Uhusiano wa Dhana ya Masharti Ukweli na Dhana ya Uchopezi

vitu viwili vinavyofanana vimetengeneza umbo la moyo

Swali

Masharti ukweli ina uhusiano wa karibu na dhana ya uchopezi. Jadili dai hili kwa mifano Dhahiri ya sentensi za Kiswahili.

Resani (2014) anadai kuwa kanuni ya masharti ukweli (ameitaja kama kanuni ya sifa ya thamani ya ukweli) ni yale ambayo unafahamu siyo ya kweli. Akifafanua zaidi kuhusu kanuni ya thamani ya ukweli, mwandishi anasema:

Usiseme yale ambayo unafahamu siyo ya kweli. Pili usiseme yale ambayo huna ithibati nayo au uhakika wa kutosha. Mfano kama wewe si msemaji wa umoja au kikundi fulani usiseme mambo yanayokihusu kikundi hicho kwenye midia au kwa wanahabari. (Resani, 2014:77)

Tunaweza kusema kwamba Nadharia ya masharti ukweli husisitiza dhana ya ukweli katika ujasiri wa maana, hivi kwamba maana sharti iwe ya kweli na ukweli huo ubainishwe bayana. Nadharia hii iliasisiwa na wanamantiki na wanafalsafa, kisha ikafafanuliwa na wanaisimu.

Mfano (a) Ukweli wa kihistoria

i/ Tanganyika ilipata uhuru wake mwaka 1961.

ii/ Rais wa kwanza wa Tanzania kufa akiwa madarakani ni John Pombe Magufuli.

          (b) Ukweli wa maarifa ya kiulimwengu

Ukweli huu hutokana na uhalisia wa kiulimwengu ambao kila mwanajamii anakuwa nao. Mfano shairi huundwa na beti, mistari, vina na mizani au mwanamke hujifungua.

   (a)ukweli wa kiisimu

Ukweli huu hubainishwa kupitia mfuatano wa maneno katika sentensi na usahihi wa mfuatano huo.

      i ) Maimuna aliolewa na Baraka (sahihi)

      ii) Baraka aliolewa na Maimuna ( si sahihi)

Kwa upande mwingine, dhana ya uchopezi imetolewa maana na wataalamu wengi kama inavyoelezwa:

Lyons (1977) anadai kuwa uchopezi ni uhusiano uliopo kati ya P na Q ambapo P na Q zinasimama kama vihusishi ambapo ukweli wa Q hujidhihirisha kutokana na ukweli wa P (na usikweli wa Q hujidhihirisha kutokana na usikweli wa P) hivyo P huchopeza Q.

Matinde (2012) anasema uchopezi ni dhana inayotumiwa na wanaisimu amali kufafanua uhusiano wa sentensi mbili au zaidi na hatimaye hufasiri maana za sentensi hizo kutokana na mtiririko wa mantiki.

Kwa ujumla, uchopezi ni uhusiano wa sentensi ambapo sentensi moja huchopeza nyingine, yaani ukweli wa sentensi moja unahakikisha ukweli wa sentensi ya pili au usikweli wa sentensi moja kubeba usikweli wa sentesi ya pili. Mifano ifuatayo inafafanua:

a. Mwalimu alifundisha somo.

b. Somo limefundishwa.

Kwa lugha ya kawaida tunaweza kusema maana ya sentensi ‘b’ ni sehemu ya sentensi ‘a’. kama sentensi ‘a’ ni kweli basi na sentensi ‘b’ ni kweli. Pia kama moja siyo kweli na ya pili si kweli.

Masharti ukweli ina uhusiano wa karibu na dhana ya uchopezi. Dai hili linajadiliwa kwa mifano Dhahiri ya sentensi za Kiswahili:

Kama mzungumzaji atakiuka masharti ukweli wapo wasikilizaji wanaweza kuchopeza au kadhaniliza maana zingine katika kauli zake na akajikuta yupo hatiani. Mtu akisema kwa mfano, Majangili ni viongozi waliochaguliwa na wananchi, msikilizaji anaweza kuchopeza kuwa kumbe hata mbunge wake ni jangili jambo ambalo linaweza kumletea matatizo mzungumzaji na pengine kujikuta katika vyombo vya sheria.

