Uhakiki wa Tamthiliya ya Mukwava wa Uhehe

Ganda la kitabu cha tamthiliya ya Mukwava wa Uhehe
Wasiliana na Mwalimu ili Kujiunga Darasa la Uhakiki wa Vitabu vyote vya Fasihi Mtaala Mpya kwa Kugusa Hapa

Mwandishi: Mugyabuso Mulokozi

Mwaka: 1979

Mhakiki: Mwalimu Makoba

Utangulizi

Nikiwa chuo kikuu cha Dar es Salaam, katika ofisi za TATAKI, mwalimu wangu, Profesa Mulokozi alinipita akiwa amebeba vitabu na nyaraka nyingi, mbele kidogo alidondosha vitabu viwili, nikasogea ili nimsaidie kuviokota, lakini nilichelewa, aliviokota haraka kisha akaendelea na safari yake. Alitembea kwa kasi iliyomshangaza kila aliyemtazama.

Haikuwa kawaida ya Mulokozi kubebelea mibuku mingi namna ile, wazo likanijia, pengine anakwenda Botswana! Agosti mwaka 2015, alialikwa Botswana kuhudhuria utetezi wa tasnifu ya PhD ya mwanafunzi wa Kezilahabi. Kezilahabi alimpokea vizuri na alikaa Gaborone kwa takribani wiki moja. Mulokozi mwenyewe alikiri wazi kuwa, kukaa na Kezilahabi ulikuwa ni wakati wa furaha na burudani sana kwake.

Pia Kezilahabi alitamani sana wabadilishane nafasi, Mulokozi aende Botswana kwa mwaka mmoja, Kezilahabi aje kwenye likizo ya ubukuzi nchini Tanzania! Kwa hivyo niliamini kuwa, mtu huyu anarejea tena Botswana.

Haikuchukua siku nyingi kuubaini ukweli, lile wazo kwamba Mulokozi alikua akienda Botswana na Tanzania angekuja Kezilahabi halikuwa la kweli, lakini ndilo lililoleta jibu kamili, ukweli ambao ulimuumiza kila mmoja wetu!

Ile siku niliyopishana naye, alikuwa akichukua vitu vyake muhimu, siku hazigandi, Profesa Mugyabuso Mlinzi Mulokozi alifikisha umri wa kustaafu na alishuka Mlimani!

Siku tuliyopokea taarifa ya kustaafu Mulokozi, tulijawa na simanzi, jua lilitambaa kinyonge, dunia ilitambua huzuni kubwa iliyotupata, ikatubembeleza kwa kutuimbia wimbo wake wa furaha, “Huuum! Huuum! Huuum!”

Pale Mlimani, alishuka mtu! Alishuka msomaji hodari, mhakiki makini na msomi mkubwa. Tuliomfahamu Mulokozi, tulikubaliana kwamba, alikuwa mbele ya Shakespeare, Ngugi na Soyinka!

Nilipokea kwa furaha niliposikia tamthiliya ya Mukwava wa Uhehe imechaguliwa kuwa miongoni mwa vitabu teule. Nilifurahi kwanza kwa sababu ya maudhui yake ya kizalendo, lakini pili ni kule kuandikwa kwake na Mugyabuso Mlinzi Mulokozi, mhakiki ni mwalimu, sasa ni zamu yangu kumfundisha Mulokozi, lakini kwa adabu zote.

Kuhusu Tamthiliya ya Mukwava wa Uhehe

Mukwava wa uhehe ni tamthiliya ya kihistoria inayoeleza ushujaa uliofanywa na mfalme Mukwava Ntasalatsi Mahinya Munyigumba. Matukio mengi ni ya kweli, hata hivyo kwa kuwa ni kazi ya fasihi, mwandishi ameweka chumvi, pilipili na ndimu kidogo ili kunogesha.

Mukwava alivamiwa na wajerumani, akapambana nao na kuwashinda, hata hivyo walirejea tena na aliendeleza mapambano kwa muda mrefu mpaka pale alipozidiwa.

Jambo linalomfanya Mukwava aonekane shujaa ni kule kukataa kwake kutawaliwa, lakini alikataa kuwauza watu wake kwa kushirikiana na wazungu, ushujaa wake tunaouona hasa pale anapokuwa tayari kufa kwa ajili ya watu wake.

