Matumizi ya Sarufi | Kidato cha Tano na Sita

Maua
Sarufi ni utaratibu wa sheria au kanuni zinazowezesha muundo wa lugha kukubalika.

Matawi ya Sarufi

1. Sarufi matamshi (fonolojia)

Tawi hili la sarufi huhusu utaratibu wa mpangilio wa vitamkwa katika maneno ya lugha. Sauti zinazotolewa katika lugha ni irabu na konsonanti. Sauti hizi zinapotumiaka katika maneno ya lugha huitwa fonimu.
Fonimu ni kipashio kidogo cha kifonolojia kinachobadili maana ya neno.
Hivyo, tawi hili la fonolojia, limejikita katika matamshi ya maneno.

2. Sarufi maana (semantiki)

Tawi hili la sarufi hujihusisha na maana mbalimbali katika tungo. Maneno hubeba maana fulani, hivyo katika tawi hili, tunaweza kubaini maana yake.
Kwa mfano: Maana ya mbuzi ni mnyama afugwaye na aliyefanana na swala.

3. Sarufi miundo (sintaksia)

Tawi hili hujihusisha na mpangilio wa maneno katika kutengeneza sentensi. Ili kupata sentensi, ni lazima kufuata mpangilio sahihi vinginevyo sentensi hiyo haitaeleweka wala kukubalika kwa watumiaji wa lugha.
Kwa mfano: Mtoto Mzuri amecheza ngoma na sasa anakwenda kulala.
Sentensi hiyo imefuata muundo sahihi na hiyo inaifanya ieleweke.

4. Sarufi maumbo (mofolojia)

Hili ni tawi la sarufi ambalo linajihusisha na maneno na aina za maneno. Pia tawi hili huyatambulisha maumbo ya umoja, wingi n.k
Kwa mfano: mtu - watu
Katika mfano huo, m- ni umbo la umoja na wa- ni umbo la wingi.

Matumizi ya mofimu

Mofimu ni kipashio kidogo chenye maana ya kisarufia au kileksika. Kipashio hicho kinaweza kuwa sehemu ya neno au neno zima.
Mofimu zenye maana ya kileksika ni zile ambazo huwa haziongezwi kipashio kingine, kwa mfano: Baba, Mama, fikiri, bora.
Mofimu zenye maana ya kisarufi ni zile ambazo huambatana na vipashio vinginie ili viweze kuleta maana. Kwa mfano: m-toto, u-so-mi.
Mzizi wa neno ni sehemu ya neno inayobaki baada ya kuondoa viambishi vyote. Kwa mfano: -chez-

Dhima za mofimu

1.Kuonesha nafsi

Kwa mfano: Ninasoma - nafsi ya kwanza umoja

2.Kuonesha njeo

Alisoma - wakati uliopita

3.Kuwakilisha hali

Analima - hali ya kuendelea kwa tendo
Hulima - hali ya mazoea

4.Kuonesha udogo wa nomino

Kipaka

5.Kuonesha ukubwa wa nomino

Jitu

6.Kuonesha urejeshi wa mtendwa na mtendewa

Anaupanda - mtendwa
Aliniandika - mtendewa

7.Kuonesha kujirejelea

Ninajisomea

8.Kuonesha uyakinishi na ukanushi

Ninasoma - sisomi

9.Kuonesha kauli mbalimbali

Limwa - kauli ya kutendwa

10.Kuzalisha maneno ya lugha

Maneno mapya hupatikana kwa kubadili mofimu tegemezi. Kwa mfano: katika mzizi lim: tunapata maneno: analima, anayelima, analimisha, analimika, analimia n.k

Viambishi

Viambishi ni mofimu zinazowekwa kwenye mzizi wa neno na kukamilisha muundo wa neno hilo. Katika lugha ya Kiswahili, viambishi vinaweza kuwekwa kabla na baada ya mzizi wa neno. Kwa mfano katika neno ‘anacheza’ kuna viambishi awali na tamati navyo tutavifahamu baada ya kutazama aina za viambishi.

