Uhakiki wa Tamthiliya ya Kilio Chetu

Uhakiki wa Tamthiliya ya Kilio Chetu


TAMTHILIYA; KILIO CHETU
MWANDISHI; MEDICAL AID FOUNDATION
MCHAPISHAJI; TANZANIA PUBLISHING HOUSE
MWAKA; 1995
JINA LA MHAKIKI; Mwalimu Daud Makoba

Kilio chetu ni tamthiliya inayovunja ukimya uliotawala miongoni mwa jamii katika kutatua matatizo makubwa ambayo chimbuko lake ni mahusiano ya kijinsia.

Katika tamthiliya hii vijana wanatoa sauti ya jitimai iliyojaa sononeko na shutuma dhidi ya wazazi, walezi na viongozi ambao wanafumbia macho suala hili nyeti. Ndiyo maana tamthiliya hii inasisitiza sana haja ya kuwapa vijana elimu juu ya mahusiano ya kijinsia badala ya hofu na vitisho ambavyo vimedhihirika kupitia hali halisi ya kuwa vimeshindwa.

FANI

MUUNDO

Tamthiliya hii imetumia muundo wa moja kwa moja. Inaanza kwa kutuonesha wazazi wakibishana juu ya kutoa elimu ya jinsia na mahusiano. Mwisho Joti mtoto ambaye hakupatiwa elimu hiyo anampa mimba mtoto mwenzake Suzi. Baadae Joti anakufa kwa UKIMWI.

Pia tamthiliya hii imegawanywa katika sehemu sita.

sehemu ya kwanza. Inaonesha jinsi ambavyo gonjwa la UKIMWI linaiteketeza, jamii wengi wao wakiwa watoto ambao hawakuwa na elimu ya jinsia na mahusiano.

sehemu ya pili. Wazazi wanabishana juu ya kuwapatia elimu ya jinsia na mahusiano watoto wao. Mama Suzi anasema jambo hilo liko kinyume na maadili, lakini Baba Anna yeye anaunga mkono suala hilo.

sehemu ya tatu. Inaeleza kuhusu watoto Joti na Suzi ambao wamekwisha anza mambo ya ngono. Pia watoto wameathiriwa na utandawazi kwani wanaangalia video za ngono bila wasiwasi.

Sehemu ya nne. Inazungumzia tabia hatarishi za Joti kuwa na wasichana wengi. Vilevile Anna kutokana na elimu ya jinsia na mahusiano aliyonayo, anaendelea kukwepa vishawishi.

Sehemu ya tano. Mtoto Suzi kapata mimba, anabaki njia panda akiwa hajui afanye nini.

Sehemu ya sita. Hii ni sehemu ya sita. Tunamuona Joti akifa kwa UKIMWI, na Suzi anabaki akiwa na mimba pamoja na maambukizi ya virusi vya UKIMWI.

MTINDO

Tamthiliya hii imetumia mtindo wa;

i.              Dayolojia – majibizano ya wahusika yametawala toka mwanzo mpaka mwisho wa tamthiliya hii.

ii.            Monolojia – mtindo huu wa masimulizi umetumika japo kwa kiasi kidogo.

iii.           Mtindo wa masimulizi ya ki ngano - mfano katika ukurasa wa 1 Mtambaji anasimulia,

            “Hapo zamani za kale paliondokea kisiwa kimoja kikubwa sana. Kisiwa kilikuwa na watu wa kila aina…”

iv.           Matumizi ya nyimbo – katika ukurasa wa 29, Anna anaimba wimbo unaokemea wanaume wanaomfuata kumlaghai.

            “Anna, Anna, Anna mie niacheni mie x 2
Msichana mdogo bado ninasoma niacheni mie.”

v.            Matumizi ya nafsi

Nafsi zote zimetumika lakini nafsi ya pili imetawala zaidi.

WAHUSIKA

JOTI

-          Mhusika mkuu

-          Hana elimu ya jinsia na mahusiano

-         Anajiingiza katika mahusiano ya kimapenzi na wasichana wengi. Wengine wakiwa wakubwa kuliko yeye.

-          Mwisho anakufa kwa UKIMWI

SUZI

-          Mhusika mkuu

-          Msichana mdogo anayesoma shule ya msingi

-          Hana elimu ya jinsia na mahusiano

-          Anajiingiza katika mahusiano ya kimapenzi na mwanafunzi mwenzake Joti, pia anaambukizwa UKIMWI na kupata mimba.

ANNA

-          Msichana mwenye elimu ya jinsia na mahusiano

-          Anakataa vishawishi vya wanaume kwa sababu anajitambua kwa sababu ya kuwa na elimu ya jinsia

MAMA SUZI

-          Anashikilia mila na tamaduni za zamani

-          Haungi mkono kuwapatia watoto elimu ya jinsia na mahusiano, anaamini kufanya hivyo ni kuwaharibu watoto

MJOMBA

-          Mwanaume mtu mzima

-          Anaunga mkono wazazi kuwapatia watoto wao elimu ya jinsia na mahusiano.

