Uhakiki wa Tamthiliya ya Shujaa Mirambo

Ganda la kitabu cha shujaa mirambo
Wasiliana na Mwalimu ili Kujiunga Darasa la Uhakiki wa Vitabu vyote vya Fasihi Mtaala Mpya kwa Kugusa Hapa

Mwandishi: Emmanuel Mbogo

Mwaka: 2021

Utangulizi

Tulikaa kwa utulivu ndani ya ukumbi wa TASUBA, tulitazama mbele kwa utulivu tukiwatazama waigizaji wakiigiza tamthiliya maarufu iliyoandikwa na Profesa Aldin Mutembei, ikaporwa na kuuziwa Medical Aid Foundation, tamthiliya yenyewe iliitwa Kilio Chetu. Pembeni yangu alikaa Emmanuel Mbogo ambaye ndiye aliyewaleta waigizaji wale na aliwaongoza katika uigizaji wao. Mbogo alivalia suruali pana ya jinzi, hata shati lake nalo lilikuwa pana. Kama ungetaka kuyafahamu mapana na marefu, basi ungemtazama Mbogo ungeyaona siku hiyo.

Hatukuongea neno, tulitazama onyesho lile bila ya sisi kutazamana. Sikuwa na jambo la kuongea na Emmanuel Mbogo, wakati elimu ilitufanya Mimi Mwalimu Makoba, Mugyabuso Mulokozi, Wole Soyinka na wasomi wengi wanaofikiri sawasawa tuufahamu ukweli kwamba dini za kigeni zilitumika kufuta utambulisho, utamaduni, na mfumo wa fikra wa Mwafrika,  tulihisi Profesa Emmanuel Mbogo bado alizikumbatia dini hizi, uandishi wake unaotumia mtindo wa kibiblia unaleta mashaka mengi kama Mbogo ni mwenzetu au mtetezi wa ushirikina wa kigeni!

Kuhusu Tamthiliya ya Shujaa Mirambo

Hii ni tamthiliya ya kihistoria inayozungumzia kisa cha mtemi Mirambo aliyepata kutawala Unyamwezi mnamo mwaka 1860 mpaka 1864.

Katika utawala wake, Mirambo alitoza kodi kwa yeyote aliyepita Unyamwezi. Waarabu walikasirishwa na jambo hili, wakaanzisha naye vita, hata hivyo kwa ushujaa mkubwa, Mirambo alishinda vita hivyo na kuwafanya Waarabu waendelee kulipa kodi.

Mirambo anakumbukwa kwa namna alivyoiongoza himaya yake akishirikiana na jeshi lake la Lugaluga. Henry Morton Stanley alipomuona Mirambo alidiriki kumfananisha na Napoleon Bonaparte.

Maudhui

Vipengele mbalimbali vya maudhui vimejadiliwa:

Dhamira

Dhamira nyingi zinajitokeza katika tamthiliya hii, miongoni mwazo ni:

Kodi

Mirambo alitoza kodi kwa kila mgeni aliyepita katika eneo lake. Mgogoro wake na Waarabu ulisababishwa na wao kukataa kulipa kodi wakitaka wafanye biashara bila ya kulipa kodi.

Upande wa Unyanyembe alikotawala Mtemi Fundikira, mwarabu hakulipa kodi, Fundikira hakuwa na uchungu na eneo lake na aliruhusu wageni wafanye wanavyotaka kwa sababu tu alipewa zawadi ya tende na kashata.

Henry Morton Stanley aliingia katika mgogoro na Mirambo kwa sababu alizuiwa kupita mpaka alipe kodi. Stanley hakuwa tayari kulipa kodi kwa sababu hakuwa mfanyabiashara, kwa ushujaa mkubwa, Mirambo alimzuia Stanley asipite katika eneo lake na badala yake alirudi unyanyembe.

Vita

Vita kati ya Mirambo na waarabu ilitokea kwa sababu Mirambo alitoza kodi. Mwarabu hakuwa tayari kulipa kodi, akaanzisha matata yaliyozaa vita, hata hivyo, Mwarabu aliishia kunyolewa ndevu zake.