Aina za viambishi

1. Viambishi awali

Hivi ni viambishi ambavyo hutokea kabla ya mzizi wa neno. Viambishi hivi huweza kuwa vya: idadi, ukubwa wa nomino, udogo wa nomino, ukanushi, njeo n.k
Katika neno Wa-na-lim-a, wa, na , na ni viambishi awali.

2. Viambishi tamati

Hivi ni viambishi ambavyo huwekwa baada ya mzizi wa neno.
Kwa mfano: Shind-an-a, an na a, ni viambishi tamati.

Kauli za kiswahili

Katika lugha ya Kiswahili, kauli huhusisha uhusiano uliopo baina ya kiima na kitenzi. Mnyambuliko wa vitenzi huzalisha kauli tofauti tofauti kama hizi zifuatazo:

Kauli ya kutenda

- piga
- cheza

Kauli ya kutendwa

- pigwa
- somwa

Kauli ya kutendewa

- katiwa
- rukiwa

Kauli ya kutendeka

- fanyika
- shukika

Kauli ya kutendea

- pigia
- lalia

Kauli ya kutendesha

- imbisha
- limisha

Kauli ya kutendana

- pendana
- katana

Kauli ya kutendua

- tegua
- pangua

Kauli ya kutendama

Kauli hii hurejelea hali ambayo watu au vitu hunaswa mahali pamoja kwa muda na kwa namna ya msuguano.
- Gandama
- Fichama

Kauli ya kutendeana

- Chezeana
- Limiana

Kauli ya kutendeshwa

- Limishwa
- Chemshwa
Hizo ni baadhi tu ya kauli za lugha ya Kiswahili.

Ngeli za nomino

Ngeli ni utaratibu wa kuweka nomino katika makundi yanayofanana au yanayowiana. Nomino za Kiswahili zinaweza kugawanywa katika makundi mbalimbali. Baadhi ya wanaisimu wamezigawanya nomino katika makundi 16 na wengine makundi 9 na wengine makundi 18.

Ngeli kwa mtazamo wa Kimapokeo/maumbo

Hiki ni kigezo kikongwe zaidi kilichotumiwa na wanasarufi mapokeo, miongoni mwao akiwa Meinhof ambao waliyaainisha majina kulingana na maumbo ya viambishi awali vya nomino. Nomino zote zote zilizokuwa na viambishi awali vinavyofanana viliwekwa katika kundi moja na kufanya ngeli moja. Kutokana na kigezo hiki kuna ngeli 18 za kiswahili.

Ngeli
Sifa za nomino za ngeli
Mfano wa nomino za ngeli
1. -Mu-
2. -Wa-
I. Nomino za viumbe vyenye uhai isipokuwa mimea.
II. Nomino zinazotokana na vitenzi vinavyowataja watu.
Mzee - wazee
Mtoto - watoto
Mfugaji - wafugaji
Mchezaji - wachezaji
3. -M-
4. -Mi-
I. Nomino za mimea
II. Nomino za vitu zinazoanza na m-
III. Nomino za matendo zinazoanza na m-
Mti - miti
Mpera - mipera
Mto - mito
Mwiko - miiko
Mchezo - michezo
5. -Ki
6. -Vi
I. Nomino za vitu zinazoanza na Ki (umoja) na Vi (wingi)
II. Nomino za vitu zinazoanza na ch (umoja) na vy- (wingi).
III. Nomino za viumbe zinazoambishwa na Ki- ya kudunisha
Kiti - viti
Chakula - vyakula
Kitoto - vitoto
7. -Ji-
8. -Ma-
I. Nomino zinazoanza na Ji- (umoja) na ma- (wingi)
II. Nomino za sehemu za mwili wa binadamu na mti
III. Nomino za mkopo zenye ma (wingi)
IV. Nomino zenye kuelezea dhana ya wingi japokuwa hazihesabiki.
Jiwe - mawe
Goti - magoti
Shati - mashati
Maji, mate, maisha…
9. -N-
10. 
I. Nomino ambazo huanza na N inayofuatwa na konsonanti, ch, d, g, j, z na y katika umoja na wingi.
ii. Nomino zinazoanza na Mb- au Mv.
iii. Nomino za mkopo
Zingatia: maumbo yote ya nomino hizi hayabadiliki kwa umoja na wingi.
Nguo, nchi, njaa
Mbuga, mboga, mvua

