee Kazembe mwenyewe kifo chake hakikuwa cha hivihivi, bali aliuliwa kichawi na mchawi Malipula akishirikiana na rafiki yake Kapedzile.
Mauaji mengine yanayosemwa kufanywa kichawi ni mauaji ya Dina, Nandi, Mama yake Gusto na Malipula.
kuna mahali tunaona uchawi ukitumiwa vizuri. Mzee Mavengi kuna wakati anatumia uchawi kumsaidia Gusto atoroke, na mwisho tunaona kwa sababu ya kuchukizwa na mambo ya uchawi, anayachoma moto mapango na huo unakuwa mwisho wa uchawi katika jamii ya Kitelevadzi.
Katika jamii yetu minong’ono ya uchawi ipo. Watu wanauogopa uchawi na ni kawaida kusikia katika mikoa fulani wazee wakiuliwa kwa tuhuma za uchawi.
Yapo matukio yaliyotikisa nchi yote yakihusisha imani za kichawi, kwa mfano, palitokea tukio la watu kulalamika nyeti zao zinapotea pale wanaposhikwa bega.
Ukitazama katika majumba mengi ya maombezi, wengi wanadai kusumbuliwa na uchawi.
Hata hivyo mbali na fununu hizo na hofu ya wanajamii, ukweli unabaki palepale, hiyo ni hofu tu. Katika jamii halisi uchawi hakuna. Hakuna mtu anayeweza kupaa na ungo, hakuna mtu anayeweza kubadilika kuwa kiumbe mwingine na hakuna anayeweza kumgeuza mwenzake msukule ilhali watu makaburini wakaona wanazika mgomba. Hizi ni hadithi tu, hadithi zinazochochewa na hofu ya mwanadamu juu ya mambo mbalimbali kama vile maradhi na kifo.
Kazi
Watu wa jamii ya Kitelevadzi walifanya kazi kwa bidii. Kazi yao kuu ilikuwa kilimo. Walilima Pareto, mahindi na njegere.
Elimu
Katika jamii ya Kitelevadzi, watu hawakupeleka watoto shule. Watoto walionekana wakichunga ng’ombe muda ambao walitakuwa kuwa darasani. Hata hivyo, Mzee Kazembe alimpeleka Gusto shule.
Upande mwingine tunamuona Malipula akiipa nafasi elimu kwa kumpeleka shule binti yake Dina.
Gusto anaamini katika elimu, hata wachawi wanamweleza kuwa, kujiunga katika uchawi, hakumzuii kuendelea na masomo yake.
Ubahiri
Rafael, kaka yake Gusto, alikuwa bahiri kupindukia. Pesa zake alizifukia chini na hakuwa na maendeleo yoyote.
“Fedha zote alizozipata kutika katika mauzo ya pareto alizifukia ardhini. Na kwa nadra alikunywa pombe ya kununua” uk 11.
Pia tunaona mtoto wa Rafael akishindwa kuendelea na shule kwa sababu alikosa ada.
Mapenzi
Tunayaona mapenzi motomoto baina ya Dina na Gusto. Walipendana kwa dhati.
Dina kwa sababu ya upendo wake kwa Gusto, anamweleza Gusto yale aliyopanga kufanya Malipula na Kapedzile. Marafiki hawa wachawi, walipanga kuiangamiza familia ya Gusto ili waweze kuchukua shamba lao.
Naye Gusto anampenda Dina, anaamua kutoroka naye kuelekea Tanga ili wote wawili waweze kujiepusha na adhabu ya kifo kutoka kwa Malipula.
Vilevile tunamuona Gusto akilipa kisasi kwa kushiriki kumuua Mzee Malipula kwa sababu alimuua Dina.
Mapenzi mengine yanaonekana kwa mzee Mavengi. Mzee huyu anampenda sana Gusto hata anamsaidiz ili asiweze kudhuliwa na wachawi. Mavengi anampenda Gusto kwa sababu alikuwa rafiki wa baba yake.
