Dhana ya Uolezi Inavyojitokeza Katika Lugha ya Kiswahili

Dira

Swali

Fasili dhana ya uolezi kisha ufafanue kwa ufasaha unavyokitokeza katika lugha ya Kiswahili.

Jibu

Kwa mujibu wa Resani (2014), Uolezi ni istilahi iliyoazimwa kutoka lugha ya Kigiriki yenye maana ya kuashiria kwa kutumia lugha. Ni kipashio muhimu cha kipragmatiki cha kuwakilisha lugha na miktadha ya kiusemi.

Akifafanua zaidi kuhusu dhana ya uolezi, mwandishi anaeleza:

Katika isimu, uolezi ni dhana inayotumiwa kurejelea hali ambayo, ili mtu aweze kuelewa maana ya maneno fulani na virai fulani vilivyotumiwa katika tamko fulani, basi hana budi kuuelewa muktadha ambamo msemaji na wasemeshwaji huwa. Maneno ambayo yana maana thabiti ya kisemantiki, lakini vilevile yana maana halisi ambayo hudabilikabadilika kutegemea wakati au mahali, basi yana sifa ya uolezi. (Resani, 2014:79)

Uolezi ni uonyeshaji maalumu wa vitu, mahali, watu, hali au uelekeo katika muktadha husika wa mazungumzo (Makoba, 2018).

Si rahisi kwa mtu asiyeelewa muktadha husika kujua ni kitu gani kinarejelewa kwa wakati huo. Mfano, ukija, yeye utamkuta pale. Maneno yaliyopigiwa msitari ni violezi na siyo rahisi kwa mtu asiyeelewa muktadha husika kuelewa vitu vilivyorejelewa na maneno hayo. Uelewekaji wa maneno hayo, unategemea muktadha.

Kiolezi hurejelea neno au kiambo ambacho huhushisha semo na mahali, nafsi na hali. Urejeleo wa kiuolezi hutegemea muktadha. Hivyo violezi ni maneno maalumu katika lugha yatumikayo kuleta urejelezi wa kimuktadha. Uolezi ni dhana itumikayo katika pragmatiki kuakisi uhusiano unaorejelewa katika muktadha wa msemaji na msikilizaji.

Kwa ujumla, uolezi ni uashiriaji unaotumia lugha. Uashiriaji huu, hufanywa katika mazungumzo na kwa yeyote asiyeelewa muktadha husika, itamuwia ngumu kuelewa kitu kinachoerejelewa. Hivyo basi, uelewekaji wa maneno hayo unategemea muktadha.

Ili kuielewa zaidi dhana ya uolezi, tutazame aina zake na kupitia aina hizo, itafafanuliwa kwa ufasaha namna uolezi unavyojitokeza katika lugha ya Kiswahili.

Uolezi nafsi, huu ni uolezi unaodhihirishwa katika usemi kwa kutumia viwakilishi vinavyorejelea nafsi, kama vile: mimi, yeye, yule, nyinyi, hawa.

Uolezi nafsi unajitokeza katika lugha ya Kiswahili kwanza, hutumiwa na msemaji anapojirejelea mwenyewe au anaporejelea msemeshwaji au mtu wa tatu katika mawasiliano. Pili, katika Kiswahili maneno haya hutumika katika hali ya umoja na wingi, na huhusiana na ngeli mahususi.

Uolezi wakati, huu ni uhusiano wa maneno fulani yanayorejelea wakati katika muktadha fulani. maneno hayo ni kama vile: sasa, leo, kesho, keshokutwa, baadaye, mtondo, mtondogoo, jana, juzi, siku zijazo na maneno mengine mengi ambayo hurejelea wakati.

Uolezi wakati unajitokeza katika lugha ya Kiswahili kwa namna mbalimbali. tutumie mfano wa wafanyabiashara wanaoogopa kukopwa, katika maduka yao hutundika ilani inayosomeka, “Bwana mkopo amesafiri, atarudi kesho.” Hufanya hivi kwa kufahamu kwamba kesho haiishi. Pia, watu wanapopanga ratiba mbalimbali kuhusu mambo kama sherehe na mengineyo, hutumia uolezi wakati.

Uolezi mahali, huu ni uolezi ambao unahusu mahali pa kitu kwa kuwiana na mahali pa tamko. Uolezi huu unaweza kuhusu mahali pa msemaji na msemeshwaji, au mahali pa watu au vitu vinavyorejelewa katika tamko.

