Uhakiki wa Wimbo Nipeni Maua Yangu wa Roma Mkatoliki

Kava la wimbo wa nipeni maua yangu likimuonesha Roma, jeneza na maua

Roma Mkatoliki ni mwanamuziki machachari anayefanya mziki wa kufokafoka maarufu kama ‘Hiphop.’ kibao cha Mr President kilimtambulisha vyema. Katika wimbo huo, msanii huyu anamsema waziwazi rais kuwa kashindwa kutimiza ahadi yake ya maisha bora kwa kila Mtanzania.

Baada ya kibao hicho, alijipatia umaarufu mkubwa na alitoa vibao vingine vikali na kama kawaida aliendelea kusema mambo mazito bila kificho.

Roma Mkatoliki hakuishia kuwasema wanasiasa tu, aliwasema hata wachungaji katika wimbo wake wa Pastor.

Roma siyo malaika, kuna wakati anakosea. Katika wimbo uitwao Tanzania anasikika akisema, “Kimbilio la waliofeli ni ualimu na upolisi” (Roma, 2008). Hapo msanii alikosea pengine ni kwa kukosa taarifa muhimu juu ya sekta nyeti ya ualimu na ile ya upolisi. Kuna hatari ya kubeba kila kinachosemwa na watu na kukitangaza zaidi na Roma hajaiepuka hatari hii.

Mwalimu Julius Nyerere aliyeleta uhuru wa Tanzania hakufeli, Mwalimu Mahatma Gandhi aliyewapatia uhuru India hakufeli, Mwalimu Nelson Mandela hakufeli, Mwalimu Mao Zedong aliyewakomboa Wachina hakufeli, kiongozi wa kwanza wa Korea Kaskazini Mwalimu Kim Il-sung hakufeli, Mwalimu Jomo Kenyatta aliyewafukuza wanzungu Kenya hakufeli, Mwalimu Kwame Nkrumah mkombozi wa Ghana hakufeli na Mwalimu Fidel Castro mjamaa wa kweli huyu na mwamba imara wa Cuba, hakufeli. Na mimi Mwalimu Makoba, Mwalimu wa Walimu na Wanafunzi, sikufeli!

Ualimu ni wito, ni mapenzi ya kweli kuelekea kuwaelimisha wengine na wala hauhusiani na alama za darasani, kwa mantiki hiyo, si kila mtu anawito wa ualimu, si kazi ambayo kila mtu ataifanya na hakuna mwalimu aliyefeli. Sijawahi kuona mwanafunzi wa kidato cha nne aliyepata daraja sifuri akaenda kusomea ualimu! Maneno ya kwamba walimu ni watu waliofeli haijulikani katika jamii yaliingizwa na nani na haileweki hata huko kufeli kunakosemwa ni kufeli kupi. Mwalimu wa sekondari kwa mfano, anafaulu kidato cha nne, anafaulu kidato cha sita, anaenda chuo kikuu, anafaulu mitihani yote kwa miaka mitatu mfululizo na kukamilika kuwa mwalimu, huyu kafeli wapi?

Wimbo wa Nipeni Maua yangu ni kilio cha msanii Roma kuona kwamba pamoja na mambo mengi aliyofanya hususani katika kuwasemea wanyonge, hapewi heshima anayostahili. Katika wimbo huu, anaendelea kuwatetea wanyonge na kuwasema mabwana wakubwa. Katika wimbo huu Roma amemshirikisha msanii mwenzake anayeitwa Abiud ambaye amekipamba vyema kiitikio chenye sauti ya simanzi ya wanyonge wanaomuita Roma, Abiud anasikika,

“Tunakupenda Roma, tunakumiss Roma,

Rudi nyumbani Roma, utusemee,

Tunakupenda baba, tunakumiss mwana,

Tunakukumbuka sana.”

Katika kiitikio hicho, wanyonge wanatamani kumuona Roma akirejea nyumbani. Msanii huyu kwa sasa anaishi Marekani. Kuna kipindi wakati akiishi Tanzania alitekwa kwa sababu ya muziki anaofanya. Inaonekana mabwana mkubwa walichoka kutukanwa wakaamua kumnyamazisha. Wengi wanaamini kisa chake cha kutekwa ndiyo kilimfanya achukue maamuzi ya kuishi Marekani. Hakuna habari rasmi katika hili. Kiitikio hicho ni kilio cha wanyonge waliokosa msemaji, sasa wanamuita shujaa wao arejee ili aendelee kuwasemea.

Katika upande wa mtindo, tunaona msanii akitumia vina vya: o, ni, le, go, ma, ja, zi na vingine vingi. Tazama mfano.

“Yaani nchi wanaifanya mti mjenzi anauona mbao

Ndege ataona makazi mkulima ataona mazao.”

Pia, tuangazie upande wa matumizi ya lugha. Msanii ametumia tamathali za semi nyingi ikiwemo mubaalagha.

“Tanzania haijaezekwa bati na wamekula pesa ya ujenzi,”

Kauli hiyo ni utiaji wa chumvi kwani nchi haiwezi kuezekwa bati.

Tamathali nyingine ya semi ni sitiari. Tazama mfano kutoka kwa msanii.

“Vipi nitafuzu kichwa suzuki engine ya Isuzu,”

Msanii anafananisha kichwa chake na gari aina ya Suzuki iliyofungwa injini ya Isuzu.

Tamathali nyingine ya semi ni tashihisi. Msanii anasema, “Mdomo unacheza sebene.” Sebene huchezwa na mwanadamu, lakini kinyume chake, tunaona mdomo umepewa sifa za kibinadamu za kucheza sebene.