Maudhui

Vipengele mbalimbali vya maudhui vilivyojitokeza katika tamthiliya hii vinajadiliwa:

Dhamira

Mwandishi anaibua dhamira mbalimbali zenye uhalisia na historia ya Tanzania:

Uzalendo

Tunamuona Mukwava akiwa mzalendo kwa nchi yake. Anakataa kuwauza watu wake kwa mzungu, anakataa watu wake kuwa watumwa. Anaamua kupigana vita akiwa tayari kufa kwa ajili ya watu wake.

“Mimi ni Mhehe. Mimi ni mfalme katika ufalme wangu kama yeye alivyo mfalme huko alikotoka. Siwezi kuogopa au kupokea amri kutoka kwa mgeni yeyote. Nitakufa kwanza! Hata konokono ni mfalme ndani ya gamba lake!” uk 29.

Mukwava ni kiongozi anayeelewa mambo vizuri. Anajua wazi lengo hasa la mzungu ni kuwatawala Waafrika, hataki kufanya urafiki na mzungu, hataki kuuza nchi.

“Kufanya urafiki na mzungu ni kuiuza nchi,” uk 30.

Mtumwa wa Mubogamasoli anaonyesha uzalendo pale anapotumwa na mmiliki wake kwenda kutoa siri za Uhehe kwa Wajerumani. Mtumwa anaona jambo hilo ni baya na ni usaliti kwa nchi, anatoa siri hiyo kwa kuivujisha kwa askari aliyeitwa Mupangile.

“Mimi ni mtu mweusi kama wewe. Naelewa uchungu wa kutawaliwa, naufahamu uovu wa kuisaliti nchi,” uk 80.

Japo ni mtumwa, lakini anakataa kuwasaliti weusi wenzake. Jambo hili ni uzalendo mkubwa kwa watu weusi wote.

Vita

Tunaelezwa kwamba, hata kabla ya majilio ya wakolini, Waafrika walijitawala wenyewe. Changamoto kubwa iliyochelewesha maendeleo ilikuwa vita.

Mukwava anasema yeye hakupenda kupigana vita na ndugu zake Waafrika, alilazimishwa tu kwa kuvamiwa.

Tunaona vita vya Wahehe wakipigana dhidi ya Wamasai na Wangoni.

Wahehe wanaposhinda vita hivi, amani inapatikana, kuvamiana kunapungua, hata hivyo, Wadachi wanaibuka katika kipindi hiki.

Mukwava anapigana vita dhidi ya Wajerumani kwa ufanisi mkuwa, anafanikiwa kuwashinda wanapomvamia kwa mara ya kwanza. Askari weusi wanaoshirikiana na Wajerumani wanakamatwa mateka. Kwa kutambua kuwa wale ni ndugu zetu, Mukwava anazuia wasiuawe.

“Hao msiwaue. Tutakaa nao tuwafundishe… usalama wa mtu mweusi utategemea umoja wa watu weusi. Umoja,” uk 83.

Vita vinapokelewa kwa hisia tofauti. Wengi hawapendi vita ila wanalazimika kupigana kwa sababu hakuna njia nyingine. Semusila hapendi vita.

“Suala hili linanikera sana, fikiri mwenyewe… wanadamu, viumbe wenye akili, wanaamua kuuana,” uk 23.

Ili kuepusha maafa ya vita, Semusila anamshauri Mukwava aunge urafiki na wazungu ili kusitisha vita. Jambo hili haliwezekani, Mukwava anaijua nia ya dhati ya watu weupe ni kuwatawala watu weusi, anaona kuunga urafiki ni kama kuwauza watu wake kwa mzungu.

Tunaona vita vikisababisha hasara kubwa. Kwanza watu wengi wanauawa na pili mali nyingi inaharibiwa na watu wanaanza kuishi maisha ya hofu.

Nafasi ya mwanamke katika jamii

Tamthiliya hii imemchora mwanamke katika namna mbalimbali:

Kwanza mwanamke amechorwa kama shujaa. Mutage ni mwanamke shujaa tena jemedari anayeliongoza jeshi la Wahehe dhidi ya adui. Analiongoza kwa ustadi wa hali ya juu kuwafukuza wamasai na anaongoza mapambano dhidi ya wajerumani.

Pili, tunaona mwanaume bado anamdharau mwanamke. Mubogamasoli anakataa kwenda vitani kwa sababu hataki kuamrishwa na mwanamke. Naye Mwamusambwa bado ana mawazo yaliyopitwa na wakati, anasikika akisema,

“Kuzaa mabinti ni kupoteza mbegu bure,” uk 85.

