KF 202 | Hakiki Madai Kuwa Ushairi wa Kiswahili Hautoki Katika Ombwe au Utupu
Kama ilivyofasiriwa na wataalamu
mbalimbali, wakiwemo wana ukale na usasa, tukianza na wanamapokeo, wao wanadai
kuwa; ushairi au utenzi ni wimbo hivyo kama shairi halimbiki halina maana.
(Amri Abed; 1954).
Shaaban Robert (1958) anasema
ushairi ni sanaa ya vina inayopambanuliwa kama nyimbo, mashairi na tenzi. zaidi
ya kuwa sanaa ya vina ushairi una ufasaha wa maneno machache au muhtasari
mawazo, maana na fikra za ndani zinapoelezwa kwa mhtasari wa ushairi huvuta
moyo kwa namna ya ajabu.
Nae Mnyampala (1970) anasema
ushairi ni msingi wa maneno ya hekima tangu kale. Ndicho kitu bora kwa maongozi
ya dunia kwa kutumia maneno ya mkato na lugha nzuri yenye kunata iliyopangwa
kwa urari wa vina na mizani na vina maalumu.
Ubora wa dhana za wana mapokeo ni
kwamba; wote wanakubaliana kuwa, ushairi ni lazima uwe na urari wa vina na
mizani.
Pia ushairi ni lazima uvute hisia
za moyo kutokana na lugha ya kinathari inayotumika. pia ushairi ni wimbo hivyo
ni lazima upangwe kwa namna itakayoweza kuimbika. vina na mizani.
Pamoja na ubora wao, wanamapokeo
nao wanaonesha udhaifu kwani wameegemea sana katika fani (lugha na kusahau
kipengele muhimu cha maudhui) kama tukirejelea fasiri ya Amri Abed. (1954).
Wanausasa nao wamefasiri ushairi
kama ifuatavyo; Mulokozi na Kahigi (1982) wanasema ushairi ni sanaa
inayopambanuliwa kwa mpangilio maalumu wa maneno fasaha na yenye muwala kwa
lugha ya mkato, picha,, sitiari au ishara katika usemi, maandishi au mahadhi ya
wimbo au kueleza tukio a hisi fulani kuhusu maisha au mazingira ya binadamu wa
njia inayogusa moyo.
Njovu na Chimela (1999) wanasema
ushairi ni sanaa inayotambulishwa na mpangilio maalumu wa sentensi au vifungu.
mpamgilio ambao una muundo maalumu au ruwaza fulani inayounda wizani, lugha ya
mkato na mafumbo pamoja na mpangilio usio wa kawaida wa vifungu fulani.
Wizani ni urari wa mapigo ya
sauti katika kuongea. Mtu anayezungumza kishairi kidogo hufanana na muimbaji
ambaye hupanga maneno yake kufuata mahadhi fulani.
Ubora wa fasili zao ni kwamba,
wote wanaona ushairi ni sanaa ya lugha inayopambanuliwa kwa mpangilio maalumu
wa maneno fasaha na yenye muwala, lugha ya mkato, picha na sitiari au ishara.
Wamezingatia vipengele vya fani
na maudhui kwa kiasi fulani wakiamini kuwa shairi hata lisipoimbika ila likawa
na maana na muundo wa kishairi basi hilo linahesabika kuwa ni shairi.
Pia wamechangia kuinuka kwa
watunzi wengi wa ushairi wa Kiswahili kutokana na kulegezwa kwa kanuni za
utunzi.
Pamoja na ubora wao, wameonekana
kuwa dhaifu kwani, mashairi yao yamepoteza utamu na mapigo ya kimuziki.
Hivyo tunaweza kusema kuwa,
ushairi ni sanaa ya lugha iliyoandikwa au kuganwa, inayoweza kuwa na urari wa
vina na mizani au isiwe nao na inayotumia lugha inayoteka hisia za wasomaji na
wasikilizaji. pia tunaweza kusema kuwa ushairi wa Kiswahili ni ushairi uliotungwa
na kughanwa unaoelezea utamaduni wa waswahili.
