Uhakiki wa Diwani ya Malenga Wapya
Mwandishi: Taasisi ya Kiswahili, Zanzibar
Wachapishaji: Oxford University Press
MWAKA: 2001
Mhakiki: Mwalimu Makoba
Kuhusu Malenga Wapya
Malenga wapya ni diwani ambayo inaangazia yale yanayotokea katika jamii. Inaangazia mambo mbalimbali yanayohusu siasa, mapenzi, uchumi, jamii na mengine mengi.
Maudhui
Vipengele mbalimbali vya maudhui vinajadiliwa, miongoni mwavyo ni:
Dhamira
Malenga hawa wapya wanaibua dhamira mbalimbali kama zinavyojadiliwa:
Uongozi mbaya
Katika shairi la PAYUKA, mshairi anasema,
“Kupayuka kwenu huko, Mbona tu kokoriko,
Sioni linalokuwa.”
Mshairi analalamika waziwazi juu ya uongozi mbaya. Viongozi kazi yao ni kupayuka majukwaani, lakini wanapokuwa ofisini hakuna lolote wanalotekeleza.
Ukombozi wa kiuchumi
Mshairi anaishauri jamii juu ya mbinu ya kujikwamua kiuchumi, mbinu hiyo ni kufanya kazi kwa bidii. Katika shairi la CHARUKA tunaambiwa kuwa,
“Charuka baba haraka, na mfano kuonyesha,
Charuka upate vuka, mikondo hii maisha,
Charukeni kina kaka, na dada nawaamsha, Basi tena kulegea, charuka chacha rukaka.”
Mshairi anawaasa watu waache kulegea, wajikaze kwelikweli katika kuyapambania maendeleo.
Ukombozi wa mwanamke
Tunamuona mwanamke akifungiwa ndani, hatakiwi kutoka kwenda kufanya kazi. Mshairi analalamika vikali juu ya jambo hili.
katika shairi la KIFUNGO ubeti wa saba mshairi anasema:
“Kwa kuwa mwanamke, ndani mnanifutia, Lazima nje nitoke, kupata ninayotaka, Nimechoshwa na upweke , sitaki kudhalilishika, Kifungo kimenichosha, minyororo nafungua.”
Kusaidia wengine
Mshairi anatukumbusha umuhimu wa kuwatendea wema wengine, katika shairi la HISANI HULIPWA anasikika akisema:
“Akuulizae, uwapo na shida, Akuteteae ukishambuliwa, Akumurikae, uwapo na giza, Hisani hulipwa”
Basi tunaaswa tutendeane wema sisi kwa sisi, kwani mwisho wa siku wema huo huweza kuturudia wenyewe.
Suala la Mapenzi
Katika shairi la UA, Mshairi anatumia taswira ya ua kumaanisha mpenzi ampendaye. Katika mapenzi haya, mshairi anapata liwazo, na furaha. Mshairi akiwa katika lindi zito la mapenzi anasikika:
“Ua limejituliza, mtini laning’inia, Mwenyewe laniliwaza, furahani lanitia, Ua sasa limepea, macho walikodolea.”
Umuhimu wa wosia
Familia nyingi huingia katika mifarakano isiyoisha kwa sababu ya kukosa wosia kutoka kwa mzazi aliyetangulia mbele za haki. Mshairi hapa anatueleza kuwa, wosia ni muhimu hasa katika kuepusha migogoro mbalimbali hapo baadae. Katika shairi la NINI WANANGU anasema:
“Shikamaneni wanangu, siku yangu ikifika. Mutamakani kichungu, musije kutawanyika, Kiondoeni kizungu, mshike mliposhika, Sizidi nasaha zangu!
Katika wosia huu, mzazi anaacha maelekezo mema kwa waliobaki. Anahamasisha umoja, hataki kamwe kuona watoto wake wanagawanyika pale atakapoondoka.
