Uhakiki wa Riwaya ya Wasifu wa Siti binti Saad

ganda la kitabu cha wasifu wa Siti binti Saad likiwa na picha ya Shaaban Robert
Wasiliana na Mwalimu ili Kujiunga Darasa la Uhakiki wa Vitabu vyote vya Fasihi Mtaala Mpya kwa Kugusa Hapa

Mwandishi: Shaaban Robert

Mhakiki: Mwalimu Makoba

Utangulizi

Wasifu wa Siti binti Saad ni riwaya inayozungumzia maisha ya Siti, mwanamke aliyeutangaza mziki wa taarabu duniani kote.

Wasifu ni riwaya ambayo huandikwa na mwandishi mwingine akisimulia maisha ya mtu fulani. Maisha ya Siti yamesimuliwa vyema na Shaaban Robert, mwandishi mahiri wa wakati wote.

Shaaban Robert hakusimuliwa maneno aliyoyaandika na Siti mwenyewe, aliipata historia hii kwa kutafuta huku na huko. Wakati Shaaban Robert alipotembelea Zanzibar, alionana na Siti, lakini hawakuweza kuzungumza sana hasa kwa sababu Siti alikuwa mgonjwa, haukupita muda Siti alifariki mnamo mwaka 1950. hili halikumzuia Shaaban Robert kuiandika historia ya Siti, aliiiandika kupitia vyanzo alivyovijua yeye mwenyewe, habari nyingi zikiwa za kweli, lakini kama ilivyo kawaida ya waandishi wengi, Shaaban katia chumvi kidogo.

Simulizi kwa ufupi

Siti binti Saad alizaliwa na wazazi masikini. Baba mkulima na mama mfinyazi wa vyungu. Kama hiyo haitoshi, Siti alikuwa na sura mbaya!

Siti hakukatishwa tamaa na historia yake, aliamua kwenda mjini kutafuta maisha. Huko watu walikitambua kipaji chake, ni kweli alinyimwa sura ya kuvutia, lakini alipewa sauti tamu ajabu iliyowalewesha wote waliomsikiliza.

Hakuchukua muda kuanza kuimba mziki wa Taarabu huko mjini Unguja. Hapo umaarufu wake ukapaa, akafikia hatua ya kuchukuliwa na kampuni kubwa la Kolombia, akafahamika duniani kote.

Siti alizunguka nchi nyingi akiimba mziki, aliitangaza nchi yake kila kona, uwezo wake wa kuimba, kama asingekuwa namba moja Afrika, basi angekuwa namba mbili.

Mwisho Shaaban Robert anatueleza kwamba, Siti alijaliwa vyote, tabia njema, sauti nzuri na uvumilivu.

Riwaya hii inaeleza kwamba, yeyote anaweza kuwa chochote. Siti muuza vyungu, alipanda hadhi mpaka kusafiri nchi nyingi duniani, akigombewa na matajiri na masultani!

Usikate tamaa!

Maudhui

Vipengele mbalimbali vya maudhui vinajadiliwa:

Dhamira

Umasikini

Familia ya Siti ilikuwa duni, baba mkulima na mama mfinyazi. Namna walivyoendesha maisha yao ilikuwa ni kwa kudra na bahati nasibu tu.

Siti mwenyewe alikuwa masikini wa kutupwa. Alivaaa kaniki mbili tu. Pia hakuwa na viatu vya kuvaa miguuni, alitembea pekupeku umbali mrefu sana.

Siti alifanya kazi ya kuuza vyungu, kazi hii haikumpa faida kubwa. Kuna wakati alijikwaa, vyungu vyote vikamwagika akarudia nyumbani akilia.

Ndoa

Tunamuona Siti akifanikiwa kuolewa na Rajabu. Pamoja na kuwa na sura mbaya, Siti aliolewa. Katika jamii yake, wanawake wenye sura nzuri ndiyo walioolewa zaidi, lakini Siti alipata bahati ya kuolewa bila kujali sana muonekano wake.

