Mwanamke Uliyekula Pesa Zangu Nakutafuta | Sehemu ya Pili
Nilikaa kona ya kulia mwishoni mwa baa nikinywa taratibu. DJ alipiga mziki mtamu hata baadhi ya wateja walinyanyuka na kuanza kucheza. Nilisikia kionjo, “Timba Mtu Mbaya”. Niliufurahia mziki, lakini sikufurahia ukubwa wa sauti iliyokuwa inasikika kutoka katika spika, nilitamani wapunguze kidogo lakini sikutaka kuwaambia kwani walishayazoea makelele hayo. Pia, mimi ni nani hata nitoe amri sauti ipunguzwe!
Nilijikagua mfukoni na kugundua kwamba, kile kikaratasi
ambacho huwa naandika pesa nimpazo yule msichana hakikuwemo. Nilisikitika kwa
kupoteza kumbukumbu zile muhimu za kihasibu. Nikiwa katika lindi la mawazo na
unywaji, ghafla juu ya meza niliona kikaratasi changu kikiwa kimeshikiliwa na
mikono laini ya kike. Alikuwa yule msichana, alitabasamu, akacheka, akakohoa kidogo
kisha akakaa juu ya meza.
“Umekuja kama ulivyoahidi… nilidhani masihara!” nilisema
kwa sauti kali ili aweze kunisikia kwa sababu ya yale makelele.
“Nimetoroka kama nilivyokuahidi, Babuu akilala hukoroma,
ukisikia miungurumo yake, haamki tena huyo,” alijibu akitabasamu.
Mhudumu alifika, msichana akaomba aletewe kinywaji kama
changu. Aliletewa haraka. Nikachukua kikaratasi kutoka mikono yake, nikatoa kalamu
na kuandika 2,000/=.
“Ulisema unaitwa Mako?” aliuliza.
“Ndiyo,” nilijibu kisha nami nikauliza, “wewe unalo
jina?”
“Kuna mtu hana jina bwana wewe? Naitwa Asi.”
“Jina zuri. Una miaka mingapi?”
“Mwezi ujao natimiza 20… wewe je?”
“Sina miaka mingi, lakini nimekuzidi miaka 10,” msichana
alicheka akiwa amefurahi, halafu nikaongeza swali, “Babuu ni nani?”
Hakunijibu kama nilivyotarajia, badala yake alinyanyuka
na kuanza kucheza, Asi alikuwa na kichwa chepesi, mafunda mawili tu, yalimfanya
achangamke kuliko mtu yeyote mule ndani.
Ulisikika wimbo katika spika zile zenye sauti kali ya
kukera, “nimekuzoeaaa… nimekuzoeaaaa… nime, nime, nime…” msichana akazungusha
kiuno chake katika hali ambayo ilinifanya nipatwe na kizunguzungu, lakini baada
ya kumtazama kwa muda mrefu, nilizoea hali ile.
Alivaa gauni refu lakini lililobana maungo yake. Gauni
hili la kumetameta, liliendana vilivyo na rangi yake tamu nyeusi.
Sasa hakutaka tena kucheza peke yake, akaninyanyua katika
kiti ili nicheze naye, lakini sikuwa na bahati, kitendo cha kusimama tu,
ulisikika mlio wa bunduki, mziki ukazima, wote tukalala chini bila kuambiwa, akabaki
kasimama mwanamume mmoja akiwa kaikamata vyema bastola yake-Glock 17.
Naifahamu vyema bastola hii ya maangamizi aina ya Glock17. Hutengenezwa na taifa la Austria lililo jirani na nchi ya Ujerumani. Sijui
mwizi yule aliipata wapi kwani ni silaha iliyotengenezwa kwa vikosi maalumu
kama wasimamizi wa sheria na majeshini. Wepesi wake na uwezo wa kubeba risasi
17, umeifanya ipendwe duniani kote.
Yule bwana mwenye bastola, alisimama wima, akaja mwenzake
ambaye hakuwa na silaha, akawa akimlazimisha dada wa mauzo, ampatie fedha.
Baada ya kusikia majibizano yao, niliona nafasi ya wokovu imewadia.
Soma: Mwanamke Uliyekula Pesa Zangu Nakutafuta |Sehemu ya Tatu