Tatu, mwanamke amechorwa kama chombo cha starehe. Von Zelewsk anaagiza aletewe ‘buibui’ ili apate kustarehe naye. Von Zelewsk aliwaita wanawake buibui.

Nne, mwanamke amechorwa kama mzalendo. Mhusika Mwanamke katika kuipigania nchi yake, anajiunga katika jeshi ili kuziba nafasi ya mume wake aliyefia vitani. Mwanamke huyu anatumwana Mukwava akapeleleze mipango ya adui.

Umoja

Mukwava alikuwa na fikra za kisasa. Aliamini katika umoja wa Afrika. Aliamini umoja ndiyo ungeweza kuwasaidia dhidi ya uvamizi wa wazungu.

Mukwava alipoona wazungu wanajiandaa kuvamia, aliomba ushirikiano kutoka kwa Merere wa Wasangu, Isike wa Wanyamwezi na Chaburuma wa Wangoni. Wote hawa, walikataa kushirikiana na Mukwava, shujaa huyu akapigana peke yake.

Mkwava aliamini kwamba, adui wa Mwafrika siyo Mwafrika mwenzake bali ni mzungu.

“Adui wa Mwafrika siyo Mwafrika mwenzake, ni mzungu,” uk 11.

Hata hivyo wapo Waafrika wengi ambao fikra zao hazikuwa sawasawa kuhusu suala la umoja. Hawa waliamini katika ukabili. Kundi hili linawakilishwa na Mubogamasoli ambaye aliamini katika ukabila. Yeye anaamini kuwa mtu yeyote ambaye siyo mhehe ni adui yao.

Chaburuma anapoombwa kuungana na Mukwava dhidi ya wazungu, anakataa kwa kusema wao ni wahehe na yeye ni mngoni.

Merere anapoombwa msaada anasema zizi ni dogo mno kwa mafahari wawili kukaa, anasema hawezi kumsaidia mtemi mwenziye.

Anapoomba msaada kwa wazee wa kimasai wanakataa kwa kusema Mungu wao kawapa ng’ombe wote duniani na yeyote mwenye ng’ombe wao watawafuata.

Upande mwingine tunamuona Isike akitoa kauli isiyoamini katika ushirikiano,

“Mzungu mwekundu sina ugomvi naye, asiponishambulia sitamshambulia, akinishambulia, nitamwonyesha kaburi lake,” uk 69.

Tunaona kuwa, laiti kama jamii za Kiafrika zingeungana pamoja, huenda zingefanikiwa kuzuia kuingia kwa ukoloni. Ukoloni uliingia kwa urahisi kwa sababu jamii nyingi zilikuwa na uadui.

Suala la dini

Mwandishi anatueleza kwamba, jamii za Kiafrika zilikuwa na dini zao kabla ya majilio ya wakoloni ambao walileta Uislamu na Ukristo.

tunaonyeshwa wahehe wakifuata tamaduni na miungu yao, kabla ya vita, mganga anaizindika nchi.

“Sasa kila kiongozi, kila mwanamke na kila askari aliyeko hapa ajiandae kwa tambiko,” uk 97.

Tunaelezwa kwamba, dini ya kikristo ilitumika kwa kiasi kikubwa katika kueneza ukoloni. Nyundo anampa moyo Kasisi kuwa kanisa lake litajaa kwani yeye na wao ni kitu kimoja.

“Usitie hofu, Padre. Kanisa lako litajaa tu. Wewe nasi ni kitu kimoja… hatuwezi kulishinda bara hili la giza bila msaada wako,” uk 38.

Nyundo anaeleza ukweli kuwa, kutawaliwa kwa mwafrika kwanza kumeanzia katika dini, dini hizi zinatumika kuwapoteza Waafrika mpaka hii leo.

Tibasima anatoroka katika jamii yake na kwenda kwa Kasisi, huko anatoa siri za Uhehe na kusaidia kuvamiwa kwake na hatimaye kuangushwa. Kwa kuwa lengo la dini hizi ni kueneza ukoloni, wanamuua Mupangile ndugu yake Tibasima kwa kuchanjiana chale.

Utajiri wa bara la Afrika

Wazungu hawakuja Afrika kwa lengo la kueneza ustaarabu kama wanavyodai. Lengo lao hasa ilikuwa kufuata utajiri uliojaa ndani ya bara hili.

