Maendeleo ya Kiswahili Kidato cha Tatu
Asili ya Kiswahili
Zipo
nadharia nyingi zinazoelezea kuhusu asili ya Kiswahili. Wengine wakisema
Kiswahili ni kiarabu, pijini, lugha ya vizalia na nadharia nyinginezo. Katika
nadhari hizo, nadharia inayosema kuwa Kiswahili ni Kibantu, inaelekea kuwa
kweli kwa sababu imejawa na ushahidi wa kuthibitisha madai yake.
Ushahidi wa kimsamiati unaothibitisha ubantu wa Kiswahili
Mizizi
ya msingi ya misamiati ya lugha ya Kiswahili na zile za kibantu hufanana sana.
Mfano:
Kiswahili |
Kikurya |
Kinyiha |
Kijita |
Maji |
Amanche |
Aminzi |
Amanji |
Jicho |
Iriso |
Iryiso |
Eliso |
Ukitazama
mifano hapo juu, utagundua kuwa, mizizi ya lugha za kibantu inafanana kwa kiasi
kikubwa na ile ya lugha ya Kiswahili.
Ushahidi wa kimuundo unaothibitisha ubantu wa Kiswahili
Muundo wa lugha za Kibantu hufanana
kwa kiasi kikubwa na ule wa lugha ya Kiswahili. Kwa mfano, namna viambishi
vinavyopachikwa katika mzizi wa maneno hufuata kanuni ileile kama inavyotumika
katika lugha ya Kiswahili yaani viambishi vinaweza kupachikwa kabla au baada ya
mzizi.
Mifano:
Kiswahili
Kisukuma Kisimbiti Kinyiha
A-na-lim-a a-le-lem-a a-ra-rem-a i-nku-lim-a
a-na-chek-a A-le-sek-a a-ra-sek-a
a-ku-sek-a
Kwa kuangalia mifano hii utagundua kwamba
katika kutenganisha viambishi hufuata kanuni moja kwamba mahali kinapokaa
kiambishi kwa mfano cha njeo, ndipo pia hukaa kwa upande wa lugha za kibantu,
kwa mfano –na- na –ra- katika lugha ya kisimbiti. Hivyo tunaweza kusema kuwa
kuna unasaba baina ya lugha hizi.
Jinsi miundo ya Kiswahili inavyofanana na miundo ya lugha nyingine za kibantu
Miundo ya sentensi za Kiswahili,
inafanana na ile ya sentensi za kibantu. Miundo yote, ina sifa ya kuwa na kiima
na kiarifu.
Kwa mfano:
Kiswahili – Juma/ anakula ugali
Kisukuma – Juma/ alelya bugali
Kukua na kuenea kwa Kiswahili nchini Tanzania katika enzi ya waarabu
Waarabu waliingia Tanganyika miaka mingi
sana iliyopita. Inakadiliwa kwamba, walifika kabla ya karne ya 10. Biashara yao
kubwa ilikuwa pembe za ndovu na kukamata watu ambao waliwauza kama watumwa. Ama
kwa ufupi, waarabu walijihusisha na biashara mbalimbali. Pamoja na biashara
hizo, waarabu walichangia kwa kiasi kikubwa sana kukua na kuenea kwa lugha ya
Kiswahili.
Ukuaji wa Kiswahili kimsamiati nchini Tanzania katika enzi ya waarabu-mchango wa waarabu katika kukua na kuenea kwa kiswahili
Waarabu hasa katika pwani ya Afrika
Mashariki walifanya biashara, ikiwamo biashara ya watumwa. Ilikuwapo misafara
mbalimbali ya biashara kutoka pwani hadi bara. Katika misafara hiyo Kiswahili
ndiyo iliyokuwa lugha ya mawasiliano hivyo Kiswahili kikaenea pia katika sehemu
za bara. Kuna mambo kadhaa waliyofanya Waarabu ambayo yalichangia kukua kwa
lugha ya Kiswahili. Waarabu walichangia kukua kwa lugha ya Kiswahili kama
ifuatavyo:
1. Biashara
Waarabu walifanya biashara kati ya
pwani na sehemu za bara, katika biashara yao walichangia uenezaji wa lugha ya Kiswahili.
Lugha kuu ya mawasiliano na ya kibiashara iliyotumiwa na wafanyabiashara wa
Kiarabu ilikuwa ni Kiswahili.
Kwa hiyo kwa njia hii waliweza kueneza
Kiswahili kuanzia pwani hadi maeneo ya bara kama vile Morogoro, Dodoma, Tabora,
Kigoma hadi Mashariki mwa Kongo.
2. Dini
Dini ilichangia ueneaji wa lugha ya
Kiswahili kupitia mawaidha na mafunzo ya madrasa. Waarabu walipokuja walitaka
kueneza dini ya Kiislamu katika maeneo waliyofikia. Hivyo, walianzisha madrasa
ambayo walitumia kufundisha huku wakitumia lugha iliyokuwa ikitumiwa ambayo ni
lugha ya Kiswahili.
