Mwanamke Uliyekula Pesa Zangu Nakutafuta | Sehemu ya Tatu

Mtu gizani

Nilinyanyuka huku nazungumza, “Mheshimiwa, huyo dada hana funguo ya kabati la fedha, mimi ni mfanyakazi mwenzake nakuja kukupatieni.”

Wakati nazungumza nilikuwa nasogea kuelekea walikosimama, nilitembea mpaka karibu kabisa na yule jamaa mwenye silaha, nikiwa nimeukunja mkono wa kushoto, huku nikichezesha mkono wa kulia wakati ninapozungumza, nilimzubaisha yule jamaa mwenye silaha, nikampiga ngumi kali ya kidevu kwa mkono wangu wa kulia na kabla hajadondoka chini, nikawahi kuikamata silaha yake. Sasa ikawa yangu, yule mwenzake alibabaika, nikamwamuru akae chini haraka.

Jamaa wale walifungwa kamba mpaka walipokuja askari kuwakamata. Hakuna aliyeweza kuamini kuwa, mahali pale palitoka kufanyika tukio la uvamizi wa silaha. Mziki uliendelea kama kawaida na watu walicheza kwa nguvu zaidi kuliko mwanzo. Hata hivyo, watu walianza kuniangalia sana, wengine wakinishukuru na kuninunulia vinywaji vya bure kwa ushujaa ambao nilionyesha.

Burudani iliendelea kutoka kwa ma Dj ambao nilitambua walikuwa wawili na walifanya kubadilishana, muda huu alisimama mwingine, mwembamba, kavaa kiatu cheusi kirefu na amenyoa kiduku. Nikasikia kionjo, “Auto waharibiee.” Nikabaini bila ya mashaka yoyote kuwa, pale palikuwa na Dj Auto Run.

Ulipigwa wimbo wa Amapiano, nikashangaa kuona Asi akiwa na filimbi mdomoni, alipuliza filimbi yake kufuatisha filimbi ya kwenye wimbo, mbali na kupiga filimbi, alicheza kwa maringo hata akawa kama kishada kilichokata kamba.

Hata hivyo, burudani ilielekea ukingoni pale Asi alipoomba arejee nyumbani kwani mida ile ingekuwa rahisi kwa Babuu kuamka. Niliagana naye, nami sikukaa sana, nikaondoka kuelekea makazi yangu.

Mengi hayajulikani kuhusu mimi na sitaki kuyasema. Lakini katika Jiji la Dar es Salaam kwa sababu sikwenda kukaa kwa muda mrefu, basi niliishi katika Nyumba ya Wageni iliyoitwa London Lodge. Nyumba hii ya kulala wageni ipo Kinondoni, pembezoni kabisa mwa mahakama ya Kinondoni, mahakama nzuri ya kisasa, na ungetazama mbele ya geti la London, ungeiona shule ya Sekondari Kambangwa.

Nilipewa chumba ambacho sikumbuki namba yake, ila nakumbuka kilikuwa chumba kilichokaribiana sana na mapokezi. Vyumba vingine vilivyokuwa mbele, vilipachikwa majina ya miji, japo sikumbuki vizuri, lakini nadhani kipo chumba ambacho kiliitwa Spain.

Ndani ya chumba changu palikuwa na kitanda cha chuma kilichokuwa na godoro laini, sofa la mtu mmoja jeusi na choo pamoja na bafu. Huduma zote nilizotaka nilizipata, na niliwaomba wenyeji wangu kwa kuwa nilikuwa mkazi wa siku nyingi, basi chumba changu kiheshimiwe, na asiingie mtu yeyote kusafisha bali shughuli zote ningezifanya mimi, na niliwaomba, funguo nitembee nayo muda wote ninapotoka. Walinielewa, maisha yangu yakawa mazuri mno. Hata hivyo palikuwa na kero moja ambayo niliivumilia, dari lilionekana kuoza na vumbi lake lilielekea kunisababishia mafua.

Maisha yangu katika nyumba hii ya wageni, kwa muda wa mwezi mmoja tu niliokuwa nimekaa, nilishudia vioja vingi, lakini kikubwa zaidi ya vyote, ilikuwa ni fumanizi. Jamaa mmoja alimfumania mke wake, lakini huyu bwana aliyemfumania naye ni jamaa aliyekuwa akimdai. Basi alifoka sana na mwisho alisikika akisema, “Mayombi, deni lako tumemalizana, hunidai tena!”

Soma: Mwanamke Uliyekula Pesa Zangu Nakutafuta |Sehemu ya Nne

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Uhakiki wa Riwaya ya Watoto wa Maman’tilie