Unyonyaji

Makampuni ya santuli yalipata faida nyingi kuliko aliyopata Siti. Suala hili linaangazia unyonyaji mkubwa wanaofanyiwa wasanii katika mataifa mbalimbali. Makampuni hujipatia faida kubwa, huku wasanii wakijipatia kiasi kidogo. Hata hivyo, hilo halikuwa tatizo kwa siti. Yeye hakuimba ili apate fedhaf, alipenda zaidi kuwafurahisha watu, alitanguliza utu mbele.

Ucheshi

Siti alikuwa na sauti tamu. Wakati mmoja alipokuwa akiimba mbele ya mtambo wa sauti kule Bombay, mmoja katika wenziwe alishikwa na majadi kwa sauti yake tamu akatamka ghafla, “Polepole, tuko mbali!”

Shaaban Robert ameweka kisa hiki kikiakisi ucheshi uliotokea wakati Siti akirekodi huko India. Siti alikuwa na sauti ambayo haikupata kusikika mahali pengine.

Uvumilivu

Siti alikuwa mvumilivu. Aliimba usiku na mchana bila kujali alipewa fedha kiasi gani, furaha yake ilikuwa kuwafurahisha watu.

Siti alisafiri kwenda mbali, kila mahali alifika bila kuchoka, hakuwahi kulalamika wala kukataa kuimba kwa sababu hakupewa malipo yake.

Japo makampuni makubwa ya kimataifa kama Kolombia yalinufaika mara elfu moja zaidi kumshinda yeye, hilo halikumsumbua, aliendelea kuimba na kuutangaza zaidi utamaduni na muziki duniani kote.

Tabia njema

Siti alikuwa mwanamke mwenye tabia njema. Alikuwa mtu wa ulimwengu, lakini alikuwa mtu wa ibada. Kamwe hakutaka kujidhalilisha ili apate fedha, yeye aliimba pekee khuku akilinda maadili yake.

Wasanii wa kizazi cha sasa hususani wenye jinsia ya kike, walio wengi hujikuta wakijiingiza katika tabia zisizofaa ikiwemo kuvaa nusu utupu, kuongea lugha mbaya za matusi na kujiuza kwa matajiri ili wapate fedha. Kwa siti hilo halikuwezekana, ilikuw ajabu mwimbaji kama yeye kushikilia maadili.

Busara

Siti binti Saad aliondokea kuwa mwanamke mwenye busara nyingi japo hakusoma. Akiwa katika kilele cha umaarufu wake, wakorofi fulani walimuonea wivu, wakatunga nyimbo zilizomkashifu. Nyimbo hizo zilimzihaki kwa kutoka kwake shamba, masikini wa kutupwa na ile sura yake mbaya!

Kinyume na wengi walivyotarajia, Siti hakuwajibu vibaya, aliwajibu kwa busara pale aliposikika akiimba katika moja ya kibao chake, “Hasara kubwa ni kukosa akili!”

Suala la elimu

Wazazi wake Siti hawakwenda shule, hawakujua kusoma wala kuandika.

Wazazi hawa, hawakujua hata tarehe aliyozaliwa mtoto wao. Miaka ya Siti ilipata kukadiliwa tu.

Naye Siti hakwenda shule, hakujua kusoma wala kuandika. Ile busara yake na matendo yake ilikuwa miujiza tu.

Japo hakwenda shule, alikuwa na kipaji kikubwa cha kukariri. Alikariri nyimbo ndefu kwa muda mfupi sana. Endapo Siti angeenda shule, angekuwa zaidi ya pale alipokuwa.

Matumizi ya fedha

Siti hakuwa na matumizi mazuri ya fedha. Alikuwa na matumizi makubwa. Japo alifanikiwa kununua nyumba mbili, kwa matumizi yake makubwa, alikuwa masikini siku zote.

