Mtihani wa Kiswahili Kidato cha Nne 2023 1

Nembo ya Mwalimu Makoba Open School yenye alama ya almasi na kitabu ndani yake.

Muda: Saa 3

Maelekezo

1. Karatasi hii ina sehemu A, B na C zenye jumla ya maswali 12.

2. Jibu maswali yote katika sehemu A na B na maswali matatu kutoka sehemu C.

3. Sehemu A in alama 15, sehemu B ina alama 40 na sehemu C ina alama 45.

4. Zingatia maelekezo ya kila sehemu na ya kila swali.

5. Simu za mkononi na vitu vyote visivyoruhusiwa havitakiwi katika chumba cha mtihani.

6. Andika namba yako ya mtihani katika kila ukurasa wa kijitabu chako cha kujibia.

Sehemu A (Alama 15)

Jibu maswali yote katika sehemu hii.

1. Chagua herufi ya jibu sahihi katika vipengele (i) hadi (x), kisha andika herufi ya jibu hilo kwenye kijitabu chako cha kujibia.

(i) “Kushindana na mtu aliyekuzidi kwa kila hali si busara.” Methali zifuatazo zinashabihisha kauli hii isipokuwa:

A Mwenye pesa si mwenzio B Nazi haishindani na jiwe C Chanda chema, huvikwa pete D mwenye nguvu mpishe E Maji yakija kasi yapishe

(ii) Bainisha sentensi yenye vielezi zaidi ya kimoja katika sentensi zifuatazo:

A vitabu vyangu vyote vimeibiwa na watoto wako.

B Mbuzi aliyepotea jana ameonekana asubuhi.

C Shule ngapi zinaweza kushiriki mashindano?

D Wengi walikuwa wanataka kwenda masomoni.

E Wanakijiji hawa wamefanya uchaguzi kwa amani.

(iii) Pande mbili zinazohusika katika lugha ya maandishi ni zipi?

A mwandishi na msikilizaji B Msikilizaji na msomaji C Mwandishi na mzungumzaji D Msomaji na msimuliaji E Msomaji na mwandishi.

(iv) Dhima ya vigelegele katika utendekaji wa sanaa za maonesho ni ipi?

A Kushirikisha na kuiondolea hadhira udhia wa kumsikiliza mtu mmoja.

B Hadhira kukata shauri juu ya mwendo wa kazi ya sanaa za maonesho.

C Kuweka alama za mapigo ya kimuziki katika kazi ya sanaa za maonesho.

D Kuonesha upeo wa furaha na burudani ya kazi ya sanaa za maonesho.

E Kuonesha mbwembwe katika kazi ya sanaa za maonesho.

(v) Njia ipi hutunza sauti pamoja na vidokezo vyake katika kuhifadhi kazi ya fasihi simulizi kati ya hizi?

A maandishi B Mikanda ya filamu C Mitandao D Kinasa sauti E Masimulizi

(vi) Kipi ni kipengele kinachohusu mjengeko wa kazi za fasihi?

A Mtindo B Muundo C Mandhari D Wahusika E Lugha

(vii) Utofauti wa kimatamshi, kimaumbo na matumizi ya maneno ya lugha kuu moja katika maeneo mbalimbali huitwa ___________

A lafudhi B lahaja C rejista D msimu E toni

(viii) Hamsini, laki, kasri na fikri ni miongoni mwa maneno yanayothibitisha kuwa Kiswahili ni________

A kiarabu B krioli C kibantu D pijini E chotara

(ix) Hoja za msingi zinazosema kuwa Kiswahili ni Kiarabu, zimeegemea katika___________

A msamiati na dini ya Kiislamu B msamiati C msamiati wa waarabu kuoa waafrika D dini ya kiislamu na biashara ya watumwa E msamiati na lugha za Kibantu

(x) Kiisimu, upi ni mtazamo sahihi kuhusu chimbuko la Kiswahili?

A Ngozini B Shungwaya kuu C kiarabu D pijini na krioli E Pwani ya Afrika mashariki

2. Oanisha maana za tamathali za semi zilizo katika orodha A na tamathali husika kutoka orodha B, kisha andika herufi ya jibu sahihi katika kijitabu chako cha kujibia.

Orodha A

Orodha B

(i) Ushangaaji wa jambo fulani, aghalabu huambatana na alama ya mshangao.

(ii) Ulinganishaji wa vitu viwili au zaidi vyenye sifa tofauti kwa kutumia viunganishi.

(iii) Uhuishwaji wa kitu kisicho binadamu kupewa uwezo wa kutenda kama binadamu.

(iv) Urudiaji wa neno, herufi au silabi ili kusisitiza jambo.

(v) Matumizi ya lugha ya kificho ili kupunguza ukali wa maneno.

