Mawasiliano | Kiswahili Kidato cha Kwanza

Wanaume wawili wakitazama simu zao
Mawasiliano ni kitendo cha kupashana habari. Inaweza kuwa kwa mdomo baina ya mtu na mtu, simu, barua au njia yoyote itakayosaidia kutoa habari sehemu fulani kuipeleka mahali pengine. Tunasema mawasiliano yamekamilika pale yanapoleta maana iliyokusudiwa. Jamii inayoishi watu, huwasiliana. Chombo kinachotumiwa kwa mawasiliano baina ya mtu na mtu kinaitwa lugha.

Lugha ni mfumo wa sauti za nasibu zilizokubaliwa na watu ili zitumike kwa mawasiliano. Lugha hujumuisha: sauti, silabi, neno na sentensi. Unapowasiliana kwa kutumia lugha ya Kiswahili ni muhimu kuzingatia: kiimbo, mkazo, matamshi na lafudhi sahihi.

Dhima ya lugha katika mawasiliano

1. Kupashana habari

Watu hupashana habari mbalimbali kwa kutumia lugha. Habari za furaha na huzuni zote hutolewa kwa kutumia lugha. Taarifa ya habari katika redio na runinga ni mfano wa namna lugha inavyotumika kama chombo cha kupashana habari.

2. Kutambulisha mtumiaji wa lugha

Kwa kusikia watu wakiwa wanazungumza, tunapata kuwafahamu watu hao ni wa jamii gani au ni wa asili ya wapi Kwa mfano, Mhehe akiwa anaongea kihehe tunapata kumtambua papo hapo kuwa mtu huyu ni mhehe.

3. Kupata maarifa kuhusu mambo mbalimbali

Watu hujifunza kwa kutumia lugha. Mwanadamu hutumia lugha kujifunza mambo mbalimbali kama: ufundi, lugha, sayansi na teknolojia, sanaa na mambo mengine mengi.

4. Kuwasilisha hisia

Lugha huweza kuwasilisha hisia mbalimbali kama upendo, furaha na huzuni. Mtu anapokuwa kakasarika, huweza kujulikana kutokana na lugha yake anayotumia. Vivyo hivyo mtu mwenye furaha, hujulikana kwa lugha yake.

5. Sehemu ya utamaduni wa watu

Lugha inabeba utamaduni wa watu. Mila, desturi na tamaduni mbalimbali, hurithishwa kutoka kizazi kimoja kwenda kingine. Methali, nahau, misemo na vitendawili ni sehemu ya utamaduni wa watumiaji wa lugha ya Kiswahili.

6. Hutumika katika shughuli za uzalishaji mali

Watu hutumia lugha wafanyapo kazi zao. Mshereheshaji awapo katika sherehe hutumia lugha ili kunogesha tukio. Mwalimu hutumia lugha kufundisha, nao mafundi ujenzi, hutumia lugha kupeana maelekezo fulani.

Umuhimu wa kutumia lugha kwa ufasaha

Kama ilivyoelezwa, lugha ni kitu muhimu kwa maendeleo ya mwanadamu. Hivyo ili kufikia mafanikio ni vyema kutumia lugha kwa ufasaha. Umuhimu wa kutumia lugha kwa ufasaha unaelezwa:

Matumizi ya lugha fasaha huepusha migogoro. Ipo migogoro inayoibuka kwa sababu lugha haikutumika kwa ufasaha. Kwa mfano, mtu anaweza akahisi amekosewa heshima endapo lugha haikutumika kwa ufasaha.

Pia, matumizi ya lugha fasaha husaidia kufikisha ujumbe uliokusudiwa. Unapotumia lugha kwa ufasaha, ujumbe huweza Kufika vyema bila upotoshaji.

Vilevile, matumizi ya lugha fasaha huepusha hatari. Yapo maeneo ambayo lugha fasaha isipotumika, tatizo kubwa linaweza kutokea. Kwa mfano, daktari asipotumia lugha kwa ufasaha anaweza kusababisha kifo kwa mgonjwa.