Nafasi ya mwanamke katika jamii

Mwanamke amechorwa katika namna mbalimbali kama inavyoelezwa:

Mwanamapinduzi

Siti ni mwanamapinduzi. Wakati wanawake wengi wakitawishwa ili kuwatumikia waume zao pekee, yeye alikataa kukaa ndani. Alitoka nje akafanya kazi ya muziki, na kuwashangaza watu namna alivyopata umaarufu na mafanikio makubwa bila kujali jinsia yake.

Ana bidii ya kazi

Siti ni mwanamke aliyekuwa na bidii kubwa ya kazi. Kutokana na bidii yake, japo aliondoka kijijini akiwa na kaniki mbili bila viatu miguuni, alifanikiwa!

Hana elimu

Siti hakujua kusoma na kuandika. Endapo angefanikiwa kupata elimu, angepaa zaidi ya pale alipokuwa.

Ana matumizi mabaya ya fedha

Japo alifanikiwa sana katika kazi yake ya muziki, Siti alikuwa na matumizi makubwa, matumizi haya yalimfanya awe masikini siku zote. Hata hivyo, alifanikiwa kununua nyumba mbili.

Ujumbe

Tunapata mafunzo mbalimbali, miongoni mwa mafunzo hayo ni:

Tufanye kazi kwa bidii

Mafanikio ya Siti yalikuja kwa sababu alifanya kazi kwa bidii. Aliimba na kusafiri bila kuchoka.

Wanawake wapewe nafasi za kufanya kazi za maendeleo

Tuachane na tamaduni zinazowaweka wanawake ndani, badala yake waruhusiwe kutoka kwenda kufanya kazi.

Elimu ya fedha itolewe kwa watu wote

Siti alikuwa masikini siku zote kwa sababu alikosa elimu ya fedha. Alikuwa na matumizi makubwa yaliyomfanya atafute hela siku zote. Endapo angepewa elimu ya fedha, huenda leo hii kungekuwa na makampuni ya muziki wake ambayo yangefanya kazi ya kuwasaidia wanamuziki wengine.

Yeyote anaweza kufanikiwa

Mtu yeyote akiamua kufanikiwa na akatia bidii katika jambo hilo, anaweza kufanikiwa.

Siti aliyekuwa muuza vyungu, asiyejua kusoma wala kuandika, aliondoka kijijini akiwa na kaniki mbili bila viatu miguuni, lakini alifanikiwa kiasi cha kuchukuliwa na kampuni kubwa la Kolombia. Kwa kipaji chake, aliwatingisha wazungu, wakaiona biashara ndani yake, nao wakamtumia sana kujipati fedha nyingi.

Migogoro

Migogoro mbalimbali imejitokeza:

Mgogoro wa Siti na Kikundi kingine cha taarab: kikundi hiki kilimwandama Siti kwa sababu ya historia yake ya umasikini, walimuimba katika nyimbo zao kwa kejeli. Hata hivo, Siti hakujali maneno yao aliendelea na kazi.

Mgogoro kati ya Siti na nafsi yake, Licha ya kujariwa ujuzi wa ususi, kushona na kufinyanga vyungu, Siti kuna jambo lingine alilokuwa analiwaza lililomfanya aliwaze, aliote mchana na usiku bila ya kupata majibu na mwisho wa siku akaamua kuhama kijijini kwao na kwenda unguja kwa madhumuni ya kuanza Maisha mapya. Mathalani katika (uk 7) mwandishi anasema;

“Alikuwa hana starehe kwa sababu mambo mawili haya, yalikuwa yakipingana katika moyo wake wakati wote. Alikuwa hana mshauri wa kushiriki naye siri kama ile.”

Falsafa

Mwandishi anaamini kuwa, tabia njema huleta mafanikio. Siti alifika pale alipo kwa sababu ya tabia yake njema. Mwandishi ameielezea tabia njema ya Siti na kutuonyesha kwamba, hapakuwa na mtu mwenye tabia njema kumshinda Siti. Mwandishi anadokeza kwamba, walikuwepo waliomzidi Siti kwa kuimba, lakini hawakufika mbali kwa sababu walikosa tabia njema.

