Mwanamke Uliyekula Pesa Zangu Nakutafuta | Sehemu ya Tisa

Bwana Mako gizani

Chafu Tatu alipenda sana kwenda katika danguro lile na alikuwa maarufu sana kwa mtindo wake. Huenda katika danguro akiwa na shilingi elfu kumi. Elfu moja ananunua sigara. Anabakiwa na elfu tisa. Elfu tatu anapata huduma kwa dada wa kwanza. Anamaliza nakutoka nje, anavuta sigara. Anatoa elfu tatu tena kwa dada wa pili, anatoka na kuvuta sigara, halafu anatoa elfu tatu kwa dada wa tatu, akimaliza hapo, anaenda nyumbani kulala. Chafu Tatu!

“Chafu Tatu,” aliita askari.

“Naam afande,” aliitika Chafu Tatu kwa adabu.

“Hela unatoa au hutoi?”

“Afande naomba unielewe, tayari nilikuwa nimeshaingia kwa dada wa pili, sasa nina elfu tatu tu,” alijibu Chafu Tatu, askari wakaangua kicheko, wakachukua ile elfu tatu na kumuachia kwa masharti kwamba, asirudie tena tabia hiyo kwani ni mara ya saba sasa anakamatwa.

Chafu Tatu alishuka katika gari lile la polisi. Nikabaki mimi na wao.

“Kijana acha kutuchelewesha, leta hera haraka,” alisisitiza askari ambaye kwa sababu ya tumbo lake kuwa kubwa sana, nilimbatiza jina, Tumbotumbo.

“Pesa zangu hazipo hapa afande,” nilijibu.

“Zipo wapi?”

“Zipo kwenye simu.”

“Twende kwa wakala ukatoe basi, mbona tunacheleweshana au unataka kurara ndani?”

“Twende tukatoe afande hakuna tatizo,” nilikubali nikaongozana na Tumbotumbo kuelekea kwa wakala.

“Jina lako nani?” aliuliza Tumbotumbo.

“Mako,” nilijibu nikitembea kawaida.

“Una jina moja kama mbwa?”

“Ndiyo,” nilijibu nikimtazama usoni, huku naongeza mwendo. Tumbotumbo akacheka akiyafinya macho yake madogo. Hapo nikakimbia haraka na kuvuka barabara inayopita magari yaendayo kwa Mama Zakaria. Tumbotumbo akanikimbiza, lakini nilishavuka barabara na sasa alishindwa kuvuka kwa sababu magari yaliyopita ni mengi. Sikumjali tena, nikaingia ndanindani huko, nikakunja kona nyingi, nilipojiridhisha, nikavuka barabara katika kituo cha Komakoma, huyoo nikaelekea katika makazi yangu.

XX    XX    XX

Sasa ilikatika miezi miwili na wiki moja tangu kumpoteza Asi. Nimefanya juhudi hii na ile kumtafuta lakini sijampata. Likizo yangu pia, ilikuwa imebakiwa na wiki tatu tu. Katika hali ya kukata tamaa, niliamua kwenda kusalimia wagonjwa katika hospitali ya Mwananyamala.

Majira ya saa kumi jioni, mwanamume aliyevalia suti ya kijivu na viatu vyeusi alionekana akipita katika geti la hospitali na kwenda moja kwa moja mpaka katika wodi ya watoto. Hakupata shida kupita getini kwa sababu ya ile suti lakini pia, ule ulikuwa muda wa kuona wagonjwa. Mwanamume huyo, alikuwa mimi Mako. Mtu mwenye jina moja kama mbwa!

Niliingia mpaka ndani ya wodi iliyohudumu watoto wadogo, vitandani walilala watoto na pembeni walikaa wazazi wao. Nilianza kwa kumsalimia mama mmoja aliyekuwa vitanda vya mwanzo karibu na mlango.

“Mama mwanao amepatiwa matibabu,” niliuliza baada ya salamu.

“Hajapatiwa baba, wamesema mpaka helaa!” alijibu Mama wa mtoto, machozi yakimlenga.

“Matibabu ni lazima, pesa italipwa baadae,” nilisema kwa sauti iliyosikika pote mle. Mama mmoja aliyekuwa kitanda cha tatu akadakia, “Mheshimiwa hata mwanangu hajapatiwa matibabu,” kabla sijakaa sawa, bibi mmoja akapaaza sauti, “Mkuu wa mkoa nisaidie mjukuu wangu hajapewa dawa siku ya tatu baba.”

Ama hakika bibi yule sijui aliwaza nini kuniita mkuu wa mkoa! Ni kweli siku tatu zilizopita, mkuu wa mkoa alibadilishwa ama wengine wanasema alitumbuliwa na wananchi hawakumfahamu vyema mkuu wao mpya ambaye hakuwa ameanza kuonekana katika Luninga.

Sasa kitendo cha yeye kuniita mimi mkuu wa mkoa, kiliamsha watu wote wodini mle, macho yao yakawa kwangu hata manesi na madaktari wakanyanyuka katika siti zao wakija mahali niliposimama.

Soma: Mwanamke Uliyekula Pesa Zangu Nakutafuta |Sehemu ya Kumi

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Uhakiki wa Tamthiliya ya Kilio Chetu