Maendeleo ya Kiswahili | Kidato cha Tano na Sita

rangi nyingi
Lugha ni mfumo wa sauti za nasibu zenye kubeba maana na zilizokubaliwa na jamii ya watu zitumike katika kuwasiliana.

Mambo ya kuzingatia katika maana ya lugha

1. Lugha ni sauti za kusemwa na mwanadamu
Hakuna kiumbe tofauti na mwanadamu ambacho kinaweza kikatumia lugha.
2. Lugha ni sauti za nasibu
Hii ni kwa sababu:
- Mwanadamu hazaliwi na lugha bali huikuta katika jamii kwa nasibu tu.
- Hakuna utaratibu maalumu wa sauti za lugha. Mpangilio uliopo, ulitokea kwa nasibu tu.
- Hakuna uhusiano wa maneno na kile kinachotajwa. Kwa mfano, neno maji halifanani na maji halisi.
3. Lugha ni sauti zenye utaratibu maalumu
Lugha hupangwa katika utaratibu maalumu ambao umekubaliwa na jamii. Kwa mfano, hatusemi,
- Asha embe ana. Bali tunasema,
- Asha ana embe.
4. Lugha ni sauti za utamaduni wa watu fulani
Lugha hurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine, hivyo, lugha ni mali ya jamii.
5. Lugha ina maana fulani
Sauti za lugha zinapowekwa katika mpangilio maalumu huleta maana.

Tabia/sifa za lugha

1. Inamhusu mwanadamu

Hakuna kiumbe kisichomwanadamu kinachoweza kuzungumza lugha. Lugha hutumiwa na mwanadamu pekee.

2. Huambatana na sauti

3. Ni mfumo wa sauti za nasibu

4. Ni sauti zilizo na utaratibu maalumu

Kila lugha huwa na utaratibu maalumu unaofafanua jinsi sauti zinavyoungana kuunda silabi na maneno na namna maneno hayo yanavyoungana kuunda vipashio vikubwa zaidi.

5. Lugha husheheni utamaduni wa watu fulani

Lugha hutambulisha utamaduni wa jamii kupitia maneno yake.
6. Lugha ina maana
Sifa hii ndiyo inayowafanya watuamiaji wa lugha kuelewana.

7. Inajitosheleza kimsamiati

8. Hupokea maneno kutoka lugha zingine

9. Lugha hubadilika kulingana na kupita kwa wakati

Aina za lugha

1. Lugha ya mazungumzo

Hii ni aina ya lugha ambayo huwasilishwa kwa njia ya mazungumzo ya mdomo.  Chanzo cha lugha hii ni kuzungumza na kikomo chake ni kusikiliza. Katika lugha hii, ni rahisi kujua hali ya mzungumzaji kama ana hasira, huzuni n.k

2. Lugha ya maandishi

Ni kiwakilishi cha lugha ya mazungumzo katika maandishi. Chanzo cha lugha hii ni kuandika na kikomo chake ni kusoma. Katika lugha hii ni vigumu kujua hali ya mwandishi kama ana hasira, huzuni, n.k

Ushahidi wa Kiswahili kuwa Kibantu

Ushahidi wa kiisimu
Ushahidi wa kiisimu ni ushahidi unaothibitisha kwa kutumia misingi ya sayansi ya lugha. Ushahidi huo ni pamoja na:

1. Msamiati

Msamiati wa msingi wa lugha ya Kiswahili na lugha za kibantu unafanana. Tofauti zinaweza kujitokeza kidogo katika matamshi au viambishi vyake, lakini siyo katika mzizi.
Kwa mfano:
Kiswahili - Mtu
Kizigua - Mntu

2. Sentensi za Kiswahili

Muundo wa sentensi za Kiswahili, unafanana na ule wa sentensi za kibantu. Miundo yote, ina sifa ya kuwa na kiima na kiarifu.
Kwa mfano:
Kiswahili - Juma anakula ugali
Kisukuma - Juma alelya bugali

3. Ngeli za nomino

Hapa kuna kufanana katika umoja na wingi pamoja na upatanisho wa kisarufi.
- kigezo cha maumbo ya nomino
Kigezo hiki hufuata maumbo ya umoja na wingi katika kuainisha nomino. Nomino nyingi za lugha za Kibantu na Kiswahili zina maumbo ya umoja na wingi.
Kwa mfano:
Kiswahili: mtu - watu
Kikurya: Omonto - Banto
- kigezo cha upatanisho wa kisarufi
Kigezo hiki kinaangalia uhusiano uliopo kati ya nomino, vivumishi na viambishi awali vya nafsi katika vitenzi vya Kiswahili na kibantu.
Kwa mfano:
Kiswahili: Baba analima - Baba wanalima
Kindali: Utata akulima - Abhatata bhakulima

4. Vitenzi vya Kiswahili na Kibantu

Vipengele vinavyothibitisha uhusiano huu ni:
A. Viambishi
Lugha ya Kiswahili hujengwa na viambisha awali na tamati pamoja na mzizi wa neno.
Kiswahili: a-na-lim-a
Kinyakyusa: I-ku-lim-a
B. Mnyumbuliko wa vitenzi
Kiswahili: kucheka, kuchekesha, kuchekelea
Kinyamwezi: Kuseka, Kusekasha, kusekelea
C. Mwishilizo wa vitenzi
Vitenzi vya lugha ya kibantu na lugha ya Kiswahili, huishia na irabu a.

