Utumizi wa Lugha | Kiswahili Kidato cha Sita

Women speaking.

Rejesta

Rejesta ni matumizi ya lugha kutokana na muktadha maalumu. Siku zote, matumizi ya lugha hutofautiana kutokana na mambo mengi.

Mambo ya kuzingatia unapotumia lugha

Wakati unatumia lugha, kuna mambo ya kuzingatia kama yanavyoelezwa:

1. Mazingira

Mazingira humwamulia mtu namna ya kutumia lugha. Kwa mfano, lugha ya hotelini ni tofauti na lugha ya kanisani. Kutokana na mazingira, tunaweza kupata lugha ya: hotelini, shuleni, ofisini, kanisani na mitaani.

2. Uhusiano baina ya wahusika

Uhusiano baina ya wahusika, hufanya matumizi ya lugha yabadilike. Mfano, lugha ya marafiki vijana, imejaa misimu mingi na maneno yasiyo na adabu. Lugha ya baba na mtoto ina maneno yenye heshima. Pia, uhusiano baina ya wahusika unatupatia lugha ya mtu na mpenzi wake, mwalimu na mwanafunzi wake, meneja na wafanyakazi wa chini yake n.k

3. Mada ya mazungumzo

Mada ya mazungumzo ndiyo inayokuamulia maneno ya kusema. Kutokana na mada ya mazungumzo tunapata lugha ya: kibiashara, kitaaluma, mahubiri, kisiasa, kisheria n.k

4. Madhumuni ya mazungumzo

Watu wanapotumia lugha huwa na lengo. Kutokana na malengo hayo, lugha inayotumiwa nayo hubadilika ili kuendana na lengo la mzungumzaji. Kama lengo la mzungumzaji ni kuomba msaada fulani, atatakiwa kutumia lugha ya unyenyekevu kama, ‘tafadhali,’ ‘samahani,’ n.k kama lengo ni kutoa amri, lugha ya mzungumzaji itakuwa na maneno yenye kuashiria amri kama vile, ondoka, cheza, soma, imba n.k

5. Utanzu wa mawasiliano

Utanzu wa mawasiliano unanafasi kubwa katika uteuzi wa lugha. Kama ni utanzu wa hotuba, majadiliano, masimulizi n.k matumiziya lugha lazima yaendane na utanzu huo.

6. Mila na desturi

Mila na desturi humlazimisha mzungumzaji kubadili lugha yake ili aendane nazo. Kutokana na mila na desturi za Waswahili, matusi hayapaswi kuzungumzwa waziwazi, hivyo, mzungumzaji anapaswa kutumia tafsida.

Mitindo mbalimbali ya lugha kutokana na mazingira

Mtindo wa lugha ni mabadiliko katika kutumia lugha. Lugha moja, ina mitindo tofauti kutokana na mazingira. Mfano, lugha inayotumika kanisani ni tofauti na lugha ya msikitini. Ifuatayo, ni mitindo mbalimbali ya lugha:

1. Mtindo wa shughuli za kiofisi na kikazi

Mtindo huu huweza kupatikana ofisini, mikutano, vikao n.k. Miongoni mwa sifa za mtindo huu ni: usahihi wa mambo yanayojadiliwa, matumizi ya msamiati unaoonesha vyeo vya watu na kutotumika kwa mafumbo, lahaja na nahau.

2. Mtindo wa mambo ya kitaaluma na kisayansi

Mtindo huu unatumika katika mambo ya kitaaluma, kama vile, Kiswahili, Kemia, Bailojia na Fizikia. Sifa za mtindo huu ni: usahihi na ukweli wa mambo yanayojadiliwa, kuwepo na mantiki katika jambo linalojadiliwa, uendeshaji wa mjadala bila kuonesha upendeleo wa mwandishi, matumizi ya istilahi za kitaaluma na kisayansi, na sifa nyinginezo.

3. Mtindo wa magazetini na shughuli za kisiasa

Katika mtindo huu sifa zake ni: upendeleo wa wazi wa mzungumzaji, kuwepo kwa mantiki katika jambo linalozungumzwa na matumizi makubwa ya istilahi na maalumu za magazetini na shughuli za kisiasa.