Ni ukweli kwamba ushairi wa
Kiswahili hautoki katika ombwe au utupu. Muda na mazingira na tamaduni za
waswahili zimechangia sana kuibuka kwa ushairi. Tunaweza kuuweka ukweli huu
katik nyakati tofautitofauti na pia kujadili kwa mujibu wa nadharia za
wataalamu mbalimbali. tuianza kuthibitisha hoja hizi kwa vipindi mbalimbali.
Ushairi wa Kiswahili kabla ya
karne ya 10. Ulikuwa tungo simulizi hasa ngoma na nyimbo. Pia ulifungamana na
ngoma za tamaduni za waswahili. Ushairi ulitungwa na kughanwa kwa gibu ila
kuandikwa. Pia gibu hii haikufuata urari wa vina na mizani.
Mfano; Nkuli mbondabonde, nkoluti
momulyego
Ndyenyama nkongeigufa nka kiino
elya muganga.
ikiwa na maana ya
Nikonge
na kupinda kama milima ya nyumba za msonge
Nile
nyama na kuiuma mifupa kama jino la muganga. (Richard Mutembei 1993;26)
kipindi hiki ushairi ulighanwa
kwa lengo la kusifu au kuiabudu miungu pamoja na shughuli nyingine za
kiutamaduni, mfano kuoza binti wanawari.
Ushairi wa Kiswahili kuanzia
mwaka 1000 BK. Waswahili waliingiliwa na walowezi kutokea uarabuni nao
waliingiliana katika mambo yote ya kiuchumi, kijamii na kiutamaduni. kutokana
na muingiliano huu waliuathiri ushairi wa Kiswahili kama sehemu ya utamaduni wa
waswahili.
Kwanza walileta dini ya kiislamu,
iliyoathiri kwa kiasi kikubwa ushairi wa waswahili.
Pili walileta taluma ya uandishi
kwa kutumia hati za kiarabu. kutokana na ujio wa waarabu, waswahili nao
walianza kushiriki mila na desturi za wageni hao na dini yao. kwa njia hii
ujuzi na tabia ama tamaduni za waswahili zilianza kubadilika na hata katika
ushairi walianza kutunga mashairi yaliyomsifu Allah na kumuomba baraka.
Pia kati ya mwaka 1000 hadi 1500,
miji ya waswahili iliendelea sana kutokana na maingiliano ya kibiashara ambayo
iliwaunganisha waswahili wa pwani na bara pia.
Katika kipindi hiki kuliibuka kwa
washairi maarufu wa Kiswahili, kama Fumo Lyongo anayeaminika kuishi maeneo ya
Pate kaskazini mwa Kenya kama ilivyonukuliwa na Ohly (1985 – 462). Katika
kipindi hiki ushairi wa Kiswahili uliendelea kuandikwa na kughanwa ukiwa na
maudhui mbalimbali, mfano, “Utenzi wa tawasifu”, na “utenzi wa kumswifu Yanga”.
Ambao ndio unasadikika kuwa ndio ushairi wa mwanzo wa Kiswahili kuandikwa mwaka
1517 na ulikuwa na lengo la kumsifu Mwanayanga.
Ushairi wa Kiswahili katika mwaka
1500 – 1750 BK. Kulitokea uvamizi wa wareno katika jamii za waswahili mwaka
1498. Kuliibuka kwa mgogoro baina ya wenyeji na wageni (Wareno) na mashairi
yaliandkwa kupinga uvamizi huo. Mojawapo ya mashairi yaliyoandikwa ni “Mzungu
Migeli” na “Portugez Afala”. (Hichens;1962.123).
Mbali na mashairi ya kupinga
uvamizi wa wareno pia yapo mashairi yaliyoandikwa kuhus maisha ya Mtume
Muhammad. Pia upo “Utenzi wa Tambuka” ulioelezea maisha na vita kati y waislamu
wa mwanzo na mfalme Herekali wa dola ya Warumi.
Kwa ujumla katika kipindi hiki
ushairi uliandikwa kuwatia moyo waswahili na maudhui ya kidini.