11. -U-
12. -N-
I. Nomino zote zinazoanza na u-umoja na N wingi.
Uso - nyuso
Uzi - nyuzi
13. -U-
14. -Ma-
Nomino zote zinazoanza na u (umoja) na ma (wingi).
Uasi - maasi
Ugonjwa - magonjwa
15. -ku-
Nomino zinazotokana na vitenzi zinazoanza na Ku- (vitenzi jina)
Kusoma
Kucheza
Kuimba
kuruka
16. PA
Huonesha mahali hasa
pahala
17. -Mu-
Huonesha mahali pa ndani
Muhali-
18. -ku-
Huonesha mahali pa mbali au mahali pakubwa zaidi au hat mahali popote.
Kuhali (kwenu)
Wanaisimu wengine kama Ashton na Broomfield waliainisha nomino baada ya Meinhof. Walifuata mtindo wa Meinhof isipokuwa waliziweka katika ngeli moja nomino za umoja na wingi ambazo zinachangia mzizi mmoja baada ya kuziona kuwa ni tofauti. Kwa uainishaji huu, walipunguza idadi ya ngeli hadi kufikia 9 tu.

Ngeli
Mifano ya nomino
1. Mu/Wa
Mtoto - watoto
Mpishi - wapishi
2. M/Mi
Mti - miti
Mwembe - miembe
3. Ki/Vi
Kiti - viti
Kitabu - vitabu
4. -N-
Ngozi, nyota
5. Ji/Ma
Jiwe - mawe
Jino - meno
6. U/N
Uzi - nyuzi
Uso - nyuso
7. U/Ma
Ugonjwa - ugonjwa
Uasi - maasi
8. Ku
Pa
Mu
Mahali: kule, pale, mle
9. Ku
Kuimba, kucheza, kuoga, kupiga…

Ubora wa kigezo cha kimofolojia/kimapokeo

1. Inasaidia kuonesha uhusiano uliopo kati ya lugha za kikoa kimoja. Kigezo hiki kinasaidia kuthibitisha kuwa, Kiswahili ni kibantu.
2. Husaidia kuonesha umoja na wingi katika nomino za kiswahili. Kwa mfano: mtoto - watoto.

Udhaifu wa kigezo cha kimofolojia

1. Baadhi ya nomino huwa na viambishi vya umoja na wingi ambavyo ni tofauti na viambishi vinavyoitambulisha ngeli hiyo.

Mfano:
KI-VI
Chakula - vyakula
JI-MA
Jambo - mambo
Ngeli hizo hapo juu, mianzo yake ni tofauti na kitambulisho cha ngeli.

2. Baadhi ya nomino hazina viambishi vyovyote

Nomino hizi hazipaswi kuingizwa katika kundi lolote, lakini ziliingizwa katika ngeli fulani fulani.
Kwa mfano nomino za kigeni ambazo hazina viambishi ziliingizwa katika ngeli ya N-, sahani, baiskeli, eroplane n.k.

3. Kuna viambishi vinavyofanana

Kwa mfano, ngeli ya kwanza inawakilishwa na kiambishi Mu-, kiambishi hiki kinajitokeza vilevile katika ngeli ya 3 na 17. Hali kadhalika vile vya ngeli ya 9 na 10,vyote vinawakilishwa na kiambishi N-. Nazo ngeli za 11 na 13 zinawakilishwa na kiambishi U-.

Kigezo cha kisintaksia/ Upatanisho wa kisarufi

Huu ni mtazamo wa kisasa wa uainishaji wa ngeli ambao umezigawa nomino katika makundi kulingana na upatanisho wa kisarufi kati ya nomino na viambishi awali vilivyo katika vitenzi, yaani vipatanishi.