Vita vingine vinaonekana kati ya Mirambo na Wafipa. Wafipa ndiyo walioanzisha matata kwa kumteka Mwanagwa mtoto wa kike wa Mirambo, na kuondoka naye.

Dini za kigeni

Tunaziona dini za kigeni zikiingia kwa kasi. Huko Unyanyembe Uislamu umeingia na Ukiristo nao umo.

“Waarabu na msikiti wao na wazungu na kanisa lao. Baadhi yetu wameanza kujiunga na ibada za miungu hii ya kigeni,” uk 17.

Mtemi Fundikira ameozesha binti yake kwa Mwarabu, watoto waliozaliwa wanafundishwa dini ya kiislamu na wanajua kusoma aya za Kurani Tukufu. Jambo hili ni ajabu kufanywa na Mnyamwezi mwenye miungu yake!

“Sasa ni wakati wa kuwashangaza. Namkaribisha mtoto Ishumael, atusomee mistari michache toka aya ya Kurani Tukufu,” uk 25.

Usaliti

Mtemi Fundikira amewasaliti wana Unyanyembe. Kwa sababu ya tamaa ya mali, anaamua kushirikiana na warabu.

“Mimi! Mimi Mzelo nilimkanya sana Mtemi Fundikira. Nikamwambia wacha! Kataa! Usimtoe binti yako Kalunde kuolewa na Mohamed, na mwarabu yule. Hayo siyo mapenzi. Hiyo ni njama ya mtego wa kumnasa tembo. Lakini Fundikira aliziba masikio yake hakunisikia. Moyo wake wa tamaa ya mali, bahashishina unafiki wa tahbasamu ndani na nje ya moyo wake. Sasa tazama leo: Unyanyembe ina watawala wawili, mtemi Fundikira mwenyewe, lakini Sultani Bargash tayari keshamleta Liwali Said Bin Salim kuwa mtawala ubia na Fundikira,”uk 18.

Usaliti wa Fundikira hauishii kwa watu wake tu, bali amemsaliti ndugu yake Mtemi Mirambo, anashirikiana na Warabu na anapanga mipango ya kumwangamiza.

Maendeleo ya teknolojia

Tunayaona maendeleo ya teknolojia katika himaya ya Mirambo. Mtaalamu Kinombo anahusika na utengenezaji wa bunduki kama zile zinazotumiwa na Warabu. Suala hili linaonyesha namna ambavyo wanyamwezi walikuwa wamepiga hatua kimaendeleo enzi za Mtemi Mirambo.

Vita vya kiuchumi

Warabu wanapigana vita vya kiuchumi dhidi ya Mirambo. Mirambo anawatoza kodi nao hawataki kulipa.

Warabu wanaupata upande dhaifu, nao ni upande wa Mtemi Fundikira, huko wanafanya biashara bila ya kulipa kodi.

Anapofariki Fundikira, Sabila anarithi kiti chake. Sabila anakataa kushirikiana na Warabu, wanakasirika na kumfanyia njama inayoondoa maisha yake. Anaingia Msakiwa ambaye anafanya kazi kwa maslahi ya Warabu.

Msakiwa akishirikiana na Warabu wenye tamaa na utajiri wa Afrika, anaanzisha vita na Mirambo, anajuta kuanzisha vita hivyo kwani yeye na Warabu wanashindwa vibaya.

Maisha baada ya kifo

Waafrika waliamini katika maisha baada ya kifo hata kabla ya majilio ya dini za kigeni. Kwa mfano, Mtemi Mirambo aliamini katika maisha baada ya kifo, hili linathibitishwa baada ya Mirambo kumuua Lugaluga.

“Tazama! Umekuwa maiti. Marehemu. Una raha, kwani huko uliko nasikia hakuna njaa wala kiu!” uk 12.

Pia tunamuona Lugaluga akiwa na imani hii, anapouawa Sabila, Lugaluga anasema,

“Hapa alipolala Mtemi Sabila, hatapata majonzi tena, kwani roho yake sasa imeungana na umati wa wahenga, huko kunako dunia isiyo na kifo, wala makaburi, wala sanda, wala machozi. Bali raha mustarehe!” uk 51.