Ushahidi wa kihistoria

Ushahidi wa kihistoria unathibitisha kuwa, Kiswahili kilizungumzwa kabla ya kuja kwa wageni. Ushahidi huu ulitolewa na wageni mbalimbali waliofika hapa Afrika ya mashariki.

1. Ugunduzi wa Ali-Idris

Huu ulifanywa huko Sicily mwaka 1100-1166 kwenye mahakama ya mfalme Roger II. Ali Idris aliweza kugundua jina la zamani la Zanzibar kuwa Unguja. Pia, anaandika majina kama: kikombe, mkono wa tembo, muriani na sukari ambayo ni ya ndizi mbalimbali zilizokuwa zikipatikana huko.

2. Ushahidi wa Marco Polo

Huyu ni mzungu ambaye alisafiri sehemu nyingi. Marco Polo aliandika hivi: “Zanzibar ni kisiwa kizuri chenye ukubwa wa mzunguko wa maili 200. watu wote wanaabudu Mungu. Wanamfalme na wanatumia lugha yao na hawalipi kodi kwa mtu.”
Maelezo hayo, yanathibitisha hoja za msingi kuhusu watu wa pwani na lugha yao.

3. Ushahidi wa Al-Masudi (915)

Al Masudi alisisitiza kuwa, Wazenji walitema lugha kwa ufasaha na walikuwa na viongozi waliowahutubia kwa lugha yao.

4. Historia ya Kilwa

Katika karne ya 10-16, habari zinahusisha kutajwa kwa majina ya utani ya Masultani, majina hayo ni: mkoma watu, nguo nyingi na hasha hazifiki. Kwa kuwa majina haya ni ya Kiswahili, basi hapana shaka kuwa, Kiswahili kilizugumzwa zamani kabla ya wageni kuja.

5. Vitabu vya Peryplus na Yu Yang Tsa Tsu

Kitabu hiki kinahusu mwongozo wa bahari ya Hindi. Kiliandikwa karne ya kwanza huko Alexandria. Kinataja habari ya vyombo kama vile ngalawa, madema na mitepe. Kinaeleza kuwa, wageni waliijua vyema lugha ya wenyeji.

6. Utenzi wa Fumo Liyongo

Utenzi huu uliandikwa karne ya 13. Kuwepo kwa shairi hili kunadhihirisha kuwako kwa lugha ya Kiswahili kabla ya hapo. Huenda Kiswahili kilianza kutumikak kabla ya karne ya 10.

Pijini

Pijini ni lugha ambayo huzuka pale ambapo wazungumzaji wa lugha mbili tofauti hukutana.

Sifa za pijini

1. Huwa na miundo sahili hasa ya kisintaksia. Pia, huambatanisha ishara za mwili. Mifano yake ni pijini za Afrika Magharibi wakati wa vita vikuu vya Dunia.
2. Idadi kubwa ya msamiati kutoka katika lugha ya tabaka la juu au tawala. Kisetla kilichotumika Kenya kati ya Masetla wazungu na waKenya kilikuwa na maneno mengi ya kiingereza.
3. Huhusisha lugha mbili tu.
4. Haina wasemaji wengi
5. Huwa na msamiati mchache, hii husaidia kujifunza.
6. Baadhi ya pijini huzuka kutokana na kukutana kwa muda mfupi kwa lugha. Kwa mfano kati ya mtalii anayetaka kuelewana na mwenyeji.

Krioli

Ni pijini ambayo imepata wazungumzaji asilia. Watu wanaozungumza pijini, wakizaa watoto na watoto hao wakaanza kuzungumza pijini kama lugha yao ya kwanza, basi lugha hiyo huitwa Krioli.

Sifa za krioli

1. Krioli ni pijini iliyo na wasemaji wenyeji
2. Krioli huwa na msamiati mwingi
3. Ina wasemaji wengi
4. Huweza kuwa lugha sanifu. Kwa mfano, Afrikaans huko Afrika ya Kusini ilikuwa Krioli na sasa ni lugha sanifu.

Kiswahili ni pijini au krioli?

Ukweli ni kwamba, Kiswahili siyo pijini wala krioli kwa hoja zifuatazo:
1.  Sintaksia ya Kiswahili haijatawaliwa na ile ya Kiarabu
2. Nusu ya msamiati wa Kiswahili hautoki katika kiarabu. Msamiati wa asili ya kiarabu ni 30% pekee.

Maana na matumizi ya lugha ya kwanza, lugha ya pili, lugha ya taifa na lugha rasmi

Lugha ya kwanza

Ni lugha ambayo mtu hujifunza utotoni mwake wakati anakua kabla hajaanza kujifunza lugha ya pili. Ni lugha ambayo mtoto hujifunza kwa kusikiliza kutoka kwa wazazi wake na majirani wanaomzunguka.

Kwa nini ni rahisi kwa mtoto kujifunza lugha ya kwanza?