“Uhehe iko kwenye mto Ruaha. Naambiwa ni nchi nzuri sana, ina milima na mabonde yenye rutuba na hewa ya baridi,” uk 44.

Mukwava hakuwa tayari kuuachia utajiri wa Mwafrika uwe wa mzungu. Alipambana kwa bidii na ameacha historia.

Ubaguzi wa rangi

Wazungu walijiona wao ni bora kuliko watu weusi. Weusi waliitwa washenzi.

“Mzungu hawezi kuondolewa hapa na mtu mweusi. Nitajinyonga kabla ya kupokea amri kutoka kwa mshenzi,” uk 45.

Mzungu anaamini kwamba yeye ndiye anayestahili kumtawala mtu mweusi, anaamini mtu mweusi hawezi kujitawala mwenyewe. Hata hivyo, Mukwava aliwapa funzo kubwa, alipowapiga pale walipomvamia, Gavana hakuamini, ilibidi afanye uchunguzi juu ya uraia wa  Nyundo (Von Zelewsk na Merkl).

Haki

Mukwava ni mpigania haki. Anataka haki itawale, kauli zake zinamfanya awekwe kundi la wapigania haki.

Mukwava alisikika akisema, “Kupigana na kushindwa ni bora kuliko kunyamaza na kuvumilia maonevu.” kwake ilikuwa bora kupigana kuliko kunyamazia uvunjifu wa haki.

Katika kupigania haki, aliongeza kwa kusema, “Mauti ni bora kuliko utumwa.” kwa Mukwava ilikuwa heri kufa kuliko kuishi kama mtumwa.

Mukwava anaamini haki ya kweli haipatikani kwa kumbembeleza mzungu au naye urafiki, anapinga jambo hilo kwa kusema, “Kufanya urafiki na mzungu ni kuuza nchi!” njia pekee ya kumshikisha adabu mzungu ni kumpiga.

Mapambano ya haki ni jambo la muhimu katika jamii yoyote ile. Kukosekana kwa haki hupelekea kukosekana kwa amani.

Uhaini

Watu waliokosa uzalendo wanaonekana katika tamthiliya hii. Mubogamasoli anafanya kitendo cha uhaini kwa kumtuma mtumwa wake aende akatoa siri za ngome ya Uhehe kwa adui.

“Mubogamasoli, wa ukoo wa Muyovela mtukufu, aliyedhulumiwa kikatili haki yake ya kuitawala uhehe, anakusalimu na kukutaka urafiki… yuko tayari kukusaidia kuikamata Kwilenga na kumpata Mukwava iwapo utakubali kumsaidia kuikamata Ivaha ya Uhehe na kuupata ufalme wa babu zake.”

Kwa kosa hili la uhaini Mubogamasoli ananyongwa.

Musatima naye anafanya kitendo cha uhaini. Anakimbilia kwa wazungu baada ya ndugu yake Mubogamasoli kunyongwa. Akiwa huko anaeleza siri zote juu ya namna ya kuiteka nchi ya Uhehe. Uhehe inaangushwa kwa sababu ya usaliti wa Musatima. Hata hivyo, anashindwa kuendana na tamaduni za kizungu, na kuamua kurudi nyumbani, anaomba msamaha na kujutia makosa yake. Mukwava anatajwa kama mtu mwenye busara na huruma, anamsamehe.

Uhuru wa kutoa maoni

Katika nchi ya Uhehe watu wana uhuru wa kutoa maoni hata ule ukosoaji mkali.

Tunamuona Mubogamasoli akiwa mkosoaji mkuu wa Mukwava. Mtu huyu alikosoa waziwazi mienendo na mbinu za Mukwava lakini Mukwava hakumdhuru.

Mubogamasoli alipinga mbele ya Mukwava kuwa wazungu hawawezi kuvamia Uhehe.

Alipinga ushirikiano wa makabila, yeye alitaka wahehe wapambane peke yao kwani mhehe ni mhehe na mtu ambaye siyo mhehe ni adui wa mhehe.

Pia alipinga jeshi kuongozwa na jemedari mwanamke.

Pamoja na upinzani huo mkali aliouonesha, Mukwava alikuwa mwanademokrasia, alikosoa hoja za Mubogamasoli kwa kusema mawazo hayo yamepitwa na muda, zama zimebadilika.

Ukatili

Wajerumani hawakuwa na huruma. Tunauona ukatili wao. Wanapovamia, wanawaua Waafrika wengi wasiokuwa na hatia.

