Dhana Mbalimbali za Lugha ya Kiswahili na Maana Zake



Swali
Huku ukitoa mifano katika lugha ya Kiswahili, jadili kwa kina kuhusu dhana zifuatazo:
1. Lugha sanifu.
2. Usanifishaji.
3. Lahaja.
4. Rejesta.
5. Sera ya lugha.
6. Sera ya utamaduni.
Majibu
1. Kwa mujibu wa kamusi ya TUKI (1981), sanifu ni kufuata taratibu au kanuni zilizokubaliwa.
Hivyo basi lugha sanifu ni lugha iliyokarabatiwa na sheria zake kama vile muundo wa sentensi, msamiati, sarufi na sifa nyinginezo,kubainishwa na kuandikwa, na kwa hivyo huzingatia sarufi maalum na upatanisho sahihi wa sentensi.
Ipo mifano ya matumizi ya lugha isiyo sanifu:
“Alipachika jina la staa huyo wa dunia kulingana na vipaji vyao vya upigaji vyenga dimbani.”
Lugha iliyotumika katika mfano huo siyo sanifu kwa sababu neno chenga halina wingi, hivyo kusema vyenga ni makosa.
Mfano mwingine ni:
“Taaluma ya kusomea ni zaidi ya elimu na hailazimishwi ila naona kuna baadhi wanajaribu kuibaka sanaa hiyo.”
Neno kubaka limetumiwa ndivyo sivyo. Siyo sahihi kuandika kuwa sanaa imebakwa kwani kubaka ni kumkamata mtu kwa nguvu na kuzini naye bila ridhaa yake. Ni wakati wa waandishi na watumiaji wa lugha kujifunza Kiswahili sanifu.
2. Kwa mujibu wa Massamba (1996), Usanifishaji wa lugha ni mchakato unaowezesha kupatikana kwa lugha moja yenye namna moja ya uzungumzaji na uandishi.
Usanifishaji hutokea katika mazingira yenye vilugha (lahaja) vingi. Ulinganifu wa vilugha hivyo ili kupata lugha moja itakayotumiwa kirahisi katika mawasiliano. Historia ya mchakato wa usanifishaji wa Kiswahili iligubikwa na malumbano juu ya lahaja ipi iwe ya msingi kati ya Kiamu, Kimvita na Kiunguja ambapo ilikubalika kwa sauti moja kuteua Kiunguja kuwa ndio msingi wa ‘Kiswahili Sanifu’ katika kikao kilichofanyika mjini Mombasa mnamo mwaka 1928 na kufuatiwa na uundwaji wa Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki mwezi Januari mwaka 1930. Kamati ilitumia muda mwingi kwenye kipindi cha miaka ya 1930 hadi 1947 katika kuweka ithibati katika mtindo wa tahajia, na sifa bainifu za kisarufi za Kiswahili Sanifu.
Kwa ujumla, usanifishaji wa lugha ni kitendo cha kuchagua lahaja moja kati ya lahaja nyingi na kuifanya lahaja hiyo kuwa lugha inayotambulika tena yenye namna moja ya uzungumzaji na uandishi. Kiunguja ni lahaja iliyochaguliwa kati ya lahaja nyingi na kutengeneza lugha ya Kiswahili. Pia, Kiswahili ni lugha sanifu na kazi ya kukisanifisha Kiswahili ilifanywa na waingereza katika enzi ya utawala wao.
3. Dhana ya lahaja imezungumzwa na wataalamu wengi kama inavyoajadiliwa kwa kina:
Msanjila (2009:124) anasema lahaja ni lugha mojawapo kati ya lugha ambazo kimsingi kuhesabiwa kuwa lugha moja isipokuwa zinatofautiana katika baadhi ya vipengele fulani fulani kama vile lafudhi, fonolojia, msamiati usiokuwa wa msingi au muundo kutokana na eneo lugha hiyo inazungumzwa.
Massamba (2002) anasema kuwa lahaja ni lugha mbalimbali za pwani zilizokuwa na uhusianao wa karibu sana. Lugha hizo ni kama vile: ci-mbalazi, ki-amu, ki-mvita, ki-jomvu, ki-mtang’ata, ki-makunduchi, ki-tumbatu, ki-mgao na ki-unguja.
Kwa ujumla, lahaja ni lugha mojawapo kati ya lugha ambazo kimsingi kuhesabiwa kuwa lugha moja isipokuwa zinatofautiana katika baadhi ya vipengele fulani fulani kama vile lafudhi, fonolojia, msamiati usiokuwa wa msingi au muundo kutokana naeneo lugha hiyo inamozungumzwa.
4. Kwa mujibu wa Wikipedia wakimnukuu Massamba (2004), rejesta ni matumizi ya lugha kulingana na muktadha maalum. Miktadha tofauti husababisha aina mbalimbali za lugha. Baadhi ya vipengele vya miktadha hiyo ni mada, eneo la matumizi ya lugha, mahusiano baina ya wahusikaumrijinsiawakati na kadhalika.