1. Walimu wa nyumbani wako wengi na wana uzoefu wa ile lugha. Walimu hawa ni mama, baba, shangazi, dada, kaka, dada, majirani n.k.
2. Lugha anayojifunza hutokea katika mazingira halisi. Kwa mfano: wanapozungumzia kula, wanakuwa wanakula na chakula kiko mezani mtoto anaona.
3. Uhusiano na wale wanaomzunguka ni mzuri. Kutokana na uhusiano kuwa mzuri, mtoto huweza kujifunza lugha kwa uhuru zaidi na kujikuta akiimudu lugha bila wasiwasi.
4. Uzoefu katika lugha ileile moja. Mtoto hukabiliana na lugha ya kwanza ikiwa ni ileile nyumbani. Hakuna mwingiliano wa lugha nyingine na pia kuna kurudiarudia kwingi.

Lugha ya pili

Hii ni lugha ambayo binadamu hujifunza baada ya kujifunza lugha yake ya kwanza. Kiswahili ni lugha ya pili kwa watu wengi wa Tanzania.

Mambo yanayotawala kujifunza lugha ya pili

- Walimu wanaokufundisha
- Vifaa vya kufundishia

Aina za mafunzo ya lugha ya pili

1. Mafunzo rasmi. Haya yanakwenda sambamba na kufuata kanuni au sheria zilizowekwa kwa ajili ya kuongoza mafunzo hayo.
2. Mafunzo yasiyo rasmi. Haya hutolewa bila kanuni maalumu.

Lugha ya taifa

Ni ile iliyochaguliwa kutumika kwa taifa zima na inaweza kutimiza wajibu wa taifa. Nchini Tanzania, lugha ya taifa ni Kiswahili. Kiliteuliwa mwaka 1964.

Mambo ya kuzingatia katika uteuzi wa lugha ya taifa

1. Iwe na uwezo wa kuwaunganisha watu na kudumisha umoja.
2. Ni muhimu kuzingatia urasmi wa lugha na wazungumzaji wake.
3. Ni muhimu kuzingatia uwezo au nguvu za watumiaji wa lugha.
4. Ni muhimu kuchagua lugha iliyokomaa, yenye maandishi na msamiati unaotosha kwa mahitaji yote ya taifa.

Changamoto zinazokikumba Kiswahili kama lugha ya taifa

1. Athari kutoka lugha za kikabila kama kichaga, kisukuma, kinyamwezi n.k
2. Matumizi mabaya ya Kiswahili katika maeneo na shughuli mbalimbali.
3. Kiingereza kinaonekana kuwa ndiyo lugha yenye hadhi.
4. Kiswahili kuhusishwa na watu wa tabaka la chini na wasio na elimu
5. Ukosefu wa sera maalumu inayofafanua dhima na hatma ya kiswahili kwa nchi zote za Afrika Mashariki.

Lugha rasmi

Ni lugha iliyochaguliwa ili itumike katika shughuli zote kama: sheria, mahakamani, ofisini, matangazo katika vyombo vya habari, biashara, shuleni n.k
Lugha rasmi hutumiwa katika kuendesha shughuli za kiserikali ambazo ni rasmi. Nchini Kenya lugha rasmi ni Kiingereza na Kiswahili, Uganda ni Kiingereza na Tanzania ni Kiswahili na Kiingereza.

Sifa za lugha rasmi

1. Inaweza kuwa sanifu au siyo, fasaha au la.
2. Inaweza kuwa lugha ya taifa au isiwe lugha ya taifa
3. Haijali ukabila wala mchanganyiko uliomo nchini
4. Inaweza kuwa lugha ya kigeni
5. Hutegemea utawala uliopo

Chimbuko la Kiswahili

Wataalamu wanatofautiana juu ya chimbuko la Kiswahili. Wataalamu hawa wamekuwa wakitofautiana katika hoja:

Hoja mbalimbali za chimbuko la kiswahili

1. Lugha ya Kiswahili inatokana na Kingozi, lugha ya mashariki mwa Kenya.
2. Kiswahili chimbuko lake ni Kishomvi kilichozungumzwa na watu wa Bagamoyo enzi hizo, pamoja na watu wa Mzizima na Kilwa.
3. Lugha ya Kiswahili iliinukia katika sehemu mbalimbali za upwa wa Afrika Mashariki. Madai haya yaliyotolewa na mtaalamu Greenville, yanaelekea kuwa kweli ukilinganisha na hoja zingine zilizopita ambayo hoja zake haziko makini na zinakosa mashiko.

Sababu za kuibuka kwa lahaja za kiswahili

Lahaja ni tofauti za lafudhi, fonolojia, msamiati na miundo katika lugha moja. Kiswahili kinazo lahaja nyingi, sababu za kuibuka lahaja hizo ni:

1. Uhamaji wa kundi fulani la watu wanaozungumza lugha moja

Kuna wakati watu walioishi pamoja walitengana kwa sababu mbalimbali ikiwemo, njaa na vita. Watu hao wakitengana, hukosa mawasiliano ya mara kwa mara na hivyo kujikuta wakikuza upekee wa namna fulani katika usemaji wao. Upekee huo unaoibuka, ndiyo lahaja.

2. Utengano wa watu kijiografia

Lahaja hizi hutokea kwa sababu ya vizuizi vya kijiografia kama: milima, mito, bahari, misitu au jangwa. Kwa mfano lugha moja inapotumiwa katika eneo pana la kijiografia linalotenganishwa na vilima na visiwa kuna uwezekano wa mawasiliano baina ya wazungumzaji hao kutengwa. Hali hii husababisha kikundi kimoja kutengwa mbali na kikundi kingine.