Wahusika wengine ni; Baba joti, Mama Joti, Baba Anna, Choggo, Mwarami, Jumbe, Chausiku, Jirani, na wengineo.

MANDHARI

Mandhari ya mjini yametumiwa na mwandishi. Pia kunayo mandhari ya;
Nyumbani, kijiweni, barabarani, n.k

MATUMIZI YA LUGHA

   Tamathali za semi


i.              Tashibiha. “Wakapukutika kama majani ya kiangazi.” Uk 1
ii.            Sitiari. “We mbwa mweusi.” Uk 10
iii.           Takriri. “vikawazoa, vikawazoa… vikawazoa.” Uk 3
iv.           Tanakali sauti. “pwi, pwi, pwi,” uk 18
v.            Tafsida. “Kafa kwa kukanyaga nyaya.” Uk 4
vi.           Mubaalagha. “mtu si mtu, kizuka si kizuka” uk 4

2.    Misemo, nahau na methali

i.              Msemo. “Wembamba wa reli treni inapita.” Uk 7
ii.            Msemo. “Kukimbilia suti na nepi hujavaa.” Uk 28
iii.           Methali. “umeula wa chuya.” Uk 29
iv.           Methali. “shukrani ya Punda ni mateke” uk 19
v.            Nahau. “nimekuvulia kofia” uk 6

3.    Picha na taswira

“Dubwana” –ugonjwa wa UKIMWI;
“Nguru” –aina ya Samaki wabaya–amefananishwa na mtu mbaya;
“Kinyago”- Suzi.

MAUDHUI

DHAMIRA

Dhamira nyingi zimejadiliwa katika tamthiliya hii, miongoni mwa dhamira hizo ni;

i.              Elimu ya jinsia na mahusiano

Jamii imekumbwa na mmomonyoko mkubwa wa maadili pamoja na maradhi hatari yasiyotibika kama UKIMWI. Hivyo wazazi wanapaswa kuwaelimisha watoto wao juu ya njia sahihi za kujikinga na matatizo haya. Katika tamthiliya tunaona pande mbili, ule unaoshikilia ukale na upande unaotaka mabadiliko. Baba Anna, anawaelimisha watoto wake juu ya madhara ya kujihusisha na ngono katika umri mdogo, Anna anaelewa na anafanikiwa kukwepa vishawishi. Hali ni tofauti kwa Mama Suzi anaamini kuwapatia watoto elimu ya jinsia na mahusiano ni kuwaharibu na kuwapoteza. Anaposhauriwa kuwapatia watoto elimu hiyo anafoka,

“Huko si ndiko kunifundishia wanangu umalaya? Umfunze mwanangu habari za ngono…”
Kutokana na kutokukubali kuwapatia wanawe elimu hii, Suzi anapewa mimba na kuambukizwa UKIMWI.

ii.            Mmomonyoko wa maadili

Maadili hayazingatiwi tena katika jamii. Watoto kwa wakubwa wote wamepotoka. Tunaona watu wazima wakitembea na watoto wadogo, mfano Chausiku anamahusiano na mtoto mdogo Joti. Pia watoto wamejiingiza katika mahusiano ya kimapenzi, Joti anamahusiano na Suzi. Watoto hawahawa wanaangalia video za ngono bila kuogopa chochote. Katika ukurasa wa 20 Joti anasikika akiwahamasisha wenzake.

“Yaap, ukimtaka Suzi, chukua. Picha ya ngono, matusi angalia!”

Mmomonyoko huu wa maadili utaondolewa endapo watoto watapatiwa elimu.

iii.           Athari ya sayansi na teknolojia

Maendeleo ya sayansi na teknolojia yameleta mabadiliko makubwa katika jamii, mfano katika tamthiliya hii, watoto wanakwenda kuangalia picha za ngono na kuwafanya waharibikiwe kifikra kwa kutamani kuigiza kile wanachokiona. Joti, mtoto kinara wa kutazama picha hizo anaambulia UKIMWI na kufa angali mtoto mdogo.

iv.           Nafasi ya mwanamke katika jamii

Nafasi ya mwanamke ni jumla ya mambo yote ayatendayo mwanamke katika kazi ya fasihi. Mengine huwa mazuri yanayostahili pongezi na machache huwa mabaya yanayostahili kukemewa kwa nguvu. Katika tamthiliya hii, mwanamke amechorwa kama;

-          Chombo cha starehe. Mfano Joti anamtumia Suzi kwa ajili ya kujistarehesha.

-          Asiyependa mabadiliko. Mama Suzi hataki kutoa elimu ya jinsia kwa wanaye.

-          Asiye na maadili. Suzi hana maadili, anajiingiza katika mahusiano ya kimapenzi katika umri mdogo.

