Matumizi ya Lugha Katika Miktadha Mbalimbali

Wanaume wanazungumza.
Matumizi ya lugha ni namna ambavyo wazungumzaji wa lugha hutumia lugha kwa kuzingatia mila, desturi na kaida mbalimbali za jamii inayohusika.

Rejesta

Rejesta ni matumizi ya lugha kulingana na muktadha fulani. Katika mazingira ya kanisani, kuna mtindo wa lugha ambao ni tofauti na lugha ya kijiweni.

Aina za rejesta

Kuna aina nyingi za rejesta kwa madhumuni ya kukidhi haja ya mawasiliano katika mazingira ,masomo na taaluma mbalimballi.Kila mazinira yana aina tofauti ya rejesta mfano rejesta ya shuleni, rejesta ya hotelini, rejesta za mitaani, rejesta za mahakamani, rejesta za sokoni na nyingine nyingi.

1. Rejesta za Mitaani

Haya ni mazungumzo yanayozungumzwa vijiweni nayo hueleweka na wazungumzaji wenyewe. Ni lugha ambayo huchipuka kutokana na kikundi cha watu ambacho ni kidogo. Mfano wa maneno yanayotumika sana mitaani ni kama vile “Mshikaji” (rafiki), Demu” (mwanamke)n.k. Kwa ujumla lugha ya mitaani ni lugha isiyo sanifu, ni lugha iliyojaa maneno ya mitaani ambayo yanaeleweka kwa wazungumzaji wenyewe.

2. Mazungumzo ya Kwenye Shughuli Maalum (Rejesta za Mahali)

Mazungumzo ya kwenye shughuli maalumu ni kama vile mazungumzo ya:
Maofisini au mahali popote pa kazi
Mahakamani
Hotelini
Hospitalini
Msikitini
Kanisani n.k
Mazungumzo ya mahotelini yana utaratibu wake ambao katika hali ya kawaida inaweza isieleweke.
Nani wali kuku?
B: Mimi
Chai moja wapi?
B: Hapa
Katika mazungumzo haya A anapouliza “Nani wali kuku”, ana maana kuwa nani anahitaji kula wali na nyama ya kuku”. Hapa hana maana ya kumwainisha mtu aitwaaye “wali kuku”.
Kwa upande wa lugha ya mahakamani ni tofauti na lugha ya hotelini. Lugha ya mahakamani inasisitiza usahihi ili kuondoa migongano miongoni mwa wanaohusika.

3. Rejesta Zinazohusu Watu

Rejesta zinazohusu watu ni yale mawasiliano yasiyo rasmi, ni yale maongezi ya kawaida ya kila siku au mazungumzo rasmi; kwa mfano mazungumzo kati ya:
Vijana wenye rika moja,
Wazee wenyewe,
Wanawake wenyewe,
Wanaume wenyewe,
Mwalimu na mwanafunzi,
Meneja na wafanyakazi wake,
Mtu na mpenzi wake, n.k.
Mazungumzo miongoni mwa marafiki wa rika moja huzungumza lugha ambayo wao wenyewe wanaielewa na sio rahisi kwa mtu wa rika lingine kuielewa lugha hiyo.

Misimu

Misimu ni maneno yasiyo rasmi ambayo huzuka na kutoweka, yale yanayobaki huwekwa katika kamusi na kuwa maneno rasmi. maneno mshikaji na dingi, ni mfano wa misimu.

Chanzo cha misimu

- Misimu huzuka kulingana na mabadiliko ya kihistoria yanayoikumba jamii husika katika nyakati mbalimbali.
- Misimu huzuka kutokana na haja ya watu kuelezea hisia zoa juu ya matukio mbalimbali yaliyotokea katika vipindi fulani kwa mfano, njaa, mafuriko, vita n.k.

Aina za misimu

- Misimu ya pekee. Hii ni misimu ambayo huelezea mahusiano ya kikundi kimoja kutoka katika utamaduni mmoja, na hujulikana miongoni mwao pekee.
- Misimu ya kitarafa. Misimu hii hujulikana na watu wengi katikia eneo kubwa, yaweza kuwa ni kata, wilaya au tarafa.
- Misimu zagao. Ni misimu iliyoenea nchi nzima au pengine kuvuka mipaka ya nchi, misimu hii husikika redioni, magazetini na hata kwenye vitabu. Msimu uliokita mizizi sana huweza kusanifishwa na kuwa msamiati rasmi.

Sifa za misimu

- Huzuka na kutoweka kufuatana na mabadiliko ya jamii.
- Ni lugha isiyo sanifu.
- Ina chuku.
- Ni lugha ya mafumbo.
- Ina maana nyingi.