Ni wazi kuwa falsafa ya maisha baada ya kifo ipo Afrika tangu zamani na si mawazo yaliyoletwa na wageni. Ukweli wa falsafa hii ni ngumu kuthibitika, wapo wanaoamini kuwa, kifo ndiyo mwisho wa yote, na wengine ndiyo hao akina Mirambo na Lugaluga, wanaoamini katika maisha baada ya kifo, maisha yenyewe yanatajwa kuwa ni maisha ya starehe.

Falsafa hii ya maisha baada ya kifo inasababishwa na akili ya mwanadamu kukataa habari kuwa, ipo siku itafika mwisho na kifo ndiyo mwisho wake. Mawazo haya ni matokeo ya akili kujitengenezea mazingira ya kuishi milele, tarajio na tamanio la walio wengi! Uwezekano wa kuishi milele ni mdogo sana, dalili kubwa zinaonyesha kuwa kifo ndiyo mwisho, kwa kuwa ukweli huu ni mchungu, nadharia nyingi zimeundwa ili kuupoza.

Umoja

Mtemi Mirambo anatamani Afrika iwe na umoja. Anaamini kupitia umoja wangeweza kupambana na maadui zao.

“Kila siku naota ndoto ya umoja wetu. Umoja wa watu weusi. Makabila yote tuwe kitu kimoja,” uk 53.

Mirambo alitamani makabila yote yawe na mfalme mmoja. Mawazo haya ni mawazo safi na yaliyokuwa mbele ya muda. Hapana shaka Stanley alimfananisha Mirambo na Napoleon Bonaparte.

Mirambo anapoona dalili za kushambuliwa na Warabu, anatuma ujumbe kwa Nyungu ya mawe, hii yote ni kwa sababu aliamini katika umoja.

“Nahitaji kutuma ujumbe wa siri kwa ndugu na rafiki yangu Mtemi Nyungu ya Mawe. Wanasema umoja ni nguvu,” uk 92.

Dini za jadi

Waafrika walikuwa na dini zao kabla ya majilio ya wageni. Wageni ndiyo walioziharibu dini hizi. Tunamuona Mirambo na watu wake wakiamini katika dini za jadi. Mtemi huyu anaheshimu mizimu na anatoa sadaka katika kaburi la marehemu mama yake.

Mirambo alipiga ramli ili aweze kuona yajayo. Majilio ya dini mpya yalipoanza, Mtemi wa Unyamwezi hakufurahishwa na jambo hili.

“Wanataka sisi tuache miungu yetu, tumwabudu Mungu wao. Itakuwaje? Wazungu nao wameanza kuleta dini ya kanisa. Na Mungu wao anayeitwa Gesu,” uk 62.

Mzelo na Gwilo wana mashaka na dini hizi za kigeni. Hawaamini kama zinaweza kuwa na nguvu kushinda miungu yao.

“Kama tulivyosema; hatuwezi kutetemeshwa na viapo vya kitabu , dini ya mungu tusiyemjua. Sisi hatuabudu msikitini wala kanisani. Sisi tunazo madhabahu zetu za asili,” uk 82.

Wazee hawa walikula kiapo juu ya kutunza siri juu ya ujio ya jeshi la Waarabu ambalo lingepambana na Mirambo. Hata hivyo, kwa uzalendo waliokuwa nao, waliwasaliti wenzao na kutuma vijana waliokwenda kumjulisha Mirambo juu ya ujio wa jeshi hilo la Waarabu, japo waliapa kutotoa siri, hawakutishwa na kiapo cha mungu wasiyemjua.

Ni kama Shujaa aliyatabiri yajayo kwa usahihi kabisa. Dini hizi zilizompa mashaka kiboko ya Warabu, sasa zimetanda katika jamii yetu. Japo nchi yenyewe haina dini, lakini watu wake waliowengi wamegawanywa katika makundi ya dini mbili. Walevi wanaotaka madaraka, hutumia dini hizi kujionyesha kwamba wanafaa, wapo ambao huenda mbali zaidi kwa kujiita kuwa wao ni chaguo la Mungu, na wengine ili wachaguliwe husisitiza kwamba ili uwe kiongozi sharti uwe na hofu ya Mungu. Hofu haiwezi kuwa sifa ya kiongozi bora, akili hizi ni matokeo ya dini za kigeni. Dini hizi za kigeni zina mashina yake na makao makuu kutoka chanzo chake. Moja ikijikita Vatican na nyingine ikitanda katika nchi za Kiarabu. Aliyekupa dini, ukawa na hofu na Mungu wake, utamnyima nini akikuomba?