Tunaona hata dini zao zinaenezwa kwa ukatili. Watu wanalazimishwa kwenda kusali na wanapomaliza wanalazimishwa kwenda kulima shamba la misheni.

Mwakiyombwe anauawa kikatili kwa kupigwa risasi kwa sababu alikataa kutaja alipokuwa Mukwava.

Mwanamke anatendewa kwa ukatili na Wajerumani, anapokamatwa, mtoto wake mdogo anabebwa miguu juu kichwa chini… jambo hili linamshangaza hata Padre wa Kijerumani na kuamrisha waache.

Nyundo (Von Zelewsk) anabaka wanawake ambao yeye anawaita Buibui. Askari wanaagizwa mara kwa mara wamletee wanawake wazuri wa kulala nao.

Ukatili wa Wajerumani unaonekana kwa watu wote, lilikuwa jambo la kawaida kuchapwa viboko hadharani, wakati mwingine bila kosa lolote.

Ujumbe

Mafunzo mbalimbali yanapatikana katika tamthiliya hii:

Adui wa mwafrika siyo mwafrika ni mzungu

waafrika walitakiwa kuungana na kuwa kitu kimoja kwani adui yao mkubwa alikuwa mzungu aliyetaka kuwatawala.

Mdharau mwiba mguu huota tende

Nyundo (Von Zelewsk) aliwadharau wahehe. Alipowavamia walimuonesha cha mtema kuni kwani alifia vitani.

Dini za kigeni zilitumika kueneza ukoloni

Tunaiona dini ya kikristo ilivyotumika kuleta ukoloni. Watu wanalazimishwa kusali na wanapomaliza wanalazimishwa kwenda kulima katika shamba la misheni. Dini hizi zililenga kuwafanya watu wawe wapole hivyo wasiendeleze mapambano ya kupinga ukoloni.

Umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu

Waafrika waliweza kushindwa mapambano ya kupinga kuingia kwa ukoloni kwa sababu hawakuwa na umoja. Kila kabila lilipiga peke yake. Laiti kama wangeungana, wangeweza kuonyesha upinzani mkubwa na pengine wangeweza kushinda na kuzuia kabisa kuingia kwa ukoloni ndani ya bara la Afrika.

Viongozi na wananchi wawe wazalendo katika nchi zao

Suala la uzalendo limeshuka katika nchi yetu. Ni ujumbe wa tamthiliya hii kwamba, bado tunahitaji kuwa wazalendo ili kuhakikisha nchi zetu zinakuwa salama dhidi ya adui.

Migogoro

Migogoro mbalimbali inajitokeza katika tamthiliya hii:

- Migogoro ya kisiasa

Wajerumani wanataka kuwatawala Waafrika, Mukwava akiwawakilisha Waafrika anapinga utawala huu wa wazungu.

Mubogamasoli haelewani na Mukwava kwa sababu anaamini yeye ndiye aliyetakiwa kurithi kiti kile cha ufalme. Anafanya kosa la uhaini la kutaka kumuondoa Mukwava madarakani, ananyongwa.

Migogoro ya kiuchumi

Mgogoro mkubwa unaibuka baina ya Wamasai na Wahehe, Wamasai wanavamia uhehe na kuiba ng’ombe kwa madai kuwa ng’ombe wote duniani ni wa kwao wao wamasai kwani wamepewa na mungu wao Ngai. Wahehe wanapigana vita kwa ustadi na kufanikiwa kuwashinda wahehe.

Wajerumani wanataka kumiliki rasilimali za uhehe. Hawataki Mukwava atoze kodi katika eneo lake, wanataka waumiliki uchumi wote wa uhehe, vita kubwa ya upinzani inaibuka.

Migogoro ya kitamaduni

Wazungu wanawalazimisha Wahehe waanze kufuata tamaduni za kigeni ikiwemo dini ya kikristo.

Musatima aliyekuwa mzee wa ukoo tena anayeheshimika, anapoingia katika dini ya ukristo anaanza kumuita baba, Padre kutoka Ujerumani.

Musatima anachanganywa na tamaduni za wazungu, anaambiwa ili kumfuata kristo ni lazima amwache mke wake mmoja!

