Ushauri wa Waandishi wa Kazi za Fasihi Kuhusu Kutawala Lugha Wanayotumia

Mwandishi anaandika katika kompyuta

Mwandishi mzuri wa kazi ya fasihi ni yule anayeweza kuitawala lugha yake. Kutokana na maarifa uliyoyapata katika kozi hii, kama ukipata muda wa kushauriana na waandishi wa kazi za fasihi ya Kiswahili ni mambo gani ya msingi yanayohusiana na lugha utakayowashauri wayazingatie? (Swali hili ni la utafiti na uchunguzi: pamoja na kusoma marejeleo mengine yanayohusiana na swali hili, wanakikundi wakusanye data kutoka kwa wanafunzi wanaosoma kozi hii na kuzitumia katika kujibu swali.)
Lugha ni roho ya kazi ya fasihi. Hivyo, kuitawala ni jambo lisiloepukika kwa waandishi. Katika kuchunguza mambo yanayohusiana na lugha ambayo waandishi wa kazi za fasihi ya Kiswahili wanapaswa wayazingatie, marejeleo mbalimbali ya wataalamu yalisomwa, pia, data zilikusanywa kutoka kwa wanafunzi wanaosoma kozi ya Elimu Mitindo ya Fasihi ya Kiswahili, wanafunzi 50 walihojiwa mnamo siku ya tarehe 24-05-2017 mpaka 27-05-2017, na haya yalikuwa majibu yao kwa ufupi:
          Asilimia 70 ya watafitiwa walishauri matumizi ya lugha isiyo na matabaka. Walidai kuwa baadhi ya waandishi wanatumia lugha ngumu ambayo ina wabagua watu wenye elimu ndogo au ambao hawakusoma. Baadhi ya watafitiwa, walikitaja kitabu cha MZINGILE kilichoandikwa na E. Kezilahabi kuwa miongoni mwa vitabu vinavyotumia lugha ngumu isiyoeleweka kwa watu wa kawaida.
          Vilevile, asilimia 30 ya watafitiwa waliwashauri waandishi wazingatie ushikamani katika kazi zao. Watafitiwa hao walidai kuwepo kwa waandishi chungu nzima ambao kazi zao zimekosa ushikamani. Mmoja kati ya watafitiwa waliotoa hoja hii, alikitaja kitabu cha DAMU YA UKOO WANGU kilichoandikwa na Keneth Paul kuwa mfano wa kitabu kisichokuwa na ushikamani.
          Pamoja na hayo, ufuatao ni ushauri wangu uliotokana na kukusanya data kwa wanafunzi, kusoma marejeleo mbalimbali ya waaalamu, pamoja na maarifa niliyoyapata katika kozi ya Elimu Mitindo ya Fasihi ya Kiswahili, waandishi katika uandishi wa kazi zao wazingatie mambo haya ya msingi:
          Waandishi wa kazi za fasihi wazingatie uakifishaji. Mtaalamu Wamitila (2007), anataja majukumu ya uakifishaji kuwa ni: Kumsaidia msomaji kutua, kupumua, kuelewa maana katika kifungu kilichoandikwa na kumsaidia msomaji kuelewa maana wazi ilivyo. Waandishi wengi hawazingatii kipengele hiki. cha kushangaza ni kwamba hata waandishi wasomi mara kadhaa wameshindwa kukitendea haki. Kwa mfano,
“Wajitetea na kuulaani uchumi kwa yale yote
Eti ndio chanzo cha mambo hayo yote” (Method na Akech, 2013:15).
Katika shairi hilo mshairi hajatumia alama ya mkato, uandishi huu unamnyima msomaji nafasi ya kupumua.
          Juu ya hayo, waandishi wazingatie matumizi ya lugha yenye ubunifu. Mwandishi mzuri hupita katika vipengele vitatu vya lugha ambavyo ni: misemo, nahau na methali, tamathali za semi na matumizi ya picha na taswira. Kwa mfano, mwandishi Shafi Adam Shafi ametumia tamathali nyingi za semi ambazo zimeipamba kazi yake ya VUTA N’KUVUTE. Miongoni mwa tamathali za semi zilizotumika katika VUTA N’KUVUTE ni: Takriri, ritifaa, lakabu, kijembe, tashibiha, sitiari na tashihisi. Hivyo waandishi waige mfano huu na wakipe nguvu kipengele hiki kwani husaidia kuongeza mvuto na kurahisisha uelewekaji wa ujumbe unaolenga kutolewa na mwandishi.
                    Tena, waandishi wahariri kazi zao kabla hazijachapwa. Uhariri wa kazi husaidia kubaini baadhi ya makosa ya kawaida ambayo hufanyika wakati wa uandishi. Ni jambo la kushangaza kuwa, mwandishi George Cleope Mapunjo katika tamthiliya yake ya SIRI YA MTOTO AJUAYE MAMA ameandika msamiati wa lugha ya Kiswahili usivyotakiwa kuandikwa katika jalada la nyuma la kitabu chake. Maneno haya yameandikwa na Mapunjo: Siri ya mtoto Ajuaye Mama ni kitabu cha Tamthiya… ni kitabu kinachoonyesha uhasilia kuhusiana na baba harali wa mtoto… kwa mujibubu
Makosa hayo yanayofanywa na mwandishi tena katika sehemu muhimu ya kitabu yanafukuza wasomaji hata kabla hawajatazama kilichoandikwa ndani. Ni muhimu waandishi wakahariri kazi zao ili kuepuka kushushwa thamani ya kazi hizo.
          Kwa kuhitimisha, msingi wa kazi ya fasihi ni lugha. Mwandishi ataweza kuitawala lugha yake endapo atazingatia mambo haya: Ushikamani, uakifishaji na kuhariri kazi. Endapo hayo yote yatazingatiwa, jamii itapata nafasi ya kusoma kazi bora za fasihi.
MAREJELEO
Kezilahabi, E. (1991). Mzingile. Nairobi: Vide~Muwa Publishers Limited.
Mapunjo, G. (2014). Siri ya Mtoto Ajuaye Mama. Dar es Salaam: Baraka Press and Stationery.
Method, S na Akech, J. (2013). Diwani ya MEA. Dar es Salaam: Meveli Publishers.
Paul, K. (2013). Damu ya Ukoo Wangu. Dar es Salaam: Karljamer Print Technology.
Shafi, A. (1999). Vuta n’Kuvute. Dar es Salaam: Mkuki na Nyota Publishers.
Wamitila, K.W. (2007). Kichocheo cha Fasihi: Simulizi na Andishi. Nairobi: Focus Publications Ltd.


Popular posts from this blog

Uhakiki wa Tamthiliya ya Kilio Chetu

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Hotuba