Nyamidze, mama yake Gusto, anampenda mtoto wake na hataki lolote baya limtokee. Anashiriki kumsaia kutoroka kijijini ili asije akaadhibiwa na Malipula.
Visasi
Mzee Malipula anaapa kulipa kisasi dhidi ya wote walioshiriki kumuua swahiba wake Kapedzile. Anamkamata Gusto na kutaka kumpeleka kwa Chikanga muona wachawi aishiye Malawi. Hata hivyo, kabla hajafanikiwa, Gusto anaokolewa na Mzee Mavengi.
Malipula analipa kisasi kwa kumuua mama na dada yake Gusto. Pia, kutokana na usaliti aliofanyiwa na binti yake, anamuua kwa radi akiwa anasafiri katika gari.
Gusto naye hayuko nyuma. Baada ya mauaji yanayofanywa na Malipula, naye analipa kisasi. Anashirikiana na Mzee Mavengi, wanakwenda na kufanikiwa kumuua Malipula.
Vijiji vya ujamaa
Riwaya inaanza kwa kuwaonyesha akina Gusto wakisaidia wanakijiji kuhamia katika vijiji vya ujamaa.
“Ni juma la pili leo tangu nifike hapa kuwasaidia ndugu wanakijiji hawa katika operesheni Sogeza; operesheni ya kuhamia katika vijiji vya maendeleo” uk 1.
Tanzania mnamo miaka ya sabini iliendesha kampeni kubwa ya kuwapeleka watu katika vijiji vya ujamaa. Vijiji hivi vilitarajiwa kufanya mengi, hata hivyo vilishindwa katika namna ya kutisha, kushangaza na kusikitisha kwa pamoja. Kicheko kingemtoka yule tu asiye na huruma!
Nafasi ya mwanamke katika jamii
Mwanamke amechorwa katika namna mbalimbali, miongoni mwazo ni:
Mwenye elimu: tunamuona Dina akiwa mwanamke msomi tena anaye endelea na masomo yake. Hata hivyo, anapoteza maisha katika ajali ya gari.
Anakandamizwa na mfumo dume: wapo wanaume katika jamii ambao hawaamini katika ustawi wa mwanamke. Wanaume hawa wanawakilishwa na Mzee Kindimba. Mzee huyu haamini katika kumsomesha mwanamke, anasikika akisema,
“Kumsomesha mtoto wa kike ni kama kumpa bangi imvuruge akili” uk 43.
Mwenye upendo wa kweli: Dina anaupendo wa kweli, alimpenda kwa dhati Gusto.
Naye Lulu ana upendo wa kweli, kutoka na mapenzi yake kwa jamii, anajitolea kama nesi katika hospitali ambayo ilikuwa na uhitaji. Lulu anafanya haya akiwa mwanafunzi na alitumika katika nafasi hii katika kipindi cha likizo yake.
Mchapakazi: Nyamidze anafanya kazi kwa bidii. Gusto anamuelezea mama yake kuwa alikuwa mchapakazi kwelikweli. Alikuwa mkulima hodari na alishiriki katika shughuli zote za nyumbani.
Mama mlezi wa familia: Nyamidze baada ya kufiwa na mumewe Mzee Kazembe, anashiriki katika kulea familia yake aliyobaki nayo peke yake. Anatunza watoto na kuangalia mashamba.
Ujumbe
Riwaya hii inatoa mafunzo mbalimbali. Miongoni mwa mafunzo hayo ni:
Ukiua kwa upanga utakufa kwa upanga
Malipula anaua watu kwa uchawi wake. Anamuua Kazembe, Dina, Nyamidze na watu wengine wengi. Mwisho naye anajikuta akifa kwa njia hiyohiyo. Mzee Mavengi baada ya kumuua Malipula, anasisitiza kwamba, sote tunapiga duara, mwisho wetu ni mmoja.