Katika jamii yetu tunashuhudia migogoro ya kila namna baada ya mzazi kuondoka. Migogoro mikubwa husababishwa na vita vya kugombea mali za urithi. Ukiona nyumba imeandikwa ‘Nyumba hii Haiuzwi, Epuka Matapeli” basi tambua kuna ndugu wamefarakana.
Ukombozi wa kifikra
Mshairi anawaonya watu kutumia fikra za wengine bila kuhoji, anawaasa wasiwe bendera fuata upepo kwani waongo ni wengi. Mambo haya anayazungumzia katika shairi la USIWEBENDERA.
“Tumia zako fikrazo, pima yanofaa, Tazama kikwazo, wapi chatokea, Pima na uwezo, wakukifanyia, Usiwe bendera, kufata upepo,”
Katika jamii taarifa za uongo zimekuwa nyingi. Wameibuka manabii wanaotibu magonjwa yaliyoshindwa kutibiwa katika hospitali za kisasa tena zenye madaktari bingwa. Manabii hawa wanatibu kwa kutumia mchanga, maji, keki na mafuta. Katika jamii ya aina hii, shtuka, usiwe bendera.
Utetezi wa haki
Katika shairi la SAMAKI MTUNGONI mwandishi anaona kuwa kwa sababu ya ukosefu wa haki watu hudhulumiwa na kuteswa anafananisha wadhulumu haki na wavuvi anasema:
“Haki yao mepotea, na heshima kuondoka, Mebaki waning’inia, mtungoni mepangika, Bwana amechachamaa, nyumbani kwenda kupika, Leo wako mtungoni, huzuni imewakumba.”
Samaki mtungoni ni shairi la kitaswira. Viongozi walaghai wanafananishwa na wavuvi, nao wanyonge wanafananishwa na samaki. Wanyonge wako mtungoni, suluhisho la mateso haya ni lipi? Sayansi imekubali kwamba, wanyonge wakiungana, huwa mwisho wa uonevu.
Falsafa
Washairi wanaamini kuwa, kufanya kazi kwa bidii kutaleta maendeleo katika jamii yetu.
Mtazamo/msimamo
Washairi wana msimamo wa kimapinduzi, wanaamini kuwa, tutapata maendeleo endapo tutaacha uvivu na kuamua kufanya kazi kwa bidii.
Ujumbe
Kufanya kazi kwa bidii ni chachu ya mendeleo.
mapenzi ya kweli ni jambo la msingi.
Kumkomboa mwanamke ni kuikomboa jamii.
Viongozi walaghai na wasaliti hawafai kwa maendeleo hivyo tunaaswa kuwa makini kuchagua viongozi bora na kuwawajibisha wasiofaa.
Viongozi na watu wenye pesa waache tabia ya kuwanyanyasa wanyonge, siku wakiungana hapatakalika.
Fani
Vipengele mbalimbali vya fani vimejitokeza:
Muundo
Idadi ya mishororo:
Tathlitha
Huu ni ushairi wenye mishororo mitatu kwa kila ubeti. Ushairi huu pia huitwa UTATU. Katika kazi hii yaMALENGA WAPYA yapo mashairi kadhaa yaliyosukwa namna hii, nayo ni kama vile PAYUKA, TUNZO, KUUNGE, UA na HALI HALISI.
Tarbia
Ni ushairi uliosukwa kwa mishororo minne kwa kila ubeti.Tarbia pia
hufahamika kama UNNE. Kidesturi shairi la huwa na mishororo
iliyogawanyika katika vipande viwili. Malenga wapya nao wameweza kuisuka kazi yao kwa kutumia muundo huu, mashairi yanayodhihirisha hilo ni pamoja na MAISHA NI KAMA NJIA, ULIMI, SISUMBUKIE KICHAA, NIPATIENI DAWA, NIPATE WAPI MWINGINE na SAMAKI MTONGONI.
Takhmisa
Ni ushairi wenye mishororo mitano katika kila ubeti.Ushairi huu huitwa pia UTANO au takhmisa. Kuna baadhi ya takhimisa hazina mgawo wa vipande viwili kama ilivyozoeleweka.Katika kazi hii malenga hawa wametumia muundo huu pia kama inavyojidhihirisha katika shairi la ISRAFU, SIHARAKIE MAISHA.