3. Utengano wa watu kitabaka

Msingi wa mwachano kitabaka unaweza kuwa uchumi, dini , elimu na siasa. Kwa sababu ya mwachano wa kitabaka, mawasiliano baina ya watu wa tabaka tofauti hupungua. Mawasiliano yakipungua, upekee huchipuka.
Hata hivyo ni vigumu kusema kuwa, jamii za zamani za Tanzania zilikuwa na lahaja za kitabaka kwa sababu hali ya kiuchumi ilikuwa chini hivyo kushindwa kuibuka kwa matabaka. Kwa sasa, lahaja zinaweza kutokea kwa sababu hii.

4. Kupita kwa wakati

Lahaja huwa haitokei kwa siku moja, lazima wakati upite. Kwa mfano, lahaja za kijiografia ili zitokee,hutegemea wakati.

Usanifishaji wa kiswahili

Kusanifisha lugha ni kulinganisha lugha na kuifanya ikubalike kwa watu wote wanaohusika kimatumizi. Mambo muhimu katika usanifishaji wa lugha ni pamoja na kuangalia usahihi wake kisarufi na kimatamshi.
Kiswahili tunachozungumza hii leo, hakikuwa hivi, kilikuwa lahaja ya Kiunguja ambayo ilisanifishwa na kuwa Kiswahili tulichonacho sasa na Waingereza.

Sababu zilizofanya kiunguja kiteuliwe kuwa msingi wa kusanifu kiswahili

Ukiachilia mbali uwepo wa lahaja nyingi kama Kipemba, Kimombasa, Kimvita, na rahaja nyinginezo, kiunguja kilichaguliwa kuwa lahaja ya usanifishaji wa kiswahili kwa sababu zifuatazo.
1. Lahaja ya kiunguja ilikuwa imeenea sehemu kubwa. Lahaja ya Kimvita, haikuwa imeenea sehemu nyingi za bara.
2. Lafudhi ya unguja ilikuwa imekwishatumika katika medani ya kitaaluma na kidini hasa Tanganyika wakati wa mjerumani na sehemu kubwa kuenezwa na wahubiri wa kidini.
3. Lahaja ya kiunguja ilikuwa rahisi zaidi kuliko lahaja zingine.
4. Lahaja ya kiunguja ilikuwa imetajirika zaidi katika msamiati, hivyo ilikidhi haja ya mawasiliano.

Kuteuliwa kwa kiunguja kulivyodumaza lahaja zingine za kiswahili

1. Kiunguja kutumiwa katika shughuli zote za mawasiliano hapa Afrika Mashariki lakini lahaja zingine hazitumiki.
2. Wingi wa watu. Kiunguja kina wasemaji wengi, hivyo lahaja zingine zimebaki na wasemaji wachache na hizi inazifanya zidumae.
3. Hadhi ya lahaja ya kiunguja. Baada ya kiunguja kusanifishwa kilipandishwa hadhi na lahaja zingine kushushwa.
4. Elimu. Kiunguja kinatumika katika elimu, wakati lahaja zingine hazitumiki. Hii inazifanya zidumae.
5. Kuandikwa kwa kamusi za lahaja ya kiunguja. Lahaja ambazo hazina kamusi, zinadidimia.
6. Matumizi ya kiunguja katika vyombo ya habari. Lahaja ya kiunguja ndiyo inayotumika katika magazeti, redio na televisheni. Lahaja zingine zinadidimia kwa sababu hazina nafasi katika vyombo vya habari.

Changamoto za kuenea kwa kiswahili katika Afrika ya Mashariki kabla ya uhuru

Kabla ya uhuru, ueneaji wa Kiswahili ulikumbana na changamoto kadha wa kadha. Hata hivyo, Kiswahili kilienea bila kujali changamoto hizo.

Kuenea kwa kiswahili nchini Tanganyika kabla ya uhuru

Kuenea kwa lugha ni kuongezeka kwa watu wanaotumia lugha hiyo. Kiswahili kilienea nchini Tanganyika wakati wa ukoloni.

Sababu za kuenea kwa Kiswahili nchini Tanganyika wakati wa ukoloni

1. Biashara 

Kulikuwa na safari za kibiashara baina ya pwani na bara zilizokuwa zikifanywa na waafrika wenyewe. Katika safari hizo, watu wa bara walikitoa Kiswahili pwani na kukieneza sehemu za bara. Waarabu nao walipokuja, waliikuta lugha ya Kiswahili ikitumika hivyo nao waliieneza katika biashara.

2. Dini

Wamishenari wa Kikristo walifika Afrika ya Mashariki kabla ya utawala wa wakoloni. Mashirika mbalimbali ya kidini kama: Roho mtakatifu kutoka ufaransa, White fathers na Church Missionary Society (CMS) chini ya Krapf yalisaidia kueneza lugha kwa sababu CMS liliandika sarufi ya kwanza ya Kimvita ya Kiswahili.
Kwa upande wa Waislamu, Waarabu walifika pwani ya Afrika Mashariki karne ya 8. walipofika, waliwakuta wenyeji wakizungumza Kiswahili. Ili waeneze dini yao vizuri, waarabu walijifunza kwa dhati lugha ya Kiswahili.

