Mfalme Anataka Kuniua | Sehemu ya Nne

 

Taji la mfalme

Haikupita muda, Mako aliletwa kwa mfalme akiwa chini ya ulinzi mkali wa askari wapandao punda. Alishushwa, naye kwa heshima akapiga mguu wa kuume mara tatu kumsalimu mfalme. Mfalme hakujibu salamu hiyo. alimtazama kwa ghadhabu Mako.

Baraza lilikaa ili kusikiliza mashtaka. Mako alivalia shati kubwa la buluu, suruali pana kiasi na viatu imara vya ngozi. Jamii ya Kanakantale, haikuwa nyuma katika teknolojia ya mavazi, watu wake walivaa mavazi ya kisasa!

Mfalme alianza kusoma mashtaka, “Mako, mkulima, mfugaji na muwindaji, unatuhumiwa kwa kosa la kujihusisha na mahusiano na mke wa mfalme, yaani Malkia wa nchi ya Kanakantale. Usiku tukiwa tumelala, nilisikia kwa masikio yangu Malkia akitamka kuwa anakupenda na anaahidi kuwa wako daima. Japo Malkia alikuwa ndotoni, haimaanishi kuwa huna mahusiano naye. Kinachotokea ndotoni ni matokeo ya kilichotendeka mchana. Una chochote cha kujitetea?”

“Mfalme wangu,” alijibu Mako, “nimekosa nini hata niwe na mahusiano na Malkia wa nchi yangu? Naruhusiwa kuoa wanawake wengi kadri ya uwezo wangu vipi niwe na Malkia. Tazama nchi hii ilivyojaa wanawake, wote hawa sijawaona hata nikaja kwa Malkia wangu mwenyewe? Mfalme tuhuma hizi siyo za kweli. Siwezi kufanya hivyo.”

Baada ya utetezi wa Mako, mfalme alikaa na baraza lake, wakajadili kwa muda. Wazee wale wenye ndevu nyeupe, walikubaliana jambo, mfalme akasoma hukumu.

“Tumekubaliana kuwa, Mako una hatia ya kuwa na mahusiano na Malkia. Ushahidi upo katika ndoto ya Malkia. Jambo hili ni kosa baya kabisa tena lisilokubalika. Hivyo, unahukumiwa adhabu ya kifo. Utakaa gerezani kwa muda wa mvua mbili, kisha utanyongwa hadharani iwe fundisho kwa wengine. Kwa kipindi chote hicho, hakuna anayeruhusiwa kuja kukuona ila kwa idhini ya mfalme.”

Mako hakuamini maneno yale. Aliinamisha kichwa chake hata mikono ikagusa zile nywele za kipilipili. Alishangazwa na hukumu ile ambayo haikutenda haki. Kukaa gerezani kwa muda wa mvua mbili maana yake ni kwamba, angekaa gerezani mpaka pale mvua ingenyesha kwa mara ya kwanza, kisha kwa mara ya pili, baada ya hapo angenyongwa.

Habari ya hukumu ya kifo cha Mako ilisambaa kama mchanga jangwani. Habari hii iliwaumiza sana wananchi wa kawaida. Mako alikuwa msaada mkubwa kwao. Hukumu hii iliumiza familia ya Mako na wote waliompenda kwa ule moyo wake wa kusaidia. Pengine habari hii ilimfurahisha mfalme peke yake kwa maana hakuna mwingine aliyefurahishwa na hukumu hii ya ajabu.

Wananchi walionekana kutoridhishwa na hukumu hii, waliwaza, kama kweli Mako ana mahusiano na Malkia, iweje basi ahukumiwe Mako peke yake naye Malkia aachwe?

Mchana wa siku hiyo Mako alitupwa gerezani akiwa kavikwa mavazi meupe. Gereza lilikuwa kubwa lililojengwa kwa miti ya mkonge. Liligawanywa katika vyumba vya watu wanne. Wafungwa hawakuruhusiwa kutoka katika vyumba isipokuwa mara moja kwa siku pale walipotakiwa kwenda kufanya usafi wa miili yao.

 Mako aliwekwa chumba kimoja na wenzake watatu, yeye akawa wa nne. Wote hao walisubiri hukumu ya kifo kwa makosa mbalimbali waliyofanya.

Soma: Mfalme Anataka Kuniua | Sehemu ya Tano


Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024

Jinsi ya Kuandika Risala | Kiswahili Kidato Cha Nne