A Tafsida

B Tashbiha

C Takriri

D Sitiari

E Tashihisi

F Tanakali sauti

G Nidaa

Sehemu B (Alama 40)

Jibu maswali yote katika sehemu hii.

3. Ukiwa kama Afisa Utalii katika eneo lako, pendekeza namna utakavyokuza na kueneza lugha ya Kiswahili kwa wageni katika vipengele (i) hadi (iv) na kutoa mfano kwa kila kimoja.

(i) Biashara

(ii) Utawala

(iii) Utamaduni

(iv) Mafunzo

4. Soma kifungu cha habari kifuatacho kisha jibu maswali yanayofuata:

Teknolojia ya habari na mawasiliano (TEKNOHAMA) hutumiwa kwa lengo la kurahisisha utendaji kazi; kuimarisha ufundishaji; uwazi na kuongeza ufanisi. TEKNOHAMA imetambuliwa na wataalamu wa elimu kuwa ni muhimu katika shughuli za ufundishaji na ujifunzaji. Lengo la kutumia TEKNOHAMA ni kurahisisha ufundishaji kwa sababu hudhihirishwa katika hali halisi kwa kutumia aina mbalimbali za TEKNOHAMA.

Dunia ya sasa imebadilika; na mambo ya kijamii na kiuchumi yanategemea sana mitandao ya kompyuta. Katika kipindi cha miongo mitano iliyopita mpaka sasa, matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano yamezidi kuenea katika elimu kote ulimwenguni.

Ili kufanikiwa ufundishaji wa mada mbalimbali, mwalimu anahitaji kutumia TEKNOHAMA kwa ajili ya kupata taarifa au habari kutoka vyanzo mbalimbali, kuendeleza ujifunzaji unaompa mwanafunzi nafasi ya kati na kumpa mwalimu jukumu la kuwa mlezi na mwenezi badala ya ule wa mjua vyote. Mwalimu wa karne hii anaweza kujihusisha na matumizi ya TEKNOHAMA katika ufundishaji wake darasani, hali inayoweza kumpa ahueni katika kazi yake.

Hata hivyo, katika nchi zinazoendelea walimu wengi hawatumii TEKNOHAMA katika ufundishaji. Hii inatokana na teknolojia hii kuhitaji muda, fedha na maarifa ya ziada kwa watumiaji. Hayo kwa jumla yanakwamisha utumiaji wa teknolojia hiyo katika elimu. Hivyo, hatuna budi kuhakikisha tunakabiliana na mambo hayo ili kuhakikisha teknolojia hiyo inatumika katika elimu ili kurahisisha mchakato wa ufundishaji na ujifunzaji.

Maswali

(a) Bainisha matumizi manne ya TEKNOHAMA katika mchakato wa ufundishaji na ujifunzaji kulingana na habari uliyosoma.

(b) Fupisha habari hiyo kwa maneno yasiyopungua 60 na yasiyozidi 70.

5. Jibu maswali haya:

(a) Kwa kutumia mfano mmoja kwa kila muundo, bainisha miundo minne ya kirai nomino.

(b) Changanua sentensi zifuatazo kwa njia ya jedwali:

(i) Umma unalalamika sana.

(ii) Simba ni mkali ila chui ndiye zaidi.

6. Toa maana ya maneno haya:

(a) Neno

(b) Kirai

(c) Kishazi

(d) Sentensi

7. “Upatanisho wa kisarufi ni kigezo kimojawapo kati ya vigezo vya kuunda ngeli za nomino.” Thibitisha dai hilo kwa kutunga sentensi ukitumia ngeli zifuatazo:

(i) U-I

(ii) LI-YA

(iii) U-ZI

(iv) I-ZI

8. Eleza tofauti za msingi mbili (2) zilizopo kati ya kirai na kishazi. Toa mifano miwili kwa kila tofauti.

Sehemu C (Alama 45)

Jibu maswali matatu kutoka katika sehemu hii.

9. Chama cha Walimu Tanzania kimeanzisha shindano la uandishi wa insha kuhusu manufaa ya elimu katika nchi ya Tanzania. Ukiwa miongoni mwa wanachama, andika insha isiyopungua maneno mia mbili na isiyozidi maneno mia mbili hamsini kuhusu shindano hilo.

10. “Matatizo ya mwanajamii huletwa na mwanajamii mwenyewe.” Thibitisha usemi huu kwa kutoa hoja tatu kwa kila riwaya kati ya riwaya mbili ulizosoma.

11. Tumia tamthiliya ya KILIO CHETU kuonesha jinsi ujinga ulivyozorotesha maendeleo katika jamii. Toa hoja sita

12. Jadili vipengele vitano vya fani vinavyopatikana katika kazi mbalimbali za fasihi kama: riwaya, tamthiliya, na mashairi.