3. Kuenea kwa Kiswahili kutokana na utawala

- Waarabu walisaidia kuenea kwa kiswahili katika biashara, dini na kuoana.
- Wajerumani walisaidia kuenea kwa kiswahili katika mambo haya: utawala ambapo Wajerumani hawa waliamua kutumia lugha hii katika shughuli zao za utawala.
katika Elimu Kiswahili kiliteuliwa kiwe lugha ya kufundishia na pia kutumika kama somo la kawaida katika shule za msingi.
katika shughuli za kilimo, manamba au vibarua walilazimishwa wajue lugha ya Kiswahili.
katika mahakama wafanyakazi waliwahoji na kuandika hukumu kwa watuhumiwa kwa kutumia lugha ya Kiswahili.
- Waingereza walisaidia kuenea kwa Kiswahili katika mambo haya: kusanifisha kiswahili, suala la manamba, suala la jeshi na suala la utawala.

Kuenea kwa kiswahili nchini Kenya kabla ya uhuru

Lugha ya Kiswahili ilitumika huko Kenya katika maeneo ya Pwani kama: Lamu, Malindi na Mombasa.
Waarabu walipoingia kufanya biashara, lugha waliyotumia ilikuwa ni Kiswahili.
Waingereza nao walipowasili Kenya, walikuta Kiswahili kimeenea kutokana na biashara za Waarabu hivyo na wao wakatumia Kiswahili.

Jinsi utawala wa Mwingereza ulivyoathiri hali ya Kiswahili nchini Kenya

Mwaka 1900 Charles Elliot ambaye alikuwa gavana wa Kenya alipendekeza matumizi ya lugha za kikabila kuliko Kiswahili.
Baadhi ya wamishenari waliomba kufundisha dini kwa lugha za kikabila.
Baadhi ya madhehebu ya kidini yalipinga matumizi ya Kiswahili kawa madai Kiswahili ni lugha iliyofungamana na Uislamu hivyo, kukuza Kiswahili ni kukuza na kueneza Uislamu.
Walowezi walipinga matumizi ya Kiingereza, waliona kuwafundisha Wakenya Kiingereza ni kama kujivua nguo mbele yao. Hivyo mpaka kufikia mwaka 1940, Kiswahili kilitumika kama lugha ya kufundishia.
Hata hivyo, mwaka 1960, gavana alitangaza Kiingereza kuwa lugha moja itakayotumika katika nyanja zote.

Matatizo ya Kiswahili nchini Kenya

1. Lugha za Kienyeji zilitumika katika kufundishia, Kiswahili kilifundishwa kama somo tu.
2. Kiswahili kilihusishwa na dini ya Kiislamu, hivyo kilienea eneo la pwani tu.
3. Misafara ya kibiashara ambayo ndiyo ingeeneza Kiswahili, ilikwamishwa na makabila makali ya Wamasai na Wakwavi. Tatizo jingine ni wanyama wakali waliokuwa katika mbuga za Tsavo.
4. Kiswahili kilionekana lugha duni na hivyo, hakikupendwa na wengi.

Kuenea kwa kiswahili nchini Uganda kabla ya uhuru

Kiswahili kiliingia Uganda mnamo karne ya 19. Chanzo cha kuibuka kwa Kiswahili nchini Uganda ni Waarabu waliokwenda kumtembelea Kabaka wa Buganda katika makao yake makuu.
Lengo la waarabu ilikuwa kuanzisha mahusiano ya kibiashara. Hivyo waarabu walitumia Kiswahili kama lugha ya kibiashara, lakini pia lugha ya kutolea elimu ya dini ya kiislamu.
Baada ya waarabu walifuata waingereza. Hawa walitambua umuhimu wa Kiswahili kama lugha ya mawasiliano katika Afrika mashariki,hivyo walikifanya kuwa lugha ya kutahiniwa shuleni toka mwaka 1927.
Hata hivyo Kiswahili kilikutana na upinzani mkubwa kutoka watu wa kabila la Baganda wakiongozwa na Kabaka Daudi Chwa ambaye alihofia matumizi ya Kiswahili yangemeza matumizi ya lugha ya Kiganda na hivyo kuwaondolea fahari yao.

Matatizo kwa ufupi

1. Waganda waliona Kiswahili ni lugha ya Kiislamu
2. Katika kufundisha mkazo zaidi ulikuwa katika lugha ya Kiingereza
3. Watawala na viongozi walipinga kuenezwa kwa Kiswahili nchini Uganda na badala yake walipendekeza lugha ya Buganda iwe lugha rasmi ya Uganda.
4. Kiswahili kilifikiriwa kuwa ni lugha ya kitumwa.

Ukuaji na uenezaji wa Kiswahili nchini Tanzania baada ya uhuru

Baada ya kupata uhuru, serikali ilifanya kila lililowezekana ili kukikuza Kiswahili.

Hatua zilizochukuliwa na serikali ya Tanzania kukuza Kiswahili baada ya uhuru

1. Kuteua kiswahili kuwa lugha ya taifa

Baada ya uhuru Kiswahili kilichaguliwa kuwa lugha ya taifa. Hatua hii ilifanya mwaka 1962 Kiswahili kitumike katika bunge na shughuli zote za serikali.

2. Kuteua Kiswahili kitumike katika kutolea elimu

Mwaka 1965 Kiswahili kilifanywa kuwa lugha ya kufundishia katika shule za msingi. Pia, Kiswahili kilifundishwa kama somo kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita.