Musatima anashindwa tamaduni hizi na ukatili wa wazungu nao unamkasirisha hasa kuhusu namna wanavyofanya mauaji ya watu mbalimbali. Anaamua kutoroka, lakini haondoki hivihivi, anamshushia kipigo Padre na kuondoka zake kurudi kuendelea na tamaduni zake za Kiafrika.

Migogoro ya wahusika

- Mubogamasoli na Mukwava

Mubogamasoli anamchukia Mukwava, anaamini kuwa kiukoo yeye ndiye aliyestahili kukalia kiti kile ambacho kiliporwa na Munyigumba, baba yake Mukwava.

Mubogamasoli anafanya kosa la uhaini kwa kupanga njama ya kumpindua Mukwava, anauawa kwa kosa hilo.

- Mubogamasoli na Mutage

Mubogamasoli hataki kutawaliwa na mwanamke, anakasirishwa na Mutage kuwa jemedari wa vita. Anasusia kwenda vitani.

- Musatima na Kasisi

Musatima anakasirishwa na taarifa anayopewa na Kasisi kuwa wao wakoloni na Kasisi wameshiriki katika kumnyonga Mupangile. Kasisi anaeleza kwamba, wanaona Musatima anafaa kufanya kazi ya kuwa chifu wa Wahehe akichukua nafasi ya Mupangile. Musatima anakasirishwa na habari za kifo cha ndugu yake, anampiga Kasisi na kutoroka.

- Musatima na Mukwava

Baada ya ndugu yake Musatima kuuliwa na Mukwava kwa sababu ya makosa ya uhaini, Musatima anaapa kulipa kisasi, anakimbilia kwa Wajerumani na kuwapa siri zinazowezesha Uhehe ivamiwe na kutekwa.

Musatima anatambua makosa yake hasa baada ya Wadachi kumuua ndugu yake mwingine, anarudi kwa Mukwava na kumuomba msamaha, Mukwava anamsamehe.

Falsafa

Mwandishi anaamini kuwa umoja ni nguvu. Msisitizo mkubwa unawekwa katika umoja na kushirikiana. Jamii za Kiafrika zilitakiwa ziungane pamoja ili kupambana na uvamizi wa wakoloni. Hata hivyo jamii hizi zilipigana pwekepweke hali iliyozifanya zitawaliwe zote.

Msimamo/mtazamo

Mwandishi anamsimamo wa kimapinduzi. Anaamini katika umoja. Watu wakiungana pamoja huwa na nguvu na huweza kutumika kama kinga ya kumshinda adui. Wenye nguvu wote wanaungana duniani. Marekani, Uingereza na mataifa mengi makubwa, yaliungana kwanza ndipo yakafika huko yalikofika.

Fani

Upande wa fani umejadiliwa vyema:

Wahusika

- Mukwava

Ni kiongozi wa Wahehe anayepinga uvamizi wa Wajerumani.

Ni mzalendo kwa nchi yake kwani anakataa kuwauza kwa mtu mweupe.

Ana upendo kwa watu wake, anamshauri mlinzi wake Mwangimba aende akaoe baada ya kuona hatari ya kufia vitani.

- Mwakiyombwe

Msemaji wa mtwa.

Ana asili ya kisangu

Hapendi vita

Anauawa na wajerumani kwa kupigwa risasi

- Mutage

Dada yake Mukwava

Jemedari wa vita

Ni mwanamke jasiri

- Mupangile

Ndugu yake Mukwava

Anakamatwa na wajerumani na kutakiwa awe chifu wa Wahehe.

Wajerumani wanamnyonga baada ya kugundua anapeleka siri zao kwa Mukwava

- Ngosingosi

Mkwe wa Mukwava

Jemedari wa vita

Anakufa kishujaa vitani

- Sekulanga

Jemedari mwingine wa kike ndani ya jeshi la Wahehe

Ni jasiri

- Musatima

Ni msaliti. Anakimbilia kwa Wadachi na kuwaeleza siri zote juu ya namna ya kuvamia Uhehe.

Ni mtu anayekubali makosa yake. Anarudi nyumbani na kuomba msamaha akikiri wazi kuwa alikosea.