Elimu ni ukombozi wa jamii
Gusto anatumia elimu yake kujiepusha na mambo ya uchawi. Anachagua kumtoa kafara mjomba yake kwa sababu mjomba alipanga kuiangamiza familia ya Gusto kwa sababu tu alilitamani shamba lao.
Gusto akiwa katika kula kiapo cha mwisho anakimbia na anasaidiwa na Mzee Mavengi katika kujificha kwake.
Elimu inaikomboa jamii ya Kitelevadzi, kwani Gusto aliyetakiwa kurithi uchawi, anageuka. Akishirikiana na Mzee Mavengi, wanafanikiwa kuondoa chembechembe zote za uchawi.
Jamii ijiepushe na imani za kishirikina
Imani za kishirikina hazina faida yoyote. Katika riwaya hii hatuoni lolote la maana linalohusiana na ushirikina, zaidi tunaona visasi na kuuana kusikokuwa na kikomo.
Wanajamii wanapaswa kupuuza habari za kuwako kwa uchawi, badala yake, wafanye kazi kwa bidii wasiokuwa na hofu yoyote.
Watu wafanye kazi kwa bidii
Katika jamii ya Kitelevadzi, watu walifanya kazi kwa bidii kubwa. Katika ufanyaji huo wa kazi walifanikiwa kuendelea vyema na maisha yao. Hivyo basi, kazi ni kipimo cha utu, kazi ndiyo imemfanya mtu akawa mtu hii leo. Tufanye kazi kwa bidii na kamwe tusikubali kuimaliza siku tukiwa tumekaa tu bila kufanya lolote la maana.
Migogoro
Aina mbalimbali za migogoro zinajitokeza katika riwaya hii, miongoni mwazo hizi zinazojadiliwa:
Migogoro ya wahusika
Mgogoro kati ya Mzee Kazembe, Kapedzile na Mzee Malipula
Chanzo cha mgogoro wa Kapedzile na Kazembe ni shamba. Na mgogoro wa Malipula na Kazembe ni mambo ya uchawi.
Mgogoro huu unasababisha vifo. Tunamuona Mzee Kazembe akidaiwa kuuliwa na Malipula. Familia ya Kazembe chini ya Gusto inamuua Kapedzile na Malipula.
Dina na Malipula
Dina ana mgogoro na baba yake. Chanzo cha mgogoro huu ni Dina kuwa na mahusiano na Gusto, mwana wa mchawi.
Dina anatoroka na Gusto, Kazembe anatumia uchawi wake na kumuua Dina bila kujali alikuwa binti yake wa kumzaa.
Malipula na Gusto
Chanzo cha mgogoro ni Gusto kuwa katika mahusiano na Dina. Mgogoro unakolea zaidi pale sababu nyingine inapoongezeka. Kapedzile anapouawa, Malipula anatambua waliofanya hivyo ni akina Gusto na wachawi wengine, anamvamia Gusto na kulazimisha ampeleke Malawi kwa Chikanga muona wachawi, Gusto anaokolewa na Mzee Mavengi.
Mgogoro wa nafsi
Gusto yupo katika mgogoro na nafsi yake pale anapoambiwa arithi mikoba ya uchawi.
Akiwa katika lindi zito la mawazo, siku ya kwanza anafanya kila linalotakiwa, lakini siku ya pili anapomtoa kafara mjomba yake, anashindwa kuvumilia na kukimbia.
Falsafa
Falsafa ya mwandishi imeegemea katika kipande kidogo cha falsafa za Kiafrika. Waafrika wengi wanaamini katika ushirikina, hivyo mwandishi anakubaliana kwanza na huo uchawi kwamba upo, lakini anataja kwamba, ushirikina ama uchawi ni jambo baya katika jamii hivyo linapaswa liondolewe.
Kwa hivyo mwandishi hakubaliani kabisa na masuala yote ya uchawi. Anauona uchawi kama jambo baya lisilotakiwa kuwa katika jamii.