Ngeli katika kigezo hiki ni hizi zifuatazo:

1. YU/A-WA

Mtu anatembea - watu wanatembea
Mtoto yu aja - watoto wanakuja

2. U-I

Mti umekauka - miti imekauka

3. LI-YA

Ua limenyauka - maua yamenyauka

4. KI-VI

Kitabu kimechanika - vitabu vimechanika

5. I-ZI

Nguo imechanika - nguo zimechanika

6. U-ZI

Uzi umekatika - nyuzi zimekatika

7. U-YA

Ugonjwa umeenea - magonjwa yameenea

8. KU-

Kuimba kunafurahisha

9. PA/MU/KU

Mahali pale panafaa
Mahali mle mnafaa
Mahali huku kunafaa

Faida za kigezo cha kisintaksia

1. Kila nomino ina kipatanishi katika kitenzi
2. Mwainisho wa upatanisho wa kisarufi hautatanishi kwa kuwa kiambishi awali huwa bayana sana kama kinarejelea kiumbe chenye uhai, kisicho na uhai au hali. Kwa mfano: ameanguka (mtu, mnyama) umeanguka (ukuta, mti, unyayo)

Matatizo ya kigezo hiki

1. Kuna vipatanishi vinafanana katika ngeli hizi. Kwa mfano, ngeli ya 2, 6, na 7 katika umoja zote zinawakilishwa na kiambishi cha ngeli u-
2. Katika ngeli ya kwanza, kipatanishi cha umoja YU ni cha kilahaja zaidi na siyo Kiswahili sanifu. Kwa mfano, mtoto yu aja.
3. Huziweka nomino za maumbo tofauti katika ngeli moja. Kwa mfano: mtu, ndege, ng’ombe, mdudu n.k

Matumizi ya Orejeshi

Orejeshi ni kiambishi kinachotumiwa kurejelea kwenye nomino ambayo huwa imetajwa kabla ya kitenzi chenyewe kutajwa.
Kwa mfano:
Uliyemtaka amelala.
Walichokula ni wali maharage

Utokeaji wa umbo la orejeshi katika ngeli za nomino

Umbo la orejeshi huweza kutokea katika mazingira haya:

1. Katikati

Mtoto aliyekuja jana amelala sokoni.
Kisu kilichonunuliwa ni butu sana.

2. Mwishoni

Jino liumalo hutolewa.
Chui akimbiaye ni mwoga.
Mtoto asomaye hufaulu.

3. Orejeshi inayopachikwa kwenye mzizi wa amba-

Kitabu ambacho umesoma kimechanika
Juma amepewa adhabu ambayo itamtesa sana.
Mtoto ambaye atafaulu atapewa zawadi.

Dhima za umbo la orejeshi katika tungo za Kiswahili

1. Hutumika kama kirejeshi

O rejeshi hurejelea kwa mtendwa au mtenda.
Kwa mfano:
Wazee waliolala.

2. Hudokeza mahali

Hudokeza mahali ambapo kitendo kimefanyika. Vidokezo vya mahali ni: po, ko na mo.
Kwa mfano:
Alipokaa ni pabaya.
Alikoenda hapajulikani.
Alimolala mna maajabu.
Po hudokeza mahali dhahiri.
Ko hudokeza mahali pasipo dhahiri.
Mo hudokeza mahali ambapo ni ndani ya kitu.

3. Hudokeza wakati

Hudokeza wakati kitendo kilipofanyika.
Kwa mfano:
- Tulipotoka walifunga mlango.
- Utakapomuona umpige risasi.

4. Hutumika kama kiunganishi

O rejeshi hutumiwa katika kitenzi cha kishazi tegemezi ili kukiunga na kitenzi kikuu cha kishazi huru ambavyo kwa pamoja huunda sentensi changamano.
Kwa mfano:
Mtoto aliyekuja jana ameondoka.
Ye imetumika kuunga sentensi, mtoto amekuja na mtoto ameondoka.

5. Hudokeza namna

Hudokeza namna au jinsi kitendo kilivyofanyika ama mtu au kiitu kilivyo na huundwa na kirejeshi -vyo-.
Kwa mfano:
Anavyocheza anafurahisha watazamaji.
Anavyovaa anachukiza walimu.

