Uhakiki wa Tamthiliya ya Usaliti Mjini

ganda la mbele la tamthiliya ya usaliti mjini
Wasiliana na Mwalimu ili Kujiunga Darasa la Uhakiki wa Vitabu vyote vya Fasihi Mtaala Mpya kwa Kugusa Hapa

Mwandishi: Francis Imbuga

Mwaka: 1976

Mhakiki: Mwalimu Makoba

Simulizi kwa Ufupi

Tamthiliya hii inahusu harakati za wanajamii kupigania haki ikiwamo kupambana na uongozi mbaya uliokithiri.

Wanafunzi wanafanya maandamano kupinga uongozi mbaya, katika maandamano hayo wanafunzi wengi wanauawa, miongoni mwao ni Adika.

 

Adika ana ndugu yake anayebaki hai, naye anaitwa Jaspa Wendo, mwanafunzi wa chuo kikuu.

Mauaji haya yanafanyika kwa sababu ya uongozi mbaya wa Bosi, kiongozi wa Kafira.

Bosi ambaye ndiye kiongozi mkuu, anashauriwa na binamu yake aitwaye Mulili. Uongozi wote mbaya, mshauri mkuu ni Mlili.

Mwisho tunaona igizo likiandaliwa ili kutoa burudani. Waigizaji wanachaguliwa, miongoni mwao ni Jaspa Wendo. Mwingine ni Mosese, mhadhiri wa chuo kikuu aliyefungwa kwa kupinga maovu ya serikali.

Katika igizo hilo, mwigizaji mmoja hakutokea, Bosi anachukua nafasi yake.

Wanapopanda jukwaani ili kuigiza, zinatakiwa silaha, tamthiliya inayoigizwa ni ya kivita. Bosi anaagiza walinzi wake walete silaha halisi. Jaspa na Mosese wanashika silaha halisi. Jaspa amepoteza ndugu yake, Jaspa anaposhika silaha, anampiga risasi Mulili kwa sababu Mulili ndiyo chanzo cha matatizo yote, ushauri wa Mulili kwa Bosi ni mbaya.

Jaspa anamuua Mulili na kumuacha Bosi akiamini Mulili ndiyo chanzo cha matatizo.

Maudhui

Dhamira

usaliti
watu walitarajia mengi mazuri baada ya uhuru kupatikana. Bosi, Tumbo na Mulili ndiyo wao pekee wanaofurahia matunda ya uhuru. Watu hawa wamewasaliti wenzao waliopigania uhuru.

Kushindwa kutimiza wajibu
viongozi wa serikali wanashindwa kutimiza wajibu wao. Kwa mfano: Kabito anapotoa malalamiko, Mulili anamuongopea Bosi kuwa siyo kweli, Bosi alitakiwa kufanya uchunguzi wa taarifa hiyo,badala yake alimuamini Mulili na kuagiza Kabito anyamazishwe.

Tamaduni
tamthiliya inapongeza tamaduni za Kiafrika. Doga na Nina wanafuata utamaduni wa kutembelea kaburi la mtoto wao aliyeuawa katika maandamano, Adika.

Kupigania haki
watu mbalimbali wanapigania haki kwa kupinga kile kinachofanywa na serikali yao. Wanafunzi wa vyuo vikuu wanaandamana kupinga serikali, Adika na wengine wanauawa.

Nafasi ya mwanamke katika jamii

- Mshauri mzuri. Regina alimshauri vyema Jaspa.

- chombo cha starehe, tunamuona Bosi akijaribu kumbaka Regina.

- Kiumbe duni. Doga anaongea kwa ukali kwa mke wake Nina.

- Mwanamke ameshikilia tamaduni zake. Nina ni mfano wa mwanamke aliyeshikilia tamaduni zake.

