Mfalme Anataka Kuniua | Sehemu ya Tisa

 

Taji la mfalme

Wakati dada anasimulia, Mfalme aligonga katika chumba kile na kumtaka Malkia aongozane naye haraka. Basi Malkia akasimama asiyetaka huku akiuliza, “Ikawaje sasa, niambie haraka niende…”

“Mako alienda Kwa mfalme…” alijibu dada akiongea haraka, “alipofika kwa mfalme wa majitu akafanya maonyesho kadhaa yaliyokusanya majitu mengi ajabu. Lile jitu lililompokea nalo likapewa cheo nyumbani kwa mfalme hata likasahau habari za umasikini wa awali. Baada ya kuwa amekaa kwa muda wa miaka miwili, Mako akamuomba mfalme huyo amsaidie kurejea Duniani kwa lengo la kuwatoa hofu ndugu na jamaa zake ambao wanaweza kudhani kuwa amekufa. Basi Mfalme wa Majitu alimsaidia Mako kurejea na tangu arejee hajarudi tena huko japo njia anaifahamu.

Alimaliza dada kusimulia. Wakati huo mfalme alikwisha fungua mlango na kumkamata mkono Malkia aliyekuwa amesimama kisha akatembea naye haraka kuelekea alikojua yeye.

***

Ilikuwa mchana siku ya pili Mako akiwa gerezani. Wenzake watatu hawakuwa na hofu, pengine wao walibakiwa na mvua nyingi zaidi. Katika hali ya kusikitisha mchana huo, wingu kubwa lilitanda na kuashiria kuwa mvua ingenyesha muda wowote. Maana yake ni kwamba, Mako angenyongwa siku inayofuata.

Wingu lilikuwa jeusi hata mchana ule ukabadilika na kuwa kama usiku. Mapigo ya moyo ya Mako yalibadilika na kudunda kwa kasi. Japo alikuwa shujaa katika jamii yake, alitawaliwa na hofu. Hofu ya kuuawa.

Upepo mkali ulivuma, wingu lile likasogezwa polepole kuelekea mashariki. Likasogea tena na tena mpaka lilipoondoka kabisa katika mji wa Kanakantale. Jua likaonekana tena. Mako akapumua kwa nguvu asiyeamini kilichotokea.

Hali ile ilimuogopesha Mako, aliona kama angezubaa basi angeuawa ilhali hakuwa na hatia. Sasa akapanga mpango wa kutoroka, aliona njia pekee ya kuepuka uonevu uliotarajiwa kutendwa dhidi yake ilikuwa ni kutoroka gerezani. Alipiga hesabu zikakamilika. Akasubiri muda wa kufunguliwa vyumbani kwenda kufanya usafi ufike.

Saa kumi jioni, wafungwa walitolewa katika vyumba vyao ili wafanye usafi wa mwili na mazingira. Zoezi hili lilitumia saa mbili pekee hivyo saa kumi na mbili wangerudishwa katika vyumba.

Mako alitembea katikati ya Athu, Sipe na Sasi. Hawakuzungumza chochote, walitembea wakipigana vikumbo na wafungwa wengine.

Walifika sehemu iliyotumika kwa ajili ya kuoga. Paliwekwa vyungu vingi vikubwa vilivyojazwa maji, wafungwa wakavua nguo zao na kuanza kuyafurahia maji yale.

Mako hakushughulika na uogaji. Jicho lake lilitembea katika uzio wa gereza. Uzio ulikuwa hatua kumi na sita kutoka aliposimama. Mbele palikuwa na askari mmoja mwanamke. Kwa kuwa uzio ulijengwa kwa miti ya mkonge iliyoacha nafasi, Mako aliweza kuona nje ya gereza. Nje palikuwa na mto uliotiririsha maji. Kuona hivyo, mwanaume akatabasamu.

Soma: Mfalme Anakata Kuniua | Sehemu ya 10

Popular posts from this blog

Uhakiki wa Tamthiliya ya Kilio Chetu

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Risala | Kiswahili Kidato Cha Nne