Makosa ya Kisarufi na Kimantiki Katika Lugha

Watumiaji wa lugha hufanya makosa mbalimbali watumiapo lugha. Ni jambo lisilowezekana kukosa makosa katika lugha fulani.

Makosa ya kisarufi

Makosa haya huangazia matamshi, maumbo na miundo ya tungo. Makosa ya kisarufi yanajumuisha:

1. Makosa ya msamiati

Katika kipindi cha mazungumzo, wazungumzaji huchanganya msamiati kama inavyooneshwa katika mfano:
Kuchanganya neno ‘nona’ na ‘nenepa’
Kwa mfano: siku hizi umenona sana. Hii siyo sahihi kwa sababu mtu husemwa amenenepa na mnyama ndiye hunona.
Kuchanganya neno ‘mazingira’ na ‘mazingara.’
Makosa ya kimsamiati yanasababishwa na:
- mzungumzaji kutokuwa na ujuzi wa kutosha wa lugha anayotumia.
- utani miongoni mwa watu.

2. Makosa ya kimuundo

Haya ni makosa ambayo hutokea katika muundo wa sentensi za kiswahili. Kwa kawaida sentensi huanza na nomino na huwa na vitenzi.
Kwa mfano:
Paka mweusi amemkamata panya kwa haraka.
Kosa la kimuundo linakuwa: mweusi paka amemkamata panya kwa haraka.
Pia, kuna makosa katika upatanisho wa kisarufi.
Kwa mfano:
Ni makosa kusema, ‘sikuwa ninajua kuwa Tunu ni dada yako.’ sahihi ni, ‘sikujua kuwa Tunu ni dada yako.’
Sisi sote tunapenda nyama - sisi wote tunapenda nyama.
Kalamu yangu imeibiwa - kalamu yangu imeibwa.
Nimekuja hapa ili kusudi niongee na ninyi - nimekuja hapa kusudi niongee na ninyi.

3. Makosa ya matamshi

Wakati mwingine watu hushindwa kutamka maneno ya Kiswahili au huchanganya na kubadili sauti za lugha.
Mifano: wakurya hutumia r badala ya l. Mimi ninaenda kurara badala ya kulala.
Wandali (Ileje) hutumia s badala ya z, dh na th. Selasini badala ya thelathini. Sahabu badala ya dhahabu.
Wapare hutumia ‘th’ badala ya ‘s’. thatha nakuelewa. Badala ya sasa.
Wanyakyusa hutumia ‘f’ badala ya ‘v’. hifi ni fiatu fyangu. Badala ya hivi ni viatu vyangu.
Makosa ya matamshi husababishwa na athari ya lugha mama.

4. Kosa la kuongeza vitamkwa

Baadhi ya wazungumzaji huongeza vitamkwa mahali visipotakiwa.
Mifano:
Amekwendaga kwao. Badala ya amekwenda kwao.
Mtoto msafi. Badala ya mtoto safi.

5. Kosa la kuacha maneno

Wazungumzaji wengine huacha maneno katika sentensi.
Damasi ameondoka kazini. Mzungumzaji anakusudia kusema Damasi ameondoka kwenda kazini.

6. Makosa ya tafsiri sisisi

Haya ni makosa yanayofanywa na mtu pale anapotafisiri neno kwa neno.
Mfano, neno la kiingereza wash out likitafsiriwa vibaya linaweza kuleta sentensi kama hii. Nyumba zimeoshwa na mvua.
Kosa jingine ni kutumia aidha…au. Wakati huu aidha yuko mjini au kazini. Sahihi ni wakati huu yuko ama kazini au mjini. Kosa hili limesababishwa na tafsiri sisisi ya neno la kiingereza, neither…nor.