Mataifa ya India, China na Korea Kaskazini yameweza kujitofautisha na bara la Afrika. Wakati sisi tukizikumbatia dini za kigeni na kuzitumia kama kigezo cha kupata viongozi, mataifa haya yamezikataa dini hizi. Wameendelea na imani zao na wameweza kujipatia maendeleo makubwa.

Katika dini hizi za kisasa, matapeli nao wametia kambi. Wapo wanaoponya magonjwa yaliyoshindikana kwa madaktari bingwa, wanadai wanatibu magonjwa haya kwa kutumia maji, mafuta na udongo. Unapofika katika ibada hizi utawaona waumini wanakula keki ya upako ili kurejesha siku zao za kuzaliwa zilizoibwa! Wanyonge wanaongopewa na kunyonywa visarafu vyao na kubaki masikini maradufu. Huu ndiyo tunauita ushirikina wa kigeni!

Uzalendo

Mirambo ni mzalendo kwa watu wake. Kwanza anakataa kushirikiana na Waarabu kwani kufanya hivyo ni kuwauza watu hawa kwa wageni.

Pia, Mirambo anatoza kodi kwa yeyote anayepita Unyamwezi. Kodi hii inatumika kwa maendeleo nchi yote ya Unyamwezi.

Mtemi Sabila naye anaonyesha uzalendo pale anapokataa kushirikiana na Waarabu baada ya kifo cha Mtemi Fundikira. Katika utawala wake, Sabila anawatoza kodi Waarabu hali inayofanya watu hawa wamchukie, wanafanya njama na kufanikiwa kumuua.

Upande mwingine tunauoa uzalendo kutoka kwa vijana wa Unyanyembe ambao wanakataa amri ya Mtemi Msakiwa akiwataka wapigane na Mirambo. Wanakataa kushirikiana na Waarabu kupigana na Mwafrika mwenzao Mirambo.

“Mzee sisi wanajeshi vijana wa Unyanyembe tumeasi… Tumejitoa! Tumejitenga! Tumeasi! Hatuko tayari kupigana vita bega kwa bega na askari wa Bargash!” uk 100.

Nafasi ya mwanamke katika jamii

Kwanza mwanamke amechorwa kama kitulizo cha mwanaume. Mirambo anapolalamika kuumwa na kichwa, anatulizwa na mkewe ambaye anammiminia mafuta kichwani. Anampaka na anambembeleza kama mtoto mdogo mpaka anapotulia. Inasemekana anapatwa na tatizo hili kwa sababu hajaenda kutoa kafara katika kaburi la mam yake.

Mwenye upendo: Bi Mkubwa alimpenda Mirambo mumewe.

Kiongozi: mwanamke amechorwa kama kiongozi wa nchi ya Unyanyembe. Kalunde anachaguliwa kuwa Mtemi wa Unyanyembe ili kukirithi kiti cha baba yake, Fundikira.

Mwenye busara: mwanamke anaonekana kuwa mwenye busara kutoka na ushauri mzuri anaotoa. Mkewe Mtemi Sabila anamshauri mumewe apunguze kunywa pombe ili waweze kupata mtoto aliyesawasawa.

Ujumbe

Tunapata mafunzo mbalimbali katika kazi hii:

Umoja ni nguvu

Mirambo anaamini katika umoja. Anatuma ujumbe kwa Mtemi Nyungu ya Mawe akimuomba ushirikiano.

Maendeleo yataletwa na viongozi wazalendo

Unyamwezi ilipata maendeleo makubwa kwa sababu ya uzalendo wa Mirambo. Alitoza kodi kwa kila mgeni aliyepita katika eneo lake. Kodi hii ilitumika kustawisha maendeleo Unyamwezi yote.

Kabla ya majilio ya dini za kigeni Wafrika waliamini katika dini zao

Waafrika waliamini katika dini za jadi. Tamthiliya hii inatuonesha Mirambo akisikitishwa na ujio wa dini mpya.

