Uhakiki wa Riwaya ya Takadini

UHAKIKI WA RIWAYA YA TAKADINI
RIWAYA: TAKADINI
MWANDISHI: BEN J HANSON
WACHAPISHAJI: METHEWS BOOKSTORE AND STATIONERS
MWAKA: 2004
MHAKIKI: DAUD MAKOBA

Muhtasari wa Riwaya

Takadini ni riwaya inayojaribu kuzungumzia matatizo ya mila na desturi yaliyopo katika jamii za Kiafrika hasa sehemu za vijijini. Mwandishi anamuonyesha mhusika mkuu Takadini aliyezaliwa na ulemavu wa ngozi jinsi anavyotengwa na watoto, watu wazima na jamii yote kwa ujumla. Mwisho tunamuona Takadini akipendwa na msichana Shingai. Pamoja na vikwazo vingi, penzi la Shingai na Takadini halikufa. Baadae Shingai anapata mimba ya Takadini, kisha anajifungua mtoto asiye mlemavu. Hapo wana jamii wanashangazwa na kujikuta wakiamini kuwa hata mlemavu anaweza kuzaa mtoto asiyemlemavu.

Uchambuzi wa Fani na Maudhui

Maudhui Katika Riwaya ya Takadini

Dhamira

Ukombozi wa Kiutamaduni

Utamaduni ni jumla ya maisha ya jamii. Katika jamii ya Zimbabwe watu wenye ulemavu hawakuruhusiwa kuishi, waliuawa kikatili. Ni katika jamii hii pia, watu waliendelea ushikilia mila na desturi zilizokuwa zinamkandamiza mwanamke. Shingai anachaguliwa mume na kulazimishwa kuolewa naye bila ridhaa yake.
Ni wakati sasa jamii inatakiwa kufunguka na kuzirekebisha mila zote zilizopitwa na wakati kwani mabadiliko ni sisi wenyewe.
Katika riwaya hii, mwanamke ameleta mabadiliko ya mila na desturi mbovu. Mwandishi anasema, “… Sekai wewe na Takadini mmebadilisha mambo mengi kijijini hapa. Kwa sasa sifikirii kama kuna mtu yeyote atakuwa na moyo wa kuharibu watoto wachanga, masope na wenye ulemavu…” (uk 26)

Mapenzi

Mapenzi yamejadiliwa katika nyanja mbili, yaani mapenzi ya kweli na yasiyokuwa ya kweli.
Sekai ana mapenzi ya kweli kwa mwanaye Takadini, ndiyo maana alikuwa tayari kufa kwa ajili yake. Shingai naye anamapenzi ya kweli kwa Takadini, kwani alimkataa Nhamo na kuolewa na Takadini bila kujali ulemavu wake. Mzee Chivero ana mapenzi ya kweli na dhati kwa Sekai. Alimtunza Sekai na mwanaye.
Kwa upande wa mapenzi yasiyokuwa ya kweli, yupo mzee Makwati, huyu hana mapenzi ya kweli kwa mwanaye Takadini, anasubiri uamuzi wa wazee ili mwanaye aweze kuuawa. sekani anampinga mumewe vikali kwa kusema, “Ni mtoto wangu wa kwanza niliyemsubiri kwa miaka mingi. Siwezi kukubali kumpoteza.” Vilevile kijiji cha mzee Makwati hakikuwa na mapenzi ya kweli kwa Takadini, kwani isingekuwa juhudi ya Sekai kutoroka na mwanaye, ni lazima mtoto angeteketezwa.

Ujasiri

Ujasiri umetumika kuleta ukombozi wa kiutamaduni katika riwaya hii. Tunamuona Sekai akitoroka nchi yake na kwenda nchi nyingine. Kutokana na ujasiri wake huo, anafanikiwa kumlinda mwanaye Takadini dhidi ya watu wote waliokuwa wanataka kumwangamiza. Vilevile yupo Shingai, msichana huyu anakataa kuolewa na Nhamo kwa sababu halikuwa chaguo lake. Chaguo la Shingai ni Takadini, mwanamume aliyempenda kwa moyo wake wote. Kwa ujasiri anasema, “Huyu ndiye mtu ninayemtaka mimi.”
Jamii yetu ni lazima iwe jasiri katika kupambana na mila zote mbaya. Isifumbie macho wala kuyaacha matatizo ya mila na desturi mbovu yaendelee kuwaumiza wanyonge.