Pia, mwandishi anaamini kuwa wema huushinda ubaya. Tunamuona Siti akiandamwa na watu wabaya wakimsema kwa kejeli. Lakini anashinda kwa sababu alikuwa mwema tena aliyejaaliwa kipaji kikubwa cha kuimba.

Msimamo/mtazamo

Mwandishi ana msimamo wa kidhanifu. Japo tabia njema huweza kuleta mafanikio, si mara zote unaweza kufanikiwa kwa sababu ya tabia yako njema. Wapo wanamuziki waliofanikiwa lakini tabia zao ni mbaya japo hii huweza kutokea kwa nadra. Dunia sasa inakubaliana kwamba, mtu anapokuwa na kipaji kikubwa, upo uwezekano wa watu kuvumilia tabia yake mbaya ili tu aweze kufanikisha malengo yao.

Pia, wema kuushinda ubaya nayo imekaa kidhanifu tu. Yapo mazingira ambayo ubaya uliushinda wema. Wapo watu wema wengi walioangushwa na watu wabaya. Tazama mfano wa marais waliokuwa na upendo kwa wananchi wao ambao waliuawa na watu wabaya, huu ni mfano mmoja katika mifano mingi ya ubaya kuushinda wema. Hata hivyo, ni vyema kutenda wema kwani nafasi ya wema kuushinda ubaya ni kubwa zaidi kuliko nafasi ya ubaya kuushinda wema japo lolote linaweza kutokea.

Fani

Vipengele mbalimbali vya fani vinajadiliwa:

Wahusika

Wahusika mbalimbali wamejitokeza wakiwamo:

- Siti binti Saad

Mwimbaji wa taarab

Alikuwa mwenye tabia njema

Hakukatishwa tamaa na umasikini wake

Alikuwa na paka wawili walioitwa Kiote na Chanjia

- Musa na Mbaruku

Kaka zake Siti.

- Masika

Dada yake Siti.

- Rajabu

Mume wake Siti

- Ali Saudi

Mtu wa kwanza kumpokea Siti na kukaa naye nyumbani kwake alipokuwa safarini kuelekea Unguja.

- Musa Bulushi

Mtu aliyeondoka na Siti kuelekea Unguja.

- Muhsini Ali

Mpiga udi mahiri

Alimfundisha Siti kiarabu na kuimba

- Subeti Ambani

Mpiga udi

- Buda Swedi

Mpiga gambusi

- Mwalimu Shaaban

Mpiga tari

Mhusika mwingine ni Mbaruku.

Mtindo

Mwandishi ametumia mtindo wa masimulizi.

Pia, ametumia mtindo wa dayolojia.

Nao mtindo wa ushairi umetumika, mwandishi anamsifia Siti kwa shairi tamu,

“Alikuwa kinanda,

Afrika Mashariki,

Na watu wakampenda…”

Matumizi ya nyimbo

Nyimbo mbalimbali zimeonekana, mfano mmojawapo ni wimbo huu:

“siri sifunue,

Wino wa rangi,

Fahamu ujue,

Kuna mambo mengi,

Wajila mwenyewe,

Kwa ujinga mwingi.”

Katika usimuliaji, nafsi ya tatu imetawala.

Mandhari

Riwaya hii imetumia mandhari halisi. Mandhari haya yanathibitishwa kwa kutajwa miji halisi kama: Fumba, unguja na Bombay India.

Mandhari mengine ni:

Mandhari ya ukumbini alipokuwa akiimba Siti.

Mandhari ya studio.

Mandhari ya nyumbani.

Muundo

Riwaya hii imetumia muundo wa moja kwa moja. Anaanza kwa kutuonesha Siti akiwa mtoto masikini kijijini, anaamua kwenda mjini kutafuta maisha na hatimaye anafanikiwa kuwa mwimbaji mkubwa wa taarab aliyesifika pande zote za dunia.

Matumizi ya lugha

Tamathali za semi na mbinu nyingine za kisanaa

- Takriri

Vyungu vizuri, vyungu vizuri…

- Tashibiha

Jasho lilimiminika kama maji mwilini mwake.

