Mfalme Anataka Kuniua | Sehemu ya Sita

Taji la Mfalme

“Nini kinakuliza Malkia wangu, ni hii habari ya Mako kuhukumiwa kunyongwa!” aliuliza dada yule aliyemsimulia malkia mkasa wa Mako na Simba mzee.

“Ndiyo, mtu asiye na hatia atakufa baada ya mvua mbili kwa sababu yangu.”

“Maskini Mako, ni aheri angebaki katika nchi ya majitu kuliko kurudi tena huku!” alijibu Dada.

“Una mkasa mwingine wa Mako nisimulie tafadhali,” alisema Malkia akifuta machozi. Dada akakaa sawa kusimulia, nao wenzake wote wakakusanyika na kutengeneza kikao cha watu watano.

“Kwa muda mrefu Bwana Mako alitamani kuitembelea Dunia aione yote akiwa juu. Ndipo alipopata wazo la kutengeneza ndege ambayo ingemsaidia kutimiza malengo yake. Umbo la ndege lilitengenezwa kwa mbao za mninga, ndani aliweka furushi kubwa la nyasi ambalo lingetumika kama kiti cha rubani, nyuma ya kiti cha rubani aliweka godoro nene, hili lingetumika kulala pale anapokuwa amechoka na muda huo ndege ingekuwa katika ‘autopilot.’ injini za ndege hii na namna ilivyofanya kazi, ilikuwa siri yake Bwana Mako.

Aliamka asubuhi kabla mkewe na mtoto wake mdogo hawajaamka. Aliandika ujumbe katika kikaratasi, “Nakwenda ziara, nitarudi baada ya siku tatu.” kisha akaelekea mpaka mahali alipoegesha ndege, akaingia humo, alipokaa vyema, akavuta kigingi cha kwanza, ndege ikaunguruma kwa sauti kubwa na kuanza kuserereka taratibu kama maharusi. Baadaye iliongeza kasi, ikaserereka kwa sekunde chache, kisha akavuta kigingi cha pili, ndege ikaanza kunyanyuka juu, hapo akatazama chini kukiona kijiji chake, loooh! Kumbe wanakijiji waliamshwa na yale makelele ya ile ndege, wote walikuwa nje ya nyumba zao, kuona hivyo, akafungua mlango haraka, akawapungia mkono na kuwafanyia ishara ya kwamba angerejea baada ya siku tatu, akimaliza kufanya hivyo, akaufunga mlango.

Ndege ilikuwa imepaa juu kiasi alichokitaka, akagusa kigingi cha tatu, ikawa sawia huku ikisonga mbele, aliweza kuiona Dunia kwa namna alivyotamani. Aliliona bara la Afrika kama alionavyo katika ramani, akaongeza mwendo zaidi, ndege ikawa inatembea mwendo wa kunguru kumi na tisa kwa saa! Alipoiona Afrika ya Kusini, alitamani atue, awacharaze bakora vijana wahuni wa pale, lakini akapanga kurejea siku nyingine.

Mpaka giza linaingia, alikuwa ameliona bara la Afrika, Amerika ya kusini na sehemu kubwa ya bara la Amerika ya kaskazini. Kwa sababu giza lilimzuia kuona, aliamua kutua Marekani ili kukikucha, apae tena na aweze kuendelea na safari yake ya udadisi. Basi akapapasa mkono wake ili akishike kigingi cha nne, masikini! Kigingi hakikuwepo, alisahau kukiweka kwa sababu ya ile haraka yake ya kutaka kuizunguka Dunia.

Ndege iliendelea kupaa, naye akawa anawaza namna ya kutua, akiendelea kuwaza, ghafla aliona kitu kama kilele cha mlima, akashika haraka kigingi cha pili, ndege ikapaa juu zaidi. Lakini kwa sababu ya kule kupaa juu kwa ghafla na kasi iliyokuwepo, Bwana Mako akateleza na kudondokea upande wa nyuma kulikokuwa na kitanda. Alijaribu kurejea katika kiti chake cha rubani lakini hakuweza, basi akabaki kuangalia jinsi ndege ilivyokuwa ikielekea juu asiyejua hatma yake.

Ndege ilikwenda juu kwa kasi kubwa kwa muda wa saa kumi na nne. Muda wote kulikuwa giza. Lakini baadae mwanga ulionekana ghafla na kumshitua Bwana Mako aliyekuwa amekata tamaa. Akiendelea kutazama vizuri ili atambue eneo hilo, ndege ilianguka chini, ikapasuka vipande viwili, bahati njema kumbe alijua angeanguka muda wowote, hivyo alikuwa tayari kajifunga katikati ya godoro na hivyo akanusurika, pengine na yeye angepasuka vipande kama ile ndege yake.

Alisimama haraka na kuanza kuchunguza mahali pale ili abaini alikuwa wapi, japo alitazama kwa jicho la udadisi hakuweza kutambua wala kufananisha. Ilikuwa sehemu ya tofauti, tambalale yenye nyasi fupi ngumu ajabu!

Soma: Mfalme Anataka Kuniua | Sehemu ya Saba

Popular posts from this blog

Uhakiki wa Tamthiliya ya Kilio Chetu

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Hotuba