Tasdisa
Ni utungo wenye mishororo sita katika kila ubeti. Pia huitwa USITA, TARDISA au TASHLITA. Ingawa tungo hizi si maarufu sana lakini inaonekana katika diwani hii kama inavyojidhihirisha katika shairi la PUNDA msanii anasema;
Toka ulipozaliwa, maishayo ni kizogo,
Hujapata kuenziwa, waishi tirigivyogo,
Nawe hujajielewa, u kiumbe hu kigogo,
Kama ungefadhiliwa, usingebeba mizigo,
Hakika ulionewa, hustahili kipigo,
Haki umeitambua, idadi japo japo kidogo.
Sabilia
Ni muundo ambao kazi ya kishairi hujengwa kwa mishororo saba au zaidi kwa ubeti. Kama ilivyo kwa tasdisa mashairi ya namna hii ni machache sana. Katika kazi ya MALENGA WAPYA kuna mfano wa shairi la muundo huu ambalo ni PASUA UWAPE UKWELI.
Idadi ya vipande
Hiki ni kigezo kingine cha kuainisha muundo wa kazi za kishairi,kwa kigezo hiki shairi laweza kuwa na
Vipande viwili ( manthawi )
Katika muundo huu mshororo wa ubeti hugawika katika sehemu mbili; sehemu ya kwanza na ya pili. Mashairi kadhaa katika diwani hii yamesukwa katika muundo huu, nayo ni pamoja na ADUI, KIFUNGO, KITENDAWILI, CHARUKA, NIPATE WAPI MWINGINE.
CHARUKA
Charuka chacharukaka, mambo kuyakimbilia,
Charuka kirukaruka,mipango kufikiria,
Charuka kikurupuka,mbali uweze fikia,
Kabla hujapotea,charuka chacharukaka.
Vipande vitatu ( ukawafi )
Kwa muundo huu mshororo wa ubeti wa shairi hugawika katika sehemu tatu; yaani sehemu ya kwanza, ya pili na ya tatu. Diwani ya MALENGA WAPYA
imetumia pia muundo huu kupitia mashairi kadhaa kama vile KWA NINI?, TUNZO na HAKI.
HAKI
Haki watutisha, tusikuandame, kwa matendo yetu,
Watukorofisha, tusikuandame, kila penye kitu,
Mbona watutwisha, miba ituchome, kwenye huu mwitu,
Tutokwe na utu!
Kipande kimoja ( utenzi )
Katika muundo huu mizani ya mishororo huwa michache kati ya 4 hadi 12 nao husimulia habari fulani au tukio fulani. Katika diwani hii msuko huu unajidhihirisha kupitia shairi la PAYUKA.
Nasikia makelele,
Ya ngoma ile ya lele,
Kuimba na kupayuka.
Kupayuka kwenu huko,
Mbona tu kokoriko,
Sioni linalokuwa.
Mbali ya idadi ya mishororo na vipande pia kituo hutumika kuainisha muundo wa kazi husika. Katika diwani hii ya MALENGA WAPYA msanii imetumia vituo tofauti kama vile:
Bahari:
Kituo cha namna hii maneno ya mshororo wa mwisho yanakaririwa kutoka
ubeti mmoja hadi mwingine.Msuko huu unajidhihirisha katika HINA
INAPAPATUKA, BAHARI na HALI HALISI.
Nusu Bahari:
Kituo cha namna hii maneno ya kipande kimoja hukariririwa ubeti mmoja hadi
mwingine wakati ya kipande cha pili hubadilikabadilika. Muundo huu umejitokeza katika shairi la CHARUKA.
