RIWAYA| SITASAHAU NILIPOLALA NA MWANAMKE JUU YA KABURI (21)
Tulifika chumbani. Chumba
kilihuzunika na hakikuvutia hata kidogo. Vitu havikukaa katika mpangilio. Nguo zilizagaa
chini, nazo suruali zilitumbukia katika masufuria makubwa yaliyobaki mchuzi. Mlikuwa
na vitanda viwili, kitanda kikubwa na kitanda kidogo.
“Kitanda hiki kidogo alilala
mjukuu wangu Chimota… nilipenda alivyoota! Washenzi wakamchukua. Utalala hapo!”
“Hicho kikubwa alilala nani?”
niliuliza swali la utani. Mzee akaujibu utani wangu.
“Nililala na bibi yako!”
Sikujibu. Alizima kibatari,
nikalala katika kitanda kidogo, naye akapachika mbavu zake katika kitanda
kikubwa.
Asubuhi ilifika. Niliamka
taratibu kitandani. Nilipotazama alipolala mzee sikumwona. Kwa kuwa nililala na
nguo zangu zote, nilifanya kazi ndogo ya kuvaa kandambili na kuelekea sebuleni.
Huku nako hakuwako.
Nilimwona mzee akiwa katika mti
mdogo wa mwarobaini. Chini aliwasha moto kwa kuni tisa na aliendelea na zoezi
la kuchoma samaki. Bila shaka yalikuwa maandalizi ya kifungua kinywa.
Nilikaa pembeni yake. “Mzee
Shikamoo!” nilimsalimia.
“Haina haja!” alijibu. Sikujali,
nilikaa nikaendelea kumtazama alivyoshughulika na wale samaki.
Hatimaye samaki walikuwa tayari
kwa kuliwa. Mzee akanituma chumvi. Nilileta. Akanituma tena pilipili, nikaleta,
akanitaka nikae mkao wa kula, nami nikatii.
Samaki walipakwa chumvi na
pilipili kiasi kwa ufundi wa hali ya juu, ukiongeza ile harufu yao na njaa
niliyoihisi tumboni, nilizidi kukaa mkao wa kula kama nilivyoshauriwa. Mate
yalinijaa mdomoni tele.
Mzee alianza kumshambulia samaki
mmoja, akachomoa mnofu mkubwa, akatafuna taratibu akifaidi uhondo. Nami
nikapeleka mkono katika samaki huyo ili nibebe pande langu la mnofu. Mzee kuona
hivyo akausukuma mkono wangu na kunitaka nitulie.
Nilitii amri. Nikatulia
ninayesubiri samaki. Mzee akamla samaki wa kwanza nikimshuhudia, akaongeza wa
pili nikitazama, mate ya uchu yamenijaa mdomoni.
Alimaliza kula samaki wote wawili
mimi nikitazama tu, akanituma maji. Nilikimbia nikayaleta haraka. Akanywa
taratibu kisha akabeua kwa shibe. “Gbuuuuuuuh!”
Alinitazama kwa huruma, akasema:
“Najua njaa ina kukeketa tumboni, nenda chumbani kwangu chini ya uvungu kuna
kiazi kikubwa, chukua ule!”
Kwa jinsi njaa ilivyouma, nilikwenda
haraka chumbani. Nikachungulia uvunguni kutafuta kiazi nilichoagizwa, sikuamini
nilichokiona uvunguni…
Itaendelea kesho…