Tofauti ya Semantiki, Pragmatiki na Semiotiki
Swali
Semantiki, pragmatiki na
semiotiki ni taaluma zinazojishughulisha na maana. Huku ukitoa mifano dhahiri,
eleza kwa ufasaha kiini cha tofauti baina ya taaluma hizo.
Jibu
Wataalamu wengi wametoa
maana ya Semantiki. King’ei (2010), Semantiki, ni taaluma ya isimu inayofafanua
maana katika lugha.
TUKI (2004), Semantiki, ni
tawi la isimu ambalo hujishughulisha na uchambuzi wa lugha katika kiwango cha
maana.
Katika mtazamo huu,
Semantiki ni utanzu wa isimu unaochunguza maana katika lugha ya mwanadamu
ukitafiti maana za fonimu, mofumu na maneno na tungo.
Nayo Pragmatiki imetolewa
maana na wataalamu wengi, Leech (1981), anasema semantiki inaangalia maana ya matamshi, maumbo na Miundo katika
lugha. Anaendelea kusema Maana ni sehemu
ya umilisi na ufahamu wa lugha, kujifunza Lugha ni kukubaliana na maana za
vipengele vyote vilivyopo katika lugha.
Richmond (2012), anasema
kwamba ni tawi la Lugha linalojihusisha na matumizi ya lugha kwa kuzingatia
Muktadha wa wazungumzaji husika. Hivyo Thomason anadai kuwa pragmantiki inahusu
zaidi mambo mawili: Matumizi na Muktadha.
Kwa ujumla, pragmatiki ni
taaluma ya semiotiki ambayo huchunguza ishara na maana zake ndani ya muktadha
wa jamii husika, ni utanzu wa isimu unaochunguza maana ya lugha ya binadamu
katika miktadha yote inayomzunguka.
Semiotiki imefasiliwa na
wataalamu mbalimbali, na hizi ni maana zilizotolewa na baadhi ya wataalamu hao.
Kwa kuanza na mtaalamu Massamba (2004), yeye anasema kuwa, semiotiki ni taaluma
ya kisayansi inayojishughulisha na uchunguzi na uchanganuzi wa mifumo ya ishara
mbalimbali ikiwa inazingatia zaidi uhusiano baina ya kiwakilishi na kitajwa.
Pia mtaalamu Ferdinand de
Saussure kama alivyonukuliwa na Morris (1971) amefasili semiotiki ni uhusiano
kati ya alama na kitu, jambo au hali ya kitu inavyowakilishwa, akaendelea alama
ni kiashiria na kitu ni kiashiriwa. Hakuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya
kiashiria na kiashiriwa.
Kwa ujumla, semiotiki ni
taaluma inayojishughulisha na uchunguzi wa ishara na alama pamoja na uhusiano
kati ya alama na kitu husika.
Zifuatazo ni tofauti kati ya Semantiki na Pragmatiki:
Semantiki hueleza maana kwa
kuzingatia misingi ya lugha yenyewe lakini pragmatiki hueleza maana kulingana
na mahusiano ya kiusemezano yanayokuwepo kati ya msemaji na msemeshwaji. Katika
pragmatiki maana hutolewa huku ikihusishwa au kutegemeana na mzungumzaji wa
lugha, hii inamaana kuwa katika pragmatiki, maana ya neno au tungo inategemea
nini mzungumzaji anakusudia kusema. Mfano, mtu anaweza kusema leo niko ovyo
akiwa na maana ya kwamba hana hela WAKATI
katika semantiki, maana hutolewa ikiwa safi na hutolewa kama jinsi
inavyopaswa kuwa kutoka katika lugha husika, na maana hiyo ndiyo huchukuliwa
kama ndiyo njia ya mawasiliano.Mfano, mtu ana kuwa wazi tu kusema kuwa leo sina
hela.
Semantiki huichukulia lugha
kuwa ni mfumo dhahania wa alama lakini pragmatiki huichukulia lugha kuwa ni
kifaa cha mawasiliano kinachoweza kutumiwa kadri ya matakwa ya msemaji.
Semantiki huelezea maana ya
msingi tu lakini pragmatiki hueleza maana inayokusudiwa na msemaji na ile
inayoeleweka kwa msemeshwaji. Neno katika semantiki ndilo hubeba maana ya
msingi na hulenga maana halisi ya neno kama jinsi ambavyo wazungumzaji wa lugha
hiyo walivyolizoea toka enzi na enzi. Maana hii ya msingi huwa haibadiliki
katika jamii zote zinazotumia neno hilo. Mfano, neno “baba” huwa na maana moja
tu ya msingi ambayo ni mzazi wa kiume wakati katika pragmatiki, hali hiyo ni
tofauti, ambapo neno hutazamwa katika mtazamo wa kidhima huku likihusishwa na
muktadha ambapo neno hilo limetumika.Mfano, neno “mtoto” hubadilika kulinga na
muktadha ambapo kwa muktadha mwingine hutumika kama mpenzi Hii ni kwa mujibu wa
Carston (1998) na Louise McNally.
