Mfalme Anataka Kuniua | Sehemu ya Tatu
“Ndugu
zangu,” alisema kwa sauti kubwa, “Wanaume msijifungie ndani, njooni nje twende
tukapambane na huyu Simba. Mkiendelea kubaki ndani hakuna atakayesalia kwa
sababu milango yetu siyo imara kiasi cha kumzuia asiivunje. Ni heri tufe
tukipigana naye kuliko tujifungie ndani naye aje atukamate kama mwewe
akamatavyo vifaranga. Je mnavyakula vya kutosha siku ngapi? Sasa hamuoni
mnawindwa na njaa pamoja na simba? Aliyetayari kupambana ajitokeze sasa.”
Zilipita
dakika tisa tangu azungumze maneno hayo. Hakuna mwanamume aliyetoka ndani kuja
nje kuungana naye, Bwana Mako akaamua kuingia msituni peke yake kumsaka Simba
mzee. Akiwa anatembea alirushiwa mkuki.
“Chukua
mkuki huo utakusaidia kupambana na simba huyo,” ilisema sauti kutoka nyumba
moja, kisha ikasikika sauti ya kufunga mlango, pakawa kimya.
“Ni
uonevu kumuua simba mzee kwa mkuki, simba mzee anauliwa kwa viganja vitupu!”
alijibu Bwana Mako kisha akapotelea msituni.
Wanakijiji
walichungulia katika madirisha yao kama wanaoangalia sinema. Ukimya ukatanda
tena kwa dakika ishirini.
Ukimya
ulivunjwa na miungurumo ya simba, wanakijiji walitazama lakini hawakumuona
simba waliishia kusikia ile miungurumo yake tu. Baadaye ikasikika sauti ya
Bwana Mako akilia kisha pakawa kimya. Kimya kuliko muda wote.
Baadaye
vilianza kusikia vishindo vikija katika kijiji. Hofu ikawajaa, wakasali kila
mtu kwa imani yake wasijetafunwa na yule simba.
Vishindo
viliendelea kusikika mpaka walipoona kitu ambacho hawakuamini. Bwana Mako
alibeba mwili wa Simba yule mzee katika mabega yake. Naye alitembea kwa
vishindo vya shujaa.
Furaha
ilirejea tena kijijini, wanakijiji walifungua milango yao wakampokea Bwana Mako
na kumshukuru kwa msaada wake. Baada ya kumaliza maombolezo ya ndugu zao
waliotafunwa na Simba yule, walifanya sherehe kubwa kufurahia ushindi wa Bwana
Mako.”
Dada
wa kazi alimaliza kusimulia mkasa wa Mako. Hata akina dada wengine nao
wakavutiwa na Mako lakini waliogopa kuonesha waziwazi kwa sababu walitambua
kuwa malkia alikwisha mpenda.
***
Ilikuwa
usiku wa manane katika jumba la kifalme. Malkia alilala na alizama katika
usingizi. Mfalme wa Kanakantale yeye hakulala. Suala la utawala ni gumu na kuna
mambo ambayo yamekuwa yakimnyima usingizi, basi akiwa kimya, alisikia malkia
akiota kwa sauti.
“Mako
nakupenda, naahidi kuwa wako daima, njoo unikumbatie Mako wangu.”
Mfalme
aliyasikia maneno hayo, pia alibaini ilikuwa ndoto tu, hata hivyo Mako
alimfahamu, alimfahamu kwa sababu ya mikasa yake ya kila siku. Kilichomtesa
mfalme ni hilo jina Mako limeingiaje katika ndoto ya Malkia.
Mfalme
aliamua kumuamsha Malkia na kumuuliza juu ya ndoto yake. Malkia hakuonekana
kukumbuka kitu. Mfalme alisimulia ilivyokuwa, pia alimueleza Malkia kuwa, ndoto
ni matokeo ya mawazo yako ya siku nzima.
Malkia
alijitetea kwa kueleza tukio lake la kukutana na Mako, alisema alikutana na mtu
huyo mchana wa siku hiyo na hakuna kingine kilichoendelea.
Japo Mfalme hakuendelea kujibishana na Malkia, hakulizishwa na utetezi. Asubuhi aliamuru askari wamtafute popote alipokuwa Mako, wampeleke kwake tayari kujibu mashtaka.