4. Mtindo wa mazungumzo ya kawaida ya kila siku

Mtindo huu ni wa maongezi yasiyo rasmi yaani maongezi ya kawaida yanayofanyika nyumbani na mahali pengine pa kawaida. Mazungumzo haya yanaweza kuwa kati ya baba, mama, mtoto n.k

Dhima ya rejesta katika lugha

Katika lugha, rejesta ina dhima au matumizi mengi, miongoni mwa dhima hizo ni hizi zilizoelezwa:

1. Kukidhi haja ya mawasiliano ya uwanja fulani maalumu

Kila eneo lina namna yake ya uzungumzaji. Ili uweze kufikisha ujumbe kijiweni, ni lazima kutumia mtindo wa kijiweni. Pia, huwezi kufikisha ujumbe kanisani kwa kutumia mtindo wa lugha za mitaani, hivyo, rejesta ina saidia kufikisha mawasiliano katika uwanja fulani maalumu.

2. Kutambulisha wazungumzaji kuwa wao ni wa kundi fulani

Rejesta huweza kutambulisha kuwa, watu fulani ni wa kanisani, msikitini, kijiweni au pengine ni wavuvi kutokana na mtindo wa mazungumzo yao.

3. Kupunguza ukali wa maneno

Rejesta inapotumiwa na kundi fulani, hupunguza ukali wa maneno kwa kutumia tafsida. Kwa mfano, badala ya kusema naenda chooni, wazungumzaji wengi husema, naenda ofisini.

4. Kupamba lugha

Rejesta hufanya lugha ivutie. Lugha ya kawaida inaweza isiwe na mvuto kama pale rejesta inapotumika. Kwa mfano, badalaya kuuliza nani kaagiza wali na kuku? Muuzaji huuliza nani wali kuku? Maneno haya yana mvuto wa aina yake.

5. Kukuza lugha

Yapo maneno yaliyotokana na rejesta na baadae yakawekwa katika msamiati wa lugha ya kiswahili na hivyo kusaidia katika ukuzaji wa lugha hii. Mifano ya maneno hayo ni: shangingi, kibaka, mlokole na dingi.

6. Kuficha ujumbe

Baadhi ya watu huongea kwa rejesta zao ili kuficha maana kwa wale wasiohusika. Kwa mfano, wanafunzi darasani wanaweza kusema, ‘naamsha majeshi,’ wakiwa na maana ya kutoroka shule.

Misimu

Misimu ni semi za muda na mahali maalum ambazo huzuka na kutoweka kutegemea mazingira maalum.

Aina za misimu

1. Misimu ya pekee

Ni misimu ambayo hutumika katika eneo moja na wale wasiohusika katika eneo hilo hawawezi kuelewa wala kuitumia.
Mfano: Wanafunzi wa shule moja, wanaweza kuwa na aina ya misimu yao. Katika shule ya Kigoma Sekondari, wanafunzi wa shule hiyo wana msimu uitwao ‘ugu’, wakiwa na maana ya kuamka usiku kusoma. Msimu huu huwezi kuukuta katika shule zingine.

2. Misimu ya kitarafa

Hii ni misimu ambayo huweza kufahamika kwa ngazi ya tarafa, kata, wilaya na hata mkoa. Misimu hii huweza kupatikana kutokana na vitu na watu waliopo katika eneo hilo.
Mkoani Dar es Salaam kuna msimu uitwao, ‘maji ya Kandoro’, ukiwa na maana ya maji yaliyofungwa katika mfuko mweupe wa plastiki. Mikoa mingine haina msimu huo.

3. Misimu zagao

Ni misimu ambayo huenea nchi nzima na wakati mwingine huvuka mipaka ya nchi.
Misimu kama: wafurukutwa, wapambe na ngangari ni misimu zagao.

Sifa za misimu

1. Huzuka na kutoweka

Misimu huzuka na kutoweka kutokana na kupita kwa wakati. Mfano, kipindi cha ujamaa kulikuwa na misimu mingi kama: kupe n.k. hii yote haipo leo hii.

2. Ni lugha isiyo sanifu

Misimu huwa nje ya lugha rasmi. Hii ni kwa sababu, huzushwa na watu wa kundi fulani kwa sababu zao maalum.

3. Ni lugha ya mafumbo

Ni vigumu kuelewa misimu kama huhusiki katika kundi linaloitumia, hii ni kwa sababu, misimu imejaa mafumbo na wasiohusika hushindwa kuelewa.

4. Ina chuku nyingi

Misimu imetiwa chumvi ama sifa zilizopitiliza. Ni rahisi kukuta vijana wakimuita mwenzao ‘mwamba’ hata kama kafanya jambo dogo.

5. Hupendwa na wengi

Wengi hupenda misimu, na wengi huitumia ili kuonesha uhodari wao katika lugha.

