Roma na Stamina Katika Upumbavu wa Kimkakati| Makala za Mwalimu

Roma na Stamina Katika Upumbavu wa Kimkakati| Makala za Mwalimu
Upumbavu wa kimkakati, ni kutumia busara ulizonazo kuupandisha juu upumbavu, ukasikika na kusifiwa kila pahala na kila mtu isipokuwa sisi!
Msanii yeyote atakaye kuifanya kazi yake kwa misingi na weledi, hana budi kuwa na falsafa moja inayoeleweka. Roma alianza akiwa na falsafa moja tu, kulisema tabaka lisilopenda kusemwa. Hata hivyo, mwishoni alianza kubadilika na nilishangaa lakini niliamini niliposikia wimbo wake uitwao ‘k’ ajabu ya mwaka ule!
Baada ya kutekwa, mambo yamebadilika zaidi! Naona sasa ule msemo wake wa “nawaachaje wanaobaki” unafanya kazi kwa kasi.
Akishirikiana na msanii mwenzake-Stamina, ametoa wimbo uitwao ‘Kiba_100’. Wakati lengo la Muziki likiwa kuburudisha, kuelimisha na kuonya, wimbo huu unalengo la peke yake! Kusambaza matusi kwa njia ya kificho. UPUMBAVU!
Ni aibu kusikiliza wimbo huu ukiwa na watu wanaokuzidi umri. Ni aibu pia, kuusikiliza pembezoni mwa watu mnaoheshimiana sana. Na itaendelea kuwa aibu kuusikiliza katika kundi la watoto wadogo! Kama ilivyo kwa ujinga kuvuma kwa kasi, wimbo huu unasikika kila kona bila kujali uchafuzi wake wa hali ya hewa.
Sijui wazazi na ndugu za mke wa Roma wanajisikiaje wanaposikia wimbo huu. Kwa kuwa muziki ni hisia, mara nyingi wanamuziki huimba yale wayafanyayo katika maisha yao halisi. Huenda kilichoimbwa ni mwigo wa maisha ya vijana hawa! Kama ni kweli, basi dunia ingali ukingoni na inakwenda kasi.
Miongoni mwa maneno ya hovyo, yaliyofichwa katika kile kiitwacho tafsida ni: usisite kunipa jicho, walishika fimbo na kuipakapaka mate, chumvini nitazama sana, zidisha utundu ninyonye mpaka…, nipe nichane nyuzi… na mengine mengi!
Swali muhimu zaidi ni kwamba, ni lipi hasa lengo la wimbo huu?

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2023

Uhakiki wa Riwaya ya Watoto wa Maman’tilie