3. Maandishi ya Kiarabu
Waarabu pia walileta hati zao
zilizotumiwa katika maandishi ya lugha ya Kiswahili. Kwa hiyo kupitia hati za
Kiarabu maandishi mbalimbali ya lugha ya Kiswahili yaliweza kuhifadhiwa. Hivyo
Kiswahili kilikua kutokana na kuhifadhiwa katika maandishi na kusomwa wakati
wowote.
4. Kuoana
Vilevile Waarabu waliofika pwani
waliweza kuoana na Wabantu. Hii ilisababisha kuzaliwa kwa watoto ambao
walizungumza lugha ya kati kutoka kwa wazazi wao. Na kwa sababu hiyo watoto
walichukua maneno mengi kutoka kwa baba na mama yao na hivyo kusababisha
kuzungumza lugha ya Kiswahili.
Kukua na kuenea kwa Kiswahili nchini Tanzania katika enzi ya wajerumani
Wajerumani waliingia katika pwani ya
Afrika Mashariki katika miaka ya 1875, walifanya kila jitihada kuwatawala
Waafrika ambapo katika utawala wao walifanya biashara, waliendesha shughuli za
kiutawala, za kidini na kielimu. Katika shughuli zote hizo Kiswahili kilitumika
kama lugha ya mawasiliano.
Walipongia katika pwani ya Afrika
Mashariki walikuta Kiswahili kimekwisha enea kwa kiasi kikubwa. Hivyo,
walishindwa kutumia lugha yao ya Kijerumani, wakaamua kujikita katika lugha ya
Kiswahili.
Wajerumani walikuza na kueneza lugha ya Kiswahili kupitia mambo haya:
1. Kutoa mafunzo ya lazima ya lugha ya Kiswahili kwa wafanyakazi wa serikali
Wajerumani waliweka sheria kwamba,
lazima kila mfanyakazi wa serikali ajue lugha ya Kiswahili. Hivyo, wafanyakazi
wote wa serikali ya kijerumani wakiwemo maakida, walijifunza lugha ya Kiswahili
ili wapate kigezo cha kuajiriwa au kubaki na ajira zao. Hata Wajerumani wenyewe
walilazimika kujifunza kiswahili ili waweze kuwasiliana na wenyeji kwa urahisi
na hivyo kurahisisha shuguli zao za kiutawala.
2. Ujenzi wa shule
Shule zilifunguliwa kufundisha watu
weusi ili waje wawe wasidizi wao katika utawala wa wajerumani, na lugha
iliyokuwa ikitumika kufundisha masomo ilikuwa ni lugha ya Kiswahili.
3. Kuenea kwa utawala wa Wajerumani nchi nzima
Kwa kuwa utawala wa Wajerumani ulikuwa
nchi nzima, basi kila ofisi palizungumzwa lugha ya Kiswahili na hii ilisaidia
Kiswahili kuweza kukua na kuenea zaidi.
4. Shughuli za kilimo
Manamba au vibarua walilazimishwa wajue
lugha ya Kiswahili. Waliporudi nyumbani, walisaidia kueneza lugha hii.
5. Mahakama
Wafanyakazi waliwahoji na kuandika
hukumu kwa watuhumiwa kwa kutumia lugha ya Kiswahili. Hivyo Kiswahili kilikua
na kuenea.
Hivyo ndivyo Wajerumani walivyosaidia
kukuza na kueneza lugha ya Kiswahili. Kumbe, pamoja na mabaya yote ya
Wajerumani, walitenda baadhi ya mema. Waswahili walisema, pamoja na ubaya
alionao fisi, hakosi mke.
Maswali
1. Kiswahili ni Kibantu kwa asili yake.
Fafanua kwa kutumia ushahidi wa kimsamiati na kimuundo.
2. fafanua tofauti iliyopo kati ya
pijini na krioli.
3. Asili ya Kiswahili ni Kiarabu. Eleza
dai hili kwa kutumia kigezo cha msamiati.
4. Lugha ya Kiswahili ilikuwa
inazungumzwa hata kabla ya ujio wa wageni. Thibitisha dai hili.
5. i. Utofauti wa kimatamshi, kimaumbo
na matumizi ya maneno ya lugha kuu moja katika maeneo mbalimbali huitwa ___________
a. lafudhi b. lahaja c. rejista d.
msimu e. toni
ii. Hamsini, laki, kasri na fikri ni
miongoni mwa maneno yanayothibitisha kuwa Kiswahili ni________
a. kiarabu b. krioli c. kibantu d.
pijini e. chotara
iii. Kiisimu, upi ni mtazamo sahihi
kuhusu chimbuko la Kiswahili?
a. Ngozini b. Shungwaya kuu c. kiarabu
d. pijini na krioli e. Pwani ya Afrika mashariki
iv. Lahaja ya Kishela inazungumzwa
katika eneo lipi kati ya haya?
a. Tanga b. Kisiwa cha lamu c. Mombasa
d. Unguja mjini e. Kisiwa cha pemba
v. Hoja za msingi zinazosema kuwa
Kiswahili ni Kiarabu, zimeegemea katika___________
a. msamiati na dini ya Kiislamu b.
msamiati c. msamiati wa waarabu kuoa waafrika d. dini ya kiislamu na biashara
ya watumwa e. msamiati na lugha za Kibantu