Mifano ya rejesta ni kama:
Rejesta za Mitaani, haya ni mazungumzo yanayozungumzwa magengeni nayo hueleweka na wazungumzaji wenyewe. Ni lugha ambayo huchipuka kutokana na kikundi cha watu ambacho ni kidogo. Mfano wa maneno yanayotumika sana mitaani ni kama vile “Mshikaji” (rafiki) Demu” (mwanamke). Kwa ujumla lugha ya mitaani ni lugha isiyo sanifu, ni lugha iliyojaa maneno ya mitaani ambayo yanaeleweka kwa wazungumzaji wenyewe.
Mazungumzo ya Kwenye Shughuli Maalum (Rejesta za Mahali):
Mazungumzo ya kwenye shughuli maalumu hayafanywi kiholela, bali yanafuata taratibu na kanuni maalum zinazojitokeza katika mazingira haya. Kutokana na kutumiwa kwake kwa muda mrefu kwenye mazingira yale yale.
Mazungumzo ya kwenye shughuli maalumu ni kama vile mazungumzo ya:
Maofisini au mahali popote pa kazi, Mahakamani, Hotelini, Hospitalini, Msikitini, Kanisani
Mazungumzo ya mahotelini yana utaratibu wake ambao katika hali ya kawaida inaweza isieleweke.
Nani wali kuku?
B: Mimi
Chai moja wapi?
B: Hapa
Katika mazungumzo haya A anapouliza “Nani wali kuku”, ana maana kuwa nani anahitaji kula wali na nyama ya kuku”. Hapa hana maana ya kumwainisha mtu aitwaaye “wali kuku”.
Kwa ujumla, rejesta ni mtindo wa lugha kutegemeana na kazi fulani, muktadha wa matumizi, lengo na uhusiano wa wanaowasiliana. Katika muktadha rasmi rejesta hurejelea upande mmoja kama vile, msamiati wa kiufundi, adabu maalum na matumizi ya lugha fasaha, mfano katika elimu, mahakamani na kadhalika.
5. Kwa mujibu wa Mekacha (2000), sera ya lugha ni jumla ya mawazo, matamko, sheria, kanuni na taratibu zenye kuelezea taratibu za utekelezaji wa mabadiliko ya nafasi na matumizi ya lugha katika jamii.
Pia, Rubin na Jernudd (1971), anasema sera ya lugha ni jumla ya matukio, shughuli au hatua mbalimbali za wazi na zisizo za wazi zinazochukuliwa hasa na dola kwa makusudi ya kuleta mabadiliko au kusitisha mabadiliko katika jamii kuhusiana na taratibu za matumizi ya lugha.
Kwa ujumla, sera ya lugha ni mawazo, matamko, sheria, kanuni na taratibu zenye kuelezea taratibu za utekelezaji wa mabadiliko ya nafasi na matumizi ya lugha katika jamii.
Sera ya lugha inapaswa kuzingatia mambo haya:
A. Namna lugha mbalimbali katika jamii zinavyopaswa kutumika kikamilifu.
B. Namna ya kujenga stadi za lugha zitakiwazo ili kukidhi mahitaji ya vipaumbele vya taifa.
C. Namna ya kutetea haki za watu, makundi ya jamii yanayotaka kujifunza na kudumisha lugha zao.
Serikali ndiyo yenye dhamana ya kutengeneza sera ya lugha. Kwa mfano, sera ya lugha nchini Tanzania, inatoa nafasi kubwa kwa lugha ya Kiswahili na lugha ya Kiingereza.
6. Sera ni utaratibu wa kuendesha jambo ili kukidhi haja za serikali, chama, dini au shirika. Utamaduni ni mila, asili, jadi na desturi za kundi la jamii fulani. Sera ya utamaduni ni taratibu zilizowekwa ili kulinda tamaduni, mila, asili, jadi na desturi za Watanzania. Bila kuwa na sera ya utamaduni, tamaduni za kigeni zinaweza kuharibu tamaduni zetu na kuzifanya zipotee.
Ipo mifano mingi inayothibitisha ufanyaji kazi wa sera ya utamaduni. Kwa mfano, wanamuziki wanaotoa picha zisizo na maadili wamekuwa wakifungiwa kazi zao kwa sababu kazi hizo haziendani na utamaduni wetu sisi Watanzania.
Sera ya utamaduni tuliyonayo nchini Tanzania ilianza kutumika mwaka 1997. pamoja na ubora ilionao, lakini bado ina mapungufu, sera hiyo siyo toshelevu kwa jamii ya sasa. Kwa mfano, kwa upande wa lugha ya Kiswahili bado sera haijaweka sheria kali dhidi ya wale wote wasiokitendea haki. Hali ya sera ya tamaduni kulega, imesababisha watangazaji wengi wa vyombo vya habari vya Kiswahili, kuchanganya lugha ya Kiswahili na Kiingereza pale wanapotangaza. Pia, hata wanapotangaza kwa lugha ya Kiswahili, wanatumia lugha mbovu ambayo ni kuharibu tamaduni zetu ikiwemo lugha hii ya taifa. Ni wakati sasa wa kupata sera mpya ya utamaduni kwani hii iliyopo imepitwa na wakati na haiendani na jamii ya sasa.
Marejeo:
TUKI. (1981). Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Nairobi. Oxford University Press.
Massamba, David 2004, "Kamusi ya Isimu na Falsafa ya Lugha", Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Msanjila, Y. (2009). Isimu Jamii: Sekondari na Vyuo. Dar es Salaam: Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili.

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Uhakiki wa Riwaya ya Watoto wa Maman’tilie