Uchopezi na Udhanilizi wa Kisemantiki Katika Kiswahili

Mwanamume mwenye rasta anafikiri jambo

Swali

Fafanua kwa kutumia mifano madhubuti kutoka katika lugha ya kiswahili uchopezi na udhanilizi wa kisemantiki.

Jibu

Uchopezi na udhanilizi ni dhana zinazopatikana katika Semantiki. Dhana hizi zinawakilisha mahusiano ya ukweli yanayochunguzwa na semantiki. Dhana hizi zinafafanuliwa kwa kutumia mifano kutoka katika lugha ya Kiswahili.

Kwa kuanza na dhana ya uchopezi inafafanuliwa kwa kutumia mifano madhubuti kutoka katika lugha ya Kiswahili.

Uchopezi ni uhusiano wa sentensi mbili ambapo ukweli wa sentensi ya pili hudhihirisha ukweli wa sentensi ya kwanza (Crystal, 1998).

Kwa mfano: Athuman amemuoa Aisha.

Aisha ameolewa.

Sentensi ya pili, inadhihirisha ukweli wa sentensi ya kwanza na hivyo kukubaliana na maana iliyotolewa na mtaalamu Crystal.

Kwa mujibu wa Lyons (1977), uchopezi ni uhusiano uliopo kati ya P na O ambapo P na Q zinasimama kama vihusishi ambapo ukweli wa Q hujidhihirisha kutokana na ukweli wa P. maana hii ya mtaalamu Lyons japo si rahisi kueleweka, lakini inarejea kuwa, katika uchopezi sentensi ya pili hudhihirisha ukweli wa sentensi ya kwanza.

Matinde (2012) anadai kuwa uchopezi ni dhana inayotumiwa na wanaisimu amali kufafanua uhusiano wa sentensi mbili au zaidi na hatimaye hufasiri maana za sentensi hizo kutokana na mtiririko wa mantiki.

Kwa ujumla, uchopezi ni dhana itumiwayo na wanaisimu maana katika kutoa ufafanuzi juu ya uhusiano wa sentensi mbili au zaidi. Pia hufasiri maana za sentensi hizo kutokana na mtiririko wa mantiki baina ya sentensi moja na nyingine.

Mahusiano ya uchopezi baina ya sentensi ni ya kimaana. Hudaiwa kuwepo pasipo kuzihusisha sentensi hizo na muktadha.

Katika dhana hii, maana ya sentensi moja huweza kuhusishwa na sentensi nyingine pasipo kurejelea muktadha.

Mifano:

A. Mwanamuziki ameuawa na majambazi.

B. Mwanamuziki amefariki.

A. Daktari amemponya mgonjwa.

B. Mgonjwa amepona.

Njia ya kawida ya kueleza uhusiano baina ya a na b hapo juu ni kwamba, mtu huweza kuchukulia kuwa a ni kweli kutokana na b yaani kama a ni kweli, basi hata b ni kweli.

Kwa mujibu wa sentensi a na b, tunaweza kusema kuwa, kwa sababu mwanamuziki ameuawa, basi bila shaka amefariki. Vivyo hivyo kwa sentensi ya pili.

Pia, zifuatazo ni aina za uchopezi:

Uchopezi wa kileksika. Huu ni uchopezi ambao lesksimu au maneno mawili au zaidi hurejea maana moja au maana iliyokaribiana.

Mifano:

A. viongozi wa Tanzania wanakula rushwa

B. Mlungura ni halali kwa viongozi wa Tanzania.

Kwa mtazamo wa uchopezi, a na b, zinachopezana.

Aina nyingine ya uchopezi ni uchopezi wa kimuundo. Hii ni aina ya uchopezi ambao hudhihirishwa na miundo ya sentensi mbili ambazo huwa na maana moja. Hii hujidhihirisha katika sentensi zenye kauli tendi na kauli tendwa.

Mifano:

A. Walimu wa shule ya msingi Kitero wamefaulisha wanafunzi wao.

B. Wanafunzi wa shule ya msingi kitero wamefaulu.

Kwa upande mwingine, udhanilizi unafafanuliwa kama ifuatavyo:

Udhanilizi ni dhana ya isimu amali ambayo hutokana na msemaji kudhani kuwa msikilizaji waka ana ufahamu au taarifa ya awali kuhusu kile anachokisema (Matinde, 2012).

Kwa mfano: Zengakona amefariki. Katika usemi huu msemaji anadhani kuwa msikilizaji ana ufahamu wa awali kuhusu mtu aitwaye Zengakona. Pia, Zengakona alikuwa mgonjwa.

Hudson (2004) anadai kuwa udhanilizi ni kile kinachodhaniwa kuwa kina ukweli katika sentensi kutokana na maelezo mengine.

Kwa mfano: mtoto amepiga chafya tena.

Usemi huu una udhanilizo kuwa mtoto alipiga chafya kabla hajapiga kwa mara nyingine.

Kwa ujumla, udhanilizi ni kipengele kilicho katikati ya mpaka wa semantiki na pragmatiki. Kimejadiliwa sana na wanasemantiki pamoja na wana pragmatiki. Hivyo ni kitengo ambacho wataalamu wengi wanakiweka katika kitengo cha pragmatiki.

Mifano ya udhanilizi:

A. Umenunua gari jingine?

B. Ulikuwa na gari kabla ya hili?

A. Nyumba ya heri ni nzuri.

B. Heri ana nyumba.

Kwa hiyo sentensi a inadhaniliza sentensi b. Jambo linalodhanilizwa huchukuliwa kuwa linafahamiwa na msemaji pamoja na msikilizaji. Katika sentensi a, kuidhaniliza sentensi b, ina maanisha kwamba, ukweli wa sentensi a lazima utokane na ukweli wa sentensi b.

