Maendeleo ya Lugha ya Kiswahili Afrika Mashariki

Pundamilia wawili.
Swali
Jadili maendeleo ya lugha ya Kiswahili katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Kila siku lugha ya Kiswahili inazidi kupata maendeleo katika nchi za Afrika Mashariki. Maendeleo haya yanaendana na kuongezeka kwa msamiati wa lugha ya Kiswahili, lakini pia,kuongezeka kwa watumiaji wa lugha ya Kiswahili. Nchi za jumuiya ya Afrika Mashariki ni: Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi na Rwanda. Lugha ya Kiswahili imepata maendeleo makubwa katika nchi hizi. Nchini Tanzania, matumizi ya Kiswahili ni makubwa zaidi kwa sababu lugha hii inatumika kuyaunganisha makabila zaidi ya 120 yaliyopo nchini humu. Kenya inafuata kwa kuwa na wazungumzaji wengi. Uganda, Burundi na Rwanda bado zinajikongoja, hata hivyo, hatua zilizopigwa na lugha ya Kiswahili katika nchi hizo si haba. Kwa mujibu wa Choge (2006), katika Afrika Mashariki, hila za watu kukidunisha na kukitokomeza Kiswahili mpaka sasa zimegonga mwamba. Kiswahili kimeimarika na kimepata nafasi ya kuingia katika mkondo wa teknolojia ya habari na mawasiliano. Yafuatayo ni maendeleo ya lugha ya Kiswahili katika nchi za jumuiya ya Afrika Mashariki:
Kiswahili kinafundishwa na kutahiniwa katika shule na vyuo katika nchi zote za ukanda wa Afrika Mashariki. Kiswahili ni somo mojawapo miongoni mwa masomo yanayofundishwa katika nchi za ukanda wa Afrika wa mashariki. Ufundishwaji wa somo la Kiswahili umezidi kuimarishwa kila mwaka ili kuweza kutoa wanafunzi wenye maarifa na ujuzi wa lugha ya Kiswahili. Hali hii imeimarisha lugha ya Kiswahili kwa kuifanya ipate wazungumzaji wengi. Mfano, wanafunzi wanao soma lugha ya Kiswahili katika nchi za Afrika mashariki, wamekuwa watumiaji wazuri wa lugha hii jambo linalohamashisha watu wengine pia wazungumze lugha ya Kiswahili na kuifanya lugha izidi kukua. Pia, kuongezeka kwa watumiaji Afrika ya Mashariki, kutafanya nchi zingine zivutiwe na kuanza kujifunza Kiswahili.
Idadi ya watu wanaozungumza lugha ya Kiswahili inaongezeka kila siku. Nchi za Afrika mashariki zimekuwa na ongezeka kubwa la wazungumzaji wa lugha ya Kiswahili. Mfano, katika nchi hizi, kila mwaka watoto karibu milioni moja hujiunga darasa la kwanza la shule za msingi ambapo Kiswahili ni somo la lazima. Pia, zaidi ya watu milioni mia moja wanazungumza lugha ya Kiswahili katika nchi za Afrika Mashariki. Kuongezeka kwa idadi ya wazungumzaji, kunaifanya lugha ya Kiswahili izidi kuongezeka thamani kila siku. Idadi hii inafungua fursa ya ajira kwa walimu wa somo la Kiswahili.
Kiswahili ni ‘lingua franca’ ya nchi zote za Afrika Mashariki. Kwa kuwa jamii ya Afrika mashariki ina wazungumzaji wa lugha nyingi, Kiswahili kimesalia kuwa lugha inayowaunganisha watu hawa wenye lugha nyingi. Mfano, huko Kenya na Uganda ukiondoa lugha za makabila, watu wengi hutumia Kiingereza. Huko Burundi watu hutumia Kirundi na huko Rwanda watu huzungumza Kinyarwanda. Lugha moja inayowaunganisha wana Afrika mashariki wenye lugha nyingi hizi ni Kiswahili. Pengine bila Kiswahili, ingekuwa vigumu sana kuwaunganisha wana Afrika mashariki. Kazi inayofanywa na lugha ya Kiswahili katika kuwaunganisha watu wa Afrika Mashariki ni sawasawa na kazi inayofanywa na lugha ya Kiingereza kuwaunganisha watu wa Dunia nzima.