- Mubogamasoli

Ni kaka yake Musatima

Ni msaliti kwa nchi yake

Anaamini alitakiwa yeye awe mfalme badala ya Mukwava

Anakataa kuongoza na mwanamke

- Semusilamugunda

Mke wa kwanza wa Mukwava

Hapendi vita

Anamshauri Mukwava ashirikiane na Wajerumani ili kuepusha vita

- Muganga

Mke mdogo wa Mukwava

Hajui madhara ya vita hivyo anavishabikia

- Nyundo (Von Zelewsk)

Kiongozi wa jeshi la Wajerumani lililomvamia Mukwava

Anawadharau Waafrika

Anauawa vitani kwa aibu

- Kasisi

Anaeneza ushirikina wa kigeni. Musatima anashirikiana naye katika kuutangaza na kuueneza, Musatima anapokutana na Mukwava, anaelezwa ukweli wake,

“Ulishirikiana na wahubiri wa dini na mila za kigeni na kuwasaidia kuwakamata kwa nguvu watu wangu. Pia, uliwafundisha kuwadharua mahoka na miungu wao wa jadi na kufuata ushirikina wa kigeni,” uk 146.

Anatumika kueneza ukoloni.

Anaunga mkono kunyongwa kwa Waafrika.

- Kaufmann

Bepari la kijerumani

Anawaza pesa muda wote

Ni mnyonyaji

- Gavana

Kiongozi wa serikali ya kikoloni

Haamini kama Wajerumani wamepigwa na Wahehe

Anaagiza uchunguzi ufanyike kama Nyundo (Von Zelewsk) na Merkl ni Wajerumani.

- Mwamusambwa

Askari shujaa wa Kihehe

Mke wake anaitwa Selugila

Ni mzalendo kwa nchi yake

- Mwachusi

Ni mzee wa baraza

Amepigana vita vingi

Anahamasisha umoja

- Mtumwa

Mtumwa wa Mubogamasoli

Siyo mhehe lakini anakataa kuwasaliti wahehe kwa sababu ni weusi kama yeye.

- Sajini Merkl

Askari wa kijerumani

Anatoroka vita baada ya kuzidiwa na wahehe

- Mwanamke

Shujaa. Baada ya mume wake kufa vitani, anachukua nafasi yake.

- Sakarani

Mjerumani katili

Anawadharau Waafrika na Afrika anaiita ‘ushenzini’

Ni malaya na mbakaji

Mandhari

Tamthiliya hii imetumia mandhari halisi. Matukio yanatendeka katika maeneo halisi, baadhi ya maeneo yanayotajwa ni:

Dar es Salaam

Ugogo

Image

Iringa (Uhehe)

Porini

Ofisini

Nyumbani

Kanisani

Shambani

Uwanjani katika tambiko la mahoka na miungu ya Kiafrika

Juu ya Kidunda (kilima)

Mtindo

Tamthiliya hii imetumia mtindo wa aina mbalimbali mojawapo ni:

Mtindo wa dayolojia. Tunaona majibishano yakitawala mwanzo mpaka mwisho mwa tamthiliya.

Mtindo wa monolojia. Kwa uchache masimulizi yanatumika hasa katika kuelekeza kile kinachotendeka jukwaani.

Mtindo wa nyimbo: tunamuona kasisi akiimba wimbo wa Askari wa yesu nendeni vitani.

Wahehe nao wanaimba wimbo wa vita,

“Nyika aa nyika,

Nyika a kuvayinga,

Nyika…”

Katika tamthiliya hii, matumizi ya nafsi zote yameonekana, hata hivyo, nafasi ya pili imetawala.

Muundo

Tamthiliya hii imetumia muundo wa moja kwa moja. Inaanza kwa kuonyesha wahehe wakishinda vita dhidi ya wamasai, kisha wanavamiwa kwa mara ya kwanza na Wajerumani ambapo Wahehe wanashinda, halafu inafuatia uvamizi wa pili wa Wajerumani ambapo ngome ya uhehe inaanguka.

Pia, tamthiliya hii ina jumla ya vitendo viwili: kitendo cha kwanza kina maonyesho sita na kitendo cha pili kina maonyesho manne.

Matumizi ya lugha

Matumizi ya lugha yanajadiliwa kupitia vipengele vyake mbalimbali:

Tamathali za semi

- Tashihisi

“Magoma yanazidi kuchaga kwa msisitizo na kwa kiburi bila hofu bila wasiwasi.”

- Mubaalagha

“Yumkini katika maisha yake hajapata kununa,” uk 2.

- Tashibiha

“Sauti yake inakata anga kama ngurumo,” uk 2

“Mpana kama dunia.”

“Waoga kama viroboto.”

“(pua)… ilikuwa ndefu kama jino la ngiri.”

- Sitiari

“Kimya, mbwa we!”