Hata hivyo, falsafa ya mwandishi imepotoka. Katika dunia hii ya sayansi na teknolojia, kila kitu kimewekwa wazi, uchawi hakuna!
Msimamo/mtazamo
Mwandishi ana msimamo wa kidhanifu. Anaelekea kuamini katika mambo ya sihiri na ushirikina kama Waafrika wengi wanavyoamini mambo hayo.
Msimamo wa mwandishi usipoeleweka vyema, japo mwishoni anaeleza kuwa uchawi ni mbaya na unapaswa kuteketezwa, jambo hili linaweza likaongeza migogoro zaidi katika jamii. Watu watauana kwa kushikana uchawi, wengine watazidi kuishi maisha ya hofu wakiamini kwamba wamerogwa!
Fani
Vipengele vya fani navyo vimepata nafasi ya kujadiliwa. Mwandishi ametumia vipengele kadha wa kadha vya fani ambavyo vinaelezwa hapa:
Wahusika
- Gusto Kazembe
Huyu ndiye mhusika mkuu.
Anarithishwa uchawi kutoka kwa baba yake Mzee Kazembe.
Ni mwanafunzi.
- Lulu Tomaso
Msichana aliyesoma shule moja na Dina.
Ana moyo wa upendo, kutokana na upungufu wa wauguzi, anautumia muda wake wa likizo kujitolea kama muuguzi katika hospitali.
Ni rafiki yake Gusto.
- Mzee Kazembe
Mchawi aliyebobea.
Ni baba yake Gusto, na ana mrithisha Gusto uchawi huo.
Kifo chake kinasemekana siyo cha hivihivi, bali kimesababishwa na Mzee Malipula.
- Nyamidze
Mama yake Gusto
Ni mchapakazi
- Nandi
Dada yake Gusto.
- John
Rafiki yake Gusto.
- Kitambi
Alituma barua ya simu akimweleza Gusto kuwa, arejee nyumbani haraka, baba yake alikuwa mahututi kitandani.
- Mzee Kindimba
Rafiki mkubwa wa Malipula.
Ana mawazo yaliyopitwa na wakati. Hakubaliani na suala la kumsomesha mtoto wa kike.
- Chikanga
Ni mganga anayefanya kazi ya kukamata wachawi.
Anaishi Malawi.
- Mzee Kiyao
Mjomba yake Dina
Anaishi Kisosora Tanga
- Stefano
Binamu yake Dina.
- Bwana Ericson
Mwalimu wake Gusto
Ana busara.
Anamshauri Gusto asiwaze kuhusu kufa kwa mpenzi wake Dina, bali ajikite katika masomo kwani ipo siku atampata mwingine atakayempenda.
- Patel
Mhindi anayejihusisha na biashara ya teksi.
- Rafael
Kaka yake Gusto.
Ni bahiri.
- Madoda, Bibi Mvyele, Mzee Mavengi, Mama Tumwene, na Simbili
Hawa wote ni wachawi.
Madoda ndiye anayetumwa kumfuata Gusto na kumpeleka mapangoni waliko wachawi wengine.
Bibi Mvyele yeye anakaimu kiti cha uchawi kwa muda tu wakati Gusto akiandaliwa.
Naye Mzee Mavengi ndiye anayehusika katika kuongoza mashambulizi ya kuvamia na kumchukua yoyote waliyemtaka.
Mandhari
Mandhari mbalimbali yamejitokeza:
Kijiji cha Kilole
Shule ya Tumbi: hii ni shule aliyosoma Gusto
Dar es Salaam: ni katika mkoa huu, shule anayosoma Gusto inapatikana.
Iringa
Njombe
Kitelevadzi: kijiji anachoishi Gusto. Hiki ni kijiji ambacho kimetawaliwa na uchawi wa kutisha.
Tanga: ni mkoa ambao Gusto anatorokea akiwa na Dina.
Madhari mengine ni haya:
Mapangoni: humu walikutana wachawi kupanga mipango yao.
