Mwanamke Uliyekula Pesa Zangu Nakutafuta | Sehemu ya 11

Mako kazini

Nilikuwa barabarani natembea, ilikuwa siku ya vurugu kwani vibanda vya wamachinga vilivyokuwa katika hifadhi ya barabara, vilikuwa vinabomolewa na kusababisha vilio vikubwa. Inasemekana mwanzoni serikali iliwaruhusu wafanye biashara, wakajenga vibanda, lakini sasa serikali hiyohiyo iliwataka waondoke kwa madai kuwa ilikuwa ina wapanga vizuri. Hata sikuelewa, nikaendelea na safari zangu.

Nilishtuka nilipopita katika nyumba aliyoishi Asi, niligundua kuwepo kwa dalili za mtu kurejea hapo. Kwanza mazingira yalisafishwa na taa ya nje haikuzimwa japo ilikuwa saa tisa mchana. Nikahisi kurejea kwa Babuu. Kisha nikaandaa jambo langu.

XX    XX    XX

Mlango ulifunguliwa saa saba usiku, mwanamume mwenye kipara akaingia, akabofya swichi iliyokuwa upande wa kushoto, taa ikawaka na hapo akajionea yale asiyoyatarajia. Chumbani palikuwa na mgeni asiyekaribishwa, tena aliikamata vyema bastola yake na alielekeza alipo, hakuonekana kuwa na masihara hata kidogo.

Mwanamume mwenye bastola ni mimi Mako, na huyo aliyeingia ni Babuu. Nilikaa kona ya mwisho ya kitanda, nikatengeneza umbali mzuri.

“Kaa pale,” nilimuelekeza Babuu. Naye akatii kwa kukaa katika kiti kilichokuwa karibu na mlango. Kiti hiki kiliongezeka, mwanzoni nilipoingia, sikukikuta.

“Wewe ni nani?” aliuliza Babuu kwa sauti nene yenye kitetemeshi.

“Naitwa Mako,” nilijibu kwa upole.

“Sina pesa humu ndani kama ni hicho ulichofuata,” alijitetea Babuu.

“Sijafuata pesa, shida yangu moja, niambie ulipompeleka Asi na wenzake.”

Maneno yangu yalimshitua, hata hivyo alijikaza akazungumza, “Wanakuhusu nini watu hao?”

“Nataka tu kujua ulipowapeleka, utaniambia au nitafute namna ya kukulazimisha?”

Katika kosa alilofanya Babuu ni kujaribu kukimbia, muda alipoingia, hakufunga mlango na nilimgundua muda mrefu kuwa alikuwa anapiga hesabu za kukimbia. Hata hakuufikia mlango, nilimsindikiza kwa teke zito, akadondoka chini kama mzigo. Sasa nikaizamisha bastola yangu katika mdomo wake.

“Utanieleza ulipompeleka Asi na wenzake?” niliuliza kwa upole kama hakuna kilichotokea.

“Mmmmh…. Mmmhh…” alilalama bastola ikiwa mdomoni, nikaitoa ili apate kusema.

“Asi yupo India hivi sasa, wenzake watatu wapo Misri, wanne wapo Oman,” alijibu, nikamtazama usoni na kugundua alichosema ni kweli.

“Unafanya biashara ya kuuza watu siyo, huko India Asi yupo mahali gani?”

“Sijui, unajua mimi kazi yangu ni kuwakusanya, kisha anakuja ajenti mkuu, Akshay, yeye ndiyo anajua wateja, mimi napewa changu tu.”

“Sasa umejuaje kama Asi yuko India?”

“Kazi yangu nyingine ni kufuatilia hati za kusafiria kwa kila mmoja, pia tunapoagana huwa najua kabisa huyu anakwenda huku na huyu anakwenda kule.”

“Wakati wote ambao hukuwepo hapa, ulikuwa wapi?”

“Ajenti alikuja, hivyo tulibadili makazi na kwenda hotelini, halafu siyo salama kukaa sehemu moja tena mwishoni mwa dili kukamilika.”

Niliachana na Babuu, nikatoka taratibu mpaka katika makazi yangu ambako nilipanga ramani ya kazi. Nikawa bize katika kompyuta yangu mpakato nikituma taarifa hii na ile kuelekea nilikokujua mwenyewe.

XX    XX    XX

Saa tisa mchana nilianza safari kuelekea India. Dar es Salaam nilipanda ndege ya Emirates, Boeing 777 EK 726, mimi na abiria wenzangu tukafika Dubai saa tatu usiku, tukapata mapumziko ya saa nyingi. Saa tisa usiku, tukapanda dege jingine la Emirates, Boeing 777 EK 510, dege hili lilitubembeza huko angani kwa muda wa saa sita, likatushusha Delhi saa tatu asubuhi.

Hapo New Delhi ama ninavyopenda kupaita kwa ufupisho, Delhi, nilifikia hoteli ya bei ndogo, Airport Hotel Mayank Residency, mimi napaita Mayank Hotel. Gharama yake ni sawa na shilingi elfu ishirini na sita tu za Kitanzania kwa siku moja. Hii ni bei ndogo mno kwa hoteli yenye hadhi ya nyota tatu. Tena jambo la kufurahisha ni kwamba, hotel hii ilikuwa karibu kabisa na Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Indira Ghandhi, hata wakati wa kwenda, nilitembea kwa miguu kwani ni umbali wa kilomita moja na nusu tu. Uwanja huu umepewa jina hili kama sehemu ya kumbukumbu ya mpigania uhuru na baba wa taifa hilo ndugu, Indira Karamchand Mahatma Ghandi.

Chumba changu kilikuwa na kitanda kimoja cha kifahari. Kushoto palikuwa na viti viwili na meza ndogo, na upande huohuo palikuwa na kabati zuri lililowekwa kioo kirefu pembeni. Upande wa kulia palikuwa na kijikabati kidogo cheusi kinacholingana na kitanda, juu yake paliwekwa simu ya mezani.

Nilipanga kuanza msako wa Asi hapohapo Delhi. Kwa vyovyote hakuna biashara yoyote ya maana ambayo Asi angesafirishwa kuja kuifanya India zaidi ya ukahaba au kama angekuwa na bahati basi angefanya kazi ya kuuza baa. Hakuna kingine cha maana ambacho angekifanya huku. Hivyo msako wangu ulijikita katika majumba yauzayo pombe na katika madanguro.

Huu ni Mwisho wa Sehemu ya Bure ya Riwaya Hii, Isome Riwaya Yote ili Kufahamu Kilichotokea kwa Tsh. 2,000/= tu. Gusa Hapa Kununua Riwaya Yote.


Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024

Jinsi ya Kuandika Risala | Kiswahili Kidato Cha Nne