-          Mwenye elimu na asiyedanganyika. Anna ana elimu ya jinsia na mahusiano, wanaume wanashindwa kumdanganya kwa pesa na maneno matamu.

UJUMBE

i.              Asiyefunzwa na mamaye hufunzwa na ulimwengu. Suzi na Joti hawakufunzwa vyema na wazazi wao, badala yake ulimwengu unawafunza.

ii.            Elimu ya jinsia na mahusiano itolewe kwa watoto. Elimu hii itawafanya waepuke vishawishi.

iii.           Sheria kali zitungwe dhidi ya watu wanaowalaghai watoto. Kuna watu wazima wanaowaingiza watoto katika vitendo vya kimapenzi kama Chausiku anavyomlaghai Joti. Sheria kali itungwe na isimamiwe kuwakomesha.

iv.           Wazazi wote washirikiane katika malezi ya watoto. Baba Anna na Mama Anna wanashirikiana katika malezi ya watoto wao. Matokeo bora yanaonekana.

MIGOGORO

Migogoro iliyojitokeza ni pamoja na;

Migogoro ya wahusika

i.              Mgogoro wa Joti na Suzi

Mgogoro huu unasababishwa na tabia ya joti kuwa na mahusiano na wasichana wengi. Suluhisho la mgogoro huu ni Joti kumuomba msamaha Suzi.

ii.            Mgogoro wa Suzi na Mama yake

Mgogoro huu unasababishwa na mama Suzi kuvikuta vidonge vya kuzuia mimba katika sketi ya mwanaye. Suluhisho la mgogoro huu ni Mjomba kumwamuru Suzi aende ndani na mazungumzo kati ya Mjomba, Mama Suzi na majirani wengine yanaendelea.

iii.           Mgogoro kati ya Mjomba na Mama Suzi

Chanzo cha mgogoro huu ni Mjomba kumshauri Mama Suzi ampe elimu ya jinsia na mahusiano binti yake. Mama Suzi anakataa na kusema kufanya hivyo ni kuwafundisha watoto umalaya.

iv.           Mgogoro kati ya Chausiku na Joti

Chausiku anamlaumu Joti kuwa anamahusiano na wasichana wengine, anaendelea kulalama kuwa, hata zawadi anazompatia anawapatia wasichana wengine. Chausiku anamtisha Joti kuwa atamchoma moto yeye na visichana vyake. KICHEKO!!

Mgogoro wa nafsi

Huu ni mgogoro ambao humpata mhusika peke yake kati yake yeye na nafsi yake.
-          Suzi anapatwa na mgogoro wa nafsi pale anapopata mimba na kuambukizwa virusi vya UKIMWI. Anabaki akilia, lakini hakujilaumu mwenyewe, bali anamlaumu mama yake kwa kushindwa kumpatia elimu ya jinsia na mahusiano. Katika ukurasa wa 40, anasema,
“Mimi na Joti tungepata bahati ya kuelimishwa tusingetumbu…”

Msimamo

Mwandishi anamsimamo wa kimapinduzi. Katika tatizo la watoto wengi kuangamia kwa ugonjwa wa UKIMWI, anashauri elimu ya jinsia na mahusiano itolewe ili kuleta ukombozi kwa jamii.

FALSAFA

Mwandishi anaamini kuwa elimu ya jinsia na mahusiano ikitolewa kwa watoto itawasaidia kupambana na hatari ya kuambukizwa virusi vya UKIMWI.

KUFAULU NA KUTOKUFAULU KWA MWANDISHI

KUFAULU

Kufaulu katika fani

-          Mwandishi ametumia lugha nyepesi inayoeleweka kwa urahisi.

-          Mwandishi ametumia wahusika ambao wameibeba vizuri dhamira kuu

-          Mwandishi ametumia muundo rahisi wa moja kwa moja ambao haumchoshi msomaji wal a kumchanganya.

Kufaulu kwa maudhui

-          Mwandishi amefaulu kufikisha dhamira katika jamii juu ya umuhimu wa kuwapatia watoto elimu ya jinsia na mahusiano.

-          Pia mwandishi ameifungua jamii na kuionya juu ya hatari ya sayansi na teknolojia endapo itatumiwa vibaya.

KUTOKUFAULU

Kutokufaulu katika fani

-          Mwandishi ametumia mandhari ya mjini pekee kana kwamba maambukizi ya virusi vya UKIMWI yanawakabili watoto waishio mjini tu.

Kutokufaulu katika maudhui

-          Ugonjwa wa UKIMWI huwapata watu wote bila kuzingatia umri. Lakini katika tamthiliya hii, wanaougua ugonjwa huu ni watoto pekee. Kwa kiasi fulani mwandishi hajafaulu.

Hata hivyo kazi hii ni bora na inastahili pongezi kwa mafunzo makubwa inayoyatoa katika jamii yetu iliyogubikwa na utandawazi.

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Risala | Kiswahili Kidato Cha Nne