Kwa mujibu wa Matinde (2012), udhanilizo una sifa kuu tatu ambazo ni:

Sifa ya kwanza, udhanilizi haubadiliki hata pale sentensi msingi inapokanushwa. Kwa mfano, sharifa ameingia darasani. Sentensi hii ikikanushwa inakuwa Sharifa hajaingia darasani. Sentensi hii inabaki na udhanilizo uleule kuwa kuna mwanafunzi anaitwa Sharifa.

Sifa ya pili, udhanilizi haubadiliki hata pale sentensi msingi inapobadilishwa na kuwa sentensi ulizi. Kwa kutumia mfano wa sentensi ya kwanza, sentensi itakuwa, Sharifa ameingia darasani? Sentensi hii bado ina udhanilizo uleule kuwa Sharifa ni mwanafunzi.

Sifa ya tatu, udhanilizi unaweza kubadilika kutokana na uchopekaji, udondoshwaji na upangaji wa vipashio katika sentensi ya msingi. Kwa mfano, Sharifa ameingia darasani kufundisha kozi ya semantiki na pragmatiki. Sentensi hii ina kipashio kipya ambacho ni, kufundisha kozi ya semantiki na pragmatiki. Kipashio hiki kimebadilisha muundo wa sentensi na bila shaka udhanilizi wake na kuwa Sharifa ni mwalimu wa kozi ya semantiki na pragmatiki.

Pia, zifuatazo ni aina za udhanilizi:

Udhanilizi wa ukweli. Udhanilizi huu unatokana na matumizi ya maneno ambayo hubainisha ukweli wa sentensi au tamko. Udhanilizi huu hubainishwa na matumizi ya vitenzi kama vile: juta, gundua, tambua na furahi. Udhanilizi huu hujitokeza katika mfano ufuatao:

Najuta kuolewa na Juma. Tunapata udhanilizi kuwa, mwongeaji ni mwanamke, ameolewa, Juma ni mumewe.

Aina nyingine ya udhanilizi ni udhanilizi wa kileksika. Huu ni udhanilizi unaotokana na muundo wa sentensi au kauli ya kwanza kusaidia kubashiri maana japo haikusema bayana. Udhanilizi huu hutegemea matumizi ya baadhi ya maneno na virai ambavyo ni mahsusi.

Kwa mfano: “Jitihada zake zimemwezesha kung’oa kisiki kile.” Ufasiri wake ni kuwa amefaulu kung’oa kisiki.

Pia, udhanilizi wa kimuundo. Katika udhanilizi huu, baadhi ya miundo ya sentensi au sehemu ya sentensi husika huchukuliwa kuwa na ukweli lakini sehemu ya pili huuliza swali. Msemaji anaweza kutumia miundo hii kuibua ukweli wa taarifa zinazotokana na sentensi.

Kwa mfano: zainabu amepigwa na nani? Hapa tunapata udhanilizi kuwa, kuna mtu anaitwa Zainabu, amepigwa lakini aliyempiga hajulikani.

Udhanilizi kinzani ni aina nyingine ya udhanilizi. Huu ni udhanilizi wa kimuundo ambao hubainisha ukinzani wa uongo na ukweli wa taarifa zilizomo kwenye usemi. Udhanilizi huu haubainishi uongo tu bali pia kinyume cha matarajio. Ukinzani hutokana na vishazi viwili vinavyokinzana katika usemi.

Kwa mfano: Ungelikuwa mwalimu ungelifundisha vizuri. Maana yake ni kwamba, huyo siyo mwalimu na hajui kufundisha vizuri).

Aina ya mwisho ya udhanilizi ni udhanilizi usokweli. Huu ni udhanilizi ambao hauna ukweli ndani yake.

Kwa mfano: Juma ameota amefunda ndoa. Maana yake ni kwamba, ndoa haijafungwa, lakini Juma alilala usingizi.

Kwa ujumla, udhanilizo na uchopezo ni dhana mbili zinazotofautiana kimtazamo na kimuundo katika sentensi. Uchopezi hutazama maana katika sentensi. Hivyo basi, kwa kifupi, udhanilizo huja na dhana na fikra sahihi kwa msemaji au msikilizaji kutokana na maelezo. Na uchopezi ni tukio la uhusiano wa sentensi au maana kutegemea mtiririko wa mantiki. Ili kuwepo na uchopezi ni lazima kuwa na sentensi mbili au zaidi zenye mahusiano ya kimantiki, ambapo ukweli wa sentensi au usemi wa kwanza. Vivyo hivyo usikweli wa sentensi ya pili hujibainisha katika sentensi ya kwanza.

Marejeleo

Leech, G. (1981) Semantics. London: Penguin.

Makoba, D. (2018) Semantiki na Pragmatiki ya Kiswahili | KI 311: Inapatikana katika         https://www.mwalimumakoba.co.tz/2018/04/semantiki-na-        pragmatiki-ya-kiswahili-    ki.html. Ilisomwa tarehe 25 Juni 2022.

Resani, M. (2014) Semantiki na Pragmatiki ya Kiswahili. Dar es Salaam:      Karljamer Print Technology.

TUKI. (2010) Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Nairobi: Oxford University Press.

Unahitaji Kufanyiwa Swali Lako? Wasiliana na Mwalimu kwa Kugusa Hapa.

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024

Uhakiki wa Riwaya ya Watoto wa Maman’tilie