6. Misimu ina maana nyingi

Hutokea mara kwa mara misimu kuwa na maana zaidi ya moja. Mfano: msimu unaotumika Mbeya unaweza kuwa na maana tofauti ukitumika Dar es Salaam. Mtumiaji wa misimu anaposema ‘kausha’, msimu huu unaweza kuleta maana zaidi ya moja. Kwanza inaweza kuwa nyamaza au inaweza kuwa na maana ya kukausha chakula aina ya ‘chipsi mayai.’

Umuhimu wa kutumia misimu katika lugha

Misimu ina umuhimu wake katika lugha kama inavyoelezwa:

1. Kukuza lugha

Baadhi ya maneno hutoka kuwa misimu na kuwa lugha rasmi. Mifano ya maneno yaliyoanza kuwa misimu na sasa ni maneno rasmi ni: magendo, marupurupu, chungu nzima, daladala na mtumba.

2. Kupamba lugha

Misimu hupamba lugha na kuwafanya watu wafurahi pale wanapozungumza. Mfano, mzungumzaji anaweza kusema, “Leo Yanga hawahemi, tuna mashambulizi chungu nzima ya kuwashikisha adabu ‘visura’ hawa!”

3. Kufanya mawasiliano yawe mafupi na yanayoeleweka

Misimu husaidia kufupisha mawasiliano kwa kutumia maneno machache na hivyo, ujumbe hueleweka kwa haraka. Mfano: daladala ni msimu unaoeleweka kwa haraka zaidi na kuokoa muda tofauti na mtu akisema, magari madogo yanayobeba abiria ambayo husafiri kutoka sehemu moja ya mji mpaka nyingine lakini ndani ya mji huohuo.

4. Kupunguza ukali wa maneno

Misimu hutumika kupunguza ukali wa maneno katika mada tofauti kama vile mapenzi, mazungumzo ya kila siku n.k mfano, mtu husema, nakwenda ‘ofisini’ badala ya kusema chooni.

5. Kuhifadhi historia ya jamii

Misimu huhifadhi historia ya jamii, hii ni kutokana na wakati ambao misimu hii ilianza kutumika.
Kipindi cha ujamaa misimu iliyotumika ilikuwa: ubepari, ubeberu, ukupe, unyonyaji, ujamaa na utaifishaji.
Wakati wa ubepari ilitumika misimu hii: ubinafsishaji, uwekezaji, vitega uchumi, utandawazi.
Wakati wa mfumo wa vyama vingi, misimu hii ilikuwa maarufu: chama tawala, mkereketwa, mfurukutwa, mpambe, wazawa, ngangari na mgombea mwenza.

6. Kuwaunganisha watu wa makundi mbalimbali

Misimu huwaunganisha watu wa makundi yote. Huwaunganisha maprofesa, madaktari, walimu na watu wengineo. Misimu kama: daladala, ubepari, vitega uchumi na utandawazi, hutumiwa na watu wa matabaka yote.

Changamoto za kutumia misimu katika lugha

1. Huharibu lugha sanifu

Misimu huwa nje ya lugha inayohusika, hivyo huharibu lugha sanifu kwa kuweka maneno mapya yasiyo sanifu.

2. Huleta msamiati wenye matusi

Matusi ni sehemu ya misimu. Misimu mingi huambatana na maana zenye matusi. Mfano: ngunguri ni msimu unaomaanisha mtu asiyetumia akili.

3. Ni lugha ya mafumbo

Siyo rahisi kuielewa misimu. Ni lugha ya mafumbo na hueleweka kwa kikundi kidogo cha watu.

4. Imetiwa chumvi nyingi

Kutokana na kutiwa chumvi nyingi, misimu haiaminiki katika jamii. Wakati mwingine, misimu huweza kupotosha.

5. Huzuka na kutoweka

Kuzuka na kutoweka kunasababisha misimu iwe na mchango mdogo katika kukuza lugha. Ni misimu michache sana ambayo hufikia hadhi ya kuwa maneno rasmi.

6. Ina maana nyingi

Kutokana na maana kuwa nyingi, hushindwa kueleweka kwa sababu kila mtu huelewa kivyake. Hii yote ni kwa sababu, misimu haina maana moja. Mfano, ni vigumu kuelewa kama beki tatu ni mfanyakazi wa ndani au ni mchezaji wa mpira anayecheza safu ya ulinzi.

Umahiri wa lugha

Umahiri wa lugha ni ujuzi wa hali ya juu wa lugha katika stadi nne za lugha yaani: kusoma, kuandika, kusikiliza na kuzungumza.
Nchini Tanzania, watu wengi ni mahiri wa lugha za makabila yao kama: kisukuma, kimakonde, kiha, kifipa na makabila mengine. Pia, watu wengi ni mahiri wa lugha ya Kiswahili ambayo ndiyo lugha inayowaunganisha watu wote.