Ujumbe

1. Baadaya ukoloni, viongozi waliobaki kuongoza Africa, waligeuka vibaraka waliofanya kazi kwa maslahi ya wakoloni walioondoka, jambo linalojulikana kama ukoloni mamboleo.

2. Bara la Afrika ni masikini kwa sababu ya uongozi mbaya.

3. Ili kuleta ukombozi wa jamii, watu wakatae maovu yote kwa kutumia njia mbalimbali ikiwamo migomo na maandamano.

4. Elimu ni chombo cha ukombozi

Migogoro

Migogoro ya wahusika

Mulili na Kabito
chanzo cha mgogoro ni tenda ya kusambaza maziwa katika Chuo Kikuu cha Kafira. Kabito anahitaji tenda hii lakini anaikosa, badala yake, Bosi anaitoa kwa Mulili.

Jaspa na Chagaga
Jaspa anamuua Chagaga kwa sababu alihusika na mauaji ya ndugu yake aliyeitwa Adika. Kwa sababu hii, Jaspa anakamatwa na kufungwa jela.

Bosi na Regina
Bosi anafanya jaribio la kumbaka Regina.

Mosese na Bosi
Mosese anaikosoa serikali ya Bosi. Mgogoro huu unapelekea Mosese kufungwa.

Fani

Wahusika

Jaspa Wendo

- Mtoto wa Doga.

- Kaka yake Adika aliyeuawa katika maandamano akipigani haki za watu.

- Ni mwanafunzi wa chuo kikuu.

- ana mahusiano na Regina dada yake na Mosese.

- Anaandaa tamthiliya ambayo ndiyo inasababisha kuuliwa kwa Mulili. Ushauri wa Mulili kwa Bosi ulisababisha nchi kukosa haki.

Adika

- Mtoto wa Doga na Nina na ni kaka yake na Jaspa.

- Ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kafira.

- Ni mpigania haki, anaandamana na wanafunzi wenzake.

- Serikali inamuua, anapigwa risasi nne katika kifua chake.

Mulili

- Binamu yake na Bosi

- Mshauri mkuu wa Bosi.

- Ni mjinga wa mambo mengi.

- Ni chanzo cha uongozi mbaya wa Bosi.

Boss

- Kiongozi mkuu wa Kafira.

- Siyo mwajibikaji kwa watu wake.

- Anadanganywa na Mulili.

- Hana maadili, anafanya jaribio la kumbaka Regina

Mosese

- Mhadhiri wa chuo kikuu.

- Ni mfungwa wa kisiasa.

- Katika mazishi ya Adika, aliyataja mabaya ya serikali mbele ya watu waliohudhuria.

- Ni kaka yake na Rejina.

Rejina

- Dada yake na Mosese.

- Anahamasisha mabadiliko Kafira.

Doga

- Baba yake na Jaspa.

- Anashikilia tamaduni.

- Anauliwa na Mulili.

Nina

- Ni mke wa Doga na ni mama yake Jaspa.

- Anashikilia tamaduni.

- Anauliwa na Mulili.

Kabito

- Ni kiongozi wa serikali

- Anauliwa kwa sababu hakubaliani na Mulili.

Tumbo

- Kiongozi wa serikali.

- Anawasaliti watu wake na hawaambii maovu yanayofanywa na serikali.

- Ni miongoni mwa watu wachache wanaokula matunda ya uhuru.

Askari

Askari jela.

- Ni katili. Anawakilisha kundi la watu watiifu kwa serikali ambao ni watiifu kwa sababu ya ujinga wao, watu hawa, hawawezi kufikiri juu ya yale wanayoyatenda kama yako sawa au la.

Matumizi ya Lugha

Tamathali za semi

i) Tashibiha

Ukweli ni kama mbegu…

Anajidai kuwa yeye ni mkubwa kama mlima

ii) sitiari

Kafira imekuwa shimo la giza.