Katika lugha ya Kiswahili, uolezi mahali upo  wa aina tatu:

Viashiria vya uolezi wa mahali pa karibu kabisa na msemaji. Kwa mfano, maneno kama hapa, huku na humu.

Viashiria vya uolezi wa mahali pa karibu kidogo na msemaji. Kwa mfano maneno kama, hapo, huko na humo na,

Viashiria vya uolezi wa mahali pa mbali na msemaji. Kwa mfano, maneno kama: pale, kule na mle.

Uolezi wa mahali unajitokeza katika lugha ya Kiswahili kwani kwa kawaida inaeleweka kuwa, maneno yanayoashiria uolezi mahali yanahusishwa na mahali alipo msemaji. Kwa mfano, katika utungo, “Duka la Mangi liko mtaa wa pili.” Kirai mtaa wa pili humaanisha mtaa wa pili kutoka hapa nilipo sasa.

Uolezi jamii ni aina nyingine ya uolezi. Uolezi jamii hurejelea taarifa za kijamii ambazo hutumiwa katika viyambo. Maana ya tungo hutegemea uhusiano wa kijamii uliopo baina ya msemaji na msemeshwaji. Maneno hupata maana kamili yanapotumiwa kuhusiana na wahusika fulani.

Uolezi jamii unajitokeza katika lugha ya Kiswahili kwa namna mbalimbali kwa mfano, mtu anapokuwa anamtambulisha mke wake anaweza sema, “Huyu ni mke wangu mpenzi.” Lakini anapomtambulisha mke kwa kusema huyu ni Mariam, inapunguza ladha fulani.

Uolezi mwingine ni uolezi matini. Huu ni uolezi ambao unaonyesha urejelezi ulio ndani ya makala. Makala hiyo inaweza kuwa ya kuandikwa au kusemwa. Kwa jina jingine, makala ya kusemwa inaitwa kilongo. Kwa mfano, tunaweza kurejelea kwa kusema, ‘hii ni hadithi ya Sungura na Fisi.’ Katika usemi huu, neno hii hurejelea sehemu ya kilongo itakayofuatia.

Uolezi matini unajitokeza kila siku katika lugha ya Kiswahili maneno ya kuongeza kama, zaidi ya hayo, kwa kuongezea, mintarafu ya hayo huonekana katika lugha. Pia maneno ya kusababisha kama, kwa sababu, kutokana na  na kwa hivyo. Mengine ni viwakati, mfano, baadaye, kwanza, baada ya muda, baada ya saa moja na virejeleo vya matukio, mfano, Maimuna anamjua yeye, hivi vyote vinajitokeza katika lugha ya Kiswahili.

Pia, uolezi mwelekeo nao ni aina ya uolezi ambao utatusaidia kuona namna uolezi unavyojitokeza katika lugha ya Kiswahili. Huu unahusu nafasi ya kitu kimoja kimwelekeo kikilinganishwa na nafasi ya kitu kingine. Uolezi mwelekeo ni pamoja na juu na chini. Maneno kama: magharibi, mashariki, kaskazini na kusini.

Hivyo basi maneno kama Afrika Mashariki, Tanzania kanda ya Magharibi, Nyanda za juu kusini, ni mifano inayodhihirisha wazi namna ambavyo uolezi unajitokeza katika lugha ya Kiswahili.

Hivyo basi, dhana ya uolezi ni dhana ambayo inaeleweka kwa urahisi na inajitokeza katika lugha ya Kiswahili. Kupita aina za uolezi, tumeweza kuona namna uolezi unavyojitokeza katika lugha ya Kiswahili, kumbe, ni vigumu sana kuuona uolezi unavyojitokeza katika lugha ya Kiswahili bila kutazama aina zake. Tunaweza kusema kuwa, uolezi katika lugha ya Kiswahili unajitokeza katika matini, jamii, mahali, wakati na nafsi.

Marejeleo

Leech, G. (1981) Semantics. London: Penguin.

Makoba, D. (2018) Semantiki na Pragmatiki ya Kiswahili | KI 311: Inapatikana katika https://www.mwalimumakoba.co.tz/2018/04/semantiki-na-pragmatiki-ya-kiswahili-ki.html. Ilisomwa tarehe 31 Mei 2022.

Resani, M. (2014) Semantiki na Pragmatiki ya Kiswahili. Dar es Salaam: Karljamer Print Technology.

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Uhakiki wa Riwaya ya Watoto wa Maman’tilie