Ngeli za Nomino | Kiswahili Kidato cha Tatu

Matone yameungana

Ngeli ni utaratibu wa kuweka nomino katika makundi yanayofanana au yanayowiana. Nomino za Kiswahili zinaweza kugawanywa katika makundi mbalimbali. Baadhi ya wanaisimu wamezigawanya nomino katika makundi 16 na wengine makundi 9 na wengine makundi 18.

Ngeli huweza kuainishwa kwa vigezo mbalimbali. Miongoni mwa vigezo hivyo ni kigezo cha upatanishi wa kisarufi au kigezo cha kisintaksia.

Upatanishi wa kisarufi ni hali ya viambishi vya maneno ndani ya tungo kukubaliana na kushikamana ili kuleta maana iliyokusudiwa. Upatanishi wa kisarufi unaweza kuonekana kati ya vipashio mbalimbali vya tungo:

Mifano:

Unyasi umeota.   =    Nyasi zimeota.

Kiazi  kitamu.  =   Viazi vitamu.

Huyu mnene.   =   Hawa wanene.

Huyu anakuja.  =   Hao wanakuja.

Mtu ambaye.  =  Watu  ambao.

Mtu aliyesafiri. = Watu waliosafiri.

Aina za tungo

Tungo ni matokeo ya kupanga pamoja vipashio sahili ili kujenga kipashio kikubwa zaidi.

Aina za tungo ni:

Neno

Neno ni silabi au mkusanyiko wa silabi zinazotamkwa na kuandikwa na zinaleta maana. Mfano, mama.

Kirai

Ni tungo yenye neno moja au zaidi lakini haina muundo wa kiima na kiarifu. Mfano, mtoto yule.

Kishazi

Kishazi ni tungo yenye kitenzi ambacho chaweza kujitosheleza na kukamilisha ujumbe uliokusudiwa na mzungumzaji au kuwa na kitenzi kisichoweza kujitegemea chenyewe. Mfano, mbuzi aliyepotea.

Sentensi

Sentensi ni tungo yenye kiima na kiarifu na inaleta maana. Mfano, mama anapika pilau jikoni.

Aina za Virai

Kuna aina tano za Virai:

- Virai nomino

- Virai vitenzi

- Virai vivumishi

- Virai vielezi

- Virai viunganishi

Virai nomino

Kirai nomino ni kirai ambacho muundo wake umekitwa kwenye nomino.

Miundo ya Virai nomino

I. Nomino peke yake. Mfano: chaki, dada, Juma.

II. Nomino mbili au zaidi. Mfano: Baba na mama.

III. Nomino na kivumishi kimoja au kadhaa. Mfano: Mtu mnene.

IV. Nomino na sentensi. Mfano: mtoto aliyemletea mama yake kuni jana.

V. Nomino, kivumishi na sentensi. Mfano: kijana yule mrefu aliyemnunulia mwanangu soda jana asubuhi.

VI. Nomino na Kirai kivumishi. Mfano: mzee mwenye duka kubwa kabisa kule kijijini.

Miundo ya virai vitenzi

I. Kitenzi peke yake. Mfano, amekufa.

II. Kitenzi na nomino moja. Mfano, amempiga Juma.

III. Kitenzi na nomino mbili. Mfano, amempa mtoto chakula.

IV. Kitenzi na kitenzi. Mfano, anapenda kusoma.

V. Kitenzi na nomino na kitenzi. Mfano, anamfundisha mtoto kusoma.

Miundo ya virai vivumishi

I. Kivumishi na kielezi chake. Mfano, zuri kabisa.

II. Kivumishi na kirani nomino. Mfano, enye duka kubwa.

III. Kivumishi na kirai kitenzi. Mfano, enye kupenda mambo makubwa.

IV. Kivumishi na kirai kivumishi. Mfano, mwingine mwenye matatizo.

V. Kivumishi na kirai kiunganishi. Mfano, zuri wa kutamanika.

Aina za vishazi

Kuna aina mbili za vishazi:

1. Kishazi huru

Hiki ni kishazi kinachotawaliwa na kitenzi kikuu.

Mfano

Anacheza mpira.

2. Kishazi tegemezi

Hiki ni kishazi ambacho kinatawaliwa na kitenzi kisaidizi.

Mfano

Mwalimu aliyefundisha darasani

Aina za vishazi tegemezi

Vishazi tegemezi vivumishi

Hivi ni vishazi ambavyo hufanya kazi ya vivumishi.

Mfano

Samaki aliyepotea jana

Vishazi tegemezi vielezi

Vishazi hivi hufanya kazi ya vielezi katika tungo.