Huyu Mulili ni mbwa mwitu aliyejivika ngozi ya kondoo

iii) Tashihisi

Hata kuta zote zina masikio katika nchi…

iv) Mubaalagha

"Nchi nzima inatetemeka Bosi akikohoa" — Mulili

v) Mdokezo

"Kama nisingekuwa askari... labda nisingefanya jambo lingine..." — Jere

i) Nahau

"Kula keki ya taifa"

"Kushika koo" (Kubana na kuzuia uhuru wa mtu) (28)

"Kukata kamba" (Kufariki dunia)

Misemo

Damu nzito kuliko maji.

Ulizaliwa peke yako, utakufa peke yako.

Setting

Mandhari ya tamthiliya hii yamejikita katika nchi ya kufikirika iitwayo Kafira.

Mandhari mengine yanayojitokeza ni kama mandhari ya barabarani, nyumbani, gerezani na katika jukwaa la kuigizia.

Mtindo

Matumizi ya dayolojia

Matumizi ya monolojia

Muundo

Tamthiliya hii imetumia muundo wa urejeshi, inaanza kwa kutuonyesha kabuli la Adika, halafu inahitimisha kwa kutueleza kilichopelekea kifo chake.

Hitimisho la Mhakiki

Sikuamini nilipoona katika orodha ya vitabu teule, tamthiliya ya Usaliti Mjini nayo imewekwa. Japo tamthiliya hii ni nzuri sana, imeandikwa na mwandishi bora, haikustahili!

Tamthiliya hii haikuandikwa kwanza kwa lugha ya Kiswahili, hii imetafsiriwa kutoka lugha ya Kiingereza, tamthiliya halisi inajulikana kwa jina la Betrayal in the City. Waliofanya tafsiri ya tamthiliya hii wametumia lugha inayofanana na Kiswahili, wametumia Kiswahili kinachokera, kisichostahili kusomwa, nami ninakiri wazi kwamba, wakati ninahakiki tamthiliya hii, niliitupa nakala ile ya Kiswahili, ikabidi nitumie nakala halisi iliyoandikwa kwa lugha ya Kiingereza.

Tazama mfano wa gamba la nyuma ulivyoandikwa, “Usaliti Mjini ni mchezo wa kuigiza unaochambua na kufafanua kwa undani madhila yanayozikumba nchi huru za bara la Afrika ambako watu wengi wanahisi kuwa maisha yao ya usoni hayapo na kama yapo, ni ya ukiwa na upweke baada ya kuharibiwa kupita kiasi cha kurekebishwa. Kwa kadiri ya maneno ya Mosese, mmoja wa wahusika, "Ilikuwa afadhali wakati tulikuwa tukingoja. Sasa hatuna tumaini lolote. Tumeharibu maisha yetu ya awali na sasa tunaendelea kuharibu maisha yetu ya usoni.”

Lugha hiyo inayofanana na Kiswahili, ndiyo iliyotumika katika kitabu kizima!

Vipo vitabu vingi vya tamthiliya vilivyoandikwa kwa lugha ya Kiswahili ambavyo vingewekwa badala ya hiki. Kitabu hiki kingebaki kusomwa katika lugha yake halisi ya kiingereza na kingeachwa katika lugha ya Kiingereza. Makosa haya ya kutumia vitabu vya tafsiri tumeyafanya katika vitabu vya orodha na takadini na hatuoni dalili ya kujifunza, zaidi tunazidi kuharibu.

Tunawapa watoto wetu wasome kitabu kilichoandikwa kwa Kiswahili kibovu kutoka Kenya kwa lengo la kumfurahisha nani?

Wasiliana na Mwalimu ili Kujiunga Darasa la Uhakiki wa Vitabu vyote vya Fasihi Mtaala Mpya kwa Kugusa Hapa

Popular posts from this blog

English Language 1 Form Six Examination 2020 2

Colonial Administrative System | History Form Three

Ubora na Udhaifu wa Uainishaji wa Ngeli za Nomino Kimofolojia