Dhima ya misimu

- Hutumika kupamba lugha.
- Hutumika kukuza lugha.
- Hutumika kutunza historia ya jamii fulani.
- Hutumika kuibua hisia mbalimbali za wazungumzaji.
- Hufurahisha na kuchekesha.

Lugha ya kimazungumzo

Lugha ya kimazungumzo ni lugha ambayo hutolewa kwa njia ya mdomo. Mazungumzo yanapotolewa kunakuwa na mzungumzaji na msikilizaji.

Lugha ya kimaandishi

Lugha ya kimaandishi ni lugha ambayo hutolewa kwa njia ya maandishi. Inapotolewa lugha hii, kunakuwa na mwandishi na msomaji.

Sifa za lugha ya kimazungumzo

Lugha ya kimazungumzo ina sifa zinazoifanya iwe tofauti na lugha zingine. Sifa hizo, zinaelezwa:
1. Hutolewa kwa njia ya mdomo.
2. Mzungumzaji hukaa ana kwa ana na msikilizaji. Hii ina maana kuwa, lugha ya mazungumzo, humkutanisha mzungumzaji na msikilizaji.
3. Huambatana na ishara za mwili.
4. Huambatana na hisia kama: kulia, kucheka, kupaza sauti na kuonyesha furaha.
5. Ina matumizi ya misimu.
6. Mzungumzaji ana nafasi ya kufuta usemi wake.

Sifa za lugha ya kimaandishi

Lugha ya kimaandishi ina sifa zake ambazo zinaifanya iwe tofauti na lugha zingine. Lugha ya kimaandishi ina sifa hizi:
1. Huwasilishwa kwa maandishi.
2. Huwawezesha watu waliombali kuwasiliana.
3. Huzingatia kanuni za lugha. Ni vigumu kukuta matumizi ya misimu katika lugha ya maandishi.
4. Mwandishi hana nafasi ya kufuta maandishi yake pale kitabu kinapotoka.
5. Haina ishara za mwili.
6. Haimkutanishi mwandishi na msomaji.

Dhima za lugha ya kimazungumzo na kimaandishi

lugha za kimazungumzo na kimandishi, zinawawezesha watu kuwasiliana kwa namna mbalimbali. Mfano, mtu anapoeleza jambo fulani.
Pia, huweza kuhifadhi kumbukumbu kwa vizazi vijavyo. Mfano, lugha ya maandishi inaweza kusomwa kwa vizazi vingi bila kupotea.

Matamshi na lafudhi ya Kiswahili

Matamshi ni namna ambavyo mtu anatamka neno au jinsi mtu anavyozungumza lugha. Unaposema fulani ana matamshi mazuri ya Kiswahili utakuwa unamaanisha anazungumza Kiswahili fasaha.
Neno moja linaweza kuzungumzwa/kutamkwa kwa namna tofauti na watu mbalimbali kutokana na sababu mbali mbali, sababu hizo ni pamoja na eneo la kijiografia anakotoka huyo mtu, kabila lake, kundi lake la kijamii mfano msanii au mwanasiasa, na elimu aliyonayo. Hizi zote zinaweza zikawa ni sababu za kufanya watu watofautiane katika matamshi.

Dhana ya matamshi huhusisha

Sauti za lugha husika
Mkazo
Kiimbo

Sauti za lugha ya Kiswahili

Sauti za lugha ya Kiswahili hujumuisha irabu na konsonanti, ambazo kwa ujumla huunda sauti 24, irabu tano na konsonanti 19 (konsonanti x na q hazipo katika matamshi ya kiswahili). Sauti za Kiswahili hutamkwa kama zilivyoandikwa, kwa mfano maneno “data” au “dengue” wewe unayatamkaje? Wengi huyatamka kama yalivyo hata kama wakiwa wanazungumza kiingereza, hii ni kwa sababu maneno ya Kiswahili hutamkwa kama yalivyoandikwa.

Mkazo

Mkazo ni pale silabi inapotamkwa kwa kukazwa. Maneno ya Kiswahili huwa na silabi moja ambayo hutamkwa kwa nguvu zaidi kuliko silabi nyingine. Unapotamka silabi iliyotiwa mkazo, sauti hupandishwa juu kiasi.
Maneno mengi ya Kiswahili, hasa yale yenye asili ya Kibantu hutia mkazo katika silabi ya pili kutoka mwisho.
Kwa mfano:ba’bu, maya’i, rama’ni (mimi nilikuwa nikitamka ra’mani), baraba'ra (njia).
Baadhi ya maneno yenye asili ya kigeni, huwa na mkazo katika silabi nyingine. Kwa mfano: bara'bara (sawa sawa), Alha’misi.

