Bwana Mako na Ndege Yake 2 | Mikasa Elfu Moja ya Bwana Mako 4

Bwana Mako na panga yake

Mkasa wa Nne

Bwana Mako na Ndege Yake
Sehemu ya Pili
Jitu lilifika nyumbani kwake likiwa limemuweka Bwana Mako mfukoni. Mke wa Jitu pamoja na watoto wake wawili, walikaa sebuleni. Jitu lilipoingia tu, watoto walilikimbilia wakifurahi kurejea kwa baba yao. Hata hivyo, Jitu halikuwa na furaha kwa sababu siku hiyo halikurudi na chochote cha kulisha familia. Kumbe Jitu lilikuwa masikini!
Jitu lilisogea mpaka alipokaa mkewe, likamshika mkono wa utosi kuashiria kwamba halikufanikiwa kupata chochote. Mke wa Jitu asiye na maneno mengi, aliwaamuru watoto waingie vyumbani kulala kuisubiri kesho.
Bwana Mako aliyaona yote haya akichungulia kutoka mfukoni mwa shati alimokuwa. Nalo jitu lilikwenda mpaka katika kitanda kikubwa likakaa na kumtoa.
Bwana Mako asiye na hofu tena, aliliamuru Jitu limuweke sikioni apate kuliambia jambo.
“Rafiki mwema,” Bwana Mako alianza kusema, “nimeona wewe ni masikini, kiasi kwamba huna chochote cha kulisha wanao. Lakini rafiki, nakuahidi kukufanya tajiri mkubwa katika jamii yako.”
“Ha! Ha! Ha!” Jitu lilicheka, “kwa umbo lako, huwezi kufanya kazi yoyote wala jambo ukaondoa umasikini wangu, nadhani utakuwa umechanganyikiwa kwa sababu ya ile ajali kiumbe mdogo.”
“Ni nani huyo unayezungumza naye?” mke wa Jitu aliuliza, kumbe muda wote alikuwa akimtazama mumewe akiwa katika maongezi.
“Kabla sijakuambia, niitie watoto ili niwaeleze kwa pamoja habari za huyu kiumbe mdogo.”
Watoto walifika na Jitu lilisimulia namna lilivyompata Bwana Mako. Mwisho Bwana Mako alikwenda kulala na watoto. Walimbeba na kurushiana kwa zamu, isingekuwa uhodari wao wa kudaka, Bwana Mako angeanguka na kuvunjika mbavu.
Siku mpya ilifika, Bwana Mako na watoto wa Jitu walikuwa wa kwanza kuamka, na tazama akishirikiana na watoto wa Jitu, alikuwa ametengeneza meza kubwa ambayo ilikuwa na kimo sawa na tumbo la majitu. Baada ya kukamilika kwa meza, akashirikiana na watoto kuipeleka nyuma ya nyumba ambako kulikuwa na ukumbi mkubwa, kisha akawaamuru watoto wakamuite baba yao.
“Niliahidi kukufanya tajiri.” alisema Bwana Mako baada ya Jitu kufika.
“Na hii meza ndiyo utajiri wenyewe?” Jitu liliuliza.
“Ndiyo, meza hii ndiyo utajiri wenyewe, lakini haiwezi kuwa utajiri bila mimi niliyekaa juu yake.”
“Sikuelewi unanichanganya!” lililalamika Jitu.
“Sikiliza rafiki mwema,” alisisitiza Bwana Mako, “watume wanao waende mjini, wawatangazie watu maneno haya: Nyumbani kwa baba yetu, kuna maonyesho hayajawahi kutokea. Mtu mkubwa kutoka sayari iitwayo Dunia, amemtembelea baba yetu, ajabu ni kwamba, pamoja na ukubwa wake huko Duniani, huku anaonekana kiumbe mdogo. Ama kweli kila mkubwa na mkubwa wake. Njoo ujionee kiumbe huyu wa ajabu kwa kiingilio cha pesa mbili tu.”
Jitu lilimwelewa Bwana Mako na liliona ubora wa wazo hilo hata likastaajabu sana uwezo wa akili ya mwanadamu kutoka Duniani.
Basi watoto wa jitu walitembea mjini wakitangaza, “Nyumbani kwa baba yetu, kuna maonyesho hayajawahi kutokea. Mtu mkubwa kutoka sayari iitwayo Dunia, amemtembelea baba yetu, ajabu ni kwamba, pamoja na ukubwa wake huko Duniani, huku anaonekana kiumbe mdogo. Ama kweli kila mkubwa na mkubwa wake. Njoo ujionee kiumbe huyu wa ajabu kwa kiingilio cha pesa mbili tu.”
Kufumba na kufumbua, majitu mengi yalijaa nyumbani kwa Jitu, yote yalitaka kumuona kiumbe kutoka duniani na yalilipa kiingilio cha pesa mbili. Yalipelekwa mpaka katika meza aliyosimama Bwana Mako. Kwa sababu yalikuwa mengi, basi yaligawanywa katika makundi ili yaweze kumuona kwa zamu.
Bwana Mako alifanya michezo ya kufurahisha, kwanza alianza kwa kupiga danadana mpira, majitu yakashangaa. Kisha akacheza mziki, halafu akaruka sarakasi, sarakasi zenyewe hazikuwa sarakasi bali zilikuwa zile za upande upande, ni ushamba tu wa majitu kushangaa sarakasi hizo. Ama naweza kusema, burudani haswaa ilikuwa ni ule udogo wa Bwana Mako katika macho ya majitu. Alitaka kufanya mchezo wa ngumi, lakini alihofia labda majitu yanaweza kuiga na kusababisha vita vya mikono mahali pale, basi badala ya ngumi, akaweka vichekesho.
Ujinga wa ndoto ni huu, utaota umeokota pesa ukiamka hakuna. Utaota umeokota dhahabu ukiamka kitandani patupu. Ila ukiota umekojoa, unakuta imooo!”
“Ha! Ha! Ha!” majitu yalicheka yakishika mbavu.
Kuna Jitu moja lilisikika likimwambia mkewe, “pesa yangu imekwenda kihalali, pesa mbili, vicheko lukuki.”
Hayo ndiyo yakawa maisha ya Bwana Mako na Jitu. Kazi hiyo iliwapatia pesa elfu mbili kila siku.  Pesa hizo ni sawa na shilingi milioni nne za Kitanzania. Jitu likawa tajiri kama lilivyoahidiwa. Halikulala tena njaa, maisha yakabadilika.
Bwana Mako hakusahau kuhusu kurejea nyumbani. Ila, alitaka ashirikiane kwanza na majitu yale ili aweze kuyafahamu zaidi. Pia, aliendelea kuikarabati ndege yake, safari hii, hakusahau kuweka kigingi cha nne, pia alifurahishwa na miti ya kule, ilikuwa migumu kama chuma.
Aliendelea kufanya maonyesho na kushangiliwa na majitu kila siku mpaka taarifa zilipomfikia mfalme wa majitu. Ujumbe ukafika haraka, kiumbe kutoka Duniani, anatakiwa barazani kwa mfalme kabla tonge la kwanza la chakula cha mchana halijaguswa.

Jiunge katika Group la whatsapp uwe wa kwanza kupokea mkasa Unaofuata Gusa Hapa Kujiunga

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024

Jinsi ya Kuandika Risala | Kiswahili Kidato Cha Nne