Makosa ya Kimantiki

Haya ni makosa ambayo yamekosa mtiririko wa fikra zilizopangwa ili kujenga hoja yenye kukubalika.
Mifano:
Usimwage kuku kwenye mchele mwingi badala ya usimwage mchele kwenye kuku wengi.
Gari imeingia chui badala ya chui ameingia ndani ya gari.
Ili kuondoa makosa yanayotokea katika lugha, ni vyema msisitizo ukawekwa shuleni ili wanafunzi wazoee kuzungumza lugha sahihi.
Pia, changamoto kubwa ipo katika vyombo vya habari. Watangazaji wengi wamekuwa wakitangaza kwa kuchanganya kiswahili na kiiingereza, hii ni hatari kubwa kwa sababu hata katika vyombo vya habari vya serikali watangazaji wanafanya makosa ya kuchanganya Kiswahili na kiingereza. Ni vyema sheria kali zitungwe ili kuweza kunusuru lugha ya Kiswahili.

Aina za tungo

Tungo ni matokeo ya kupanga pamoja vipashio sahili ili kujenga kipashio kikubwa zaidi.
Aina za tungo ni:

Neno

Neno ni silabi au mkusanyiko wa silabi zinazotamkwa na kuandikwa na zinaleta maana. Mfano, mama.

Kirai

Ni tungo yenye neno moja au zaidi lakini haina muundo wa kiima na kiarifu. Mfano, mtoto yule.

Kishazi

Kishazi ni tungo yenye kitenzi ambacho chaweza kujitosheleza na kukamilisha ujumbe uliokusudiwa na mzungumzaji au kuwa na kitenzi kisichoweza kujitegemea chenyewe. Mfano, mbuzi aliyepotea.

Sentensi

Sentensi ni tungo yenye kiima na kiarifu na inaleta maana. Mfano, mama anapika pilau jikoni.

Aina za Virai

Kuna aina tano za Virai:
- Virai nomino
- Virai vitenzi
- Virai vivumishi
- Virai vielezi
- Virai viunganishi

Virai nomino

Kirai nomino ni kirai ambacho muundo wake umekitwa kwenye nomino.

Miundo ya Virai nomino

I. Nomino peke yake. Mfano: chaki, dada, Juma.
II. Nomino mbili au zaidi. Mfano: Baba na mama.
III. Nomino na kivumishi kimoja au kadhaa. Mfano: Mtu mnene.
IV. Nomino na sentensi. Mfano: mtoto aliyemletea mama yake kuni jana.
V. Nomino, kivumishi na sentensi. Mfano: kijana yule mrefu aliyemnunulia mwanangu soda jana asubuhi.
VI. Nomino na Kirai kivumishi. Mfano: mzee mwenye duka kubwa kabisa kule kijijini.

Miundo ya virai vitenzi

I. Kitenzi peke yake. Mfano, amekufa.
II. Kitenzi na nomino moja. Mfano, amempiga Juma.
III. Kitenzi na nomino mbili. Mfano, amempa mtoto chakula.
IV. Kitenzi na kitenzi. Mfano, anapenda kusoma.
V. Kitenzi na nomino na kitenzi. Mfano, anamfundisha mtoto kusoma.

Miundo ya virai vivumishi

I. Kivumishi na kielezi chake. Mfano, zuri kabisa.
II. Kivumishi na kirani nomino. Mfano, enye duka kubwa.
III. Kivumishi na kirai kitenzi. Mfano, enye kupenda mambo makubwa.
IV. Kivumishi na kirai kivumishi. Mfano, mwingine mwenye matatizo.
V. Kivumishi na kirai kiunganishi. Mfano, zuri wa kutamanika.