Nafasi ya Mwanamke Katika Jamii

Mwanamke amejadiliwa kwa mazuri na mabaya yake:
-      Jasiri na mwenye kutetea haki. Sekai ni jasiri, anatetea haki ya mwanaye – haki ya kuishi.
-      Mama mlezi wa familia. Wanawake waliachiwa jukumu la kulea familia kama mama Shingai.
-      Duni. Baadhi ya wanaume walikuwa wakiwapiga na kuwadharau wake zao. Mwandishi anasema, “Nhariswa alimpiga mkewe kichwani na usoni mara kadhaa lakini mkewe hakuweza kujibu.” (uk 19).
-      Mwanamapinduzi. Sekai na Shingai wanaleta mabadiliko katika jamii yao. Silaha kubwa waliyotumia ni ujasiri.

Malezi

Wanawake waliachiwa jukumu la kulea familia. Baba Shingai anauliza, “Hukumfundisha mwanao maana ya tendo hilo, we?” (uk 96).
Hii inaonyesha ni jinsi gani hata kwenye jamii yetu wanavyohangaika na malezi ya watoto peke yao. Suala la malezi sio la kumwachia mama peke yake, bali ni jambo ambalo linatakiwa litekelezwe na wazazi wote wawili.

Ujumbe

Ujumbe ni funzo litolewalo na kazi ya fasihi. Mafunzo mengi yametolewa katika riwaya hii.
i.             Binadamu wote ni sawa.
ii.            Uchungu wa mwana aujuaye mzazi.
iii.           Ndoa ni makubaliano ya watu wawili na haipaswi kuingiliwa na mtu yeyote.
iv.          Malezi ya watoto yasimamiwe na wazazi wote wawili.
v.           Jamii iachane na mila potofu.

Migogoro

Migogoro ya wahusika
-      Sekai na jamii ya Makwati. Huu unasababishwa na Sekai kujifungua mtoto sope. Suluhisho la mgogoro huu ni Sekai kutoroka nchini kwake na kwenda kuishi ugenini.
-      Nhamo na Takadini. Huu unasababishwa na Takadini kupendwa na Shingai, msichana aliyeamrishwa kuolewa na Nhamo. Hakuna suluhisho la mgogoro huu.
-      Shingai na wazazi wake. Wazazi wa Shingai wanamkataza asiolewe na takadini kwani alikuwa sope. Suluhisho la mgogoro huu ni Shingai kukaidi agizo la wazazi wake na kuamua kuolewa na Takadini.
Mgogoro wa nafsi
Mgogoro huu unampata Sekai baada ya kuzaa mtoto Sope. Anafikiria kuhusu suluhisho la maisha ya mwanaye anayewindwa auawe na wananchi wanaoshikilia mila na imani potofu. Suluhisho la mgogoro huu ni Sekai kukimbilia nchi ya mbali.
Migogoro mingine iliyojitokeza ni migogoro ya kiuchumi, kiutamaduni, kisiasa na kijamii.

Falsafa

Mwandishi anaamini kuwa, wanadamu wote ni sawa.

Mtazamo/Msimamo

Mwandishi ana msimamo wa kimapinduzi kwani anaitaka jamii itumie ujasiri kuyaondoa matatizo yote yasababishwayo na mila na desturi zilizopitwa na wakati.

Uchambuzi wa fani na Vipengele Vyake

Fani ni ule ufundi wa kisanaa anaoutumia msanii katika kazi zake. Fani ndiyo hutupatia kile kiitwacho maudhui. Katika riwaya hii, fani imechambuliwa kama ifuatavyo:

Wahusika

Takadini

-      Ni mtoto wa kwanza wa Sekai
-      Ni mlemavu wa ngozi na mguu
-      Ni mhanga wa mila na desturi zinazowabagua walemavu
-      Anapata mtoto asiyemlemavu

Sekai

-      Ni mke wa kwanza wa mzee Makwati
-      Ni mama yake Takadini
-      Ni mwanamapinduzi
-      Ni mfano wa kuigwa na jamii

Makwati

-      Ni baba yake Takadini
-      Ni mwoga
-      Ni mkale

Chivero

-      Ni mganga wa kienyeji
-      Ni mshauri mkuu wa mtemi Masasa
-      Aliwapokea Sekai na Takadini

Mtemi masasa

-      Ana hekima
-      Ana wake wengi
-      Ni shujaa

Shingai

-      Ni mke wa Takadini
-      Ana msimamo
-      Ni mwanamapinduzi
Wahusika wengine ni: Darai, Rambidzai, Manyamombe, Mukaru, Chumbiri na Makaure.

Matumizi ya Lugha

Nahau

Ni maneno ambayo hubeba maana tofauti na neno lenyewe lilivyo.
“Lakini mbwa huyu amepoteza meno yake yote.” (uk 31).
MISEMO
“Maisha ni matamu.” (uk 83).

Tamathali za Semi

-      Tashibiha
“Giza jepesi liibaki ukutani kama mgeni asiyekaribishwa.” (uk 5).
“Mtoto alionekana mweupe sawa na funza mkubwa.” (uk 16).
-      Tashihisi
“Ndege mbalimbali wakiimba kuikaribisha siku mpya.” (uk 5).
“Ubongo wake ulioathirika kwa mawazo uliufukuza usingizi.” (uk 17).
-      Ritifaa
“Mababu zangu wamenitimizia ombi langu kuu…” (uk 1).
-      Tafsida
“Akamshambulia hata sehemu zake za siri.” (uk 83).
“Walifanya tena tendo la ndoa.” (uk 117).
-      Takriri
“Wewe ni sope, sope, sope.” (uk 62).
-      Mdokezo
“Sukuma mara moja tena…” (uk 125).
-      Nidaa. Kauli hii huonyesha kushangazwa kwa jambo.
“Kumbe maisha ni matamu!” (uk 83).

Muundo

Riwaya hii imetumia muundo wa moja kwa moja. Tunamuona Sekai akijifungua mtoto sope, anatoroka na mwanaye ili kumuokoa dhidi ya watu wa jamii yake. Sekai anakwenda kuishi uhamishoni, akiwa huko, mwanaye Takadini anapata mke na mtoto.

Mtindo

Mwandishi ametumia:
-      Masimulizi na dayolojia
-      Matumizi ya nyimbo. Rumbidzai aliimba;
…Mheshimiwa wetu amemiliki mavuno,
Kwa mikono yake halisi,
Kutokana na mashamba yetu wote,
Lakini ni kipi alichoambulia kutoka ardhi hii isiyomea kitu?

Mandhari

Riwaya hii imetuma mandari ya kijijini katika maeneo kama, barabarani, shambani, porini, chumbani, nyumbani n.k

Jina la Kitabu

Jina la kitabu linasadifu yaliyomo kwani walemavu wanauawa ilhari hawakupenda kuzaliwa hivyo na wala sio kosa lao bali ni mapenzi ya Mungu. Takadini yaani sisi tumekosa nini? Linaonyesha jinsi walemavu wanavyouawa pasipokuwa na hatia yoyote ile.

Kufaulu na Kutofaulu kwa Mwandishi

Kufaulu kwa Mwandishi katika Maudhui

-      Ameonyesha matatizo yanayowapata watu wenye ulemavu
-      Ameonyesha sababu ya watu wenye ulemavu kutokukubalika ni mila na desturi.
-      Ametoa suluhisho la matatizo hayo kuwa ni kuachana na mila hizo.

Kufaulu Kifani

-      Ametumia lugha inayoeleweka na ina tamathali nyingi za semi.
-      Ametumia nafsi zote tatu.
-      Ameteua jina zuri la kitabu ambalo linasadifu yaliyomo.

Kutofaulu Kimaudhui

-      Hajaonyesha jinsi matatizo ya mila na desturi yanavyoweza kuwaathiri walemavu wengine.

Kutofaulu Kifani

-      Ametumia idadi kubwa ya wahusika ambao hawabebi dhamira zozote.
-      Hajaonyesha watu wa jamii ya Takadini walilipokeaje suala la kijana huyo kupata mtoto asiye na  ulemavu.

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Uhakiki wa Riwaya ya Watoto wa Maman’tilie