Ushairi wa Kiswahili katika
kipindi hii ya . ushairi vilevile ulijikita zaidi katika fasihi ya dini na
kutafakari maisha kwa ujumla. Kipindi hiki tungo nyingi za maisha ya mtume
Muhammad zilitungwa. mfano “Utenzi wa Kiyama” uliokuwa kielezea maisha ya
ahera.
Pia kulikuwa na tungo za
kiutamaduni. mfano “Utenzi wa Mwanakupona” uliotungwa na Bi Mwanakupona kumhusu
bintiye.
Pia katika kipindi hiki jamii
kubwa za waswahili zilikuwa katika harakati ya kutafuta uhuru kutoka kwa
wakoloni, mashairi mengi yaliandikwa pia. mfano Muyaka bin Haji wa Mombasa,
alitunga mashairi kupinga uvamizi wa waarabu wa Oman. Baadhi walinyongwa kwa
kukataa kutawaliwa.
Ushairi wa Kiswahili katika karne
ya 19. Ulishuhudiwa ujio wa wakoloni katika kipindi hiki.
Wakoloni wa kwanza walikuwa
wajerumani ambao walitamalaki 1885 – 1914. Ushairi katika kipindi hiki ulihusu
vita vya wenyeji dhidi ya wakoloni wa kijerumani. Mfano “Utenzi wa vita vya
Wadachi uliadikwa katika kipindi hiki.
Wajerumani waliacha athari katika
ushairi wa Kiswahili ikiwemo; kuanza kutumika kwa hati za kirumi, ufunguzi wa
shule, waliosoma walijifunza uandishi wa mashairi, kuanzishwa kwa magazeti,
magazeti haya yalikuwa na kurasa maalumu kwa ajili ya mashairi na ni katika
kipindi hiki waswahili Shaaban Robert na Mathias Mnyampala waliibuka.
Katika kipindi cha waingereza
shule zilimarishwa zaidi na magazeti yaliongezwa zaidi. pia yakaanza kuibuka mashairi
ambayo hayakuwa na viwango.
Ushairi wa Kiswahili katika
kipindi cha uhuru. kupatikana kwa uhuru kulileta mkondo mpya wa uandishi wa
mashairi. Mashairi mengi yakawa ni ya kuwasifu wapigania uhuru. mfano Saadan
Kandoro, “Tumshukuru maanani”.
Kipindi cha uhuru pia kilikuwa
kipindi cha kuibuka kwa mashairi ya kihakiki ambayo hayakuwa katika mkondo wa
kikasuku. mfano Seif Khatib aliandika “Fungate ya Uhuru.”
Katika kipindi hiki pia paliibuka
mgogoro wa ushairi kati ya wanausasa na wanamapokeo. Mgogoro huu ni mrefu na
unahitaji mjadala wa peke yake. Kwa ufupi tu wanausasa hawakukubali kufungwa na
sheri ya urari wa vina na mizani katika shairi.
Ushairi wa Kiswahili katika
kipindi cha utandawazi. Utandawazi umeimarika katika kipindi cha miaka ya 1990.
umeingiza athari nyingi za kigeni katika ushairi mojawapo ya athari hizo ni
kuibuka kwa ushairi mpya kama bongofleva na taarabu.
Hivyo ni kweli kabisa kuwa
ushairi wa Kiswahili haukutoka katika ombwe au utupu bali umepitia katika
vipindi mbalimbali ambamo ushairi huu umechota mambo na sifa kadha wa kadha.
Hata hivyo ushairi wa Kiswahili katika kipindi cha ubepari umebadilika mno,
hasa ukizingatia katka kipindi hiki kila kitu huwa ni biashara.
MAREJEO
Samwel. M.(2015). Umahiri Katika Fasihi ya Kiswahili.
Mevel Publishers. Dar es salaam
Hyslop, G (1957) Afadhali Mchawi. Nairobi.EALB
Kahigi, KK & M.M Mulokozi
(1973) Mashairi ya Kisasa. Dar es
salaam: Tanzania Publishing House