Tena, lugha fasaha ni muhimu kwani huokoa muda. Lugha inapotumika vyema, huokoa muda na kuepusha kurudia kuelekeza jambo ambalo lilishatolewa ufafanuzi.

Matumizi ya lugha fasaha humfanya mtu aheshimike na kukubalika na watu. Unapotumia lugha fasaha, watu hukuchukulia kuwa mtu mwema mwenye kuaminika. Kwa mfano, siyo rahisi kukubalika na watu kama unatumia lugha ya matusi, watu watakuona mhuni na hawatakuamini.

Ni muhimu kutumia lugha kwa ufasaha ili kuendeleza mawasiliano. Lugha isipotumika kwa ufasaha, kila kitu kitaharibika, biashara zitakufa na hakuna kitakachotendeka kwa sababu lugha ndiyo chombo kinachowaunganisha watu na kuwafanya waelewane.

Hivyo basi, ni muhimu kutumia lugha kwa ufasaha, kwani kushindwa kufanya hivyo kunaweza kusababisha matatizo makubwa.

Kiswahili ni lugha ya kibantu inayozungumzwa kama lugha mama au lugha ya pili katika ukanda wa pwani ya Mashariki mwa Afrika.

Kibantu ni jina jumuishi linalotumika kutaja lugha zote zinazotumia maneno yanayoishia na –tu, ntu, nhu, nu n.k. hivyo hakuna lugha maalumu ijulikanayo kama kibantu.

Watu wanaozungumza Kiswahili kama lugha mama hujulikana kama Waswahili. Jina hili hurejelea lugha yao na siyo kabila kwani hakuna kabila la Waswahili. Kiswahili kinatumia Tanzania na Kenya kama lugha ya taifa.

Pamoja na kwamba Kiswahili ni lugha ya Kibantu, baadhi ya maneno yamekopwa kutoka lugha mbalimbali kama vile: kiarabu, kireno na kiingereza.

Inasemekana kuna lahaja 15 za Kiswahili. Kwa upande wa Afrika ya Mashariki, lahaja zinazojulikana sana ni:

Kiunguja; kinachozungumzwa katika kisiwa cha Unguja na ambacho kilisanifishwa kuwa Kiswahili sanifu. Kipemba; kinachozungumzwa katika Kisiwa cha Pemba. Kitumbatu; kinachozungumzwa katika Kisiwa cha Tumbatu, Kimvita; kinachozungumzwa Mombasa na Kiamu; kinachozungumzwa katika Kisiwa cha Lamu huko Kenya. Pamoja na Lahaja hizo zote, Kiswahili sanifu ndicho hufundishwa shuleni.

Lugha mama ni ile lugha ya kwanza ambayo mtu hujifunza.

Faida za kusoma lugha ya Kiswahili

Kiswahili kinatoa fursa za Ajira. Baadhi ya Watanzania wenye elimu ya Kiswahili hujipatia fedha kwa kufundisha somo hili. Pia, Kiswahili kinakua na kuhitajika katika mataifa mengi kama Afrika Kusini hivyo kutoa fursa ya Ajira kwa Watanzania.

Kiswahili kinasaidia watu kuwasiliana kwa lugha fasaha.

Kiswahili ni sehemu ya utamaduni wa Mtanzania.

Kiswahili hujenga ubunifu na tabia ya udadisi. Mfano uandishi wa kazi za kifasihi.

Kiswahili kinamwezesha mtu kujipatia maarifa hasa pale anaposoma maandiko ya Kiswahili.

Hivyo basi, Kiswahili kama zilivyo lugha zingine, kina uwezo wa kufundisha maarifa ya uchumi, sanaa na sayansi.

Lafudhi na Matamshi ya Kiswahili

Lafudhi ni jinsi mtu anavyotamka maneno. Lafudhi humfanya mzungumzaji atambulike eneo analotoka. Lafudhi huweza kusababishwa na lugha mama au eneo analotoka mzungumzaji.