Vilevile kuna matumizi ya lugha ya picha na taswira. Msanii anasema, “Tanzania haijaezekwa bati na wamekula pesa ya ujenzi,” hapa msanii anatujenge picha ya nchi ya Tanzania ikiwa haijaezekwa bati, tunaona nyumba isiyoezekwa na haina dalili za kuezekwa kwa sababu pesa za ujenzi zimeliwa na viongozi. Hapo kuna taswira ya bati na pesa ya ujenzi. Bati ni maendeleo. Hivyo msanii anaposema Tanzania haijaezekwa bati anamaanisha Tanzania haina maendeleo. Taswira nyingine ni pesa ya ujenzi, hii ni pesa ya maendeleo. Inaweza kuwa pesa kwa ajili ya kujenga shule, barabara, hospitali na huduma nyingine muhimu katika jamii.

msanii anaongeza picha nyingine pale anaposema,

“Yaani nchi wanaifanya mti mjenzi anauona mbao,

Ndege ataona makazi mkulima ataona mazao,

Mganga atauona dawa na mpishi atauona kuni,

Ataemiliki mwenye power sisi atatusagia kunguni,”

Tunachorewa picha ya nchi iliyogeuzwa mti. Tunawaona wajenzi, ndege na waganga wakiutumia mti huo kwa kadri ya uwezo wao. Taswira zinazoonekana hapo ni taswira ya mti, taswira hii ina maana ya nchi ya Tanzania. Taswira nyingine ni mjenzi, ndege, mkulima, mganga, mpishi na ‘mwenye power’. mjenzi na wenzake wakulima, waganga na wapishi wanajaribu kuutumia mti huo vyema, lakini mtu mwenye maamuzi ni ‘mwenye power’. ‘mwenye power’ anawakilisha mwenye mamlaka. Inaonekana kwamba, pamoja na kwamba nchi ya Tanzania ni ya watu wote, kwa mtazamo wa msanii, mwenye mamlaka ndiyo ana sauti zaidi ya kufaidi rasilimali za taifa na wengine wakibaki kubahatisha.

Mti mkubwa umezungukwa na wakulima, madaktari, ndege na wajenzi
Mfano wa mti unaotajwa na Roma
Msanii anasema “Mbona vyuma vimekaza halafu mama anaificha grease,” vyuma kukaza ni hali ya maisha kuwa ngumu, ‘grease’ ni chochote kinachorahisisha maisha. Kwa mfano, utoaji wa ajira, kushuka kwa bei za bidhaa, kupunguzwa kwa kodi na mengine mengi.

Msanii hajasahau kutumia ucheshi katika kazi yake, hapa anasikika akisema,

“Mi sio CCM sio CHADEMA hili niliweke wazi,

Ila ukiweka CCM na Andazi ntachagua Andazi,”

Pia, msanii ametumia misimu, anasikika akisema, “anaupiga mwingi,” ikiwa na maana ya kufanya jambo vizuri.

Tunaona matumizi ya nahau ‘ng’ata sikio’, “Na ninamkubali na nitamng’ata sikio kama hujui,” msanii anaonyesha kwamba anamkubali kiongozi wake na anaouwezo wa kuzungumza naye.

Katika upande wa dhamira, msanii anaibua dhamira nyingi ikiwemo: rushwa, matumizi mabaya ya madaraka, uhuru wa kusema, kupoteza matumaini, ukosefu wa ajira, unafiki, unyonyaji, umasikini, matabaka, ujinga, katiba mpya, udikteta na uzalendo.

Katika dhamira ya kupoteza matumaini, msanii anasikika akifoka kwa sauti yake nyembamba, “Simuamini mtawala na mpinzani simsadiki,” hii inadhihirisha wazi namna ambavyo wananchi hawana imani na watawala wao na wamekosa watetezi kwani hata wapinzani wakati mwingine wamekuwa wakitetea maslahi yao. Mnamo mwaka 2015 mpaka 2021, Tanzania ilishuhudia wabunge wa upinzani wakinunuliwa kama karanga na kuwatelekeza wanachi waliowachagua. Pia, kumekuwa na malalamiko yasiyo na uthibitisho hivi karibuni kuwa kuna baadhi ya viongozi wakubwa wa vyama vya upinzani wameramba asali. Pengine matukio haya ndiyo yamemfanya msanii apoteze matumaini. Watawala wanaharibu mambo na wapinzani hawaaminiki.

Msanii anatuachia ujumbe ufuatao: kwanza, wapinzani wafanye kazi ya kuwatetea wananchi na kamwe wasitumikie matumbo yao. Pili, kuwe na uhuru wa kusema kwani mengi yanayosemwa yanalenga katika kuijenga jamii. Tatu, serikali itoe ajira kwa vijana na nne, siasa inamhusu kila mtu hivyo ni vyema kama kila mwananchi atashiriki katika shughuli za kisiasa.

Kwa kuhitimisha, Nipeni Maua Yangu ni wimbo wa watu wa tabaka la chini, wale ambao hawaridhishwi na yale yanayotendwa na viongozi wao. Pia, ni ushauri mzuri kwa viongozi wasikivu na ni shambulizi kali kwa viongozi wasiopenda kukosolewa. Msanii Roma ameendelea kuwa sauti ya wanyonge na hakika anastahili kupewa maua yake.

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024

Jinsi ya Kuandika Risala | Kiswahili Kidato Cha Nne