3. Kuunda baraza la Kiswahili la taifa (BAKITA)

Baraza hili liliundwa mwaka 1967 na lilipewa kazi ya kuratibu shughuli zote za ukuzaji na uendelezaji wa lugha ya Kiswahili kote nchini.

4. Kuanzisha taasisi ya elimu ya watu wazima

Taasisi hii ilianzishwa mwaka 1963. madhumuni makubwa ya taasisi hii ilikuwa ni kuwapa fursa ya kusoma watu wazima ambao hawakuwahi kupata nafasi ya kwenda shule wakiwa wadogo. Kote nchini, elimu ya watu wazima ilifundishwa kwa kutumia Kiswahili.

5. Kuunda asasi za kueneza na kukuza Kiswahili

Asasi hizi ziliundwa na serikali ili zifanye kazi ya kujenga, kuendeleza na kueneza Kiswahili. Kamati ya lugha ya Afrika Mashariki ilipandishwa hadhi na kufanywa Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI). asasi zingine zilizoanzishwa ni pamoja na: BAMITA, BAKIZA, UKUTA, Chama cha Kiswahili cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Vyombo mbalimbali vya kukuza na kueneza Kiswahili nchini

Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI) na sasa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI)
Kamati ya lugha ya Afrika mashariki mwaka 1954, ilibadilishwa jina na kujulikana kama kamati ya Kiswahili Afrika mashariki. Mwaka 1964, iliingizwa katika Chuo Kikuu kishiriki cha Dar es Salaam na ikajulikana kama chuo cha uchunguzi wa lugha ya Kiswahili. Mwaka 1970 baada ya kuanzishwa chuo kikuu cha Dar es Salaam ilijulikana kama Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI), baadae mwaka 2009 ikajulikana kama Taasisi ya Taaluma za Kiswahili.

Dhima za TATAKI

I. Kufanya utafiti ili kuiendeleza na kuikuza lugha ya Kiswahili
II. Kuendeleza uchapishaji wa jarida la Kiswahili likiwa na makala ya kitaaluma na kawaida.
III. Kukusanya taarifa zote za sasa zilizopo ulimwenguni zinazohusu lugha ya Kiswahili
IV. Kutafsiri maandishi yafaayo katika lugha ya Kiswahili
V. Kufundisha taaluma mbalimbali za Kiswahili

Mafanikio ya TATAKI

i. Imefanikiwa kutoa majarida mbalimbali ya Mulika na Jarida la Kiswahili ambayo huchambua vipengele mbalimbali vya lugha.
ii. Imetoa kamusi mbalimbali kama vile, kamusi ya Kiswahili Sanifu (1981) na kamusi zingine.
iii. Imechapisha vitabu mbalimbali vya fasihi ya Kiswahili na sarufi. Mfano: pete (1978) na SAMIKISA (1999)
iv. Imetafsiri vitabu vya masomo mbalimbali kwa lugha ya Kiswahili.

Matatizo ya TATAKI

i. Uhaba wa fedha za kuendesha shughuli za utafiti wa Kiswahili
ii. Uhaba wa wataalamu
iii. Uhaba wa vifaa vya kufanyia kazi.

Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA)

Baraza liliundwa kwa sheria ya bunge Na: 27 ya mwaka 1967 kwa shabaha ya kukuza, kuimarisha na kuendeleza Kiswahili.

Majukumu ya BAKITA

1. Kuratibu na kusimamamia maendeleo na matumizi ya Kiswahili chote.
2. Kushirikiana na vyombo vingine nchini ambavyo vinajishughulisha na maendeleo ya Kiswahili.
3. Kuhimiza matumizi ya Kiswahili katika shughuli maalum na pia katika shughuli zisizo maalumu.
4. Kutoa huduma za tafsiri na ukalimani kwa serikali

Mafanikio ya BAKITA

1. Imeandaa istilahi za taaluma mbalimbali: Fizikia, biashara, kemia n.k
2. Inatoa majarida mbalimbali yanayohusu lugha ya Kiswahili. Kwa mfano jarida la Lugha yetu.
3. Inaendesha vipindi vinavyohusu lugha ya Kiswahili kwenye vyombo vya habari.
4. Imefanya tafsiri mbalimbali kwa watu binafsi na serikali.

Matatizo ya BAKITA

1. Uhaba wa fedha
2. Upungufu wa wataalamu wa Kiswahili.

Chama cha Usanifu wa Kiswahili na Ushairi Tanzania (UKUTA)

Chama hiki kiliundwa mwaka 1959. Mwenyekiti wa chama hiki alikuwa marehemu Mahamoud Hamdouny (Jitu Kali), aliyekuwa mshairi maarufu na masikani yake yakiwa Dodoma.

Malengo ya UKUTA

i. Kulinda, kuhifadhi na kustawisha lugha ya Kiswahili, ushairi na utamaduni wake.
ii. Kufanya kazi zitakazostawisha ushairi kuwa sehemu ya mitaala ya Kiswahili nchini na nje ya nchi.
iii. Kuhamasisha na kuamsha ari ya wale wanaotaka kutunga vitabu mbalimbali.
iv. Kutoa huduma ya ufasiri na ukalimani katika mikutano ya kitaifa na kimataifa.
v. Kushirikiana na taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi katika kukiendeleza Kiswahili.

