Riwaya| Sitasahau Nilipolala na Mwanamke Juu ya Kaburi (26)

Riwaya| Sitasahau Nilipolala na Mwanamke Juu ya Kaburi (26)

Walinilaza juu ya jiwe. Kisu kikali kikaandaliwa kuigawanya shingo yangu. Aliyeshika kisu kikali alisogea taratibu mahali nilipolazwa, akaanza kukishusha taratibu kama aliyetaka kuchinja kuku.
Hakufanikiwa, ghafla kitu kama radi kilipiga. Watu wale wote wakadondoka chini waliopoteza fahamu zao. Baada ya hapo, akatokea mzee aliyejaa misuli – Samike.
“Asante, wangeniua wapuuzi hawa!” nilishukuru nisiyeamini kisanga kilichotokea.
“Ondoa hofu, mapambano lazima yaendelee Mako!” alijibu mzee.
“Lakini mzee, nguvu zangu mimi ni ndogo sana kupambana na hawa watu, kwa nini usiingilie wewe?”
“Hapana… mimi sasa ni mzee nisiye na ubunifu mpya. Vita hivi vinahitaji akili na nguvu. Usichoke kupambana, nipo nyuma yako, penye shida nitatokea kama nilivyotokea leo. Adui zako nitawachonganisha wapigane wao kama nilivyoyachonganisha majoka uliyokutana nayo,” alimaliza kuzungumza mzee kisha akapotea.
Niliendelea na safari katika nchi ile ya Matumbawe. Nilitembea kuelekea nisipopajua kama kawaida yangu. Nilijihisi mpweke. Punde yule ndege akarejea tena. Safari hii alipiga kelele nyingi na kuimba kwa sauti kali. Yote kwa sababu sasa tulizoeana vilivyo.

Wakati nikiendelea kutembea mchana ule, mbele yangu niliona watu wengi wakiwa wamevalia mavazi ya vita, bila shaka walikuwa askari wa nchi ya Matumbawe wakiilinda mipaka dhidi ya wavamizi. Niliwaona wakiwa wameshika mapanga na marungu ambayo yangetosha kumwaga ubongo wa yeyote ambaye angenasa katika mikono yao. Rafiki yangu ndege alitoweka, nami nikajificha chini ya shimo dogo huku nikiwachungulia maadui.
Walitembea taratibu wasio na wasiwasi. Hawakutambua kama kuna kiumbe kipya kilikuwa ndani ya nchi yao. Nilishuhudia askari mmoja aliyekuwa na pua kubwa isivyokawaida akiwasihi wenzake wawe makini. Kwa ukubwa wa pua ya askari huyu, bila shaka alikuwa kitengo cha kunusa nyayo za maadui.
Wenzake walitulia, yeye akaanza kunusa taratibu. “Kuna mtuuu!” alipiga kelele. Nikaogopa.
Aliwaongoza wenzake kuelekea mahali nilipojificha. Kuona hivyo, nikatambaa kama nyoka chini kwa chini mpaka upande wa pili uliokuwa na mti mkubwa. Nilisimama hapo nikaanza kukimbia mithili ya swala aliyefukuzwa na chui.
Nilionekana. Wote wakaanza kunikimbiza, nami nikakimbia kwa bidii kuyanusuru maisha yangu. Kwa kuwa msitu ulikuwa mnene, nilikimbia hata nikapotea machoni mwa adui. Hapo nikaanza kutembea kwa tahadhari kubwa.
Walikuwa askari wenye maarifa ya vita. Walikubaliana kusambaa msituni ili waweze kuniwinda na kunikamata mzima mzima. Mipango yao niliisikia nikiwa katika harakati za kuwatoroka kwani hawakujua kunong’ona.
Nikiendelea kunyata taratibu kuwakimbia mabazazi wale, nilikutana na mmoja! Aliponiona akacheka. Hakuujua moto wangu niliouwasha katika TAHARUKI. Haraka bila salamu nilimrukia nikampiga teke kali la shingo, alidondoka chini. Nilimuacha pale akisubiri mazishi.

Niliendelea kujikokota ndani ya msitu. Ile roho yangu ya mapigano ikawa imenivaa, nilikuwa tayari kwa lolote. Hata hivyo, niliogopa kiasi kama ilivyo kwa watu wengine.
Nilirushiwa rungu kubwa nikakwepa. Aliyerusha sikumwona. Ilitosha kutambua sasa sikuwa salama, nilikuwa hatarini nikipambana na mpuuzi asiyeonekana. Nikiendelea kushangaa, mgongoni nilichapwa na ubapa wa panga, nikagugumia maumivu makali.
“Kama unaweza kupigana jitokeze…” nilisema kwa sauti, nikiwa nimekunja ngumi tayari kwa mtifuano.
Niliyemwomba ajitokeze alijitokeza. Sikuamini, alikuwa ni mtoto mdogo ambaye kwa makadilio asingezidi miaka tisa wala kupungua miaka nane. Alivaa suruali pana nyeusi na shati la kung’aa ambalo hata hivyo, halikuwa na vishikizo. Kifua chake laini kama kidali cha kuku, kilionekana kikiwa kimeufunika moyo uliodunda taratibu. Alinichapa teke la mguu nikashindwa kusimama na kujikuta nikipiga magoti bila kupenda.
Nikiwa chini nimepiga magoti nisiye na ujanja wowote, alichomoa kamba ngumu za katani akanifunga mikono. Akiwa amekunja midomo kwa hasira, alisema:
“Naitwa Chimota. Hakuna aliyethubutu kuniambia nijitokeze akabaki salama!” alinichapa kofi zito, nikapoteza fahamu.
Itaendelea Jumapili…
“Si ruhusa kuchukua hadithi hii na kuiweka katika mfumo wa sauti, kutoa kitabu, kuweka katika blogu au ‘website’ nyingine, au kufanya chochote kile bila kuwasiliana na mmiliki! Hatua kali zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayekiuka!”
Daud Makoba 0754 89 53 21


TAZAMA POVU LA MWALIMU MAKOBA KWA WASANII WAVAA HOVYO

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024

Vichekesho vya Kuchekesha na Kuvunja Mbavu 1