Kimalizio
Katika kituo cha namna hii mshororo wa mwisho hubadilikabadilika kutoka
ubeti mmoja hadi mwingine.Muundo huu umetumika vilivyo katika diwani hii hasa katika mashairi ya NINI WANANGU?, UTANIKUMBUKA, SOKOMOKO BAHARINI
Matumizi ya lugha
Katika shairi la SAMAKI MTUNGONI kuna taswira ya samaki ikiwakilisha watu wa tabaka la chini (watawaliwa), taswira ya mvuvi ni watu wa tabaka la juu (viongozi) na taswira ya mtungo ni sheria, kanuni au taratibu zinazotumiwa kuwabana watu wa tabaka la chini.
Njiwa mpenzi shairi la NIPATE WAPI MWINGINE?
Punda- tabaka linalokandamizwa (shairi la PUNDA)
Ua – mwanamke/ msichana (shairi la UA)
METHALI
Kuna methali mbalimbali zimetumiwa katika diwani hii; mfano
Subira yavuta heri (shairi la SIHARAKIE MAISHA)
Aisifie mvua kaloa mwilini mwake (shairi la SISUMBUKIE KICHAA)
Fahari – wapiganapo nyasi ndizo huonewa (SOKOMOKO BAHARINI)
MISEMO
Siharakie maisha (SIHARIKIE MAISHA)
Sisumbukie kichaa (SISUMBUKIE KICHAA)
Sokomoko baharini (SOKOMOKO BAHARINI)
TAMATHALI ZA SEMI
TASHIBIHA
Ubaguzi umezama kama nguzo (shairi la TUNZO)
Maisha ni kama njia (shairi la MAISHA NI KAMA NJIA)
Yametolewa na kombe mithili ya gome la mti (shairi la BAHARI)
TASHIHISI
Samaki wakasirika (shairi la SAMAKI MTUNGONI)
Njaa imetuvamia (shairi la ADUI)
Ua limejituliza (shairi la UA)
Ulimi ninakuasa (shairi la ULIMI)
TASHITITI
Katika shairi la MWABAJA MWASEMA NINI?
Nasikia mwatunga,mwatungani washairi
TANAKALI SAUTI
Parakacha mlio wa majani makvu (shairi la KWA NINI?)
Kokoriko – shairi la MKULIMA
TAKRIRI
Kuna takriri kituo cha mfano shairi la KWA NINI?
MKATO WA MANENO
Kuna maneno yamekatwa ili kuepuka urari wa vina na mizani mfano
“anong’ona (shairi la KWA NINI?).
Mtindo
Malenga wapya kama wanavyojiita, wamekuja na mtindo wa kisasa. Katika baadhi ya mashairi, tunaona mtindo wa kisasa ukitumika. Mtindo huu haufuati urari wa vina na mizani.
Hata hivyo, mtindo wa kimapokeo haujaachwa. Tunaona mashairi mengi yakiwa na urari wa vina na mizani.
Hitimisho la Mhakiki
Mwaka 2001 kilitoka kitabu hiki kilichoitwa malenga wapya, zingatia kwamba ipo nakala iliyotoka mwaka 1997. Katika diwani hii, mashairi hayakuandikwa na mtu mmoja. Bali lilikuwa kusanyiko la malenga waliojiita wapya huku TAKILUKI wakiwezesha kufanikiwa kwa jambo hili.
Miaka mingi imepita tangu tuwaone hawa malengo wapya, kwa kupita huku kwa miaka tunaweza sasa kuhoji ni upi upya wao? Lakini wako wapi malenga hawa?
Malenga wapya walikuwa wanafunzi wa Kiswahili huko Zanzibar. Mashairi haya yalikusanywa kwao wakiwa bado masomoni. Baada ya masomo kila mmoja alishika njia yake. Palitakiwa kupatikana mtu wa kuwaunganisha ili wajikokote na kutoa diwani nyingine tena, lakini kama wasemavyo waswahili, mkono mtupu haulambwi, pengine hakuna faida yoyote ya kifedha waliyoipata kwa kuandika mashairi haya.
Kwani fedha ni kila kitu, hapana? Ninawapa wito na wazo jema, malenga wapya wajikusanye, waje na jambo jipya kabla hawajapitwa na wakati.
