Mfalme Anataka Kuniua | Sehemu ya Tano

 

Taji la Mfalme

Aliweza kuwatambua watu hao. Mmoja aliitwa Sasi, kosa lake Wizi. Wala hakusingiziwa. Sasi alikuwa mwizi aliyechukiwa na watu wote. Wa pili alikuwa Athu, yeye alifungwa kwa kosa la uharifu kama Sasi. Naye hakusingiziwa, alikuwa mwizi wa mifugo aliyechukiwa na wafugaji wote. Wa tatu aliitwa Sipe, alifungwa kwa hofu ya mfalme. Mfalme alimuogopa Sipe kuwa ipo siku angempindua. Sipe alikuwa mtu mwenye maneno ya busara. Mara chache alitabiri mambo yakatokea, hii ilimpa hofu mfalme kwa kuona Sipe atapendwa na watu kuliko yeye na kuleta mapinduzi. Sipe alionewa!

“Hamjambo ndugu zangu?” Alisalimia Mako.

“Hatujambo,” walijibu. Sipe akaendelea, “Hakuna aliyesalama, hata wewe Mako umeletwa humu? Umefanya kosa gani hasa?”

“Ni uonevu tu,” alijibu Mako, akikaa katika kitanda cha majani, “nina mvua mbili za kunifanya niendelee kuwa hai. Nimehukumiwa kunyongwa kwa kosa la kuonekana katika ndoto ya malkia. Malkia kaota kwa sauti akisema ananipenda na hawezi kuniacha milele!”

Wote walicheka, lakini kicheko cha huruma. Hawakuwahi kusikia hukumu ya kustaajabisha kama hii.

Katika hali isiyotarajiwa, mvua kubwa ilinyesha, simanzi ikawakumba wafungwa wale wanne. Ilibaki mvua moja tu, Mako anyongwe!

Japo Mako ni jasiri, kunyesha kwa mvua kulimtetemesha na kumkata maini. Alikiweka kichwa chake katikati ya magoti, asiyeamini hukumu hiyo ya aina yake.

Hata usingizi ulipotaka kumchukua, ulishindwa na hata ulipomchukua, aliota ndoto mbaya akaamka haraka. Baridi ilikuwa kali, lakini kijasho kilimtoka.

Kwa mbali kupitia dirishani, malkia wa nchi ya Kanakantale alionekana akibishana na mfalme. Malkia alivaa vazi refu, pana, jeupe aliloliburuza atembeapo. Mfalme alivaa suruali nyeusi na shati jeupe.

“Umemhukumu kumfunga mtu asiye na hatia, mbaya zaidi anatakiwa kunyongwa… haki iko wapi?” alilalamika Malkia.

“Mimi ndiyo mfalme, wewe ni mwanamke tu. Huna haki ya kuhoji maamuzi haya yametoka wapi? Nchi nzima haithubutu kunihoji utaweza wewe?”

“Hata kama. Hukutakiwa kutoa hukumu ya kifo kwa mtu asiye na hatia. Kumbuka mtu huyu ana familia inayomtegemea. Ana ndugu na jamaa wanaompenda, pia, hukumu hii inawafikirisha watu kama wana mfalme anayejielewa sawasawa…”

Mfalme aliyechoka kubishana, akamchapa kofi kali malkia na kuacha alama ya vidole vitano vionekane katika mashavu laini ya mke huyu wa mfalme. Malkia akalia kwa uchungu lakini walinzi hawakuweza kumsaidia kwa sababu aliyempiga kofi ni mfalme!

Kuona hivyo, akatoka na kuelekea katika chumba cha wale dada wa kazi wanne, dada hawa wamekuwa wasaidizi wake wa muda mrefu nao hukaa chumba kimoja kikubwa katika kona ya kulia ya Kasri la mfalme wa Kanakantale.

Malkia aliingia humo akibubujikwa na machozi, wasaidizi wakampokea na kumkarisha katika kitanda kikubwa cha manyoya.

Soma: Mfalme Anataka Kuniua | Sehemu ya Sita

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2023

Sifa Bainifu za Irabu ya Kiswahili Sanifu