Ntoto, wanakwendaga, ninawaonapo, kurara, badara, erimu, kurima,

Silabi ni sehemu ya neno inayoundwa na konsonanti na irabu au irabu peke yake na hutamkwa kwa pamoja na mara moja kama fungu moja la sauti. Kwa mfano, neno mama limeundwa na silabi mbili ambazo ni $ma$ $ma$.

Muundo wa silabi za Kiswahili

Irabu pekee: kwa mfano, ua.

Konsonati moja na irabu moja: kwa mfano, silabi ‘la’ na ‘la’ katika neno lala.

Konsonanti mbili au zaidi na irabu moja: Kwa mfano, silabi ‘mba’ katika neno shamba.

Konsonanti moja, kiyeyusho kimoja na irabu moja.kwa mfano, silabi ‘pya’ katika neno jipya.

Konsonanti mbili, kiyeyusho kimoja na irabu moja. kwa mfano, silabi ‘mbwa’ katika neno pambwa.

Irabu za Kiswahili ni a, e, i, o na u.

Konsonanti za Kiswahili ni b, ch, d, dh, f, g, gh, h, j, k, l, m, n, ng’, ny, p, r, s, sh, t, th, v na z.

Viyeyusho ni ‘w’ na ‘y’

Sauti ni sehemu ndogo ya neno ambayo haiwezi kugawanyika zaidi. sauti huweza kutamkwa kwa kutumia mapafu, koo, midomo, ulimi, ufizi na meno.

Sauti zimegawanyika katika sehemu mbili: irabu na konsonanti.

Irabu ni sauti ambazo hutamkwa bila kuzuia mkondohewa. Kwa mfano, irabu a, e, i, o, u.

Konsonanti hutamkwa kwa kuzuia mkondo hewa. Kwa mfano, t, ng’ na kadhalika.

Katika lugha, watu huweza kufanya makosa mbalimbali. mojawapo ya makosa hayo ni makosa ya matamshi.

Mkazo

Mkazo ni pale silabi inapotamkwa kwa kukazwa. Katika lugha ya Kiswahili kuna namna ya kutamka maneno ili kuleta maana mbali mbali, kwa mfano neno “barabara” litaleta maana husika kulingana na jinsi lilivyotamkwa. Hivyo, Maneno ya Kiswahili huwa na silabi moja ambayo hutamkwa kwa nguvu zaidi kuliko silabi nyingine. Unapotamka silabi iliyotiwa mkazo, sauti hupandishwa juu kiasi.

Maneno mengi ya Kiswahili, hasa yale yenye asili ya Kibantu hutia mkazo katika silabi ya pili kutoka mwisho.

Kwa mfano:ba’bu, maya’i, rama’ni (watu wengi hutamka ra’mani), baraba'ra (njia). Baadhi ya maneno yenye asili ya kigeni, huwa na mkazo katika silabi nyingine. Kwa mfano: bara'bara (sawa sawa), Alha’misi.

Kiimbo

Ni utaratibu maalum wa upandaji na ushukaji wa mawimbi ya sauti unaojitokeza katika utamkaji wa lugha fulani.

Katika utaratibu wa utamkaji, dhana ya Kiimbo huandamana pia na dhana ya kidatu (yaani, kiwango cha juu, cha chini au cha kati cha sauti katika usemaji), Kwa hivyo ni muhimu hapa kueleza tofauti zilizopo baina ya kiimbo na kidatu.

Wakati kiimbo kina maana ya kupanda na kushuka kwa mawimbi ya sauti ya lugha, kidatu kina maana ya kiwango cha sauti isikikayo, wakati wa utamkaji ama kuwa juu, kuwa katikati au kuwa chini.

Aina za viimbo

Kiimbo cha maelezo: Kiimbo cha maelezo ni kile ambacho kwa kawaida msemaji wa lugha akiwa kwenye kidatu chochote kile mawimbi sauti ya usemaji wake yanakuwa takriban katika mstari ulionyooka. Mfano, Mwalimu anafundisha.