Ukiua kwa upanga utakufa kwa upanga

Msakiwa alihusika katika kumuua Mtemi Sabila. Anapoanzisha vita dhidi ya Mirambo, anashindwa vita hivyo na kujikuta akiwa mateka wa Mirambo ambaye anapanga kumpatika kifo cha mateso makali.

Migogoro

Migogoro mbalimbali inaonekana ndani ya tamthiliya hii:

Mgogoro kati ya Mirambo na Asimu

huu ni mgogoro wa kiuchumi. Asimu hataki kulipa kodi, anapelekwa mbele ya Mirambo, baada ya Mkwara mkali, analipa kodi na kuendelea na safari yake.

Mirambo na Stanley

Stanley anakasirika kuzuiwa kupita Unyamwezi mpaka alipe kodi. Yeye anadai hafanyi biashara, anapita njia tu. Mirambo anamfukuza na kumfanya arudi Unyanyembe.

Mirambo na Msakiwa

Mirambo anamchukia Msakiwa kwa sababu amemuua Mtemi Sabila aliyekuwa mzalendo kwa watu wa Unyanyembe. Shujaa anaposhinda vita, Msakiwa anachukuliwa mateka.

Sabila na Waarabu

Huu ni mgogoro wa kisiasa. Waarabu wamekasirika kwa sababu wanaona Sabila amewasaliti kwa kutofanya yale yaliyokuwa yakifanywa na Fundikira. Sabila anawatoza kodi Waarabu jambo ambalo halikuzoeleka. Mwisho Waarabu wanafanya njama na Sabila anauawa kwa kuchomwa mshale wenye sumu kali.

Mirambo na Lugaluga

Mirambo anamlaumu Lugaluga kwa nini aliruhusu Mwanangwa atekwe na Wafipa bila ya yeye kupambana nao. Mirambo anafanya maamuzi magumu, anamuua Lugaluga.

Mirambo na Wafipa

Huu ni mgogoro wa kijamii. Wafipa ndiyo wanaoanzisha matata kwa kumteka Mwanangwa, mtoto wa kike wa Mirambo. Unyamwezi inajibu kwa kuanzisha vita.

Falsafa

Mwandishi Emmanuel Mbogo anaelekea kuamini kuwa, maendeleo ya kweli yataletwa na viongozi wazalendo. Tunamuona Mirambo akiwa mzalendo wa kweli ambaye hakucheka na wageni ambao lengo lao ilikuwa kuuchukua utajiri wa Afrika.

Msimamo/Mtazamo

Mwandishi ana msimamo wa kimapinduzi. anaamini viongozi wakiwa wazalendo, wakatoza kodi na kuitumia vyema, jamii zitapata maendeleo.

Fani

Vipengele mbalimbali vya fani vimejadiliwa katika tamthiliya ya Shujaa Mirambo.

Wahusika

- Mirambo

Mtemi wa Wanyamwezi

Shujaa

Mzalendo kwa nchi yake

- Lugaluga

Askari wa Mirambo

Wanavuta bangi ili kupandisha morari.

- Asimu

Mwarabu mfanyabiashara

Anakamatwa kwa kosa la kukataa kulipa kodi.

- Mtemi Fundikira

Anatawala unyanyembe

Anashirikiana na Warabu

Siyo kiongozi imara kwani amewasaliti watu wake kwa zawadi za tende na kashata kutoka kwa Waarabu.

- Setia

Mke mdogo wa Mirambo

- Mwanangwa

Binti yake Mirambo

Anatekwa na wafipa

- Solosolo, Marando, Simba, na Masanja

Viongozi wa jeshi la Lugaluga

- Mohamed

Mzee mwarabu

Mume wa Karunde, mtoto wa Mtemi Fundikira

- Said

Liwali wa Unyanyembe aliyewekwa na Sultan Bargash kusimamia maslahi ya Waarabu Unyanyembe

- Mzelo na Gwilo

Wazee katika nchi ya Unyanyembe

Washauri wa baraza la Mtemi Fundikira

Hawafurahishwi na ushirikiano unaofanywa kati ya Fundikira na Waarabu

Wanatoa siri kwa Mirambo juu ya ujio wa jeshi la Waarabu ili ajipange mapema kukabiliana nao.