Changamoto za UKUTA

i. Kukosa fedha
ii. Serikali haichukui wajibu wake wa kuisaidia taasisi hii

Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima

Taasisi ya elimu ya watu wazima ilianzishwa mwaka 1960 kama sehemu ya kitengo cha mafunzo ya ziada ya chuo kikuu kishiriki cha makerere Kampala Uganda. Mwaka 1963, taasisi ikawa chini ya chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Ilipofika mwaka 1975, taasisi hii ikaundwa rasmi kama taasisi ya elimu ya watu wazima kwa sheria ya bunge na kuwa chombo cha kushughulikia kisomo cha manufaa nchi nzima.

Changamoto za Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima

i. Ukosefu wa fedha za kuendeshea taasisi
ii. Elimu ya watu wazima imesahaulika. Kwa mfano hapo zamani kulikuwa na maadhimisho ya elimu ya watu wazima nchi nzima, lakini hivi sasa, hakuna tena maadhimisho hayo

Mafanikio ya Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima

i. Kutoa masomo ya jioni kwa watu wazima katika stadi za kusoma na kuandika.
ii. Kutoa masomo kwa njia ya posta kwa kidato cha kwanza hadi cha sita kwa somo la Kiswahili
iii. Kuanzisha maktaba makao makuu ya taasisi ambayo huwasaidia wanafunzi kupata vitabu na majarida mbalimbali ya Kiswahili
Vyombo vingine vilivyoanzishwa kwa lengo la kukuza Kiswahili ni:
Taasisi ya Elimu Tanzania
Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni Zanzibar (TAKILUKI)
Umoja wa waandishi wa vitabu Tanzania (UWAVITA)
Baraza la Mitihani la Taifa (BAMITA)
Baraza la Kiswahili la Zanzibar (BAKIZA)

Ukuaji na uenezaji wa Kiswahili nchini Kenya baada ya uhuru

Baada ya uhuru wa Kenya mwaka 1963, serikali ya Kenya ilichukua hatua mbalimbali kuhakikisha Kiswahili kinakua nchini humo.

Hatua zilizochukuliwa na serikali ya Kenya katika kukuza Kiswahili

1. Kutumia Kiswahili katika siasa

Kiswahili kilitumiwa katika mikutano mingi ya kisiasa nchini Kenya hata ikawa lugha ya umma huo. Kwa mfano: mikutano ya rais Jomo Kenyatta ilifanywa kwa lugha ya Kiswahili.

2. Kuundwa kwa vyombo vinavyokuza Kiswahili

Vyombo mbalimbali viliundwa ili kukuza Kiswahili. Miongoni mwa vyombo hivyo ni: Chama cha Kiswahili Kenya (CHAKIKE) na Chama cha Kiswahili cha Taifa Kenya (CHAKITA).

3. Uchapaji wa vitabu na kamusi

Mfumo wa soko huria umetoa nafasi kwa uchapishaji wa vitabu vya Kiswahili na kamusi. Mpaka sasa kuna vitabu vingi sana vilivyochapishwa na kuandikwa na wakenya. Kwa mfano: kamusi ya methali chake Wamitila, Misingi ya Sarufi ya Kiswahili chao Habwe na Karanja na Fonolojia na Mofolojia ya Kiswahili Sanifu yake Mgullu.

4. Kuteuliwa kwa Kiswahili kuwa lugha ya taifa

Mwaka 1965 Dkt Waiyaki akiwa mmoja wa mawaziri alitangaza Kiswahili kuwa lugha ya taifa. Kila mahali nchini Kenya, ilisisitizwa lugha hiyo itiliwe mkazo.

Madhumuni ya vyombo vya serikali na visivyo vya serikali katika kukuza Kiswahili nchini Kenya

1. Chama cha Kiswahili cha Kenya (CHAKIKE)

Kilianzishwa mwaka 1980 na kusajiliwa rasmi mwaka 1981.

Madhumuni ya CHAKIKE

i. Kuviunganisha vyama mbalimbali vya Kiswahili nchini ili sauti ya Kiswahili iwe na nguvu
ii. Kushirikiana na vyama vya kimataifa vya nchi jirani
iii. Kuhimiza wanafunzi washiriki katika mashindano ya Kiswahili
iv. Kuwasaidia walimu wa Kiswahili kuwa walimu bora zaidi katika mafundisho yao ya Kiswahili.

2. Chama cha Kiswahili cha Taifa (CHAKITA)

Chama hiki kilibuniwa mwaka 1998. kupitia juhudi ya chama hiki, Kiswahili kimekuwa lugha ya taifa na rasmi nchini kwa mujibu wa katiba ya Kenya ya mwaka 2010.

Madhumuni ya CHAKITA

I. Kuendeleza ufundishaji wa lugha ya Kiswahili Kisayansi
II. Kushirikisha lugha, fasihi na isimu ya Kiswahili
III. Kushirikisha lugha ya Kiswahili kama chombo cha maendeleo ya kitaifa
IV. Kuwezesha ufanyikaji wa utafiti kuhusu masuala muhimu katika lugha.