Kiimbo cha maulizo: Kiimbo cha kuuliza hujitokeza kwa kutumia viwango tofauti vya kidatu kutegemeana na aina ya swali linaloulizwa. Mfano, mwalimu anafundisha?

Kiimbo cha amri: kiimbo cha amri hakitofautiani sana na kiimbo cha maulizo. Kiimbo cha amri, mzungumzaji hutumia kidatu cha juu zaidi kuliko ilivyo katika kiimbo cha maelezo. Mfano, njoo hapa!

Sababu ya makosa ya matamshi ni:

Athari za lugha mama au mazingira aliyomo mzungumzaji. Mfano mzungumzaji wa Musoma, huweza kusema, rara badala ya lala.

Zoezi la Marudio

1. chagua jibu sahihi katika maswali yafuatayo:

i. Watu wanapowasiliana huwa wana lengo gani?

A. kutambulisha utamaduni B. kutunza historia C. kupashana habari D. kuelimisha jamii E. kuburudisha jamii.

ii. Katika mazungumzo, kiimbo ni nini?

A. Kupanda na kushuka kwa mawimbi ya sauti. B. kuzungumza na kuongea kwa sauti C. Kuzungumza na kupandisha mawimbi ya sauti. D. Kuzungumza na kushusha mawimbi ya sauti E. Kuzungumza nak ushuka kwa mawimbi ya sauti.

iii. Sentensi hii haina maana zaidi ya moja…

A. Kaka amefua nguo B. Nipe sahani ya kulia C. Suedi amenunua mbuzi D. Eva amenunua kanga E. Joni amempigia mpira

iv. Dhana ipi kati ya zifuatazo huonyesha utambulisho wa mzungumzaji?

A. Matamshi B. sauti C. Silabi D. Mkazo E. Lafudhi

v. Neno shurutishwa limeundwa na silabi ngapi?

A. Tano B. Nne C. Tatu D. Sita E. Kumi

2. Oanisha maana ya dhana katika orodha A na dhana zinazohusika kutoka orodha B kwa kuchagua herufi ya jibu sahihi.

Orodha A

Orodha B

i. Sehemu ya neno inayotamkwa mara moja na kwa pamoja kama fungu moja la sauti.

ii. Utamkaji wa maneno unaozingatia kanuni za sarufi ya lugha.

iii. Nguvu inayotumika kutamka sehemu falani ya neno.

iv. Vitamkwa vinavyotamkwa na binadamu kwa kutumia viungo sauti.

v. Jinsi mtu anavyotamka maneno ya lugha.

A. Lafudhi

B. Matamshi

C. Kiimbo

D. Mkazo

E. Silabi

F. Lugha

G. Sauti

3. Bainisha maneno yenye makosa katika sentensi zifuatazo kwa kuyapigia msitari kisha  andisha sentensi hizo kwa usahihi.

a. Wanafunzi wenye bidii hawatakagi kupata alama ndogo.

b. Shule yetu ina samani mbalimbali kama: meza, viti na vitanda.

c. Napenda kuwajulisha kuwa, marehemu amefariki leo asubuhi.

d. Ngombe wetu ana ndama wawili.

e. chakula cha leo kimemzuru bwana shamba.

4. matumizi ya kiimbo husaidia kubainisha lengo la mzungumzaji. Fafanua malengo ya mzungumzaji katika sentensi zifuatazo:

a. Mama anapika kwa furaha.

b. Mama, pika kwa furaha.

c. Mama anapika kwa furaha?

d. Mama anapika kwa furaha!

5. Eleza maana ya msamiati ufuatao kisha tunga sentensi moja kwa kila msamiati.

a. tovuti b. simu c. mtandao d. bando e. kompyuta

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Uhakiki wa Riwaya ya Watoto wa Maman’tilie