“Ngome hii ni mwamba.”

- Mubaalagha

“Hakuna bunduki duniani iwezayo kupenya.”

- Takriri

“Ligombo langu! Ligombo langu!”

- Kuchanganya lugha

Matumizi ya lugha ya kihehe, kama ‘kamwene’ na matumizi ya lugha ya kifaransa kama ‘Guten morgen’ na maneno ya kilatini kama ‘emmite spritum tuum’.

Misemo

“Daima mhehe ni mshindi,” uk 8.

“Hata miti huweza kuwa na masikio.”

“Usimwone simba kalala ukamdhania paka.”

“Kufia nchi ni fahari.”

“Adui unayepgana naye ndani ya nyumba yako ni hatari zaidi kuliko audi mnayepambana kiungani,” uk 73.

Kumpa adui kidoso vitani ni mwiko.”

Methali

“Ukuni mmoja hauwaki mekoni.”

“Jifya moja haliinjiki chungu.”

“Akutanguliaye chanoni hukuzidi tonge.”

“Machozi hayayeyushi chuma.”

“Mauti ni bora kuliko utumwa.”

“Mvi huona mbali.”

“Kwa muoga huenda kicheko na kwa shujaa huenda kilio.”

“Mtungi hauwi mwamba kwa kujidai umwamba.”

“Mwenziyo akinyolewa wewe tia maji.”

“Kufa kufaana.”

“Mjumbe hauawi.”

Taswira

Buibui-mwanamke

Maoni ya mhakiki

Tamthiliya ya Mukwava wa uhehe ni tamthiliya bora inayofaa kusomwa.

Katika maudhui, mwandishi amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuibua umuhimu wa uzalendo. Uzalendo bado unahitajika katika nchi zetu ili tuweze sasa kupambana na ukoloni mamboleo. Bila uzalendo viongozi wetu wataishia kuwa vibaraka wanaotumika na wazungu kuwanyonya ndugu zao Waafrika.

Mwandishi hakuandika tu bila uchunguzi, Mulokozi alifanya utafiti ndiyo sababu kazi yake imeshiba utamaduni wa kihehe. Ndani ya tamthiliya hii tunayaona matumizi ya Kijerumani, Kilatini, na Kihehe. Anataja majina kama yanavyotajwa na wenyeji na si majina yaliyoandikwa na wageni. Badala ya Wahehe, anataja Vahehe, badala ya Ruaha anataja Ruvaha na badala ya Mkwawa, anataja Mukwava.

Mwandishi amefaulu kwa kiwango kikubwa sana kuelimisha Waafrika kuhusu imani zao. Anawakumbusha kwamba, hizi imani mpya ni ushirikina wa kigeni. Imani zetu zilikuwepo, nao ni mahoka na mababu. Mulokozi haandiki kitu asichokiishi. Katika maisha yake halisi, mtu huyu haamini katika dini za kizungu, aliyakataa majina ya kigeni na akabakia Mugyabuso Mlinzi Mulokozi.

Changamoto ni sehemu ya maisha ya shujaa yoyote. Mulokozi amekwenda kinyume na utamaduni wa Mtanzania, hajatumia tafsida pale inapotakiwa kuwekwa, katumia lugha kali inayotisha na kuwafokea wasomaji, katika ukurasa wa 20, anatumia maneno makali, “Penye uyoga hapakosi mavi.” Hii ni lugha kali ambayo ingeweza kufichwa na tafsida!

Upande mwingine tunaona kuwa, mkasa umeegemea katika uhalisia wa historia ya kweli ya shujaa Mukwava, hata hivyo, Mulokozi ameonekana akitia chumvi katika matukio kadhaa. Jambo hili linawachanganya wasomaji, kwanza hawaelewi ni wapi hasa katia chumvi na wapi ni maelezo ya kweli.

Mukwava wa uhehe itabakia kuwa tamthiliya ya aina yake inayomtukuza Mwafrika, na kuyaonyesha mapungufu ya mzungu na tamaduni zake.

Wasiliana na Mwalimu ili Kujiunga Darasa la Uhakiki wa Vitabu vyote vya Fasihi Mtaala Mpya kwa Kugusa Hapa

Popular posts from this blog

SMS 20 za Mahaba Makali Kumtumia Mpenzi Wako

SMS 20 za Vichekesho Zinazochekesha Sana

Uhakiki wa Tamthiliya ya Kilio Chetu