Kiimbo

Ni utaratibu maalum wa upandaji na ushukaji wa mawimbi ya sauti unaojitokeza katika utamkaji wa lugha fulani.
Katika utaratibu wa utamkaji, dhana ya Kiimbo huandamana pia na dhana ya kidatu ( yaani , kiwango cha juu, cha chini au cha kati cha sauti katika usemaj), Kwa hivyo ni muhimu hapa kueleza tofauti zilizopo baina ya kiimbo na kidatu. Wakati kiimbo kina maana ya kupanda na kushuka kwa mawimbi ya sauti ya lugha, kidatu kina maana ya kiwango cha sauti isikikayo, wakati wa utamkaji ama kuwa juu, kuwa katikati au kuwa chini.

Lafudhi ya Kiswahili

Lafudhi ni matamshi ya msemaji wa lugha fulani ambayo yanatokana na athari za kimazingira. Mazingira hayo yanaweza kuwa eneo atokalo mtu, mahali alikosomea, kiwango chake cha elimu au tabaka lake la kijamii.
Lugha ya Kiswahili ni lugha ya pili kwa watumiaji wengi wa afrika mashariki, kwa hiyo hii inafanya kuwatambua wazungumzaji wa Kiswahili kulingana na makabila yao au maeneo wanakotoka. Kwa mfano, kwa hapa Tanzania tunaweza kuwatambua watu wa mwanza kwa lafudhi yao, watu wa mtwara kwa lafudhi yao, watu wa pemba kwa lafudhi yao au watu wa Musoma kwa lafudhi yao.

Utata katika mawasiliano

Utata ni hali ya neno au sentensi kuwa na maana zaidi ya moja. Kwa hiyo tungo tata ni tungo ambayo inaweza kuwa na maana zaidi ya moja.

Sababu za Utata

1. Neno kuwa na maana zaidi ya moja, kwa mfano neno mbuzi, kata n.k.
2. Kutozingatia taratibu za uandishi, Mfano; Tulimkuta Nyamizi na rafiki yake, Mazala ukilinganisha na, Tulimkuta Nyamizi na rafiki yake Mazala. Katika sentensi hizi alama (,) ndio huleta tofauti, sentensi ya kwanza inamaana kulikuwa na watu wawili Nyamizi na rafiki yake aitwaye Mazala na sentensi ya pili isiyo na alama (,) inamaanisha kulikuwa na watu wawili Nyamizi na mtu mwingine ambaye ni rafiki yake Mazala.
3. Kutumia maneno bila kuzingatia muktadha wa matumizi ya maneno hayo. Mfano, ukitumia maneno ya kijiweni kanisani, utasababisha utata.
4. Utamkaji wa maneno. Wakati mwingine utata unaweza kujitokeza katika matamshi tu, ili hali katika maandishi utata hauonekani. Kwa mfano; Mimina wewe, katika maandishi linaweza kuandikwa mimi na wewe, na hivyo kuondoa utata.
5. Mjengo wa maneno. Utata huu huzuka katika vitenzi kama pigia. Chanzo cha utata katika kitenzi hiki ni kiambishi –i-. Kiambishi hiki kinaweza kumaanisha: kwa ajili ya…, kwa sababu ya.., kwa kutumia chombo fulani.., au mahali fulani.

Maswali

1. Nini maana ya utumizi wa lugha?
2. Taja mambo manne yanayotakiwa kuzingatiwa wakati wa mazungumzo.
3. Lugha ya kumwonya mtu inatofautianaje na lugha ya kumpa mtu nasaha?
4. Lugha inayotumiwa kati ya baba na mtoto inatofautianaje na lugha inayotumiwa na marafiki wa rika moja?
5. Rejesta ni nini?
6. Taja dhima tano za rejesta.
7. Andika mazungumzo mafupi kati ya daktari na mgonjwa wakiwa hospitali.
8. Orodhesha baadhi ya maneno na misemo inayotumika: kanisani, msikitini na katika somo la Kiswahili.
9. Misimu ni nini?
10. Taja vyanzo vya kuzuka kwa misimu.
11. Orodhesha misimu mitano unayoifahamu.
12. Taja misimu ambayo imevuka mipaka ya nchi.
13. Nini maana ya tungo tata?
14. Eleza maana mbili kwa kila tungo katika tungo hizi:
A. Baba Ali amerudi B. Unamwitia nini? C.
15. Nini maana ya lugha ya kimazungumzo?
16. Taja miktadha ambayo lugha ya kimazungumzo hutumika.
17. Taja faida tatu na hasara tatu za lugha ya kimazungumzo.
18. Taja mambo mawili yanayoweza kusababisha watu wasiweze kuelewana wanapozungumza.
19. Eleza uzungumzaji huu ni wa jamii gani?
A. “Chacha wewe mbona unachukua chiatu changu!”
B. E bhatoto hamuyambo?

Popular posts from this blog

Uhakiki wa Tamthiliya ya Kilio Chetu

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Risala | Kiswahili Kidato Cha Nne