Maandishi kwa Kiswahili yanachapishwa kwa wingi katika nchi za Afrika Mashariki. Nchini Tanzania vitabu vingi vya Kiswahili vinaandikwa mfano: vitabu vya sarufi, fasihi na aina nyinginezo za vitabu. Pia, huko Kenya kuna waandishi wengi wa kazi za Kiswahili kama Profesa Wamitila. Waandishi wa kazi za Kiswahili wapo wengi Afrika Mashariki. Kutokana na kukua kwa teknolojia, sasa Kiswahili kinaandikwa mitandaoni na kinajipatia wasomaji wengi na kufanya idadi ya watumiaji iongezeka maradufu. Hivyo ni ukweli kuwa, Kiswahili ni lugha ambayo inaendana na maendeleo makubwa ya kiteknolojia Duniani.
Wasanii wa muziki Afrika Mashariki wanaimba kwa lugha ya Kiswahili. Huko nchini Kenya, kundi la muziki la ‘sauti soul’, huimba nyimbo zake kwa lugha ya Kiswahili. Jose Chameleon wa Uganda, huimba nyimbo zake kwa lugha ya Kiswahili. Pia, mwanamuziki Kidumu wa Burundi, amekuwa akiimba nyimbo zake kwa lugha ya Kiswahili. Nchini Tanzania, wanamuziki wengi zaidi wanatumia lugha ya Kiswahili. Mifano, Diamond na Alikiba. Wanamuziki wa Afrika mashariki wamegundua kuwa, kuna biashara nzuri ya mziki ukiimb kwa lugha ya Kiswahili tofauti na ukimba kwa lugha ya Kiingereza.
Kiswahili kinatumika katika vyombo vya habari. Vyombo vya habari vya Afrika mashariki kama redio, televisheni na magazeti, vinatumia lugha ya Kiswahili kufikisha habari kwa wananchi. Nchini Tanzania, gazeti la Mwananchi, Redio ya taifa (TBC), na televisheni ya ITV, Kiswahili kinatumika katika kurusha matangazo. Ipo mifano mingi ya Televisheni, magazeti na redio yanayorusha matangazo kwa Kiswahili katika nchi nyingi zaidi za Afrika Mashariki.
Ipo mpango ya kukifanya Kiswahili kuwa lugha ya kufundishia kutoka shule za msingi mpaka chuo Kikuu. Mpango huu ulitajwa katika sera ya elimu ya mwaka 2014 ambayo ilisema kuwa, nchini Tanzania lugha ya Kiswahili itatumika kama lugha ya kufundishia shule za msingi mpaka chuo kikuu. Mpango huu ukifanikiwa nchini Tanzania, basi hapana shaka kuwa, utaweza kufanikiwa hata katika nchi zingine za Afrika Mashariki kama: Kenya, Uganda, Burundi na Rwanda.
Kuongezeka kwa msamiati wa lugha ya Kiswahili. Maneno mengi yameongezeka katika lugha ya Kiswahili. Miongoni mwa maneno hayo ni kama: mubashara, tafrija mchapalo, vibanzi na sharubati. Hii ni ishara kuwa, lugha ya Kiswahili inaweza kutumika sehemu yoyote kwa sababu ina msamiati wa kutosha. Maneno ya wapinzani wa lugha ya Kiswahili kuwa lugha hii haina msamiati wa kutosha hayana nafasi tena.
Maendeleo haya ya lugha ya Kiswahili Afrika ya Mashariki hayajapatikana kwa usiku mmoja. Mapambano yalianza hata kabla ya ukoloni, wakati wa ukoloni na baada ya kupata uhuru. Bado kiswahili kinapiga hatua bila kujali changamoto zilizopo ambazo ni: baadhi ya watu kuamini Kiswahili hakistahili kupewa hadhi ikiwemo hadhi ya kutumika kufundishia chuo Kikuu. Changamoto nyingine ni ulegevu wa sera ya lugha, ulegevu huu unafanya lugha za kigeni zipate mianya ya kupenya na kukifanya Kiswahili kisipewe nafasi. Pia, mawimbi mazito ya tamaduni za kigeni, yanawafanya vijana wetu wapuuze lugha ya Kiswahili. Changamoto hii inasababishwa kwa kiasi kikubwa na vyombo vya habari. Yote kwa yote, lugha ya Kiswahili imepiga hatua kubwa. Ni wajibu wa kila mwana Afrika ya Mashariki kuhakikisha kuwa lugha ya Kiswahili inakua na kufika mbali.
Marejeo
John James na Mduda FAustiono. (2012). Kiswahili Kidato cha Tano na Sita. Dar es Salaam: Oxford University Press.
Kiango, J.G. (hakuna mwaka). Nafasi ya Kiswahili Katika Ujenzi wa Jamii Mpya ya Afrika Mashariki (makala). University of Dar es Salaam, Tanzania.
Mbunda, F. (1976). Mwalimu wa Kiswahili. DSM: OUP.

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Uhakiki wa Tamthiliya ya Kilio Chetu

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024