Mfalme Anataka Kuniua | Sehemu ya Nane

 

Taji la Mfalme

Siku mpya ilifika, Bwana Mako na watoto wa Jitu walikuwa wa kwanza kuamka, na tazama akishirikiana na watoto wa Jitu, alikuwa ametengeneza meza kubwa ambayo ilikuwa na kimo sawa na tumbo la majitu. Baada ya kukamilika kwa meza, akashirikiana na watoto kuipeleka nyuma ya nyumba ambako kulikuwa na ukumbi mkubwa, kisha akawaamuru watoto wakamuite baba yao.

“Niliahidi kukufanya tajiri.” alisema Bwana Mako baada ya Jitu kufika.

“Na hii meza ndiyo utajiri wenyewe?” Jitu liliuliza.

“Ndiyo, meza hii ndiyo utajiri wenyewe, lakini haiwezi kuwa utajiri bila mimi niliyekaa juu yake.”

“Sikuelewi unanichanganya!” lililalamika Jitu.

“Sikiliza rafiki mwema,” alisisitiza Bwana Mako, “watume wanao waende mjini, wawatangazie watu maneno haya: Nyumbani kwa baba yetu, kuna maonyesho hayajawahi kutokea. Mtu mkubwa kutoka sayari iitwayo Dunia, amemtembelea baba yetu, ajabu ni kwamba, pamoja na ukubwa wake huko Duniani, huku anaonekana kiumbe mdogo. Ama kweli kila mkubwa na mkubwa wake. Njoo ujionee kiumbe huyu wa ajabu kwa kiingilio cha pesa mbili tu.”

Jitu lilimwelewa Bwana Mako na liliona ubora wa wazo hilo hata likastaajabu sana uwezo wa akili ya mwanadamu kutoka Duniani.

Basi watoto wa jitu walitembea mjini wakitangaza, “Nyumbani kwa baba yetu, kuna maonyesho hayajawahi kutokea. Mtu mkubwa kutoka sayari iitwayo Dunia, amemtembelea baba yetu, ajabu ni kwamba, pamoja na ukubwa wake huko Duniani, huku anaonekana kiumbe mdogo. Ama kweli kila mkubwa na mkubwa wake. Njoo ujionee kiumbe huyu wa ajabu kwa kiingilio cha pesa mbili tu.”

Kufumba na kufumbua, majitu mengi yalijaa nyumbani kwa Jitu, yote yalitaka kumuona kiumbe kutoka duniani na yalilipa kiingilio cha pesa mbili. Yalipelekwa mpaka katika meza aliyosimama Bwana Mako. Kwa sababu yalikuwa mengi, basi yaligawanywa katika makundi ili yaweze kumuona kwa zamu.

Bwana Mako alifanya michezo ya kufurahisha, kwanza alianza kwa kupiga danadana mpira, majitu yakashangaa. Kisha akacheza mziki, halafu akaruka sarakasi, sarakasi zenyewe hazikuwa sarakasi bali zilikuwa zile za upande upande, ni ushamba tu wa majitu kushangaa sarakasi hizo. Ama naweza kusema, burudani haswaa ilikuwa ni ule udogo wa Bwana Mako katika macho ya majitu. Alitaka kufanya mchezo wa ngumi, lakini alihofia labda majitu yanaweza kuiga na kusababisha vita vya mikono mahali pale, basi badala ya ngumi, akaweka vichekesho.

“Ujinga wa ndoto ni huu, utaota umeokota pesa ukiamka hakuna. Utaota umeokota dhahabu ukiamka kitandani patupu. Ila ukiota umekojoa, unakuta imooo!”

“Ha! Ha! Ha!” majitu yalicheka yakishika mbavu.

Kuna Jitu moja lilisikika likimwambia mkewe, “pesa yangu imekwenda kihalali, pesa mbili, vicheko lukuki.”

Hayo ndiyo yakawa maisha ya Bwana Mako na Jitu. Kazi hiyo iliwapatia pesa elfu mbili kila siku.  Pesa hizo ni sawa na shilingi milioni nne za Kitanzania. Jitu likawa tajiri kama lilivyoahidiwa. Halikulala tena njaa, maisha yakabadilika.

Bwana Mako hakusahau kuhusu kurejea nyumbani. Ila, alitaka ashirikiane kwanza na majitu yale ili aweze kuyafahamu zaidi. Pia, aliendelea kuikarabati ndege yake, safari hii, hakusahau kuweka kigingi cha nne, pia alifurahishwa na miti ya kule, ilikuwa migumu kama chuma.

Aliendelea kufanya maonyesho na kushangiliwa na majitu kila siku mpaka taarifa zilipomfikia mfalme wa majitu. Ujumbe ukafika haraka, kiumbe kutoka Duniani, anatakiwa barazani kwa mfalme kabla tonge la kwanza la chakula cha mchana halijaguswa…”

Soma: Mfalme Anataka Kuniua | Sehemu ya Tisa

Popular posts from this blog

Uhakiki wa Tamthiliya ya Kilio Chetu

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Risala | Kiswahili Kidato Cha Nne