Mwanamke Uliyekula Pesa Zangu Nakutafuta | Sehemu ya Nne

Mwanamume gizani
Mara kwa mara niliendelea kupita alikoishi Asi, kama kawaida yake, aliomba pesa ndogo, nikampa kisha nikaandika katika kikaratasi changu. Sasa jumla ilifika Shilingi elfu kumi na tisa za Kitanzania.

Katika kumbukumbu nzuri, nakumbuka kwenda Coco Beach na Asi, huko tulikula mihogo ya kuchoma, tukaogelea na kuzungumza mengi.

“Bwana Mako,” Asi aliniita.

“Naam,” niliitika.

“Uliwezaje kuwadhibiti wale wezi wa siku ile, tena wakiwa na silaha?”

“Unajua…” nilisema nikitafakari namna ya kubadili mazungumzo ili asinichimbe sana. “Katika Jiji hili la Dar es Salaam, kuna watu wanajiona wao ni wababe mno na huwaambii chochote. Achana na huo mkasa, nakumbuka siku moja nikitoka katika matembezi yangu, jamaa mmoja alisimama katikati ya njia na kuniamrisha nitoe pesa.

“Jamaa yule wala hakuwa na silaha yoyote na alikuwa peke yake. Nilimuuliza, Unajiamini nini kutaka kuniibia mimi tena ukiwa peke yako? Jamaa akawa mkali na akaanza kusogea nilipokuwa. Alipofika hatua tatu ili aweze kunifikia, nilimpiga ‘jebu’ moja iliyofuatiwa na ‘right’ akadondoka chini huku analia, Umenipiga na jiwe, umenipiga na jiwe! Nilimsogelea alipodondoka na kumuonyesha mikono yangu huku nikisema, “Siyo jiwe ni ngumi!”

Asi alicheka sana, sikutaraji kama simulizi ya mkasa wa mapigano inaweza kumchekesha mtu. Msichana alicheka, nikaona kabisa mbavu zinamuuma na almanusura adondoke na kiti kama isingekuwa kuwahi kukikamata.

Ni katika siku hiyo niligundua kuwa Asi alikuwa mgeni katika Jiji la Dar es Salaam, binti huyu alitoka Tanga na alikuwa na jambo fulani na Babuu. Hata hivyo, hakunieleza Babuu ni nani na alifuata nini hapa mjini.

Tulikaa mpaka saa 12 jioni, tukaanza kurudi nyumbani kwa mwendo wa kutembea polepole. Mimi kushoto, Asi kulia.

Tulichukua njia za ndanindani tukaibukia katika kanisa la Mtakatifu Petro. Ni katika kanisa hili, Marehemu Rais John Pombe Magufuli, alizungumza kwa mara ya mwisho kabla hajafikwa na mauti. Nakumbuka katika hotuba yake alisema hajakataza watu kuvaa barakoa ili kujikinga na Ugonjwa wa UVIKO-19, wengine wakiuita Korona. Ila alisisitiza kwamba, barakoa zingine ni mbaya na tuwe makini.

Hakuishia hapo, alimpongeza paroko kwa kitendo chake cha kutovaa barakoa, na alishangazwa na Masista wawili waliokuwa wamevaa barakoa. Nakumbuka alisema, “Anayeilinda nafsi yake, ataipoteza.”

Yeye hakuvaa barakoa, na hakukataza watu kuvaa barakoa, ila hakuziamini barakoa kutoka mataifa ya nje. Kuna mahali aliwapongeza sana watu waliokuwa wamevaa barakoa za kushona wao wenyewe. Alisikika akisema, “Vita ya uchumi ni mbaya.”

Alikuwa mzalendo kwelikweli aliyetamani taifa lake lipende vyake. Ndiyo maana hata katika kupambana na gonjwa la Korona, alihamasisha watu wajifukize.

Niliendelea kuuchapa mwendo na Asi, sasa tulivuka barabara ya Ali Hassan Mwinyi, kushoto tukauona ubalozi wa Ufaransa.

“Unaona jengo lile?” nilimuuliza Asi aliyekuwa kanishika mkono.

“Naliona,” msichana alijibu.

“Pale ndiyo gaidi Hamza aliwasumbua sana askari. Kile kijengo kidogo cha pembeni kile cha kukaa mlinzi, alijificha humo na kuanza kuwachachafya askari na ‘SMG’ mbili alizopora kwa askari haohao.”

“Walikufa askari wengi eeeh?”

“Sina uhakika, ila nakadiria walikufa watano.”

“Kwa nini Hamza aliamua kufanya hivyo?”

“Baada ya tukio, baadhi ya watu walisema alidhurumiwa madini yake na askari hivyo alikuwa katika harakati za kulipa kisasi. Hata hivyo, uchunguzi ulipotoka, vyombo vya sheria vilisema Hamza alikuwa kijana wa hovyo tu na hakudhurumiwa chochote ila alikuwa mtu wa hovyo, gaidi. Vyombo vya sheria vikasema tena na kuwaomba sana wazazi wasizae watoto wa hovyo kama Hamza.”

“Utajuaje kama umezaa mtoto wa hovyo?” aliuliza Asi akinitazama, mbele akapita muuza karanga, nikamsimamisha na kununua za shilingi mia tano zikiwa zimewekwa katika kikaratasi, chache nikamimina katika kiganja cha Asi, nyingi nikabaki nazo. Usinione mchoyo, baadae nilimuongeza.

“Mtoto wa hovyo…” nilikumbusha nikitafuna karanga. “Ni ngumu kufahamu, lakini simlaumu aliyesema hivyo pengine zilikuwa ni hasira za kupoteza askari wake. Laiti kama ningekuwepo siku hiyo, ningehesabu risasi anazorusha Hamza, zingefika risasi sitini, basi ningebaini bunduki zake mbili zimekwisha risasi, na hapo ndipo ningejitokeza mbele yake na kumkamata kama kuku.”

Asi alinitazama, akatabasamu, halafu akajisogeza karibu yangu zaidi, tukaendelea kutembea, tukitafuna na kuzungumza.

Mwisho tulivuka Barabara ya Kawawa. Tukakiona kituo cha Mwendokasi cha Morocco. Mradi wa mwendo kasi ulilenga kupunguza kero ya usafiri, lakini mimi sikuona upunguzaji wa kero hiyo. Niliishia kusikitika tu kuona jinsi abiria wa Mbezi walivyojazana kwenye huo mwendokasi, wengine walikosa pa kukanyaga wakiwa humohumo kwenye mwendokasi. Mtu pekee aliyekuwa amekaa kwa huru mwendokasini humo, alikuwa ni dereva. Akina siye waliibiana, wakauzidisha umasikini wao maradufu. Halafu kauli chafu za madereva, ati “We mzee geuka kule shika bomba!” Kauli gani hizi? Kauli za kishwaini ushenzi.

Tuliukanyaga mdogomdogo nikiwa na kiumbe mdogo wa kike. Tena, nilimsindikiza mpaka mitaa ya kwao na tuliagana, mimi nikarudi katika makazi yangu ya muda. London Lodge.

Soma: Mwanamke Uliyekula Pesa Zangu Nakutafuta |Sehemu ya Tano


Popular posts from this blog

Uhakiki wa Tamthiliya ya Kilio Chetu

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Risala | Kiswahili Kidato Cha Nne