Semantiki na pragmatiki ni
mapacha wawili wanafanana na kutofautiana kwa kuwa kilengwa chao ni kimoja. Kwa
hiyo, mtumiaji wa lugha anapaswa kuzifahamu zote mbili kwa kuwa ni vigumu
kupata maana katika semantiki tu, bali maana nyingine huhitaji kuhusishwa na
muktadha husika.
Tofauti nyingine ni, Maana
ya kipragmatiki kwa kiasi kikubwa huathiriwa na nia au kusudio au saikolojia ya
mzungumzaji na siyo kama jinsi ambavyo sentensi inavyomaanisha.Mfano, mtu
anaweza kutumia neno ambapo akawa na lengo la kuficha uma isijue nini
kinaendelea kwani anaweza kusema umekiona wapi kitabu changu leo wakati huo
akiwa na maana ya mpenzi wake WAKATI katika semantiki, kusudio na nia ya
mzungumzaji ni sharti ikubaliane na kanuni za lugha husika, ikiwa ni pamoja na
kufuata taratibu za muundo wa sentensi yaani mpangilio wa viambajengo katika
sentensi.Mfano, mtu ana kuwa huru kuongea kile ambacho anakimaanisha yaani kama
ni kitabu basi anakuwa anamaanisha kitabu kweli na sio vinginevyo (Carston, 1998).
Katika semantiki viwango
vinavyochunguzwa ni pamoja na fonimu→mofu→maneno→virai
na sentensi lakini Pragmatiki huchunguza zaidi namna lugha ianvyotumika katika
muktadha mbalimbali. Mfano, muktadha wa buchani mtu anaweza kusema mimi utumbo
na akaeleweka vizuri kabisa.
Semantiki imegawanyika
katika matawi mawili yaani semantiki ya kileksika ambayo hujihusisha na maana
za maneno na mahusiano ya maana katika sentensi na tawi la pili ni semantiki ya
virai au sentensi ambayo hujihusisha na maana za maneno katika kiwango cha
kisintaksia WAKATI HUO Pragmatiki hujidhihirisha katika mazingira mawili yaani
maana inayopatikana katika mazingira ya kiisimu. Mfano, kuna baadhi ya maneno
hayawezi kupata maana mpaka yatumike na maneno mengine katika sentensi, maneno
hayo kama vile na, juu ya kwa. Mfano, amekuja kwa basi. Sura ya pili ni maana
inayopatikana katika matumizi yake katika muktadha fulani katika ulimwengu wa
watumia lugha .Mfano, maana za maneno zitakazotumika katika muktadha wa stendi,
mfano mtu anaweza kusema nitafutie vichwa vitatu na akaeleweka vizuri katika
muktadha huo.
Kwa upande wa semiotiki,
tunasema kuwa:
Alama zinazoshughulikiwa huwa
katika maumbo mbalimbali. Zinaweza kuwa katika umbo la maneno, picha, sauti,
harufu, ladha, vitendo au vitu.
Maana katika semantiki
huangalia pia maneno kihistoria na kisasa yaani etimolojia.
Pia, semiotiki ni kama bwawa
ambamo semantiki huchota baadhi ya alama na kuzitumia katika mfumo wa lugha.
Semantiki ni taaluma ndogo ndani ya taaluma kubwa ya semiotiki.
Lakini ieleweke kwamba,
alama zinazotumiwa katika lugha hazina uhusiano wa moja kwa moja kati yake na
maana inayohusishwa na alama hizo yaani lugha ni mfumo wa sauti za kinasibu, si
usababishi au ufanano.
Hivyo basi Semantiki
inatofautiana na semiotiki kwani semantiki inashughulikia alama za lugha yaani
kila lugha huwa na alama zinazoashiria kitu fulani wakati alama za semiotiki
hazihusu lugha yaani huwa ni maana za mawasiliano, mfano ishara za mawingu,
wanyama kama bundi ishara ya uchawi.
Kwa kuhitimisha: Semantiki,
semiotiki na pragmatiki, zinatumika sana katika na watumiaji wa lugha katika
ulimwengu na ni vigumu kuzitofautisha kwani hujikita kuchunguza maana za maneno
katika muktadha tofauti tofauti kama sehemu ya mfumo wa mazungumzo sambamba na
kufafanua mfumo fungamanifu wa mazungumzo katika lugha. Hata hivyo, kuzisoma
taaluma hizi kutaondoa ugumu huo.
Marejeo
Alghamdi, R
(2013)Similarities and Differences between Semantics and Pragmatics.
Carston,R (1998) The
Semantics/Pragmatics Distinction: a view from relevance theory. Katika UCL
Working Papers in Linguistics.
Geoffrey Finch (2012),
Linguistic; Terms and Concepts. Palgrave. Macmillan publishers.
Massamba P. B. D (2004)
Kamusi ya Isimu na Falsafa ya Lugha. Dar es Salaam: TUKI.
Morris, Charles W. (1971),
Writings on the general theory of signs, The Hague: Mouton.
Peirce, Charles S (1934),
Collected papers: Volume V. Pragmatism and pragmaticism. Cambridge, MA, USA:
Harvard University Press.