Ukuaji na ueneaji wa Kiswahili nchini Uganda baada ya uhuru

Baada ya Uganda kupata uhuru wake mwaka 1962, ulitokea mzozo mkubwa wa kuchagua lugha ya taifa. Mzozo huu ulisababishwa na ukabila ambapo, kila kabila lilitaka lugha yake itumike kama lugha ya taifa.
Kabila la Baganda ndiyo lilikuwa mbele katika mzozo huu na lilishikiria mkazo wa kuipa hadhi lugha yake ya Kiganda. Mwisho kila kabila liliamua kutumia lugha yake katika shughuli za kiserikali.
Ni katika ujio wa Iddi Amini ndiyo tunaona Kiswahili kikifanikiwa kupenyeza kidogo ambapo kiongozi huyu aliamuru Kiswahili kitumike hususani katika jeshi.
Pia, baada ya ujio wa Yoweri Museveni madarakani, Kiswahili kimepata nafasi kubwa nchini Uganda na sasa kinatumika katika shughuli nyingi ikiwemo biashara, jeshi na mazungumzo ya kawaida.

Sababu zilizosaidia kukua kwa kiswahili nchini Uganda

1. Vyombo vya habari

Kutoka mwaka 1973 kwa amri ya Idi Amini, Kiswahili kilianza kutangazwa katika televisheni na redio.

2. Kuteuliwa kuwa lugha ya taifa

Mwaka 2005 lugha ya Kiswahili ilitambuliwa kama lugha ya taifa na lugha rasmi nchini Uganda. Kutokana na hali hii, Kiswahili kinatumiwa katika shughuli mbalimbali nchini Uganda na matumizi yake katika nyanja mbalimbali yamepanuka pia.

3. Baraza la mitihani la Uganda

Hiki ni chombo kingine kinachosaidia kukuza na kueneza Kiswahili nchini Uganda. Baraza hili hutahini wanafunzi wanaofanya mitihani ya viwango vyote vya elimu nchini Uganda, wanajeshi wote pamoja na askari polisi wa magereza ambao hutumia Kiswahili kuwasiliana na raia.

4. Chuo Kikuu cha Makerere

Kiswahili kilianza kufundishwa katika idara ya lugha mwaka 1970. katika chuo hicho, wanafunzi hufundishwa kozi ngumu kwa wale waliokwisha mudu Kiswahili na kozi maalumu kwa wale wanaojifunza Kiswahili kwa mara ya kwanza.

5. Vita vya Uganda na Tanzania

Mwaka 1979, majeshi ya Tanzania yalifanikiwa kumfukuza Idi Amini ambaye alivamia Tanzania akidai sehemu ya ardhi ya Tanzania. Baada ya kufukuzwa kwa Idi Amini majeshi haya yalisalia Uganda yakilinda usalama wa raia na kuimarisha utawala wa Obote.
Majeshi haya yakiwa huko Uganda, yalitumia lugha ya Kiswahili na hivyo, lugha hii ikaenea na kukua zaidi nchini Uganda.

6. Kuundwa kwa jumuiya ya Afrika Mashariki

Lugha rasmi katika jumuiya hii ni Kiswahili. Hivyo kwa kuwa Uganda ni miongoni mwa nchi wanachama wa jumuiya hii, hana budi kujifunza Kiswahili. Hivyo serikali ya Uganda imepitisha amri kuwa, lugha ya Kiswahili itafundishwa na kuwa somo la lazima katika shule za msingi na sekondari.

Ukuaji na ueneaji wa kiswahili Duniani

Lugha ya Kiswahili imekua na kuenea. Haitumiki Afrika pekee, bali ipo katika mabara yote: Asia, Ulaya, Australia na Amerika.

Jinsi Kiswahili kilivyoenea na kukua katika nchi mbalimbali duniani

Kuna namna mbalimbali ambazo zimesaidia kukua na kuenea kwa Kiswahili barani Afrika na ulimwenguni kwa jumla. Sababu hizo ni pamoja na:

I. Urahisi wa lugha yenyewe

Matamshi ya lugha ya Kiswahili yamerahisishwa kiasi cha kumwezesha kila mwenye kutaka kujifunza Kiswahili akimudu kwa haraka sana. Pia, miundo na maumbo yake ni rahisi.

II. Vyombo vya habari

Lugha ya Kiswahili inatumika kutangazia vyombo vya habari vya kimataifa kama vile: Voice of Amerika, British Broadcasting Corporation (BBC), Radio Deutchewelle, Radio China International na Radio France.

III. Mfumo wa elimu

Kuna vyuo vingi duniani vinavyofundisha lugha ya Kiswahili, vyuo hivyo vipo: Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Sudani, Ghana, Botswana, Afrika Kusini, Lesotho, Swazland, Nigeria, Misri, Uingereza, Ujerumani, Canada na vyuo vingine duniani.

IV. Sayansi na teknolojia

Kiswahili ndiyo lugha ya kwanza ya Kiafrika kutumika katika teknolojia ya mawasiliano. Kiswahili kinatumika katika mifumo mbalimbali ya intanenti kama: Tafsiri za google na menyu ya kiswahili katika matumizi ya simu.

V. Muziki

Wanamuziki wenye hadhi kuu wamekipandisha hadhi Kiswahili kwa sababu ya kuimba kwa lugha hii. Wanamuziki hao ni: marehemu Michael Jackson, Miriam Makeba, Pepe Kale na Sam Mangwana.

VI. Kutumiwa katika umoja wa Afrika (AU)

Kutumika kwa lugha hii katika vikao vya umoja wa Afrika kumeifanya ikue na kuenea kwa kasi Afrika na duniani kote.

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2023

Uhakiki wa Riwaya ya Watoto wa Maman’tilie