Jina lake lilianza kuvuma kama ngoma katika hewa.

Yalikuwa safi kama yungiyungi.

Akaimba mchana na usiku kama kurumbizi.

- Mubaalagha

Furaha isiyoelezeka kwa ulimi wala kalamu.

Siti alikuwa na sauti ya kulevya.

- Tashihisi

Sauti ya Siti ilipenya sikioni ikatekenya mwili na kila mtu kwa ladha yake.

- Lugha kali

Siti alikuwa hana nafsi sasa ya kuweka tako lake kitini.

- Mjalizo

Hawakubuni neno, hawakusheheni neno, hawakujaribu neno.

- Tabaini

Tanakuzi (au tabaini) ni mbinu ya kifasihi inayotumia maneno mawili au zaidi yanayokinzana kwa maana, lakini yanapowekwa pamoja hutoa wazo la kina au la kuvutia. Mbinu hii hutumika kuonyesha hali tata, hisia mchanganyiko, au ukweli wenye utata wa maisha, kwa njia ya kisanii. Katika riwaya, tabaini hii imetumika,

“Ilikuwa zuio au pingamizi, jeuri au kiburi, udanganyifu au ugomvi, ushenzi au utovu hayo yote yalipingwa.”

Misemo

Chema kilijiuza, kibaya kilijitembeza.

Methali

Asiyeweza kuumba, kutuumbua hawezi.

Cheka uchafu, usicheke kilema.

Ukikosa uta na mshale hufumi kilicho mbele.

Maoni ya mhakiki kuhusu kufaulu au kutofaulu

Shaaban Robert ni mwandishi mahiri, haya ni maisha halisi ya Siti binti Saad, Shaaban Robert amefaulu vyema kuisimulia historia ya mwimbaji huyu mahiri. Amesaidia sana kutunza kumbukumbu za mwanamuziki huyu nguli.

Mwandishi amefaulu kuibua maudhui mbalimbali ikiwemo kuhamasisha watu kuwa na adabu njema na kufanya kazi kwa bidii. Wasifu wa Siti unatukumbusha kuwa, tusikate tamaa, mafanikio huja penye uvumilivu, bidii ya kazi na adabu njema.

Upande wa fani mwandishi amefaulu kutumia lugha vizuri, Kiswahili cha Shaaban Robert kimekomaa, kimenyooka na kinaongeza msamiati kwa wasomaji.

Kazi hii ina tamathali nyingi za semi, methali na nahau.

Hata hivyo yapo maeneo ambayo mwandishi hajafaulu. Hii ni simulizi ya maisha halisi ya Siti, hata hivyo mwandishi kampamba Siti kwa kutia chumvi nyingi. Adabu anayotajwa kuwa nayo Siti, sauti yake, vinamfanya Siti awe kama hakuwa mtu wa kawaida, hili linawaacha wasomaji vinywa wazi wakiwaza kama yanayosemwa ni kweli ama porojo za Shaaban Robert.

Hakuna mwanadamu asiyekuwa na mapungufu. Shaaban kaeleza makamilifu mengi ya Siti huku akidokeza pungufu moja tu, kwamba, Siti hakuwa mtumiaji mzuri wa fedha.

Kwa kuhitimisha, mwandishi Shaaban Robert alifanya kazi nzuri sana kuandika Wasifu wa Siti. Waandishi wengi waliokuja kuandika maisha ya Siti, waliusoma kwanza wasifu ulioandikwa na Shaaban Robert.

Wasiliana na Mwalimu ili Kujiunga Darasa la Uhakiki wa Vitabu vyote vya Fasihi Mtaala Mpya kwa Kugusa Hapa

Popular posts from this blog

Uhakiki wa Riwaya ya Watoto wa Maman’tilie

SMS 20 za Vichekesho Zinazochekesha Sana

Uhakiki wa Tamthiliya ya Ngoswe Penzi Kitovu cha Uzembe