Aina za vishazi

Kuna aina mbili za vishazi:
1. Kishazi huru
Hiki ni kishazi kinachotawaliwa na kitenzi kikuu.
Mfano
Anacheza mpira.
2. Kishazi tegemezi
Hiki ni kishazi ambacho kinatawaliwa na kitenzi kisaidizi.
Mfano
Mwalimu aliyefundisha darasani

Aina za vishazi tegemezi

Vishazi tegemezi vivumishi
Hivi ni vishazi ambavyo hufanya kazi ya vivumishi.
Mfano
Samaki aliyepotea jana
Vishazi tegemezi vielezi
Vishazi hivi hufanya kazi ya vielezi katika tungo.
Mfano
Kijana alilala aliposemwa

Muundo wa sentensi

Sentensi ina sehemu kuu mbili:
Kiima
Ni sehemu katika sentensi inayojaza nafasi ya mtenda au mtendewa wa jambo linaloelezwa.
Mfano
Baba anacheza mpira
Kiarifu
Ni sehemu katika sentensi inayojazwa na maneno yanayoarifu tendo lililofanywa, linalofanywa na litakalofanywa.
Mfano
Juma ni mkulima.

Dhima za Vishazi

1. Kufanya kazi ya kivumishi katika tungo.
Mfano, chakula kilichopikwa jana
2. Kufanya kazi ya vielezi katika tungo.
Mfano, mtoto alilia alipopigwa.

Uchanganuzi wa sentensi

Uchanganuzi wa sentensi ni kitendo cha kuigawa sentensi katika sehemu mbalimbali ambazo huunda sentensi hiyo.

Hatua muhimu katika uchanganuzi wa sentensi

1. Taja aina ya sentensi, kama ni sahili, ambatano au changamano.
2. Taja sehemu zake kuu, yaani kiima na kiarifu.
3. Taja sehemu kuu za kiima na kiarifu au za kirai nomino na kirai kitenzi.
4. Taja aina zote za maneno zilizomo katika sentensi hiyo.
5. Iandike upya sentensi hiyo.

Maswali ya uchanganuzi wa sentensi

Tumia maarifa uliyoyapata kidato cha nne, kujibu maswali haya ya uchanganuzi wa sentensi:
1. Katika sentensi hizi, kila sentensi ichanganue kwa njia ya mishale, matawi, maneno na visanduku:
I. Zacharia ni mtu mkarimu sana.
II. Mtoto aliyekimbia shule, amerudi mjini.
III. Baba anacheza na mama anapika.

Uundaji wa maneno

Uundaji wa maneno ni utengenezaji wa maneno mapya katika lugha.

Sababu za uundaji wa maneno

1. Kukuza msamiati kwa ajili ya matumizi ya lugha ya kila siku.
2. Kuweza kutafsiri mengi kutoka lugha yako au ya kigeni.
3. Kupata msamiati utakaokubalika katika shughuli mahususi za kila siku. Mfano: benki, forodhani au jeshini.
4. Kukuza msamiati ili utumike katika masuala ya kitaifa kama utamaduni.

Njia mbalimbali za uundaji wa maneno

1. Kutohoa

Kutohoa ni njia ya kuchukua maneno katika lugha nyingine na kuyaingiza katika lugha nyingine. Kiswahili kimetohoa neno la kiingereza ‘tractor’ na kuwa trekta. Neno la kireno bibo. Neno la kijerumani ‘pilao’ na kuwa ‘pilau’ na maneno mengi kutoka lugha nyingi.

2. Miambatano

Ni njia ya uundaji wa maneno ambayo huunga maneno mawili au zaidi kutengeneza neno jipya.
Mfano
Mwananchi, mchezakwao, mpigamaji, njugumawe n.k

3. Mpangilio tofauti wa mofimu

Mfano, neno lima likibadilishwa mpangilio, linatoa maneno mengine kama: mali, imla, lami, mila, n.k

4. Kufananisha sauti, umbo, sura au tabia

Mifano: pikipiki, mtutu, nyau, kifaru, beberu (mtu anayeonea wengine).

5. kufupisha maneno

Kwa mfano, shemeji - shem, Dar es Salaam - Dar, Televisheni - TV, Baraza la Mitihani la Taifa - BAMITA n.k

6. Urudufishaji

Mifano: polepole, nungunungu, kiwiliwili, kizunguzungu n.k

7. Kuambisha viambishi nyambuaji

Mifano, soma - msomi, taifa - taifisha, refu - refusha, haraka - harakisha n.k

Popular posts from this blog

Uhakiki wa Tamthiliya ya Kilio Chetu

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Hotuba