Watu wanaposemezana huzingatia kanuni za masharti ukweli na uchopezi. Watu huzingatia kwamba kauli wanazosema haziwezi kuzua maana nyingine ambayo si ya kweli. Hivyo basi watu wanaposemezana, wanaelekea kuzingatia kanuni hizi ambazo wamejiwekea wenyewe katika jamii. Kwa mfano, mtu anaposema, “John amemuoa Neema.” Anazingatia taarifa yake ieleweke kuwa John ameoa na wala hajaolewa na Neema.

Uchopezi hutokana na ukweli wa msemaji. Uchopezi hutokana na mfuatano wa kimantiki baina ya sentensi moja na nyingine. Kwa mfano,

(a) Mfalme wa kusadikika ameuawa na mamluki.

(b) Mfalme wa kusadikika amefariki.

Katika mfano huo, hatuwezi kupata ukweli wa (b) kama (a) ingekuwa uongo.

Masharti ukweli yanaamrisha kwamba kama hujui ukweli wa jambo fulani usiliseme ili kuepusha uchopezi wa maana isiyohusika au kuharibu habari nzima. Hivyo basi huwezi kupata dhana ya uchopezi bila kuwa na ukweli vinginevyo utakuwa hatiani kwa kusambaza uzushi. Kwa mfano, kama huna uhakika juu ya taarifa za kifo za kiongozi fulani, ni vyema kukaa kimya ili kuepuka kusababisha matatizo makubwa zaidi.

Huwezi kupata ukweli wa sentensi ya pili bila kuwa na ukweli wa sentensi ya kwanza. Kwa mfano:

(a) Keto alimuua Nyati.

(b) Nyati alikufa.

Katika mfano huo, tunaweza kusema kwamba, maana ya sentensi (b) ni sehemu ya sentensi (a) ni kweli basi na sentensi (b) ni kweli pia kama moja si kweli na ya pili si kweli pia.

Uzingatiaji wa ukweli: kama sentensi A inaendana na sentensi B, na sentensi A ni kweli, hivyo sentensi B nayo ni kweli bila shaka. Hii ina maana kwamba, ukweli wa sentensi A unapatikana hata tukienda katika sentensi B. haya yamepatikana kwa kuzingatia maana.

Kufanana kwingine kupo katika kubaini uongo. Kama sentensi A inachopeza sentensi B, na sentensi B ni uongo, hivyo basi hata sentensi A ni uongo. Hii ina maana kwamba, uongo wa sentensi B unamaanisha kwamba sentensi A siyo kweli.

Vilevile, uhusiano mwingine wa dhana hizi ni katika kutegemeana. Kama sentensi A inachopeza sentensi B na sentensi B inachopeza sentensi A basi sentensi hizi zinahusiana na zinategemeana na tofauti ndogo inaweza kuzitenganisha na kuharibu maana.

Kwa kuhitimisha, uhusiano wa masharti ukweli unatusaidia kuelewa ukweli na uongo katika sentensi. Pia husaidia kuona na kubaini mtiririko mzuri wa mawazo katika mazungumzo. Ili kuwepo na uchopezi ni lazima kuwepo na sentensi mbili au zaidi zenye uhusiano au mahusiano ya kimantiki na ambapo ukweli wa sentensi au usemi wa pili hubainishwa na ukweli wa sentensi au usemi wa kwanza. Vivyo hivyo, usikweli wa sentensi ya pili hujibainisha katika sentensi ya kwanza.

Marejeleo

Leech, G. (1981) Semantics. London: Penguin.

Makoba, D. (2018) Semantiki na Pragmatiki ya Kiswahili | KI 311: Inapatikana katika https://www.mwalimumakoba.co.tz/2018/04/semantiki- na- pragmatiki-ya-kiswahili- ki.html. Ilisomwa tarehe 03 Mei 2023.

Resani, M. (2014) Semantiki na Pragmatiki ya Kiswahili. Dar es Salaam: Karljamer Print Technology.

TUKI. (2010) Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Nairobi: Oxford University Press.

Unahitaji Kufanyiwa Swali Lako? Wasiliana na Mwalimu kwa Kugusa Hapa.

Popular posts from this blog

Uhakiki wa Tamthiliya ya Kilio Chetu

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Risala | Kiswahili Kidato Cha Nne