- Sabila

Shujaa

Mzalendo

Anakataa kuendeleza usaliti wa Fundikira, yeye anawatoza kodi Waarabu

Anauliwa na Waarabu

- Ishumael na Mwajuma

Watoto wa Kalunde na Shekhe Mohamed

- Kinombo

Mtaalamu wa Unyamwezi anayejihusisha na utengenezaji wa silaha za kisasa za wakati huo.

- Kimanga

Mganga anayepiga ramli mbele ya mfalme Mirambo

Anamiliki jeshi la mbwa na mbweha

- Mtemi Msakiwa

Mtemi wa Unyanyembe

Inasemekana ndiye aliyetumwa na Waarabu ili kumuua Mtemi Sabila

Anashirikiana na Waarabu katika kutaka kumwangamiza Mirambo

Ni kibaraka wa Warabu na msaliti wa Waafrika.

- Stanley

Mzungu jeuri na mwandishi wa habari kutoka Marekani aliyekuja Afrika kumtafuta David Livingstone

Anakatazwa kupita Unyamwezi mpaka alipe kodi.

Anashangazwa na mbinu za upambanaji anazotumia Shujaa Mirambo, anamfananisha na Napoleon Bonaparte.

- Abdallah na Katilo

Wapelelezi

Wapiganaji wa jeshi la Sultan Bargash

- Amir

Kamanda wa jeshi la Waarabu

Wahusika wengine ni: Magu, Gambu, na Simo.

Mandhari

Tamthiliya hii imetumia mandhari halisi na miji halisi inatajwa: miji hiyo ni pamoja na:

Tabora ilipokuwa himaya ya Mirambo

Kigoma alipokuwa akielekea Stanley kumtafuta David Livingstone

Pwani yalipokuwa makazi ya Sultan Bargash

Unyanyembe alipokuwa akitawala Mtemi Fundikira.

Madhari mengine ni mandhari ya: nyumbani, msituni, chumbani, na uwanjani.

Muundo

Tamthiliya hii imetumia muundo wa moja kwa moja. Inaanza kuwa kuonyesha uadui wa Mirambo na Waarabu na inaisha kuwa vita kati ya Waarabu na Mirambo. Waarabu wanashindwa katika vita hivyo.

Pia, tamthiliya hii ina jumla ya maonyesho kumi na moja. Onyesho la kwanza linafungua kwa kuonyesha ufalme wa Mirambo ulivyokuwa. Na onyesho la mwisho linaonyesha vita Unyanyembe na namna Mirambo alivyoshinda vita hivi.

Maonyesho hayo yote yanaweza kuwa katika mpangilio huu: Urambo, Unyanyembe, Ikulu ya Mtemi Fundikira, Urambo, Unyanyembe, Unyanyembe, Urambo, Unyanyembe, Unyanyembe Ikulu ya Mtemi Msakiwa, Unyanyembe, Urambo, Vita Unyanyembe.

Mtindo

Mitindo mbalimbali imetumika:

Mtindo wa dayolojia umeonekana kutawala.

Pia, monolojia inaonekana ikiwa kama maelekezo yanayoelekeza namna vitendo vinavyopaswa kufanyika.

Vilevile kuna matumizi ya mtindo wa nyimbo. Wimbo wa msiba unaimbwa ndani ya tamthiliya hii.

Mtindo wa kishairi nao umetumika kama inavyonukuliwa katika mfano huu:

“Tazama shari ya shujaa Mirambo?

Wote wanamsifu kwa zao nyimbo,” uk 67.

Tena tamthiliya hii imetumia mtindo wa nafsi zote tatu.

Matumizi ya lugha

Matumizi ya lugha yanajitokeza katika vipengele mbalimbali:

Tamathali za semi

Sitiari

“Mimi ni simba,” uk 2.

Onomatopea

“Twaa! Bumuuu!” uk 3.

Takriri

“Hapana! Hapana!” Uk 4.

Mdokezo

Tafadhali bwana…

Tashihisi

Jambia langu litaramba na kunywa damu ya Mtemi Sabila!

