Msimamo wa Massamba Kuhusu Asili ya Lugha ya Kiswahili

Barabara ya vumbi.


Jadili kwa mifano na hoja maridhawa msimamo wa Massamba (2002) kuhusu asili ya lugha ya Kiswahili.

Fasili ya lugha kwa mujibu wa crystal (1992) anasema, lugha ni mfumo wa sauti nasibu, ishara au maandishi kwa ajili ya mawasiliano na kujieleza katika jamii ya watu. Katika fasili yake ametaja mambo makuu matano ambayo ni mfumo, sauti za nasibu, sautialama na ishara, jamii ya wanadamu, mawasiliano na kujieleza/kujitambulisha.
Massamba na wenzake (1999), lugha ni mfumo wa sauti za nasibu ambazo hutumiwa na jamii kwa madhumuni ya mawasiliano kati yao.
Neno asili lina maana ya jinsi jambo lilivyoanza au lilivyotokea. Zipo nadharia kadhaa kuhusu asili ya lugha ya Kiswahili. Ya kwanza ni ile isemayo kwamba Kiswahili kimetokana na lugha ya kiarabu, ya pili ni ile isemayo kuwa Kiswahili kimetokana na mchanganyiko wa lugha ya kiarabu na lugha za kibantu zilizokuwa katika upwa wa Afrika Mashariki, ya tatu inasema kuwa Kiswahili ni lugha ya Kibantu iliyoathiriwa sana na lugha ya Kiarabu na ya nne inadai kwamba, lugha ya Kiswahili iliibuka kutokana na mchanganyiko wa lugha kadhaa za kibantu zilizokuwa katika upwa wa Afrika Mashariki na ikaathiriwa sana na kiarabu, kimsamiati katika kukua kwake.
Madai ya Kiswahili kutokana na kiarabu. Nadharia hii imeegemezwa kwenye wingi wa maneno yenye asili ya Kiarabu na dini ya Kiislamu. Hapa kuna madai ya aina mbili: kwanza inadaiwa kwamba maneno mengi yenye asili ya Kiarabu yaliyomo katika lugha hii ni ishara kwamba lugha hii ilianza kama pijini ya kiarabu. Pili inadaiwa kwamba kwa kuwa Kiswahili kilianzia pwani, kwa kuwa idadi kubwa sana ya wenyeji wa pwani ni Waislamu, na kwa kuwa Uislamu uliletwa na Waarabu, basi Kiswahili nacho kililetwa na waarabu.
Madai haya yote hayana ukweli kwa sababu hoja zake hazishawishi wala hazina nguvu. Ukweli ni kuwa, lugha ya Kiswahili imetokea kuwa na maneno ya mkopo yenye asili ya Kiarabu kutokana na ukweli kuwa, kulikuwa na mawasiliano ya karne nyingi baina ya wenyeji wa pwani na wafanyabiashara wa kiarabu. Wasemaji wa lugha mbili tofauti wanapokuwa na mawasiliano ya muda mrefu hawaachi kuathiriana kilugha. Pia, Kiswahili hakijachukua maneno ya Kiarabu pekee. Kinayo maneno kutoka lugha mbalimbali kama: Kiajemi, Kihindi, Kireno, Kijerumani na Kiingereza.
Jambo la msingi kuhusu nadharia ya Kiswahili kutokana na Kiarabu ni kuwa, lugha kuwa na maneno mengi ya mkopo kutoka lugha nyingine peke yake haiifanyi lugha hiyo isemekane kuwa imetokana na hiyo lugha nyingine. Jambo la muhimu kuzingatia ni muundo wa lugha kifonolojia, kimofolojia, kimsamiati na kisintaksia.
Nadharia nyingine inadai kuwa lugha ya Kiswahili ilitokana na mchanganyiko wa lugha ya Kiarabu na pwani ya Afrika Mashariki yaani lugha ya Kiswahili ni lugha chotara. Nadharia hii imekuwa ikichochewa na maandishi wa wataalamu mbalimbali wa kigeni. Madai yanayotolewa na watetezi wa nadharia hii ni kwamba, kwa kipindi cha karne nyingi wafanyabiashara wa Kiarabu walikuwa wakija katika upwa wa Afrika Mashariki. Katika kuendesha shughuli zao, ilibidi Waarabu waunde namna fulani ya lugha ili waweze kuwasiliana. Hapo ndipo ilipotokea lugha hiyo chotara.
Hoja kuwa Kiswahili ni lugha chotara haina ukweli kwa sababu kama Kiswahili kingekuwa pijini iliyotokana Kiarabu, sarufi ya lugha ya Kiswahili isingechukua muundo wa lugha za kibantu.
Msimamo wa Massamba (2002) kuhusu asili ya lugha ya Kiswahili ni kuwa, Kiswahili kimetokana na Kibantu kama inavyoelezwa:
Tunapokuwa tunalinganisha lugha katika kiwango cha kifonolojia kuna mengi ya kuzingatia, lakini muhimu ni mpangilio wa vitamkwa kuunda silabi na kanuni mbalimbali za kujenga maneno. Katika lugha ya Kiswahili silabi huunda muundo wa : I = Irabu peke yake, k.m a; KI = Konsonanti na Irabu, k.m. ba, ma, ta; kI = Kiyeyusho na Irabu, k.m. mba, nga, nje; KkI = Konsonanti, Kiyeyusho, Irabu, k.m. kwa, mwa, bwa; KKkI = Konsonanti, Konsonanti, Kiyeyusho, irabu, k.m. mbwa, ngwa, n.k. kanuni hizi hizi ndizo pia zinazotumiwa na lugha zote za Kibantu zijulikanazo.
Maneno yote ya Kiswahili yasiyotokana na mkopo yanafuata utaratibu wa viambishi na mizizi. Viambishi vinaweza kutangulia mzizi,k.m. m - toto, wa - toto, ki - jiko, vi - jiko au vinaweza kuwa mwishoni mwa mzizi, k.m. tamk - a, tamk - I -a. Lugha zote za Kibantu pia zinafuata utaratibu huo huo. Chunguza mifano ifuatayo:
Kiswahili mwa-ana che-ka ku-la
Ci-Gogo mwa-ana se-ka kulya
Ci-Ruli o-mwa-ana se-ka o-ku-lya
Kihacha o-mo-ana se-ka ku-rya
Mifano hii inaonyesha wazi kwamba muundo wa silabi katika lugha hizi zote ni ule ule.
Msamiati wa msingi ni ule unaohusu mambo ambayo hayabadilikibadiliki kutokana na mabadiliko ya utamaduni; ni msamiati ambao unahusu vitu vya asili, kama vile sehemu za mwili kama kichwa, macho, mkono, mgongo, tumbo, sehemu za siri, mguu, kiuno, n.k. au sehemu za mazingira ya asili kama vile jua, mwezi, ardhi, milima n.k Msamiati kama huu ndio ambao huweza kutudhihirishia kuwa lugha fulani imo katika kundi gani. Ukiuchunguza msamiati wa msingi uliomo katika Kiswahili utaona kwamba ni ule ule unaojitokeza katika lugha nyingine za Kibantu. Tofauti zinaweza kujitokeza katikamatamshi au mabadiliko kidogo ya viambishi vyake lakini si katika mizizi. Ifuatayo ni mifano ya maneno ya msamiati wa msingi kutoka lugha hizo zilizotajwa hapo juu.
Kiswahili Ci-Gogo Ci-Ruri Kihacha
Kichwa mutwe omutwe omutwe
Macho meso ameeso amiiso
Mgongo mugongo omugoongo omugoongo
Mguu mugulu okuguru okuguru
Kiuno ciuno cibunu kibuno
Ama kuhusu sintaksia pia tunaona kwamba hali ni ileile. Utaratibu wa muundo wa msingi wa sentensi za Kiswahili ni ule ambao, kwa mujibu wa sarufi za kimapokeo unachukua mpangilio wa Kima - Prediketa - Yambwa. Utaratibu huu unajidhihirisha wazi katika mfano huu.
Juma amekwenda shambani
(kiima) (Prediketa) (Yambwa)
Pamoja na kwamba mpangilio huo unaweza kubadilishwa, lakini ubadilishaji wake nao huwa una mpango na maana maalumu, kama, kwa mfano, kusisitiza kitu au kukifanya kichomoze katika mazungumzo. Lugha zote zenye asili ya kibantu hufuta utaratibu huo wa msingi ambao lugha ya Kiswahili inaufuata. Ili kuweza kupata picha kamili ya kile kisemwacho hapa linganisha sentensi ya Kiswahili na sentensi ya Ci-Ruri na Kihacha katika mfano ufuatao:
LUGHA
KIIMA
PREDIKETA
YAMBWA
Kiswahili
Mwalimu wetu
amekwenda
shambani
Ci-Ruri
Mwalimu weswe
aagenda
mwisaambu
Kihacha
Mwalimu wetu
agiiyi
kumuguundu
Kwa kuhitimisha, msimamo wa Massamba kuhusu asili ya lugha ya Kiswahili ni kuwa Kiswahili ni Kibantu. Hii ni kwa sababu sarufi ya lugha ya Kiswahili kwa kila hali inazingatia kabisa taratibu na kanuni za lugha za kibantu. Hivyo basi kuna kila sababu ya kusema kwamba, lugha ya Kiswahili kusema kweli ni lugha ya kibantu wala si lugha ya Kiarabu au lugha chotara kama inavyodaiwa na baadhi ya watu.

Marejeo

Crystal, D. (1985). A Dictionary of Linguistics and Phonetics. Oxford. Basil Blackwell.
Massamba na wenzake. (1999). Sarufi Miundo ya Kiswahili Sanifu. Dar es Salaam: Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili.
Massamba, D. (2002). Historia ya Kiswahili: 50 BK hadi 1500 BK. Nairobi: Jomo Kenyatta Foundation.Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024

Uhakiki wa Riwaya ya Watoto wa Maman’tilie