Nyumbani
Bwenini
Shuleni
Ofisini
Ndani ya gari
Angani: wachawi wanatumia anga kupaa kwenda kule wakutakako. Mzee Mavengi na Gusto ni miongoni mwa wachawi wanaolitumia anga vyema.
Muundo
Riwaya hii imetumia muundo wa urejeshi ikiwa na jumla ya sura tisa. Simulizi inaanza kwa kumuonesha Gusto akiwa likizo ya masomo yake ya Chuo Kikuu, anaitumia likizo hiyo kuwasaidia wanakijiji kuhamia katika kijiji cha ujamaa. Baadaye Gusto anasimulia mkasa uliomtokea miaka kadhaa iliyopita. Ni ndani ya mkasa huu ndimo inamojengwa simulizi ya mirathi ya hatari.
Mtindo
- Katika masimulizi ya riwaya hii, mtindo wa nafsi ya kwanza umetawala.
- Vipengele vingine vya mtindo ni:
- Monolojia
- Dayolojia
- Mbali na hayo, mwandishi ametumiwa mtindo wa barua. Katika ukurasa wa 24, Gusto anapokea barua kutoka kwa mpenzi wake Dina, Gusto anapewa pole ya kufiwa na baba yake Mzee Kazembe.
Matumizi ya lugha
Vipengele mbalimbali vya lugha vimetumika:
Tamathali za semi
- Tabaini
Baba yangu hakuwa mtu mkwasi, lakini pia, hakuwa hohehahe.
- Tashibiha
Nilimfuata Madoda kama kondoo
Sifa zake zikaenea kijijini kama moto katika nyasi.
Nilikuwa nikishikilia uhai kama mpanda farasi.
Maneno hayo yaliniuma kama sumu ya nyigu.
Methali
Aponaye vitani huishi kupigana tena.
Yaliyopita si ndwele, mradi tugange yajayo.
Majuto ni mjukuu.
Neno la akataye roho si la kukataa.
Mtegemea Mungu si mtumwa.
Kila chenye mwanzo kina mwisho
Dawa ya moto ni moto.
Misemo
Waliozaliwa na bahati hurejea na bahati kaburini.
Waoga hufa maradufu kabla ya kifo halisi.
Maoni ya mhakiki
Mirathi ya hatari ni kitabu kilichopitwa na wakati. Kinazungumzia mambo ambayo dunia haiyajadili tena kwani, hayana ukweli.
Mwandishi hajafaulu kwa kiwango kikubwa katika maudhui yake. Yeye anaeleza dhamira za uchawi. Dhamira zake zinawaaminisha wasomaji kuwa uchawi upo. Dhamira hizi hazina uhalisia wowote na mambo halisi ya jamii. Endapo zisiposomwa kwa tahadhari, basi riwaya hii inaweza kuwapa hofu wanafunzi, walimu na wasomaji.
Kigezo kwamba Waafrika wana amini katika uchawi na kuwaandikia kazi za fasihi zinazoendana na uchawi huo, hatuwasaidii, badala yake tunazidi kuwadidimiza katika lindi la ujinga. Ingependeza kama Mirathi ya hatari kingeonyesha humo ndani yake kuwa, mambo ya uchawi ni uzushi mtupu. Badala yake kimeonyesha mambo hayo kuwa yanayowezekana.
Jamii zote ziliamini katika ushirikina hapo kale, lakini jamii nyingi zilizoendelea zimeachana na imani hizi kwani hazina ukweli wowote.
Hata hivyo, hakuna aliyembaya kwa asilimia 100. mwandishi amefaulu katika matumizi mazuri ya lugha.
Kazi ya mwandishi imetumia Kiswahili kilicho katika kiwango cha juu. Kazi yake ni matokeo ya tafiti hasa kwani hajatumia lugha moja, kuna maeneo katumia lugha ya kihehe.
Lugha iliyotumika inapambwa zaidi na matumizi ya tamathali za semi, misemo na methali za kila aina.