Mfano

Kijana alilala aliposemwa

Muundo wa sentensi

Sentensi ina sehemu kuu mbili:

Kiima

Ni sehemu katika sentensi inayojaza nafasi ya mtenda au mtendewa wa jambo linaloelezwa.

Mfano

Baba anacheza mpira

Kiarifu

Ni sehemu katika sentensi inayojazwa na maneno yanayoarifu tendo lililofanywa, linalofanywa na litakalofanywa.

Mfano

Juma ni mkulima.

Dhima za Vishazi

1. Kufanya kazi ya kivumishi katika tungo.

Mfano, chakula kilichopikwa jana

2. Kufanya kazi ya vielezi katika tungo.

Mfano, mtoto alilia alipopigwa.

Uchanganuzi wa sentensi

Uchanganuzi wa sentensi ni kitendo cha kuigawa sentensi katika sehemu mbalimbali ambazo huunda sentensi hiyo.

Hatua muhimu katika uchanganuzi wa sentensi

1. Taja aina ya sentensi, kama ni sahili, ambatano au changamano.

2. Taja sehemu zake kuu, yaani kiima na kiarifu.

3. Taja sehemu kuu za kiima na kiarifu au za kirai nomino na kirai kitenzi.

4. Taja aina zote za maneno zilizomo katika sentensi hiyo.

5. Iandike upya sentensi hiyo.

Kuchanganua sentensi kwa njia ya majedwali

Mama anapika chakula.

Sentensi Sahili

KN

KT

N

T

N

Mama

anapika

Chakula.


Simba aliyeunguruma, amerudishwa mbugani.

Sentensi Changamano

KN

KT

N

TS

T

E

Simba

aliyeunguruma

amerudishwa

Mbugani.

Mama anapika chakula na baba anafua nguo.

Sentensi Ambatano

S1

 

S2

KN

KT

 

KN

KT

N

T

N

U

N

T

N

Mama

anapika

chakula

na

baba

anafua

Nguo.

Maswali Ya Kiswahili Kidato cha Tatu Mada ya Ngeli za Nomino

1.   Upatanisho wa kisarufi hufanya nomino mbalimbali kuwa katika kundi moja. Fikiria nomino tano na kwa kutumia sentensi moja kwa kila nomino zipange katika makundi yake.

2.   Uchanganuzi wa sentensi hufanyika hatua kwa hatua. Ukitumia hatua hizo changanua sentensi ifuatayo kwa njia ya jedwali Wale wawili watakuwa wamepimwa virusi vya UKIMWI hivyo afya zao zitakuwa nzuri.

3.   Eleza tofauti za msingi mbili (2) zilizopo kati ya kirai na kishazi. Toa mifano miwili kwa kila tofauti.

4.   Ni kigezo kipi kinachotumika katika kuunda ngeli za kimapokeo? Dhihirisha utumiaji wa kigezo hicho kwa kutunga sentensi tano (5) za ngeli tofauti.

5.   Eleza maana ya upatanisho wa kisarufi. Fafanua jibu lako kwa kutoa mifano minne.

6.   Kwa kutumia mifano, taja miundo mitano ya kirai nomino.

7.   “Upatanisho wa kisarufi ni kigezo kimojawapo kati ya vigezo vya kuunda ngeli za nomino.” Thibitisha dai hilo kwa kutunga sentensi ukitumia ngeli zifuatazo:

(a) UI

(b) LIYA

(c) UZI

(d) IZI

(e) UYA

8.   Katika kila sentensi uliyopewa, orodhesha vishazi huru katika Safu A na vishazi tegemezi katika safu B.

(a) Ngoma hailii vizuri kwa kuwa imepasuka.

(b) Watoto walioandikishwa watakuja kesho.

(c) Kiongozi atakayefunga mkutano amepelekewa taarifa.

(d) Mtawatambua walio wasikivu.

(e) Kitabu ulichopewa kina kurasa nyingi.

9.   Fafanua dhana zifuatazo kisha tunga sentensi moja kwa kila dhana:

a)   Kirai

b)   Kishazi

c)   Sentensi

10.       Tunga tungo moja kwa kila kipengele (i) – (iv) ukizingatia viambajengo vya kila moja:

     I.        Kishazi tegemezi + Kishazi huru

   II.        Kishazi huru

  III.        Kishazi tegemezi

 IV.        Kishazi huru + Kishazi huru

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024

Jinsi ya Kuandika Risala | Kiswahili Kidato Cha Nne