Mfalme Anataka Kuniua | Sehemu ya 10
Mako
alitembea taratibu mpaka aliposimama askari. Umbali wa askari mmoja na mwingine
ulikuwa hatua hamsini na tano. Alipomfikia, alimsabahi.
“Hujambo
Ai.”
“Sijambo
Mako, pole,” alijibu askari, kisha akaendelea, “umefuata nini hapa, huruhusiwi
kuwa eneo hili, nikuchome singe?”
“Ni
bora kufa kwa kuchomwa singe kuliko kunyongwa bila hatia. Sikiliza Ai, nipo
hapa kwa sababu nataka unisaidie. Nisaidie kuchelewa kupiga filimbi.”
“Mako,
unataka nikusaidie kutoroka?”
“Kutoroka
nitatoroka mwenyewe, nisaidie kuchelewa kupiga filimbi. Usipige filimbi mpaka
nitakapozama mtoni.”
Ai
ni binti yatima, wazazi wake walifariki kwa ajali ya mtumbwi alipokuwa na umri
wa miaka kumi na nne. Hakuzaliwa mjini Kanakantale, alizaliwa kijijini
Kanakado, hata hivyo baada ya kupoteza wazazi, alichukuliwa na dada yake mpaka
hapo Kanakantale.
Alipofika
Kanakantale, maisha ya dada yake yalikuwa magumu tena ya ufukara wa kutisha.
Yeye na dada yake walifanya kazi ya kuuza matunda kandokando ya barabara za
mji.
Siku
moja Mako akipita mjini, alimuona binti mrefu mweupe akiuza matunda. Alimfuata
na kumuuliza mambo mengi. Mwisho alibaini mtoto yule alipenda sana elimu ila
hakupata nafasi. Basi Mako akachukua jukumu la kumsomesha Ai mpaka leo hii ni
askari katika gereza la Kanakantale.
Basi
Mako alimtazama Ai usoni, akabaini Ai asingeweza kumsaliti, akakimbia kwa kasi
mpaka ulipo uzio wa gereza, kisha akapanda kwa nguvu na kuruka upande wa pili.
Baada ya hapo akakimbia kwa kasi kama roketi, mpaka mtoni, kikasikika kishindo
cha mwanaume, ‘chubwii’.
Kuona
hivyo, Ai akapiga filimbi, ‘pyeeeeeee!’
“Mako
ametorokaaaaaah!” alitamka kwa sauti askari mwanamke. Askari wengi, waume kwa
wake wakasogea tayari kuanza msako.
Msako
wa mfungwa aliyetoroka ulianza. Ai alikuwa na wakuu wake akijaribu kueleza
ilivyokuwa. Alieleza katika hali ya kushangaza, mfungwa huyo alimfuata
akimuomba msaada wa kupatiwa huduma ya matibabu kwani alidai anaumwa. Lakini
ghafla mfungwa alikimbia, akaruka ukuta na kuelekea mtoni.
Vikosi
vya askari wakiongozwa na mbwa wakali, viliingia msituni. Wengine walipanda
mitumbwi na kuelea mtoni wakimsaka Mako.
Jioni
hiyohiyo katika nchi ya Kanakantale, ilitangazwa yeyote atakayesaidia kupatikana
kwake, angezawadia ng’ombe elfu moja. Zoezi la kumtafuta likawa siyo la askari
pekee, likawa la watu wote. Kila mmoja akitamani kuukimbia umasikini kwa kutoa
taarifa za mtu huyo aliyetoroka jela.
Mashujaa
wa vita wakaingia kila eneo kumsaka. Mako alitafutwa na jamii nzima!
Mako
aliibuka katika maji, akatembea kwa tahadhari mpaka katika kichaka akajificha.
Alikaa hapo mpaka giza nene lilipotanda. Alianza kutembea kuelekea alikokujua
yeye. Alitembea kandokando ya barabara lakini palipokuwa na miti ili
asionekane. Mako alijua kuficha umbo!
Wakati
akiendelea kutembea tena aliyeloa chapachapa, aliona picha kubwa katika mti
mmojawapo, ilikuwa picha yake na iliandikwa maneno, YEYOTE ATAKAYESAIDIA
KUKAMATWA KWA MAKO, ATAZAWADIWA NG’OMBE ELFU MOJA. Haraka alilichukua tangazo
hilo na kulichana. Hata hivyo, asingeweza kuyachana mabango yote ambayo mpaka
muda huo yalienea nchi nzima.
Ghafla
mbele yake aliona kundi kubwa la askari wakija na mienge ya moto. Akadondoka
chini kama furushi kisha akatambaa mithili ya nyoka mpaka katika mtalo mkubwa.
Askari waliendelea kuja wakiwa na mbwa wao. Kadri walivyozidi kusogea
alipojificha Mako, ndivyo mbwa wale walivyozidi kubweka kwa sauti. “Woooh!
Wooooh! Woooh!”
Huu ni Mwisho wa Sehemu ya bure ya Riwaya hii, Isome Riwaya yote ili kufahamu kilichotokea kwa Tsh. 2,000/= tu. Gusa Hapa Kununua Riwaya yote.