Mubaalagha

Mirambo akamwagia Staneli mkojo wa nyati mwili mzima

Taswira

Warabu weusi - Waafrika waliobeba tamaduni za kiarabu.

Methali

Kufa kufaana

Akili ni nywele kila mtu ana zake!

Sikio la kufa huwa halisikii dawa

Umoja ni nguvu

Kuchanganya lugha

Mwangaluka

Asalam Aleykum

Misemo

Wakione cha mtema kuni

Amani ni bora kuliko vita

Nahau

Kilemba cha ukoka

Maoni ya mhakiki

Shujaa Mirambo ni tamthiliya ya aina yake. Mwandishi amefanikiwa sana kupandikiza fikra za kizalendo, wasomaji wanajengwa kupenda nchi zao na kuwa tayari kuwa lolote ili kuzilinda.

Mwandishi anaibua ukweli ambao wengi hawaufahamu. Watu hudhani ustaarabu wote katika bara la Afrika uliletwa na wazungu, jambo hili siyo sahihi, Waafrika walikuwa na tawala zao hata kabla ya majilio ya wazungu.

Mwandishi amefanikiwa kwa kiwango cha juu kabisa kuonyesha namna ambavyo Afrika ya sasa imepotea na mambo yanakwenda mbagombago, Afrika ya kina Mirambo ilikuwa imara tena yenye uchumi wa kujitegemea ikwa tofati sana na hii inayoongoza kwa kutembeza bakuli kuomba misaada.

Fani imetendewa haki na mwandishi, kwanza ametumia lugha rasmi inayoeleweka na wasomaji wengi.

Katika kazi hii ya kihistoria, mwandishi amefanya tafiti na amejadili mandhari halisi kama matukio yalivyotokea huko Tabora.

Hata hivyo kuna maeneo mwandishi ameshindwa kuyatendea haki. Eneo mojawapo ni pale alipoanzisha tukio halafu akashindwa kulimaliza, haieleweki kama pengine alisahau au aliamua tu kwa kiburi cha uprofesa (professorial arrogance). Mwandishi anatutajia tukio la kutekwa kwa Mwanangwa, mtoto wa kike wa Mirambo, hatuoni hatma ya tukio hili kama binti huyu alirejeshwa na kama vita kati ya Wanyamwezi na Wafipa ilitokea. Hata hivyo japo hajamalizia kisa hiki, inasemekana Lugaluga walivamia Ufipa na maafa makubwa yaliwakuta Wafipa wote. Historia inawalaumu Lugaluga kwa kufanya ukatili wa kutisha, kwani wanawake wa Kifipa walikatwa matiti yao.

Mapungufu mengine katika kazi hii ni upotoshaji wa historia. Mwandishi amepotosha historia hasa katika kisa cha Stanley. Ni kweli Stanley alishirikiana na Waarabu, lakini siyo kweli kwamba alionana na Mirambo ana kwa ana kama inavyoelezwa na mwandishi. Mzungu huyu alipotaka kupita, alizuiwa na Lugaluga na hakuonana na Mirambo. Alionana na Mirambo pale aliporudi Afrika kwa mara ya pili mnamo mwaka 1874, utamaduni wa Mwafrika ukashinda, Stanley akachanjwa chale akiwa na Mirambo ndipo ukatengenezwa undugu kati ya mwandishi huyu wa habari na shujaa Mirambo.

Emmanuel Mbogo atasalia kuwa miongoni mwa waandishi nguli walioitendea haki fasihi ya Kiswahili. Kazi zake haandiki kwa kukurupuka, hufanya tafiti kisha akaandika akiwa na lengo la kuleta kitu fulani katika jamii. Shujaa Mirambo, ni simulizi ya kweli inayotukumbusha kuhusu ushujaa uliofanywa na Mirambo. Ushujaa huu unapaswa kuendelezwa na viongozi wapya wajao.

Wasiliana na Mwalimu ili Kujiunga Darasa la Uhakiki wa Vitabu vyote vya Fasihi Mtaala Mpya kwa Kugusa Hapa

Popular posts from this blog

SMS 20 za Mahaba Makali Kumtumia Mpenzi Wako

SMS 20 za Vichekesho Zinazochekesha Sana

Uhakiki wa Tamthiliya ya Kilio Chetu