Mambo yanayomwezesha mtu kuwa mahiri wa lugha

1.   Kusomea lugha kwa kiwango cha juu

Mtu anaposomea lugha fulani, hupata ujuzi katika msamiati, sarufi, matamshi pamoja na maana na hiyo humfanya awe mahiri wa lugha hiyo.

2.   Kutumia lugha kila siku

Mtu anayetumia lugha kila siku, uwezo wake huongezeka na kumfanya aweze kuimudu lugha husika. Mfano, kama mtu anatumia lugha ya Kiswahili kila siku katika mazungumzo yake, ni lazima mtu huyo atakuwa mahiri wa lugha ya Kiswahili.

3.   Kuwa karibu na wajuzi wa lugha

Mtu anapokuwa karibu na wajuzi wa lugha, hufaidika kwa kuweza kufundishwa matumizi ya lugha hiyo pamoja na kuiga jinsi wanavyotumia lugha wajuzi. Mfano, mtu anayetoka uingereza, anapofika nchini Tanzania na kuwa karibu na wajuzi wa lugha huweza kujifunza lugha hiyo na hatimaye kuwa mahiri.

4.   Kuwakosoa na kuwasahihisha waharibifu wa lugha

Anayekosoa huwa mahiri kwa kuonesha uwezo wake na kuwa bora zaidi. Pia, wanaokosolewa huweza kuwa mahiri kwa kujifunza njia sahihi za kutumia lugha.

Athari za umahiri wa lugha

Umahiri wa lugha una athari zake. Watu ambao ni mahiri wa lugha zaidi ya moja, hukumbwa na athari hizi:

1.   Matamshi

Matamshi huweza kumbainisha mtu anatoka wapi. Mfano, mahiri wa lugha ya kikurya na Kiswahili hushindwa kutofautisha r na l. unaweza kumsikia mkurya akisema, twende mbere tukarare.

2.   Msamiati

Mahiri wa lugha ya Kiswahili na Kiingereza hujikuta wakichanganya msamiati wa lugha hizo. Mfano, msemaji anaweza kusema, ‘tunatakiwa kuwa serious kwa sababu hii application ina wahusika wengi.’

3.   Sarufi

Muundo wa lugha ya kwanza unaweza kumuathiri mahiri katika kuzungumza lugha ya pili. Katika lugha ya Kinyamwezi, mtu anapozungumza na mtu wanayeheshimiana sana, hutumia wingi badala ya umoja. Hivyo, mahiri huyu anaweza kuchukua muundo huo na kuweka katika lugha ya pili na kutengeneza sentensi hii. ‘Baba ndiyo mmefika?’. Katika mfano huo, baba ni mmoja lakini mzungumzaji katumia wingi kwa sababu ya athari za umahiri.

4.   Maana

Kuna athari ya maana kwa watu wanaozungumza zaidi ya lugha moja. Mfano, katika kinyamwezi,neno igolo lina maana ya kesho na keshokutwa. Kwa hiyo, mnyamwezi anaweza kuathiriwa na kujikuta akisema, ‘nitakwenda jana.’ Au ‘nilikwenda keshokutwa.’

Mambo yanayopoteza umahiri wa lugha

Yapo mambo yanayoweza kuupoteza umahiri wa lugha, miongoni mwa mambo hayo ni:

1.   Kutotumia lugha hiyo kwa matumizi ya kila siku

Mahiri akiacha kutumia lugha kwa matumizi yake ya kila siku, umahiri hupotea. Watanzania wengi wamepoteza umahiri wa lugha zao za kikabila kwa sababu ya kutozitumia kila siku.

2.   Kutosomea lugha hiyo kwa kiwango cha juu

Usiposomea lugha kwa kiwango cha juu, utapoteza umahiri kwa sababu ya kufanya makosa mbalimbali ya kimatamshi, kisintaksia, kisemantiki na kimuundo. Mfano, Watanzania wengi ni mahiri wa lugha ya Kiswahili, lakini wanapoteza umahiri wao kwa sababu hawajasomea lugha hiyo kwa kiwango cha juu.

3.   Hamahama ya watu

Watu wanapo hama kutoka sehemu moja kwenda nyingine huwafanya wajifunze lugha ya eneo wanalokwenda. Hii hupoteza umahiri wa lugha yao ya awali. Mfano, watu wengi wanaohama kutoka kijijini kwenda mjini, wanapoteza umahiri wa lugha zao za kikabila.