Majibu

1

(i) C

(ii) B

(iii) E

(iv) D

(v) D

(vi) B

(vii) B

(viii) A

(ix) A

(x) E

2

(i) G

(ii) B

(iii) E

(iv) C

(v) A

3

(i) Kama Afisa Utalii, nitakuza na kueneza lugha ya Kiswahili kwa wageni katika biashara kwa kuhakikisha biashara inafanyika kwa lugha ya Kiswahili na wageni wote wanaojihusisha na biashara wafundishwa lugha hii.

(ii) Katika utawala nitakuza na kueneza lugha ya Kiswahili kwa kuhakikisha kwamba, shughuli zote za utawala, mfano mazungumzo ofisini na nyaraka mbalimbali zinawekwa katika lugha ya Kiswahili.

(iii) Katika utamaduni nitakuza na kueneza lugha ya Kiswahili kwa kuwaelimisha watu waupende na kujivunia utamaduni wao ikiwemo lugha ya Kiswahili.

(iv) Katika mafunzo nitahakikisha kwamba kuna vituo vingi vya mafunzo ya lugha ya Kiswahili ambapo wageni wataweza kujifunza bila kuwa na tatizo lolote.

4

(a) Matumizi manne ya TEKNOHAMA katika mchakato wa ufundishaji na ujifunzaji ni: kupata taarifa kutoka vyanzo mbalimbali, kuendeleza ujifunzaji unaompa mwanafunzi nafasi ya kati na kumpa mwalimu jukumu la kuwa mlezi na mwenezi badala ya ule wa mjua vyote, uwazi na kuongeza ufanisi, na kurahisisha utandaji kazi.

(b) TEKNOHAMA ni muhimu na haiepukiki kwa sababu ya faida zake ambazo ni kurahisisha mambo. Teknolojia ni jambo lililoingia kwa kasi duniani na sasa haikwepeki. Teknolojia imemsaidia mwalimu katika ufundishaji wake wa masomo.

Hata hivyo, kwa sababu ya umasikini, walimu wengi hawatumii teknolojia kama inavyotakiwa. Pamoja na changamoto hii ya umasikini, ni vyema masuluhisho yakatafutwa ili kuwezesha kupata faida za teknolojia.

5

(a) Miundo minne ya kirai nomino ni:

Nomino peke yake. Mfano: chaki, dada, Juma.

Nomino mbili au zaidi. Mfano: Baba na mama.

Nomino na kivumishi kimoja au kadhaa. Mfano: Mtu mnene.

Nomino na sentensi. Mfano: mtoto aliyemletea mama yake kuni jana.

Hiyo ndiyo miundo minne ya kirai nomino.

(b)

Sentensi ambatani

S1

 

S2

KN

KT

 

KN

KT

N

t

V

U

N

V

Simba

ni

mkali

ila

chui

ndiye zaidi

6

(a) Neno ni silabi au mkusanyiko wa silabi zinazotamkwa na kuandikwa na zinaleta maana. Mfano, mama.

(b) Kirai ni tungo yenye neno moja au zaidi lakini haina muundo wa kiima na kiarifu. Mfano, mtoto yule.

(c) Kishazi ni tungo yenye kitenzi ambacho chaweza kujitosheleza na kukamilisha ujumbe uliokusudiwa na mzungumzaji au kuwa na kitenzi kisichoweza kujitegemea chenyewe. Mfano, mbuzi aliyepotea.

(d) Sentensi ni tungo yenye kiima na kiarifu na inaleta maana. Mfano, mama anapika pilau jikoni.

7

(i) Mti umekauka. Miti imekauka.

(ii) Ua limenyauka. Maua yamenyauka.

(iii) Uzi umekatika. Nyuzi zimekatika.

(iv) Nguo imechanika. Nguo zimechanika.

8 Tofauti za msingi mbili zilizopo baina ya Kirai na Kishazi ni:

Kirai ni tungo yenye neno moja au zaidi lakini haina muundo wa kiima na kiarifu. Mfano, mtoto yule, lakini Kishazi ni tungo yenye kitenzi ambacho chaweza kujitosheleza na kukamilisha ujumbe uliokusudiwa na mzungumzaji au kuwa na kitenzi kisichoweza kujitegemea chenyewe. Mfano, mbuzi aliyepotea.

Kirai hakiwezi kujitegemea peke yake kikaleta maana. Kwa mfano, baba haileti maana iliyokamilika. Lakini kishazi kinaleta maana iliyokamilika kwa mfano, Mbuzi amepotea.

Jipatie Majibu yote ya Mtihani Huu, Wasiliana Nasi kwa Kugusa Hapa

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Risala | Kiswahili Kidato Cha Nne

Uhakiki wa Tamthiliya ya Kilio Chetu