Tofuati ya Mtindo wa Mazungumzo na Mtindo wa Maandishi
Swali halisi: Kuna tofauti gani kati ya mtindo wa mazungumzo (Nkrumah) na mtindo wa maandishi (waandishi uliowasoma)? Toa hoja zako ukiegemeza mifano kutoka katika mdahalo wa lugha ya Kiswahili wa tarehe 19 Machi, 2017 Nkrumah.
Wamitila (2003), anasema ‘mtindo ni jumla
ya mbinu au sifa zinazomwezesha mwandishi kuwasilisha ujumbe wake,
huelezea mwandishi anavyounda kazi yake’.
Leech (1969), anasema mtindo ni namna ya
uzungumzaji, uandishi au utendaji wa jambo fulani.
Kwa ujumla mtindo ni matumizi ya lugha
yafanywayo na mwandishi au mzungumzaji kwa njia au namna maalum, Pia kupitia
mtindo tunapata mtindo wa mazungumzo ambao huwasilishwa kwa njia ya mdomo na
mtindo wa maandishi ambao kuwasilishwa kwake huwa ni kwa maandishi.
Kwa kuegemea mifano kutoka mdahalo
uliofanyika Nkrumah, tofauti kati ya mtindo wa mazungumzo na mtindo wa
maandishi inaweza kutolewa kwa ufafanuzi kama ifuatavyo;
Tofauti ya kwanza iko katika msamiati.
Mtindo wa mazungumzo mara nyingi huchagua msamiati ambao huwa sio rasmi.
Msamiati huo huitwa misimu, misimu hutumiwa kwa lengo la kufanya mazungumzo
yavutie na sababu nyinginezo. Mfano, katika ukumbi wa Nkrumah, dokta Manoko
alitumia msamiati wa kiingereza ‘extension officer’ akiwa na maana ya mtu wa
idara ya nyuki. Pia profesa kiwara kutoka Muhimbiri alisema, “Mdahalo
umejitokeza kwa sababu watu tuna matende
kichwani” ‘matende kichwani’ sio msamiati rasmi katika lugha ya kiswahili.
Pia dokta Kahangwa alisikika akisema, “acha maneno weka mziki.” Lakini katika
lugha ya maandishi, msamiati rasmi hutumiwa zaidi na matumizi ya msamiati usio
rasmi huepukwa. Massamba na wenzake, (2012), wametumia msamiati rasmi, maneno
kama, ‘tungo, virai, vishazi na sentensi’ yametumika.
Tofauti nyingine iko katika utendaji. Mtindo
wa mazungumzo una ushirikishaji wa hadhira. Hadhira hushiriki kwa kupiga
makofi, kutikisa kichwa kukubali au kukataa au kumalizia baadhi ya maneno.
Mfano katika mdahalo wa Nkrumah mzungumzaji Adolph Mkenda aliposema “nimefurahi
kuona Mkumbo hajafika.” Hadhira ilipiga makofi na kuangua kicheko. Pia Mama
Salma Kikwete aliishirikisha hadhira pale alipouliza “usione vya elea…” hadhira
nayo ilimalizia kwa kusema “vimeundwa”. Pia kuna wakati hadhira ilimkejeli
Dokta Kadeghe azungumze lugha ya kiingereza kwa sababu tu alikuwa akiitetea
lugha hiyo. Lakini katika mtindo wa maandishi, hadhira huwa haishirikishwi moja
kwa moja. Mfano Nyerere, (1994:59) anaposema “kumbadili waziri mkuu, si jambo
la ajabu. Anaweza kujiuzulu, anaweza kufukuzwa na nchi isitikisike. Lakini
huwezi kumtikisa rais wa nchi bila kuitikisa nchi yenyewe.” Katika kifungu
hicho cha maneno na kitabu kwa ujumla yake hadhira hana nafasi ya kuuliza
swali, kushauri wala kupiga makofi hivyo hakuna ushirikishwaji wa hadhira.
Tofauti nyingine ipo katika sintaksia,
ambapo mtindo wa mazungumzo hutumia sentensi ndefu na maneno mengi. Mfano
katika mdahalo wa Nkrumah, mbunge wa Afrika Mashariki Shyrose Bhanji, alitumia
sentensi ndefundefu mpaka muda wake wa kuzungumza ukaisha na kumfanya akatishwe
na Profesa Mutembei, hata hivyo Shyrose alikataa na kuendelea kuzungumza.
Katika lugha ya maandishi, sentensi fupifupi hutumika pamoja na maneno machache
ili kuepuka gharama ya karatasi nyingi na kumchosha msomaji. Mfano Hussein,
(1969), “Mama tazama – nyumba ya Kinjekitile! Moshi!” uandishi huo umetumia
sentensi fupifupi kwa makusudi maalumu.
Tofauti nyingine ni tofauti ya
kifonolojia ambapo sifa za kiarudhi kama mkazo, kiimbo na lafudhi huweza kuonekana.
Kwa upande wa lafudhi ni rahisi kumtambua mzungumzaji eneo analotoka kwa
kusikiliza lafudhi yake, mfano mzungumzaji Dokta Sima kwa lafudhi yake ilikuwa
ni rahisi kutambua kwamba, alitokea Arusha. Katika lugha ya maandishi si rahisi
kutambua lafudhi, mkazo wala kiimbo. Mfano, Semzaba (2008), huwezi kuitambua
lafudhi yake pale unaposoma kitabu chake.
Mtindo wa mazungumzo na ule wa
maandishi umetofautiana kwa kiasi kikubwa. Lakini pamoja na utofautiano huo,
kuna mwingiliano wa baadhi ya vipengele katika mitindo hii, mfano, mtindo wa
mazungumzo na ule wa maandishi hutegemea mwandishi au mzungumzaji ambaye ndiye
huchochea mada husika. Kupitia elimu mitindo, mitindo mingi huweza kujadiliwa
kwa marefu na mapana yake.
Marejeleo
Wamitila,
K.W. (2003) Kichocheo cha Fasihi Simulizi
na Andishi. Nairobi: Focus Publishers.
Leech
G. (1969). A Linguistic Guide to English
Poetry. London: Longman.
Hussein
A. (1969). Kinjekitile. Dar es
Salaam: Oxford University Press.
Nyerere
J. (1994). Uongozi Wetu na Hatma ya
Tanzania. Dar es Salaam: Mkuki na Nyota Publishers Ltd.
Semzaba
E. (2008). Marimba ya Majaliwa. Dar
es Salaam: E&D Vision Publishing.
Massamba
na wenzake. (2012). Sarufi Miundo ya
Kiswahili Sanifu. Dar es Salaam: Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili.