Mfumo wa Maombi ya Ajira za Serikali Unavyoweza Kukupa Kazi

Nembo ya mfumo wa maombi ya ajira ikiwa na alama ya bibi na bwana
Katika zama hizi za maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, mfumo wa maombi ya ajira za serikali umebadilika kutoka kuchaguliwa moja kwa moja mpaka kuomba mwenyewe tena kwa njia za kidigiti.

Waombaji wengi kwa sababu ya elimu ndogo ya matumizi ya vifaa vya kiteknolojia, wamekuwa wakifanya makosa makubwa waombapo nafasi za kazi.

Ajira za serikali zimekuwa zikiombwa kwa njia nyingi lakini njia maarufu ni: Mfumo wa maombi ya ajira TAMISEMI na Recruitment Portal-Ajira.

Katika mfumo wa Recrutment Portal, wengi wakiuita Ajira Portal, kazi nyingi hutangazwa kutoka waajiri mbalimbali. Ni jukumu la mwombaji kuandika barua ya kazi na kutengeneza wasifu pamoja na kutuma vyeti vyake tayari kwa maombi yake kufanyiwa kazi.

Katika Mfumo wa Maombi ya Ajira TAMISEMI, nyingi ya kazi ziombwazo ni Ajira za Walimu na Ajira za Kada ya Afya. Serikali inapotoa ajira hizi hutangaza na waombaji huruhusiwa kuanza kutuma maombi yao.

Katika mfumo wa Maombi ya Ajira TAMISEMI, waombaji wengi wamekuwa wakilalamikia kero mbalimbali lakini kubwa zaidi ni tovuti kutumia muda mrefu kufunguka. Hali hiyo imepelekea waombaji watumie muda mwingi katika kufanya maombi hali inayoathiri shughuli zingine za kimaendeleo.

Jinsi ya Kutumia Mfumo wa Maombi ya Ajira ili Uweze Kupata Kazi

Japo wapo waombaji ambao wamekuwa wakiomba kazi kwa usahihi na kukosa kazi hizo, lakini wapo waombaji wengi ambao wanakosa kazi kwa sababu ya kukosea kufanya maombi. Baadhi hufanyiwa maombi na watu wengine hivyo kujikuta wakikosea baadhi ya taarifa na wengine hufanya wenyewe.

Endapo unahitaji kupata kazi katika mfumo wa maombi ya ajira, zingatia mambo haya:

1. Hakikisha Una Barua ya Maombi ya Kazi Iliyoandikwa kwa Usahihi 

Barua ya maombi ya kazi iandikwe kwa mkono au kwa kompyuta lakini ni sharti barua hii isainiwe na wewe mwombaji. Zingatia kwamba, kama tangazo la kazi limeandikwa kwa lugha ya Kiswahili na wewe barua yako iandikwe kwa lugha ya Kiswahili. Jifunze hapa jinsi ya kuandika barua ya maombi ya kazi inayokubalika katika mfumo wa maombi ya kazi za serikali.

Pia, unapomaliza kuandika barua yako, ni vyema kama utaenda stationery utaitoa na kuweka saini yako, kisha una 'scan' kuiambatanisha.

2. Hakikisha Una Wasifu Ulioandikwa Katika Namna Sahihi

Wasifu wako uwe na vitu vyote muhimu vinavyotakiwa. Tazama mfano wa wasifu unaokubalika katika mfumo wa maombi ya kazi.

Zingatia kwamba, wasifu wako uwe na taarifa zako wewe pekee. Uandikwe kwa kutumia mwandiko wa aina moja tena unaosomeka vizuri. Jitahidi usichanganye taarifa muhimu kama vile namba ya simu na barua pepe.

3. Uwe na Namba ya Kitambulisho cha Taifa

Hii hutumika katika kufungua akaunti yako. Kama huna, ni rahisi sana kupata namba yako ya kitambulisho cha taifa. Fika katika ofisi ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa-NIDA kisha fuata maelekezo na utaweza kupata namba ya kitambulisho chako cha taifa.

Zingatia kwamba, namba ya kitambulisho cha taifa ni taarifa binafsi na watu wasiohusika hawapaswi kuiona kwani ikionekana kwa watu wabaya inaweza kutumika kufanya matukio ya uhalifu.

4. Chagua Maombi Yako kwa Usahihi

Kama unaomba katika sekta ya afya weka hapo na kama unaomba katika sekta ya Elimu chagua vyema.

Kamwe usichanganye maombi kwani kufanya hivyo kutafanya ukose kazi unayoomba. Nyongeza ya hapo ni kwamba, kama wewe ni mwalimu wa shule ya msingi usiweke sekondari. Kama wewe ni muuguzi usiweke sehemu ya daktari wa meno nakadhalika. Hivyo basi, weka eneo lako husika.

5. Hakikisha Kwamba Maombi Yako Yamekamilika na Umeona Uthibitisho Kwamba Yamekamilika

Miongoni mwa njia zinazotumika kuthibitisha kuwa umefanya maombi yako kwa usahihi ni kuona ujumbe unaosema maombi yako yamekamilika kwa asilimia mia moja.

Epuka kutuma maombi ambayo hayajakamilika kwani hayataweza kufanyiwa kazi.

Mfumo wa maombi ya ajira ukionyesha hali ya ukamilifu wa ujazaji wa maombi
Maombi yaliyokamilika katika mfumo wa maombi ya ajira-TAMISEMI

6. Hakikisha Kabla Hujatuma Maombi, Umesoma Vizuri Tangazo la Kazi Lililotolewa

Wapo waombaji wengi wamekuwa wakiomba kazi ambazo hazipo katika tangazo. Kuomba kazi ambayo haijatangazwa hususani kazi za serikali, hakuwezi kukufanya upate kazi bali utapoteza muda wako bure.

Hivyo basi, hakikisha unaomba kazi iliyotangazwa na lisome tangazo la kazi kabla ya kuanza kuomba kazi hiyo. Vilevile fuata maelekezo yanayotolewa katika tangazo la kazi.

7. Hakikisha Vyeti Ulivyoambatanisha Vinasomeka Vizuri

Hili limekuwa tatizo kwa waombaji wengi kwani wamekuwa wakiambatanisha vyeti walivyovipiga picha kwa simu ambazo nyingi yake zinatoa picha zenye ubora hafifu na kufanya vyeti visisomeke. Unapoomba kazi katika mfumo huu, ni vyema kama utaenda ‘stationery’ ili uweze ku’scan’ vyeti vyako kuleta ubora unaotakiwa na kuvifanya visomeke pale vinapopitiwa.

Fahamu kwamba, endapo vyeti vyako havisomeki, maombi yako hayatafanyiwa kazi na yatatupiliwa mbali.

8. Kama Unaomba Kwa Mara Nyingine Hakiki Taarifa Zako na Weka Barua Mpya

Waombaji wanaoomba kwa mara nyingine wahakikishe wanaweka barua mpya. Pia, wahakiki vyeti walivyotuma kama vipo sawa na kama kuna kitu hakipo sawa, wafanye mabadiliko.

Vilevile waombaji wapya wanatakiwa kujaza upya vituo wanavyotaka kufanyia kazi. Kumekuwa na imani kuwa ukijaza vituo vilivyo vijijini unakuwa na nafasi kubwa ya kupata kazi kuliko wale wanaojaza vituo vya mjini. Hilo halina ukweli kwani mtu anapewa kazi kulingana na kukidhi vigezo muhimu kama vile: kuwa na taaluma inayotakiwa, mwaka wa kumaliza, umri wake, ufaulu wa masomo nakadhalika. Unapoomba kazi, weka sehemu unayoipenda kutoka moyoni mwako.

9. Fanya Maombi Haya Wewe Mwenyewe na Unapofanyiwa na Mtu Mwingine Hakikisha Upo na Unafuatilia Kila Hatua Inavyokwenda 

Wapo watu ambao hawalipi uzito stahiki suala la maombi ya kazi za serikali. Wanatuma watu wawafanyie maombi huku wao wakiwa hawajui lolote linaloendelea huko zaidi ya kupewa taarifa maombi yamekamilika. Kama hujui namna maombi yanavyofanywa, usiogope, jifunze na utaelewa. Kuutumia mfumo wa maombi ya ajira za serikali ni rahisi kuliko masomo uliyosoma chuo.

Ni vyema kama utaomba kazi wewe mwenyewe na kama utafanyiwa na mtu mwingine, hakikisha unaingia katika akaunti yako ili kufanya uhakiki wa mambo mbalimbali na kujiridhisha.

Kutafuta kazi ni changamoto lakini usikate tamaa. Endelea kutuma maombi ya kazi kila kazi zinapotangazwa. Inaweza kuchukua muda, lakini siku moja utapata kazi uitakayo. Usisikilize maneno yanayosemwa kila siku kuhusu ajira. Ni kweli kuna tatizo la upungufu wa ajira lakini watu wanapata kazi kila siku. Watu wengi wamekata tamaa ya kutafuta kazi kabisa kwa sababu ya maneno wanayosikia mtaani kuhusu ugumu wa kupata kazi. Muhimu ni kwamba, unapoendelea kutafuta kazi uitakayo, hakikisha unajishughulisha na kazi mbalimbali unazozimudu. Pale matangazo ya kazi yanapotoka, omba haraka na kamwe usikatishwe tamaa na maneno kuwa huwezi kupata kazi mpaka iwe ‘hivi au vile.’ Tunakubali ‘hivi au vile’ ipo, lakini nawafahamu watu wengi waliopata kazi bila ‘hivi au vile.’

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Uhakiki wa Tamthiliya ya Kilio Chetu