4.   Mfumo wa elimu

Shule za msingi zinatumia lugha ya Kiswahili kufundishia, hivyo wanafunzi wanapoteza umahiri wa lugha zao za kikabila. Pia, umahiri wa Kiswahili unapotea pale wanafunzi wanapoanza kusoma shule za sekondari ambako lugha ya Kiingereza hutumika kufundishia.

5.   Kutokuwa karibu na wajuzi wa lugha hiyo

Mtu anapokuwa mbali na wajuzi wa lugha, umahiri wake hupungua kwani anakuwa hana msukumo wa kuzungumza lugha kwa ufasaha. Mfano, mtu anapotoka mjini kwenda kijijini, umahiri wa lugha ya Kiswahili unaweza ukapungua kwa sababu huko kijijini watu wengi wanatumia lugha za kikabila.

6.   Kasumba

Baadhi ya mahiri wa lugha ya Kiswahili na Kiingereza wana kasumba ya kudharau lugha ya Kiswahili na kuitukuza lugha ya kiingereza. Hii hufanya umahiri wao wa lugha ya Kiswahili kupungua.

Utata katika mawasiliano

Utata ni hali ya neno au sentensi kuwa na maana zaidi ya moja. Kwa mfano, sentensi inayosema, ‘mtoto anaendesha’ ina utata kwa sababu maana mbili zinaibuka. Moja ikiwa ni kuendesha chombo cha barabarani kama gari, au ana maradhi ya tumbo la kuhara.

Sababu za utata

Zipo sababu nyingi za utata katika mawasiliano. Miongoni mwa sababu hizo ni hizi zinazoelezwa:

1.   Neno kuwa na maana zaidi ya moja

Yapo maneno mengi ya Kiswahili ambayo yana maana zaidi ya moja. Baadhi ya maneno hayo ni: kaa, nyanya na paa. Kaa ina maana ya kukaa chini, lakini, inaweza kuwa na maana ya mdudu. Nyanya ni kiungo, hata hivyo maana nyingine ya nyanya ni bibi. Paa ina maana ya kitendo cha kuelea angani au paa mnyama aishie msituni.

2.   Kutozingatia taratibu za uandishi

Alama za uandishi hufanya maana ibadilike hata kama maneno katika sentensi ni yaleyale. Mfano, tulimkuta baba na mtoto wake, Rajabu. Sentensi hiyo ina maana, tulimkuta baba akiwa na mtoto wake aitwaye Rajabu. Kama mkato usingewekwa, maana ingebadilika na ingekuwa, tulimkuta baba akiwa na mtoto wa Rajabu.

3.   Utumiaji wa maneno yenye maana iliyofichika

Maneno yenye maana ya picha huleta utata. Mfano, ninalo ua nyumbani kwangu. Neno hili linaleta utata kwa sababu inawezekana ua ni mmea au ua ni msichana.

4.   Kuwepo kwa mofimu yenye kauli ya kutendea

Mfano, ‘amempigia ngoma.’ Katika sentensi hiyo, maana nyingi zinaibuka, moja ikiwa, amepiga ngoma ili amfurahishe, amempiga na kifaa kiitwacho ngoma, au amempiga kwa sababu ya ngoma.

5.   Matumizi ya vimilikishi

Vimilikishi navyo ni sababu ya utata. Mfano, matumizi ya kimilikishi ake katika sentensi hii yanasababisha utata. ‘Ali atajenga kibanda chake.’ Hapo haijulikana kama atajenga kibanda chake mwenyewe, au Ali atajenga kibanda chake mtu mwingine.

6.   Makosa ya kisarufi na kimantiki

Mfano wa makosa hayo ni: ‘Wewe mama, mwanao amerudi shule?’ Sentensi hiyo ina maana ya kurudi shule yaani kitendo cha kwenda tena shule, au kurudi shule yaani kurudi nyumbani kutoka shule.

Jinsi ya kuondoa utata katika mawasiliano

Zipo njia nyingi za kuondoa utata katika mawasiliano, miongoni mwa njia hizo ni:
1.   Kuwe na mkazo wa sauti unaoonesha dhahiri neno gani lipewe uzito zaidi. Hii itumike katika lugha ya mazungumzo.
2.   Matumizi sahihi ya alama za uandishi kama: mkato, kituo na alama nyinginezo.
3.   Kuepuka makosa ya kimantiki na kisarufi. Miongoni mwa makosa hayo ni kosa la kuacha maneno. Mfano, Damasi ameondoka kazini. Badala ya kusema Damasi ameondoka kwenda kazini.

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024

Jinsi ya Kuandika Risala | Kiswahili Kidato Cha Nne